Sunday, 29 March 2015

Mapokezi makubwa yaisubiri timu ya nyika ya Tanzania
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa ya riadha ya Tanzania iliyoshiriki mashindano ya mbio za nyika ya dunia nchini China wanarejea Jumatatu kishujaa baada ya kushika nafasi ya sita.

Mwanariadha wa Tanzania, Ismail Juma ndiye aliyeitoa kimasomaso Tanzania baada ya kumaliza wa tisa, huku wengine wakimaliza nje ya nafasi 10 bora.

Mkimbiaji huyo ni bado chipukizi lakini alionesha uwezo mkubwa kwa ufanya vizuri katika mbio hizo.

Mwaka 2017 mbio hizo za dunia zitafanyika nchini Uganda na Tanzania imepania kuanza maandalizi mapema ili kuhakikisha inafanya vizuri zaidi.

Tutajitahidi mwaka 2017 tuiandae timu vizuri ili iweze kufanya vizuri zaidi katika mbio hizo nchini uganda, alisema Katibi Mkuu wa Riadha Tanzania Suleiman Nyambui.

Mwanariadha Fabian Nelson yeye atawasili mapema Jumatatu na ndege ya Qatal saa saba mchana wakati wengine watakuja baadae na Emirates wakiwa na kocha wao Francis John.

Mbali na hao wanariadha wengine waliomo katika timu ya Tanzania ni pamoja na Bazil John, Alphonce Felix na Panga.

Alisema kuwa vijana hao wakifanya mazoezi vizuri wanaweza kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki katika mbio za mita 5,000 na 10,000.

Michezo ya Olimpiki 2016 itafanyika Rio de Jeneiro nchini Brazil.

Nyambui alisema anatarajia wadau mbalimbali wa riadha watajitokeza kutoa mapokezi ya aina yake kwa wanariadha hao ambao wamefanya kile ambacho hakijawahi kufanywa kwa muda mrefu na wanariadha wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment