Tuesday 31 October 2017

Tottenham, Real Madrid kuwania kutinga mchujo

LONDON, England

TOTTENHAM na Real Madrid zinakutana kesho katika moja ya mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, huku kila moja ikiwa na nafasi ya kufuzu kucheza kwa hatua ya 16 bora kutoka katika Kundi H.

 

Timu yoyote itakayoshinda kesho inaweza kufuzu kucheza hatua hiyo, ambayo inajulikana kama raundi ya mwanzo ya mtoano.

 

Tottenham Hotspur FC na mabingwa watetezi Real Madrid zinakutana kwenye Uwanja wa Wembley, kila moja ikijua umuhimu wa mchezo huo katika kusonga mbele katika mashindano hayo.

Baada ya timu hizo kutoka sare ya kufungana 1-1 katika mchezo wao wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Santiago Bernabéu Hispania katika raudi ya tatu, timu hizo zinalingana kwa pointi kileleni mwa msimamo wa kundi lao.

Timu hizo zinalingana kila kitu katika msimamo wa kundi hilo, ambapo kila moja ina pointi saba, huku Tottenham ikiongoza na kufuatiwa na Real.

 

Timu zinazofuata katika msimamo wa kundi hilo, Borussia Dortmund na APOEL FC kila moja ina pointi moja.

Tottenham haijawahi kuifunga Madrid, ambapo imepoteza mechi tatu kati ya tano walizokutana huko nyuma, huku wakitoka sare mara mbili.

 

Bao la kujifunga la Raphaël Varane katika mchezo wao watatu ndio pekee, ambao Tottenham imewahi kufunga ilipocheza dhidi ya Real Madrid katika dakika 450 walizocheza.

MECHI WALIZOKUTANA

Mchezo wa kwanza wa Tottenham kukutana na Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ulikuwa katika msimu wa mwaka 2010/11, ambao ulimalizika kwa Real kushinda 4-0 nyumbani katika mchezo wa kwanza wa robo fainali.

Mabao hayo yalifungwa na Emmanuel Adebayor katika dakika ya nne na 57 na mengine yaliwekwa kimiani na Ángel Di María (72) na Cristiano Ronaldo (87), huku Tottenham ikicheza muda mwingi wakiwa 10 baada ya Peter Crouch kutolewa nje baada ya kupewa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 15.

 

Ronaldo ndiye aliyefunga bao pekee katika mchezo wa marudiano uliofanyika kwenye Uwanja wa White Hart Lane wakati Merengues wakikamilisha ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Tottenham, ambayo ilikuwa na akina Gareth Bale na Luka Modrić, ambao wote kwa sasa wapo Real Madrid.

MAN CITY VS NAPOLI

Mchezo mwingine wa leo utakaovuta hisia za wapenzi wengi wa soka ni ule utakaowakutanisha vinara wa Ligi Kuu ya England, Manchester City dhidi ya Napoli.

Manchester City haijafungwa hata mchezo mmoja na imejikusanyia pointi tisa baada ya kushuka dimbani mara tatu, inacheza na Napoli iliyopo katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu tu.

Man City inataka kushinda mchezo huo wa leo ili kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kutoka katika Kundi F.

MECHI ZINGINE

Mechi zingine kesho zitakuwa kati ya Beşiktaş            itakayocheza dhidi ya Monaco wakati Sevilla            itaikaribisha Spartak Moskva huku Shakhtar Donetsk ikipepetana na Feyenoord.


Mechi nyingine ni Liverpool itakuwa na kibaruia kizito kwenye uwanja wake wa Anfield wakati itakapoikaribisha Maribor huku Porto   itacheza dhidi ya RB Leipzig,na Borussia Dortmund            watacheza na APOEL.

Makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya

Kundi F

PosTeamPWDLGFGAGDPts
1Manchester City33008179
2Shakhtar Donetsk32014406
3Napoli31025503
4Feyenoord300329-70

Kundi G

PosTeamPWDLGFGAGDPts
1Beşiktaş33007259
2RB Leipzig311145-14
3Porto31026603
4Monaco301226-41

Kundi H

PosTeamPWDLGFGAGDPts
1Tottenham Hotspur32107257
2Real Madrid32107257
3Borussia Dortmund301237-41
4APOEL301217-61

BMT yaendesha mafunzo kwa walimu wa michezo

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja.

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) linaendesha mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari ili kuendeleza michezo nchini.

Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja alisema jana kwa njia ya simu kuwa, kwa sasa mafunzo hayo yako katika tarafa ya Ntebele wilani Kyela mkoani Mbeya.

Alisema kozi hiyo inatarajia kumalizika Jumamosi, ambapo walimu 49 kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari wanahudhuria mafunzo hayo.

Kiganja alisema kuwa mafunzo yanayotolewa ni pamoja na yale ya ufundishaji soka, mpira wa wavu, netiboli, riadha, mazoezi ya viungo na utawala katika michezo.

Alisema kuwa mbali nay eye (Kiganja) wakufunzi wengine wa mafunzo hayo ya wiki mbili ni pamoja na Danny Korosso, Richard Mganga na Damian Chonya, ambaye anafundisha netiboli.

Alisema baada ya hapo mafunzo hayo yataendelea ama Songwe, Rukwa au Mtwara kutegemea na utayari wa mahali husika kwa ajili ya mafunzo hayo.

Juganja alisema kuwa wameamua kutoa mafunzo tarafani ili kuwapunguzia washiriki gharama za nauli na malazi.

“Tumeamua kuwafuata na kuendesha ya mafunzo ya michezo huko huko ili kuwapunguzia gharama ya nauli na malazi, “alisema Kiganja.


Alisema tayari mafunzo hayo yalishafanyika jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya walimu 80 walihitimu katika mafunzo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Monday 30 October 2017

Kivumbi mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kesho

Baadhi ya wachezaji wa Basel ya Uswisi wakifanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi kesho Jumanne.

ZURICH, Uswisi

RAUNDI ya nne ya Ligi ya Mabigwa wa Ulaya hatua ya makundi inaendelea tena kesho, huku Bayern Munich, Chelsea, Manchester United, Barcelona na Atletico Madrid ni miongoni mwa timu zitakazoshuka dimbani.

Tayari kila timu imeshacheza mechi tatu na leo na kesho zinakamiisha mechi nne kila moja na kubakisha mbili ili kukamilisha hatua ya makundi kabla ya kufuzu kwa 16 bora au hatua ya kwanza ya mtoano.

Timu mbili za kwanza kutoka katika kila kundi zitakuwa zimefuzu kucheza hatua hiyo ya timu 16 bora.

BAYERN MUNICH

Bayern Munich wanatarajia kukabiliana na Celtic iliyo tofauti kabisa katika mchezo wa Kundi B utakaofanyika leo jijini Glasgow tofauti na kikosi walichocheza nacho awali, ambacho walikifunga mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza Ujerumani.

Mshambuliaji Leigh Griffiths anasema kuwa Celtic kwa sasa wako vizuri zaidi na mabingwa hao wa Ujerumani wasitarajie kupata mteremko.

 

Kimsimamo, Celtic wako katika nafasi ya tatu katika Kundi B, lakini sasa imefikia rekodi yao waliyoiweka miaka 100 iliyopita ya kucheza mechi 62 za nyumbani bila kufungwa.

Timu hiyo inajua kuwa itakuwa nje ya mashindano hayo endapo itapoteza mchezo huo na Paris St-Germain (PSG) itakwepa kipigo cha nyumbani kutoka kwa Anderlecht.

"Mchezo utakuwa tofauti kabisa hapa, hasa kutokana na mashabiki kuwa nyuma yetu, “ alisema Griffiths.

"Katika kipindi cha pili [mchezo wa ugenini] tulicheza vizuri zaidi. Tulitengeneza nafasi kibao za kufunga mabao.

Endapo kikosi cha kocha Brendan Rodgers kitatolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa leo, watabaki kusaka nafasi ya tatu ili kufuzu kucheza Ligi ya Ulaya katika mechi mbili za mwisho hatua ya makundi.

Rodgers alikuwa kocha wa Liverpool F.C. kuanzia mwaka 2012 hadi 2015 kabla ya kutua Celtic, hivyo leo atakuwa akipambana na timu yake yazamani.

Nyumbani, Celtic inaoongoza katika Ligi Kuu ya Scotland, lakini Griffiths anasema kuwa walikatishwa tamaa kupoteza pointi mbili Jumamosi baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Kilmarnock.

 

Wakati winga Patrick Roberts ataukosa mchezo huo dhidi ya mabingwa hao wa Ujerumani kutokana na maumivu, kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes ana uhakika Robert Lewandowski atakuwa fiti kwa mchezo huo.

Wakati huohuo, beki wa kulia wa Ujerumani Joshua Kimmich anategemea timu yao itafuzu kwa hatua ya 16 bora huku ikiwa imebakisha mechi mbili kabla ya kukamilisha hatua ya makundi wakati watakaposafiri kwenda Glasgow.

CHELSEA DIMBANI

Kocha wa Chelsea, Antonio Conte anasema kuwa anatumaini ataweza kumchagua kiungo N'Golo Kante kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Roma utakaofanyika leo.

Kante aliumia nyama za paja wakati akiichezea timu ya taifa ya Ufaransa mapema mwezi huu na alikosa mechi tano za awali za Chelsea, ikiwemo ile waliotoka sare ya 3-3 nyumbani dhidi ya Roma siku 11 zilizopita.

Kimsimamo Chelsea inaongoza katika Kundi C ikiwa na pointi saba na inaweza kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya 16 bora endapo itapata ushindi katika mchezo wake huo wa Italia leo.

Kocha Conte anasema kuwa hawezi kuthubutu kumchezesha Kante endapo mchezaji huyo Mfaransa hatakuwa fiti vya kutosha.

"Yeye (Kante) anaweza kuwa tayari," alisema kocha huyo Muitalia wakati alipozungumza na waandishi wa habari. Najua sana umuhimu wa mchezaji huyu. Nataka kuhakikisha kuwa yuko tayari….”

Sare na Roma katika Uwanja wa Stamford Bridge ilikuja baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu kufungwa mfululizo na kuwaacha wakiwa pointi tisa tofauti na vinara Manchester City.

Hatahivyo, ushindi wa timu hiyo katika ligi dhidi ya Watford na ule wa Bournemouth na kuifunga Everton katika Kombe la Ligi, kumeiongezea nguvu timu hiyo.

"Ulikuwa ushindi mzuri (1-0 dhidi ya Bournemouth Jumamosi) kwa kujijengea kujiamini, ushindi mzuri kabla ya mchezo mwingine mgumu dhidi ya Roma katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, “alisema.

"Ushindi ulikuwa muhimu kutupa mwendelezo kushinda dhidi ya Watford, na Everton katika (Kombe la Ligi), na sasa tunajiandaa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Roma.”

Alvaro Morata anatarajia kuanza katika mchezo huo wa leo, licha ya kutofunga katika mechi nne tangu aliporejea kutoka katika maumivu ya nyama za paja aliyoyapata walipocheza na kufungwa na Manchester City mwezi uliopita.

 

VINARA BARCELONA

Barcelona wenyewe leo watakuwa dimbani kupepetana na Olympiakos Piraeus katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi.

Barcelona ambao wanashuka uwanjani leo huku wakiwa wanaoongoza katika kundi lao kwa kuwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu hadi sasa.

Mbali na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Barcelona pia inaongoza katika Ligi Kuu ya Hispania ya La Liga ikiwa pointi nne dhidi ya Valencia iliyopo katika nafasi ya pili.

 

MANCHESTER UNITED

Manchester United leo wanashuka dimbani kucheza dhidi ya Benfica katika mchezo itakaofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford ikiwa imeshinda mechi zake zote tatu na kujikusanyia pointi tisa.

Katika ligi ya nyumbani, Manchester United iko katika nafasi nzuri kwani iko nyuma ya vinara wa Ligi Kuu ya England Man City.

MECHI ZINGINE LEO

Leo Oktoba 30 mechi zingine zitakazofanyika ni ile ya Atlético Madrid itakayokuwa mwenyeji wa Qarabağ katika mchezo utakaofanyikia kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitano, Sporting CP     itaikaribisha Juventus katika mchezo mwingine.

Nayo Basel itakwaana na CSKA Moskva         katika mchezo mwingine wa mashindano hayo huku PSG watatoana jasho na Anderlecht katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Parc des Princes.

Nyalandu atema ubunge na nyadhifa zote CCM

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (pichani), leo ametangaza rasmi kujiondoa katika Chama cha Mapinduzi na kuomba kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo au Chadema.

Kauli hiyo ameitoa leo, ambapo alisema anajivua nyadhifa zote alizonazo ndani ya Chama cha Mapinduzi, ukiwemo Ubunge, mbao ameutumkia kwa zaidi ya vipndi vinne.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Singida, chama hicho mkoa humo kimebainisha kufurahishwa na hatua hiyo na kudai kuwa alikuwa mzigo jimboni kwake.

Nyalandu baada ya kutangaza kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge wa Singida Kaskazini na kuihama CCM, alikiomba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumpokea.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Martha Mlata, alisema pamoja na kwamba hajapata taarifa rasmi za kujiuzulu ubunge na kuhama chama kwa Nyalandu, amefurahi kama itakuwa ni kweli mbunge huyo ameachia nafasi ya ubunge.

“Mimi kama Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida nafurahi kama kweli ameondoka, kwa sababu kwa kweli alikuwa ni mzigo ndani ya chama. Nimeteseka sana kuliweka jimbo lake vizuri,” alisisitiza Mlata.

Alisema mbunge huyo alikuwa hatimizi majukumu yake ya kibunge ndani ya jimbo lake, hafanyi ziara zozote jimboni wala kuhudhuria vikao vya Bunge.

“Niseme ukweli tumefurahi na nina uhakika hata vijana wetu kule jimboni kwake wamefurahi. Afadhali maana ametusaidia kumpata mtu atakayelitendea haki jimbo lile,” alisema.

Awali, wakati akitangaza kuhama chama chake na kujiuzulu nafasi ya ubunge jijini Arusha leo, Nyalandu alisema ameamu kujiuzulu  nafasi zake zote ndani ya chama hicho ikiwemo ujumbe wa Halmashauri Kuu pamoja na nafasi zote za uongozi ndani ya Chama hicho.

Pia alisema tayari amemwandikia Spika wa Bunge Job Ndugai, barua ya kujiuzulu nafasi yake ya ubunge aliyoitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2000 hadi sasa.

Alisema amechukua  uamuzi huo  kutokana na kutoridhishwa kwake  na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu.

Aidha, alitaja sababu nyingine kuwa ni ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzake na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa kibunge wa kutunga sheria na kuisimamia serikali kutokuwa uhuru.


 “Najiuzulu nafasi zangu zote na naomba Chadema wanipokee kwa mikono miwili na pia natoa fursa kwa wananchi wachague mtu wanayemtaka  mara uchaguzi utakapotangazwa, lakini kwa sasa nakihama Chama cha Mapinduzi, “alisema.

Sunday 29 October 2017

Wafanyakazi TAA kupatiwa mafunzo ya kazi

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw.Richard Mayongela (wa tatu kulia), jana akiandika mambo mbalimbali katika mkutano na wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Mwanza. Wa pili kushoto ni Meneja wa kiwanja hicho Bi. Esther Madale na wa kwanza kulia ni Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Agustino Magele.


Na Mwandishi Wetu

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wataendelezwa kwa kupata mafunzo mbalimbali, ili kuongeza weledi na tija kazini, imeelezwa.

Kauli hiyo ambayo ni moja ya malengo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela jana alipoongea na wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Mwanza pamoja na Kituo cha Zimamoto na Uokoaji, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi.

Bw. Mayongela alisema  wafanyakazi wakipata mafunzo zaidi ya kazi zao wataisaidia serikari kufanikisha moja ya malengo yake makuu ya kukuza uchumi, ambapo watakuwa na mbinu za kisasa zikiwemo za ukusanyaji wa mapato kwa uaminifu na uadilifu, ambapo viwanja vya ndege ni moja ya vyanzo vya mapato hayo.

Hata hivyo, alisema  atapitia majalada ya wafanyakazi wote ili kubaini waliojiendeleza kwa mafunzo mbalimbali, lakini wanafanyakazi zisizo za kada zao,  hivyo ataangalia uwezekano wa kuhamishiwa kwenye kada zao ili waweze kufanya kazi kwa weledi zaidi.

Edger Mwankuga aliyesimama jana akiwasilisha hoja zake mbalimbali mbele ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (hayupo pichani) alipokutana na wafanyakazi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.

“Wapo wafanyakazi wa kada mbalimbali waliojiendeleza, lakini hadi sasa bado wapo kwenye kada walizoajiriwa nazo na zipo tofauti na sasa, nitangalia uwezekano wa kupangiwa kada zao ili waweze kuenda na kasi ya kazi zinazowahusu,” alisema Bw.Mayongela.

Pia malengo yake mengine alisema atahakikisha anaboresha maslahi ya wafanyakazi wa ngazi ya chini ili kunyanyua ari na tija kazini, ambapo kwa sasa wamekata tamaa kutokana na maslahi duni yasiyolingana na kazi zao.

Lakini aliwaasa wafanyakazi wenye mamlaka ya kuingia mikataba na wafanyabiashara, kubadilika na kuhakikisha wanatumia vyema sheria zinazowaruhusu kuingia mkataba baina yao na sio kukiuka, kwani inaweza kuwaletea matatizo, endapo itabainika kuwepo kwa udanganyifu uliosababisha upotevu wa mapato ya serikali, kwa kuwa atahakikisha TAA inajitosheleza kimapato na kujiendesha kwa baadhi  ya mambo ya ndani bila kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu.

Alisema kwa sasa TAA imekuwa ikinyooshewa kidole kwa kusemwa vibaya na wadau mbalimbali, lakini  kupitia umoja na mshikamano wa wafanyakazi atahakikisha anarudisha taswira nzuri iliyokuwepo na kujenga Mamlaka mpya yenye kuaminika.

Pia alizungumzia uadilifu na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi, kuacha mara moja vitendo vinavyoweza kuhujumu jitihada na vipaumbele kwa mwaka huu wa fedha 2017/18 hadi kufikia 2020/21.


Wafanyakazi wa idara mbalimbali za kiwanja cha ndege cha Mwanza na kikosi cha zimamoto na uokoaji, wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela alipokutana nao jana kujadili masuala mbalimbali ya kiuendeshaji.

“Mimi ni mgeni katika nafasi hii (ya Ukurugenzi), lakini ninachoomba tufanye kazi kwa bidii, mvunje makundi na tukosoane kwa kujenga na sio kubomoa, na viongozi muache kupendelea mtende haki kwa wafanyakazi wote, tukiwa na lengo la kuijenga TAA yenye mwelekeo mpya,”alisema Bw. Mayongela.