Tuesday 15 January 2019

DStv kuonesha Mubashara Michuano ya SportPesa 2019


Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice-Tanzania, Jacqueline Woiso akizungumza na waandishi wa habari wa wakati wa kutangazwa rasmi kwa ushirika kati ya SportPesa na SuperSport ambapo SuperSport kupitia DStv itarusha mubashara michuano hiyo itakayoanza wiki ijayo hapa jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji na Udhibiti wa SportPesa Tanzania Tarimba Abas.

Na Mwandishi Wetu
KING’AMUZI cha DStv ndicho pekee kitaonesha mubashara mashindano ya tatu ya SportPesa yatakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Januari 22 hadi 27 na kushindanisha timu za Tanzania na Kenya ili kumpata mshindi atakayecheza na Everton, imeelezwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice-Tanzania, Jacqueline Woiso alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa mashindano ya kombe hilo yataoneshwa na DStv kupitia Super Sports, ambayo ndio iliyopata udhini ya kuonesha mashindano hayo kama mshirika rasmi.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Udhibiti wa SportsPesa Tarimba Abas (Katikati) akizungumza wakati wa kutangazwa rasmi kwa ushirika kati ya SportPesa na SuperSport ambapo SuperSport kupitia DStv itarusha mubashara michuano hiyo itakayoanza wiki ijayo hapa jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice TanzaniaJacqueline Woiso na Mkuu wa Uendeshaji Baraka Shelukindo (kushoto)

Mbali na vigogo vya soka Tanzania vya Simba na Yanga, timu zingine zitakazoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Mbao FC pamoja na Singida United za Tanzania wakati zile za Kenya ni Gor Mahia, AFC Leopard, Bandari na Kariobangi.

Gor Mahia ndio washindi wa kihistoria baada ya kulitwaa taji hilo mara mbili na kufanikiwa kucheza mara mbili dhidi ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Michuano hiyo itakuwa na mvuto wa aina yake kwani mbali na ukubwa, umaarufu na utani wa timu shiriki, pia kila timu itataka kutwaa kombe hili na hatimaye kupata fursa ya kucheza na moja ya timu maarufu ya soka nchini Uingereza – Everton FC.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Udhibiti wa SportsPesa Tarimba Abas (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Uendeshaji wa MultiChoice Tanzania Baraka Shelukindo wakati wa hafla ya kutangazwa rasmi kwa ushirika kati ya SportPesa na SuperSport ambapo SuperSport kupitia DStv itarusha mubashara michuano hiyo itakayoanza wiki ijayo hapa jijini Dar es Salaam.

Woiso alisema  jana kuwa SuperSport kupitia DStv itarusha mubashara mashindano hayo yatakayoanza wiki ijayo jijini Dar es Salaam.

 “Tunafurahi kuujulisha umma wa watanzania kuwa hamu yao ya kushuhudia michuano hii mubashara kupitia DStv sasa imepatiwa jibu, sasa watashuhudia burudani hii ya aina yake tena kuanzia kifurushi cha chini kabisa cha Bomba,” alisema Jacqueline.

 “Michezo yote itaonekana kupitia DStv SuperSport 9, ambayo inapatikana katika vifurushi vyote. Tumeamua kufanya hivyo ili kuwapa watanzania fursa ya kushuhudia mashindano haya ambayo yanazidi kujipatia umaarufu kila uchao”.

Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Jacqueline Woiso akimkabidhi mpira Mkurugenzi wa Uendeshaji na Udhibiti wa SportsPesa Tarimba Abas muda mfupi baada ya kutangaza rasmi ushirika kati ya SportPesa na SuperSport ambapo SuperSport kupitia DStv itarusha mubashara michuano hiyo itakayoanza wiki ijayo hapa jijini Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas amesema “Tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo miaka mitatu iliyopita, mashindano haya yamekua moja ya mashindano makubwa na yanayopendwa sana Afrika Mashariki yote.

Hili ni jambo kubwa sana kwani wachezaji wetu wataweza kuonesha vipaji na viwango vyao na hivyo kuwatangaza kote duniani. Natoa rai kwa timu zinazoshiriki kuhakikisha zinaonesha viwango vya juu  kabisa kwani huu ni ulingo muhimu wa kuonesha uwezo na ujuzi wao wa soka kwa timu husika lakini pia na kwa wachezaji,” alisema Tarimba.

 Mshindi wa Kombe la SportPesa 2019 atajishindia dola za Marekani 30,000 pamoja na kucheza dhidi ya Everton, moja ya timu maarufu kabisa za soka Uingereza wakati mshindi wa pili atapata dola za Marekani 10,000 wakati mshindi wa tatu atapata dola 7,500 na mshindi wa nne dola 5,000. Timu zote zitakazo tolewa robo fainali zitapata dola 2,500 kila moja.

Michuano ya Kombe la SportPesa ilianza rasmi mwaka 2017 katika michuano iliyofanyika hapa Tanzania, ambapo mshindi – Gor Mahia alicheza na Everton hapa hapa Tanzania. Msimu wa pili wa mashindano hayo yalifanyika huko Nakuru Kenya mwaka jana, mshindi kwa mara ya pili Gor Mahia alikwenda kucheza na Everton huko Liverpool Uingereza mwezi Novemba.

Thursday 10 January 2019

JNIA Yajipanga Madhubuti Kiusalama

Mkurugenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo. 

Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam umesema kuwa umejipanga mathubuti kiusalama.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha wakati akitoa ufafanuzi kuhusu madai ya abiria kuchukua muda mrefu katika jengo la pili la abiria wakati wakiwasili kiwanjani hapo kabla ya kutoka nje ya jengo hilo.
Mbali na madai hayo, pia Rwegasha alitolea ufafanuzi madai ya msanii maarufu nchini Ray Kigosi kuwa aliibiwa raba na perfume kiwanjani hapo kutoka katika begi lake wakati akisafiri kwenda Dubai akitokea JNIA tarehe 3 Jan, 2019.
Alisema kuwa mtangazaji wa Radio Clouds, Ephahimu Kibonde alilalamika katika kipindi cha Jahazi kuwa, alitumia saa mbili kabla ya kutoka nje ya Kiwanja hicho baada ya kuwasili akitokea Afrika Kusini.
Kibonde alishangaa abiria raia wa Tanzania kuchukua muda mrefu Kiwanjani hapo wakati  alitakiwa kutumia muda mfupi kwa kuwa hana mambo mengi ya kukaguliwa,  tofauti na wale wanaotoka nje ya nchi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Idara ya Uhamiaji JNIA, Kanankira Mbise (kuhoto) akizungumza huku Mkurugenzi wa kiwanja hicho, Paul Rwegasha akimsikiliza.
Rwegasha alisema kuwa JNIA imefungwa kamera za usalama za CCTV katika maeneo yote ili kuhakikisha usalama wa abiria na mali zao wakati wakiwasili au kuondoka nchini kupitia kiwanjani hapo.
 Alisema kuwa mbali na mifumo mathubuti ya ulinzi na usalama, pia uongozi wa kiwanja hicho unasera ya kutotoa msamaha kwa Mtumishi yeyote atakayefanya udokozi na uwizi wa mali za abiria, ambapo akibainika anapelekwa kwenye vyombo vya sheria na kufukuzwa kazi moja kwa moja.
“Kamwe hatutamvumilia mfanyakazi yeyote mwenye tabia za kidokozi, ambaye atabainika kuiba mzigo wa abiria, kwani tutamtimua mara moja, na hilo kila mfanyakazi analijua ipo katika sera yetu,, “alisema Rwegasha.
Damas Temba (kushoto), ambaye ni Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiwanjani hapo akizungumza sula la usalama.
Aliomba watu wanapopata matatizo au changamoto kiwanjani hapo, kwanza wawasiliane na uongozi wa kiwanja ili kupata ufafanuzi na utatuzi wa matatizo yao kwa haraka, ambapo mwenendo wake utaangaliwa kwenye kamera za usalama ambazo zipo tangu abiria akiingia kiwanjani hadi anapopanda ndege, badala ya kukimbilia kuandika kwenye mitandao ya kijamii, kwani kufanya hivyo sio tu kunadhalilisha kiwanja, bali na nchi nzima kwa ujumla.
Akizungumzia Jengo la tatu la abiria linalojengwa maeneo ya Kipawa, Rwegasha alisema kuwa wanatarajia kuanza kulitumia mara baada ya kukamilika kwani kwa sasa kuna maeneo yanaendelea na ujenzi, licha ya nje kuonekana kama jengo hilo limekamilka. Jengo hili linatarajiwa kukabidhiwa kwa serikali Mei 2019.
Naye Kanankira Mbise, ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Idara ya Uhamiaji kiwanjani hapo alisema kuwa, idara yake imekuwa ikihakikisha inafanya shughuli zake kwa haraka na kufuata taratibu ili kuondoa msongamano wa abiria wanaowasili kutoka nje ya nchi.
Kwa upande mwingine, naye Damas Temba, ambaye ni Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiwanjani hapo alisema wananchi wanatakiwa kupata elimu zaidi ya kodi, kwani kuna vitu vikiingizwa nchini lazima vilipiwe kodi, hata kama ni zawadi, ambazo zikiwa ni nyingi.
“Abiria wanaosafiri na usafiri wa ndege wasione eneo la Forodha kama ni adui watoe ushirikiano kwa kuwa wakweli wa vitu walivyobeba, kwani hata zawadi zinalipiwa ushuru, mfano mtu anaweza akawa na begi lililojaa nguo na kudai ni zawadi, au saa za mkononi zaidi ya tatu, zipo sheria kabisa zenye kuonesha na kuzungumzia hili,” amesisitiza Temba.
Pia alisema mizigo lazima ikaguliwe kwa ajili ya usalama na mambo mengine, lakini wanajitahidi kufanya mambo kwa haraka ili kuepusha msongamano wa watu katika eneo la Forodha.
Hatahivyo, katika kipindi cha jana Jumatano cha Jahazi katika Radio ya Clouds, Kibonde alionekana kushangazwa tena na maelezo ya Temba kuwa hata zawadi  zinatozwa kodi.

Tuesday 8 January 2019

Bonanza la Shimiwi Kufanyika Dodoma Mwezi Ujao

Mchezo wa netiboli nao utakuwepo katika bonanza hilo la michezo la Shimiwi.

Na Mwandishi Wetu
BONANZA la Michezo la Shirikisho ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi) litafanyika jijini Dodoma Februari 2 na 3 kwenye Uwanja wa Jamhuri, imeelezwa.

Tamasha hilo litatanguliwa na mkutano wa viongozi wa michezo, ambao ni wenyeviti na makatibu wa klabu za michezo za Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Shimiwi Moshi Makuka, mbali na mazoezi ya viungo na mbio za pole (jogging), tamasha hilo litahusisha michezo ya mpira wa miguu, netiboli na ule wa kuvuta kamba.

Makuka alisema katika taarifa hiyo ni matumaini yake kuwa waajiri watatoa ruhusa kwa wahusika ili kuhakikisha bonanza hilo la michezo linafana kwa kushirikisha watu wengi bila kukosa.
Mkutano huo utafanyika Februari Mosi kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufuatiwa na bonanza hilo litakalofanyika kwa siku mbili kuanzia Februari 2 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kuanzia saa 12:30 asubuhi.

Alisema kuwa waajiri mbali na kutoa ruhusa, pia wanatakiwa kuwapatia wafanyakazi wao nauli na posho ya kujikimu ili waweze kushiriki vizuri katika mkutano na bonanza hilo la michezo katika siku zilizotajwa.