Saturday, 30 January 2016

yanga yachezea kichapo cha kwanza kutoka kwa Coastal, Simba yaisambaratisha African Sports kwa mabao 4-0 
Na Waandishi Wetu
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga jana ilipoteza mchezo wa kwanza katika ligi hiyo baada ya kufungwa mabao 2-0 na Costal Union, huku watani zao Simba wakiondoka na pointi zote tatu dhidi ya African Sports kwa ushindi wa mabao 4-0.

Ushindi huo, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 36 baada ya kucheza mechi 16, sasa ikizidiwa pointi tatu tu na Yanga, wanaoongoza kwa pointi 39 sawa na Azam FC ambayo jana haikucheza bambaykila mmoja.aada ya kuwa nchini Zambia kucheza `Bonanza'.
 
Simba iliyocheza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ilipata bao lake la kwanza dakika ya 14 kupitia kwa mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza aliyefumua shuti kali kwa mguu wa kushoto baada ya pasi ya beki Hassan Kessy.

Kessy mwenyewe akafunga dakika ya 30 kuipatia Simba SC bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib na kumchambua vizuri kipa Zakaria Mwaluko.

Kiiza akamlamba chenga kipa Mwaluko baada ya kupata pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto kuifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 42.

Hajji Ugando akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 75 baada ya kupokea nzuri ya kiungo aliyekuwa katika kiwango kizuri.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Hassan Kessy, Abdi Banda, Juuko Murshid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto/Mussa Mgosi dk86, Jonas  Mkude, Haji Ugando/Said Ndemla dk76, Ibrahim Hajib na Hamisi Kizza/Brian Majwega dk67. 

African Sports; Zakaria Mwaluko, Mwaita Gereza, Halfan Twenye, Juma Shemvuni, Rahim Juma, Mussa Chambega/Hussein Amir dk51, Ally Ramadhani, Pera Ramadhani, Hamad Mbumba, Rajab Isihaka na James Mendy/Mohammed Issa dk56.

KWA UPANDE WA YANGA:

Yanga imefungwa mabao 2-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na matokeo hayo yanawafanya wabaki na pointi zao 39 baada ya kucheza mechi 16, sawa na Azam FC iliyocheza mechi 15.

Coastal Union walipata bao lao la kwanza dakika ya 27 kupitia kwa beki wa zamani wa Simba,   Miraj Adam aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu lililomparaza mikononi kipa Deo Munishi ‘Dida’ kabla ya kutinga nyavuni.

Refa Andrew Shamba wa Pwani aliwapa nafasi ya kupiga faulo Coastal Union, baada Miraj Adam mwenyewe kuangushwa na beki wa Yanga, Kelvin Yondan nje kidogo ya boksi.

Mshambuliaji chipukizi, Juma Mahadhi aliifungia bao la pili Coastal Union dakika ya 62 baada ya pasi nzuri ya Hamad Juma.

Bao hilo liliwavunja nguvu kabisa wachezaji wa Yanga SC na kujikuta wanacheza bila malengo. Refa Andrew Shamba alimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Yanga, Kevin Yondan dakika ya 100.
Awali, dakika ya 97 Shamba alijichanganya kwa kumuonyesha kadi nyekundu Said Jeilan badala ya njano.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratias Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Paul Nonga dk76, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Issoufou Boubacar dk80.

Coastal Union; Fikirini Bakari, Hamad Juma, Adeyoum Ahmed, Said Jeilan, Miraji Adam, Sabo Youssouf, Juma Mahadhi/Omar Wayne dk86, Ayoub Yahya/Mtenge Juma dk97, Chidiebele Abasarim, Ally Ahmed  na Ismail Mohammed.


CONGO DR YAWAFUNGISHA VIRAGO WENYEJI RWANDA KWA KUIFUNGA 2-1 KATIKA MUDA WA NYONGEZAKIGALI, Rwanda
JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ilihitaji muda wa ziada kuwaondosha wenyeji Rwanda katika mashindan ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani (Chan), baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa robo fainali jijini hapa.

Doxa Gikanji aliipatia Congo bao la kuongoza dakika 10 tangu kuanza kwa mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Amohoro.

Hatahivyo, wenyeji walisawazisha dakika 12 baada ya mapumziko kwa bao lililowekwa kimiani na Ernest Sugira.

Padou Bompunga aliifungia Congo bao la ushindi katika muda wa nyongez na hiyo ikiwa na maana kuwa washindi hao sasa watakutana ama na Zambia au Guinea katika nusu fainali itakayopigwa Jumatano.

Congo, ambayo iliwahi kutwaa taji hilo mwaka 2009, ilipata uongozi wa mchezo wakati Rwanda iliposhindwa kuokoa vizuri mpira na mpira huo kuangukia kwa Gikanji aliyekuwa nje ya eneo la hatari na kupiga shuti kali na kumuacha kipa wa Rwanda Eric Ndayishimiye akishindwa kuokoa shuti hilo.

Dakika tisa baadae, huku Chui hai wa Congo wakiwa wametawala, Jonathan Bolingi alipiga shuti lililogonga mwamba.

Bao la kusawazisha la Rwanda la kipindi cha pili lilipatikana kutoka kwa Sugira likiwa ni bao lake la tatu.

Mchezaji huyo alifunga bao hilo baada ya kufanikiwa kuwa nyuma ya mabeki wa Congo, na kupiga shuti lililompita kipa Ley Matampi.

Muda mfupi baadae mchezaji huyo nusura afunge baada ya kuitoka beki ya Congo na Matampi akiwa yeye na kipa, alipiga juu ya wavu wa goli.

Timu zote zilishambuliana kwa zamu kabla ya filimbi ya mwisho, lakini hadi dakika 90 za kawaida za mchezo zinamalizika, timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1.

Wakati muda ukiendelea kuyoyoma watu wakitarajia timu hizo zitapigiana penalty kumpata mshindi, Bompunga alipiga mpira wa kichwa cha nyuma na mpira kumpita Ndayishimiye.

Serena Williams atolewa nishai na kibonde Australian OpenMELBOURNE, Australia
MCHEZAJI Angelique Kerber huku akishangiliwa na mashabiki kwenye Uwanja wa Rod Laver Arena leo Jumamosi usiku ikiwa ni zaidi ya saa mbili alikiangusha kigogo Serena Williams na kutwaa taji la micbuano ya tenisi ya Australian Open.

Kerber alimchapa Serena ambaye ni bingwa namba moja kwa ubora katika mchezo huo duniani kwa upande wa wanawake kwa 6-4, 3-6, 6-3. Ni taji la kwanza kubwa kwa Kerber, na ni la kwanza kwa mchezaji wa Ujerumani katika karne hii.

Kerber, ambaye ana umri wa miaka 28 na ni mwaka wake wa 14 katika katika mchezo huo, alikuwa akicheza fainali yake ya kwanza ya mashindano makubwa, ambapo alianza mmchezo huo kwa kuokoa mpira uliopigwa na bingwa huyo mara 21, kabla hajafanya matokeo ya kuongoza kwa 2-0.

Bingwa huyo alijikuta mipira mingi aliyoipiga iliishia kwa Kerber, na Kerber alifanya kweli na kuendelea kumsambaratisha mpizani wake.

Williams lionesha kuzinduka katika seti ya pili baada ya kucheza vizuri na kumuwezesha kufikia hatua hiyo bila ya kupoteza seti hiyo. Mchezo huo uliendelea na mshindi kuamriwa katika seti ya tatu.

Mashabiki walipagawa baada ya Kerber akipomsambaratisha Williams katika mchezo wa kwanza.
Ilikuwa ni kawaida kwa mashabiki uwanjani hapo kulipuka kwa furaha kwa kumshangilia Kerber. 

Mashabiki wa mchezo wa tenisi wa Australia mi kawaida yao kumshangilia mchezaji asiyepewa nafasi ya kushinda, lakini Williams alisema kuwa huo ni uwanja anbo amekuwa akihisi kupendwa sana.

Williams aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi kuwa, ilikuwa miujiza kucheza fainali hapa. Baada ya kushinda hii na mataji mengine mawli makubwa  mwaka jana. Alitarajia kuanza taratibu mashindano hayo. Alikuwa nje ya uwanja kwa miezi minne akiuguza maumivu ya kufungwa katika nusu fainali ya mashindano ya U.S. Open. Alitarajia kuanza taratibu, alisema.

Sunday, 24 January 2016

TAARIFA KWA WANAYANGA KUPITIA VYOMBO YA HABARI ILIYOTOLEWA NA MAJI LEO JUMAPILI JANUARI 24

Mwenyekiti wa Yanga Yussuf Manji akizungumzana waandishi wa habari. Kushoto ni Makamu wake, Sanga.
1. Baada ya kuupitia uamuzi wa Kamati ya Nidhamu kuamua sababu kuvunja mkataba kati ya klabu Yanga na mchezaji Haruna Niyonzima, nilihisi kulikuwa kuna kasoro hasa kwa mchezaji anayelipwa mshahara wa Sh milioni 6 anaweza vipi kupuuzia maisha yake na kuanzisha mgogoro usiokuwa na tija kwa maisha ya kipato. (angalia kiambatanisho 1)
 
Niliamua uchunguzi wa ndani ufanyike katika suala hilo zima na mwisho, Jonas Tiboroha alibainika kuwa hakuwasilisha ushahidi ya mawasiliano sahihi kwa Kamati ya Nidhamu kuhusiana na Haruna Niyonzima, hali iliyosababisha kamati kuchukua uamuzi ambao haukuwa sahihi kwa sababu;
 
Kulifanyika mambo ambayo hayakuwa sahihi, mfano barua za Niyonzima kutoka kwa Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa) ambazo zilitumwa kwa TFF na kupokelewa kama ambavyo Azam FC walipokea ya mchezaji wao kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu wao. Lakini barua ya Niyonzima kuja Yanga, ilionekana haikupokelewa kama ilivyokuwa kwa barua yake ya utetezi na ile ya kuomba radhi alizoandika, nazo zilipokelewa lakini hazikuwasilishwa kwenye kamati ya nidhanmu na hili, mhusika ni Tiboroha. Ukiachana na kamati kufanya uamuzi usio sahihi, hili pia limemjengea mchezaji chuki kubwa kwa wanachama na mashabiki. (angalia kiambatanisho 2 & kiambatanisho 3)
 
Kamati ya Utendaji (EXCOM), bada ya kupitia kwa kina iliona uamuzi ilichukua haukuwa haukuwa ya haki kutokana na kupotoshwa na Tiboroha tena aliendelea kuipotosha kamati kwa makusudi kutokana na kuficha nyaraka hizo ili Niyonzima afukuzwe. Tulifikia maamuzi Tiboroha alikuwa na ajenda yake binafsi.
Hii kama ilikuwa haijagunduliwa mapema, ilikuwa na hatari ya kusababisha upotevu kifedha za Yanga kulingana na kanuni za TFF/FIFA na ukilichimba suala hili kwa undani, kwa kufuata weledi. Kamwe hauwezi kusema yalikuwa ni makosa ya kibinadamu badala yake ni chuki ya kibinadamu ambayo haistahili kufanywa na kiongozi wa Klabu kubwa yenye heshima kama Yanga.
Zaidi, Katika hali nyingine, uamuzi wa Kamati ya Nidhamu uliandikwa na Gazeti la Uhuru na mwisho wa uchunguzi ulidhibitisha mtoa habari hizo alikuwa ni Tiboroha, akilenga kutaka kuuchafua uongozi wa Klabu, mchezaji mwenyewe dhidi ya jamii na kuusukuma uongozi kufanya uamuzi usio sahihi kwa faida zake yeye binafsi na si klabu.
2. Aidha, EXCOM ilifanya uchunguzi wa ziada na kugundua vitendo, Tiboroha hakuweza kufikia malengo aliyekuwa ameyawekewa na EXCOM kwa kuwa zaidi alionekana kutaka kujiendeleza binafsi, kusikika peke yake na kujulikana mwenyewe kama “Mungu Mtu”, jambo ambalo lilichochea kelele ndani ya klabu kama vile yeye ni malaika:

Angalia kiambatanisho (3), eti Mwenyekiti wa Matawi (nafasi ambayo haitambuliki kwenye katiba ya Yanga), amekuwa akiniagiza kubadili nafasi za  waajiriwa, mfano ile ya (Tiboroha) ni lazima abaki kwa sababu mchango wake ni mkubwa na bila yeye hatuwezi kushinda au kufanya vizuri. Ukisoma barua yake utafikiri Tiboroha alikuwa akifanya kazi zake bure wakati anajua alikuwa ni mwajiriwa wa Klabu, tena kazi zake nyingi alikuwa akizifanya kwa kufuata “maagizo”  anayopewa kama mwajiriwa. Tayari kupinga kuondolewa kwake kumeanza kuripotiwa kwenye vyombo vya habari kama shinikizo la chinichini kupitia Msumi, huenda anafikiri kufanya hivyo inanitisha ili nibadili mambo kwa matakwa ya wasioelewa mamlaka ya Katiba. Naendelea kukumbusha Tiboroha alikuwa mwajiriwa anayelipwa mshahara (angalia kiambatanisho 4) huku mimi kama Mwenyekiti au Wajumbe wa EXCOM tumekuwa tukijitolea na kutolipwa hata posho. 
Ajabu Kichekesho zaidi, kila kizuri kilichokuwa kikifanyika, vyombo vya habari viliripoti kuwa ni kazi nzuri ya Tiboroha, lakini wakasahau kila zuri, yeye alikuwa ni mtekelezaji tu baada ya kuagizwa kutoka kwangu mimi mwenyekiti au baada ya ushauri wa kamati ya utendaji na baada ya hapo, yeye alipewa kibali cha kutekeleza jambo husika. Kila zuri lilikuwa lake, mabaya yakiwemo yale ya kuisaidia TFF kuiangamiza shingo ya Yanga, aliyeficha kapuni.
Kuna taarifa kwenye vyombo vya habari ambazo zilithibitisha wazi kuwa Tiboroha alipania kujijenga binafsi kama Katibu Mkuu Bora zaidi kuwahi kutokea Yanga; hoja potofu kwa sababu wakati akiwa Katibu, hata mwalimu wa Klabu alifanikiwa kupatikana kwa ubingwa moja tu. Lakini akasahau kabla yake, Yanga ilishachukua ubingwa mara 24. Tena, propaganda ya kuwa yeye ndiye aliyeisaidia  Klabu kusajili wachezaji wa kiwango cha juu zaidi huku akijua wazi kwamba wachezaji hao walikuwa ni pendekezo la Kocha Mkuu, huu ni uputofu wa hali ya juu kabisa. 
Ndani ya miezi yake 12 ya uongozi amechangia kushuka kwa kasi kubwa kwa mapato ya klabu huku matumizi ya klabu yakipanda mara nne zaidi kutoka Sh milioni 500 kwa mwaka hadi sasa takriban Sh bilioni 2. Kabla hajaja klabuni, tulikuwa tumekaribia kujikomboa na kuanza kujitegemea. Hii pia ni kwa yeye kukubaliana na ujinga wa kuitetea TFF ambayo mikataba yake, kwa kiasi kikubwa imeporomosha mapato yetu na kutuweka katika wakati mgumu kabisa, ajabu Tiboroha alikuwa upande huo.  
3.   Masuala ya kupotosha ya Tiboroha si mapya:
a. Wakati FIFA ilipoialika Yanga kwenye semina ya mafunzo iliyofanyika nchini Ghana, Tiboroha alijichagua mwenyewe asafiri kwa niaba ya Klabu bila kuitaarifa EXCOM, halafu akachukua “Cheti cha ugonjwa” na kukiwasilisha kwa mwajiri wake Yanga ili apate nafasi ya kusafiri kwenda nchini Ghana. Kujichagua yeye mwenyewe, ilikuwa ni kutofuata weledi.
b. Daktari (jina linahifadhiwa) aliajiriwa kwa ajili ya mechi dhidi ya MGAMBO likiwa ni pendekezo la Tiboroha, lakini baadaye Kamati ya Mashindano (baada ya kuwa imesababisha tatizo ndani ya Klabu), iligundua daktari huyo alikuwa ni mwanachama tena mwenye kadi wa Simba, akaondolewa’ pia.

c. Ngoma alipewa taarifa na Tiboroha kwamba anatakiwa kwenda kufanya majaribio na klabu moja nchini Uturuki. Tiboroha alifanya hivyo akijua Ngoma alikuwa anakwenda kushiriki michuano ya MAPINDUZI Cup, mbaya zaidi hakuwa amewasiliana na EXCOM kuhusiana na hilo kabla kumfahamisha mchezaji na kumpa taarifa hiyo. Baadaye kocha Kocha Mkuu, alilalamika kwamba kufanya vile ilikuwa ni kuondoa morali ya mchezaji katika michuano hiyo ya MAPINDUZI CUP na baada ya hapo, angekuwa akiwaza kuhusiana na Uturuki tu. Mwisho, kocha alisema, Ngoma alicheza chini ya kiwango katika michuano hiyo, akiamini Yanga inamzuia kusonga mbele kimaisha.

d. BDF ya Botswana ilianzima US$ 5,000/- ambazo hadi sasa hazijarejeshwa: EXCOM iligundua taarifa kuhusiana na deni hili, imekuwa ikifichwa na hakuna maelezo mrejesho kuhusiana hilo kutoka kwa Tiboroha ambaye amekuwa na ukaribu na wahusika kutoka Botswana.

e. Kuna mtu aliajiriwa kama Katibu Muktasi (PS) pamoja na mtu mwingine pia, lakini haikuidhinisha wala mwanasheria wa Yanga, hakutaarifiwa kuhusiana na hilo lilifanyika bila ridhaa ya EXCOM, badala yake alilifanya kwa kuwa anaona yeye ni mtu maarufu sana!

f. Hakufuata ushauri aliopewa na wataalamu wa TRA, hali iliyosababisha akaunti za Yanga kufungwa, hivyo mimi kulazimika kuanza kutoa fedha zangu za mfukoni katika uendeshaji wa Klabu kwa kipindi chote na wakati huo wachezaji walikuwa wakidai mishahara na tuko katikati ya msimu. 

g. Alikuwa akitetea maslahi ya TFF na sio Yanga na kukubali kila TFF ilichokipendekeza. Mtu mwenye akili anaweza kufanya hivyo utadhani alikuwa mwajiriwa wa TFF na si Yanga? Hii inaonyesha hakuwa akifanya kazi kwa maslahi ya Yanga kama ilivyotakiwa, angalia katika masuala dhidi ya TFF, ukijumuisha.

h. Lile la kushindwa kumpigania msemaji Msemaji wa Klabu, Jerry Murro asifungiwe na TFF, huku akimchimba huku akijua alikuwa akipitia taarifa zote kabla ya Jerry kuzitoa. Alikuwa na roho mbaya kwa kuwa Jerry alipata umaarufu zaidi kwa wanachama kutokana na kuipigania klabu.

i. Ukiangalia hayo juu, ni kati ya machache ambayo nimeona ninaweza kuyaanika kwenye vyombo vya habari, lakini yako mengi ambayo ni nyeti na haitakuwa sahihi kuyaanika kwenye vyombo vya habari kwa maslahi ya klabu. Yanga ilianza kung’amua mambo yanayomhusu Tiboroha muda sasa, alipoona mengi yamegundulika. Januari 14, 2016 aliandika barua kuomba radhi kwangu, akikiri kufanya makosa na kusema alikuwa akiyajutia. (angalia kiambatanisho 6)


4. Sisi, hatukukubaliana na kutoa msamaha kutokana na hofu ya unafiki wake, na nilitoa ushauri; kwamba vizuri akachukua hatua ya kujiuzulu mara moja na huenda ingekuwa vizuri aeleze ana matatizo ya kifamilia pia kiafya, lengo lilikuwa ni kumpa nafasi ya kuachana na Yanga kwa amani pia kuilinda familia maisha yake huko mbeleni. Lakini nilimtaka ahakikishe zile fedha tunazowadai BDF kutoka Botswana, mara moja zinawasilishwa Klabuni na baada ya hapo, rasmi atakuwa amejiondoa.

5. Tiboroha alikubaliana na hilo na kuandika barua ya kujiuzulu alioiwasilisha Januari 22, 2016 (angalia kiambatanisho 7)

6. Pamoja na kumshauri ili ajiuzulu kwa heshima, lakini alionekana kuanza kutengeneza “Presha ya wanachama” kama vile mtu aliyeonewa. Kuna mkutano wa ujanjaujanja uliitishwa makao makuu ya Klabu, Tiboroha akiwa mshiriki mkuu nyuma ya pazia, hii ilikuwa ni Januari 23, 2016. Lengo ni kutengeneza hali ya hofu kwa Wanachama, jambo ambalo si sahihi. (angalia kiambatanisho 8)

7. Kwa yote hayo hapo juu:
a. Kamati ya Utendaji (EXCOM) inapenda kutoa taarifa kuwa imevunja mkataba wa Tiboroha kama Katibu Mkuu wa Yanga.
a. Klabu inatangaza, mara moja kuwa: 
i. Baraka Deudeit atashikilia nafasi hiyo ya Katibu Mkuu wa klabu.
ii. Omar Kaya atachukua majukumu yanayohusiana na wanachama wa klabu. Pia atahakikisha anasimamia mikutano yote ya matawi, kusaidia maandalizi ya uchaguzi ujao pamoja na masuala ya wanachama wapya.
iii. Jerry Muro ataendelea kubaki katika nafasi ya msemaji wa klabu,
iv. Faidhal Mike ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha cha Klabu, akisaidiwa na Justina ambaye amepandishwa cheo na kuwa mhasibu mkuu msaidizi,
 
v. Klabu ipo katika kipindi cha kuboresha kitengo cha masoko cha klabu na hivi karibuni itatangazwa lakini kabla ya hivyo, Omar atashikilia kwa muda kitengo hicho.
vi. Mwanasheria Frank Chacha kama mkuu wa kitengo cha Sheria Klabuni, yeye tunamuacha aendelee na mambo yake na masuala yote ya kisheria, klabu itayafanya kutumia wanasheria, nje ya klabu.

8. Kuhusiana na uchaguzi na maneno ya kinafiki ya nungunungu ya chinichini kuwa eti ninaogopa uchaguzi; huku wakiwa hawajui kuwa katika maisha yangu sijawahi kushindwa uchaguzi: Ukweli mimi ndiyo nimekuwa nikusukuma kuitishwa kwa uchaguzi uitishwe ili nistaafu kupitia nafasi yangu ya uenyekiti. Nilimwaandika Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, kuitisha uchaguzi mara moja, akishindwa basi itabidi niivunje Kamati ya Uchaguzi na kuunda nyingine. (angalia kiambatanisho 9)

9. Kutokana na kuuguliwa na baba yake mzazi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi alishindwa kutekeleza hilo na akaamua kujiuzulu. (angalia kiambatanisho 10)

10. Ikiwa ni sehemu ya majukumu yangu, kwa ushauri wa EXCOM niliomba kwao majina mapya ya Kamati ya Uchaguzi ili mchakato ufanyike (angalia kiambatanisho 11)
Hitimisho, nimegundua potofu ya kufikiri Tiboroha ni Katibu Mkuu wa kuchaguliwa, badala yake ni mwajiriwa wa kawaida ambaye aliingia mkataba kwa maslahi ya mapato yake. Tena kosa kumchukulia kama mtu ambaye amekuwa akitoa fedha zake za mfukoni kwa ajili ya kuendesha Klabu, mtu ambaye mimi nilipendekeza aajiriwe kama nililivyopendekeza kwa Mwalusako, Njovu, Mwesigwa, Maximo na wengine na nina mamlaka ya kuamua hatma ya mwajiriwa kulinda heshima na maslahi ya Klabu.
 
Kwa sababu mimi nimewekea dhamira ya uchaguzi ufanyike kwa haraka, huu unaweza ukawa wakati mwafaka wa wanachama kumpa Tiboroha imani ya kura zao ili awanie nafasi Mwenyekiti wa Klabu na wanipe uhuru wangu wa kuendelea na mambo yangu mengine, ambayo yapo karibu na moyo wangu kama vile kusaidi mandeleo ya Mbagala Kuu.
 
Katika maisha yangu, sijawahi kutanguliza au kupigania cheo, ndani ya Yanga maendeleo yanaonekana lakini wapo watu ndani ya Yanga wanaona mandeleo ipo kwake. Basi tuache demokrasia itawale; lakini na mimi nitatangaza kugombea tena nafasi hiyo, ingawa sidhani kama nitamaliza kipindi chote cha uongozi iwapo nitashinda kwa kuwa kutoka awali nilieleza Yanga kuwa yenye mafanikio ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika lakini hilo halitawezekana bila ya Klabu kumiliki uwanja wake binafsi pale Jangwani.
  Daima Mbele, Nyuma Mwiko _____________ YUSUF MANJI (MWENYEKITI YOUNG AFRICANS SPORTS CLUB)

Saturday, 23 January 2016

Balozi wa Kuwait azindua kisima katika shamba la Mrisho Mpoto katika kijiji cha Kibogolwa, MkurangaBalozi wa kuwait nchini Tanzania, Jasem Alnajem (wa pili kushoto), akizindua kisima walichomjengea msanii mahiri wa mashahiri, Mrisho Mpoto kushoto) katika kijiji chake huko Mkuranga leo Jumamosi

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
SERIKALI ya Kuwait imeahidi kuwasaidia wananchi wa kijiji cha Kibogolwa kitongoji cha Kibamba Mkuranga mkoani Pwani, ili kuharakisha maendeleo katika eneo hilo.

Hayo yalisemwa leo na Balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, Jasem Alnajem wakati akizindua kisima kirefu kilichojengwa
 katika shamba la msanii nguli wa mashahiri, Mrisho Mpoto ``Mjombakijijini hapo.
Mrisho Mpoto akizungumza katika kijiji cha Kibogolwa, Kibamba Mkuranga leo wakati balozi wa Kuwait akizindua kisima katika mradi wa msanii huyo wa Kutoka Shambani.
Kisima hicho ni sehemu ya mradi wa Kutoka Shambani wa Mjomba uliopo katika zaidi ya hekali 40 akiwa na lengo la kuanzisha shughuli kubwa za kilimo kwa vijana wasio na mbele wa nyuma.

Balozi Alnajem akijibu risala ya mwenyekiti wa kijiji hicho, Salima Mussa aliyesema wanakabiliwa na matatizo kibao yakiwemo ya watoto wao kusoma mbali, kutokuwa na msikiti, zahanati na barabara mbovu.
Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jasem alnajem akifungua maji na watoto wakati wa kuzindua kisima Mkuranga leo.
Alnajem alisema suala la zahati watalidajili ili kuona jinsi gabi watakavyo lishughulikia wakati lile la madrasa na msikiti alisema hilo hakina shaka watapajengewa mara moja.

Karibu kaya 150 zitanufaika na maji hayo, ambayo kisima chake kimegharimu kiasi cha zaidi y ash. Milioni 12.

Mratibu wa Mpoto Foundation, Mwalimu Steph (kushoto) akizungumza wakati wa kukabidhiwa kisima na balozi wa Kuwait, Jasem alnajem (kulia) katika kijiji cha Kibogolwa leo Jumamosi.
Naye mratibu wa mradi huo uliopo chini ya Mpoto Foundation, Mwalimu Steph aliushukuru ubalozi wa Kuwait kwa kuwachimbia kisima hicho na kukubali kutatua matatizo mbalimbali ya taasisi hiyo pamoja na yake ya wanakijiji.

Alisema kuwa mradi huo utasaidia kukomboa vijana wengi ambao hawana cha kufanya mitaani na kubaki kujiingiza katika masuala ya dawa za kulevya na ulevi mwingine.

Balozi wa Kuwait nchini Tanzania baada ya kumtwisha ndoo ya maji mwanakijiji mmoja wa kibogolwa leo Jumamosi baada ya kuzindua kisiwa kilichojengwa kwa msaada wa nchini yake.
Nao wananchi wa eneo hilo wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti waliishukuru Kuwait na kusema maji hayo yatawapunguzia sana na matatizo ya kwenda mbali kuchota majia, ambayo pia hayakuwa salama.

Mussa alisema kuwa walikuwa wakitumia muda mwingi kwenda kusaka maji na kushindwa kufanya kazi zingine za kimaendeleo.
 
Katika mradi wa Kutoka Shambani, Mpoto kwa kuanzia ataanza na vijana 50, ambapo tayari kuna maombi ya vijana 3,500 wanaotaka kuingia katika mradi huo, utakaowawezesha kujifunza kilimo na sanaa.