![]() |
Baadhi ya wanariadha wakichuana katika mbio za Ngorongoro Marathoni mwaka jana. |
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya vinywaji baridi ya Coca Cola ndio mdhamini mkuu mpya wa
mbio za Ngorongoro Marathoni zitakazofanyika Aprili 18.
Mmoja wa waratibu wa mbio hizo Meta Petro alisema kuwa Coca Cola
imeungana na Kampuni ya Zara Charity kudhamini mashindano hayo makubwa ya kila
mwaka.
Alisema kuwa awali Kampuni ya Simu za mkononi ya Tigo ndio ilikuwa
mdhamini mkuu wa mbio hizo ambazo huanzia katika lango kuu la kuingilia na
kutokea katika Bonde la Ngorongoro, lakini mwaka huu Coca Cola ndio watadhamini
mbio hizo.
Hatahivyo, Petro hakusema sababu za Tigo kutodhamini tena mbio
hizo lakini alisiaitiza kuwa tayari wanariadha kibao nyota wa Tanzania
wanaendelea kujiandikisha kwa ajili ya mbio hizo, ambazo kila mwaka zimekuwa
zikiongezeka msisimko wake.
Aidha, Petro alisema kuwa waandaaji wameongeza zawadi kwa
washindi, ambapo mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake, kila
mmoja ataondoka na kitita cha Sh. Milioni 1.2, wakati mwaka jana mshindi wa
nafasi hiyo alipewa sh. Milioni 1 kwa mwanaume na mwanamke 500,000, mshindi wa
pili mwaka huu atapewa sh. 600,000 wakati mwaka jana alipata 500,000 na
wanawake alipata 200,000.
Kwa mshindi wa tatu mwaka huu ataondoka na sh. 400,000 wakati
mwaka jana mshindi wa nafasi hiyo kwa wanaume alipewa sh.300,000 na kwa
wanawake alipewa 200,000.
Alisema kuwa mbio za mwaka huu wanatarajia wanariadha zaidi
kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki mbio hizo ambazo hutumika kupiga vita
ugonjwa hatari wa malaria na kutangaza utalii wa ndani na nje.
No comments:
Post a Comment