Saturday 13 April 2019

Klabu 10 Zawania Ubingwa Taifa wa Kuogelea


Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya klabu 10 zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa ya taifa ya mchezo wa kuogelea yatakayofanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Upanga jijini Dar es Salaam kuanzia leo.

Klabu ambazo zitashiriki katika mashindano hayo ni Bluefins, Champion Rise, Mis Piranhas, klabu ya kuogelea ya Mwanza (MSC), FK Blue na Wahoo ya Zanzibar.

Nyingine zitakazochuana katika mpambano hou ni pamoja na ISM-Moshi, ISM-Arusha, FK Blue Marlins, Talis-IST na mabingwa watetezi, Dar es Salaam Swim Club (DSC).
Mashindano hayo ambayo yatamalizika kesho Jumapili, yamedhaminiwa na IST, Azam, Pepsi, Asas, Samsung, DTB Bank, Kaka’s, Food Lovers na Snow Cream.

Wadhamini wengine ni Kastipharn Ltd, Ruru Logistics, Knight Support, Oppotune Travel ltd, Pyramid Consumers, Print Galore, ITV Media, Clouds FM, Subway, NMB Bank and Umoja Grand Belt na  Road Restaurant.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mashindano hayo, Hadija Shebe alisema kuwa waogeleaji wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi wamewasili tayari kwa mashindano hayo.
Waogeleaji  hao ni Sonia Tumiotto, Maia Tumiotto , Collins Saliboko, Dennis Mhini, Chichi Zengeni, Natalia Sanford, Smriti Gorkarn  na Delvin Barick ambao wote wanasoma Uingereza.

Wengine ni  Christian Shirima anayetokea nchini Ukraine,  Isam Sepetu (Afrika Kusini), Hilal Hemed Hilal na Kangeta wanaotokea klabu ya Hamilton Aquatic ya Dubai.

Alisema kuwa mashindano hayo yamepangwa kuanza saa 2.00 leo na waogeleaji watashindana katika staili tano, ambazo ni Freestyle, Breaststroke, Butterfly, Backstroke na Individual Medley.

Kwa mujibu wa Hadija, waogeleaji hao pia watashindana katika relay katika mashindano ambayo yamepitishwa na Shirikisho la Mchezo wa kuogelea Duniani (Fina) kuwa ya kutafuta alama za kufuzu mashindano ya Dunia yaliyopangwa kufanyika nchini Korea  Julai.

Kwa mujibu wa Hadija, kutakuwa na jumla ya vipengele  vya mashindano 108 na kila klabu imetakiwa kuwakilishwa na waogeleaji wawili katika kila kipengele cha mashindano ambavyo pia vimepangwa kutokana na umri.

Stars Yapangwa na Vigogo Senegal, Algeria Afcon 2019

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ikiwa mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

CAIRO, Misri
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imepangwa pamoja na majirani zao wa Kenya, Senegal pamoja na Algeria katika Kundi C la fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon 2019, zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri.

Taifa Stars ambayo kwa mara ya kwanza inashiriki hatua ya fainali hiyo baada ya miaka 39, ilijikuta katika kundi hilo baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) kupanga ratiba hiyo jana usiku.

Sasa Stars itakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha inatinga hatua ya mtoano kwa kupitia nafasi mbili za moja kwa moja,ambazo hutolewa kwa timu mbili za kwanza au kupitia `best looser’ endapo itafanya vizuri lakini itashindwa kupata nafasi mbili za kwanza.

Aidha, wenyeji Misri, Pharaohs, wamepangwa pamoja na Zimbabwe au Chui,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR) pamoja na Uganda, ambao walikuwa kundi moja na Tanzania katika hatua ya kufuzu.

Katika Kundi B, timu ya taifa ya Nigeria ya Super Eagles itakabiliana na timu mbili ambazo zimefuzu kwa mara ya kwanza katika Afcon, ambazo ni Burundi na Madagascar pamoja na Guinea.

Mmoja kati ya wachezaji wachezaji kivutio katika mashindano ya mwaka huu, Sadio Mané mwenyewe atakuwepo na timu yake ya Senegal katika Kundi C, ambalo iko Taifa Stars.

Katika Kundi D, Hervé Renard atakutana tena na Ivory Coast. Simba hao wa Milima ya Atlas itawabidi kuwa makini na Afrika Kusini pamoja na nchi ndogo ya Namibia.
Katika Kundi E, Tunisia watakabiliana na Mali pamoja na Mauritania,  ambayo inashiriki kwa bmara ya kwanza fainali hizo, pamoja na Angola.

Mabingwa watetezi Cameroon wenyewe watakabiliana na Black Stars ya Ghana, Benin na Guinea Bissau.

Kufanyika kwa mara ya kwanza kwa fainali hizo katika kipindi cha Juni kutawawezesha wachezaji wote wa Afrika wanaocheza soka Ulaya kuwemo katika timu zao za taifa, kwani wakati huo ligi zote za Ulaya zinakuwa zimemalizika.

Pia hizo zitakuwa fainali kubwa kabisa za Afcon, ambazo zitashirikisha timu 24 kwa mara ya kwanza baada ya huko nyuma kushirikisha timu 16 tu na zilikuwa zikianza Januari hadi Februari.

Kocha wa Morocco Herve Renard atakuwa akiangali kushinda mara ya tatu taji hilo la Afrika, akiwa na timu ya tatu. Simba hao wa Atlas wako katika Kundi D, pamoja na timu ya Ivory Coast aliyowahi kushindwa nayo taji hilo. Zingine ni Afrika Kusini pamoja na majirani zao Namibia.

Mchezo wa kwanza wa mashindano hayo utawakutanisha wenyeji Misri ambao watacheza na Chui wa Zimbabwe, huku Misri wakitarajia kuwa na nyota wa Liverpool Mohamed Salah katika kikosi chao katika mchezo utakaofanyika Juni 21 kwenye Uwanja wa Cairo.

Timu mbili kati ya tatu ambazo zinashiriki kwa mara ya kwanza fainali hizo, Madagascar na Burundi – ziko katika Kundi B pamoja na Nigeria na Guinea.

Ratiba kamili ya Makundi:

Kundi A: Misri, DR Congo, Uganda, Zimbabwe

Kundi B: Nigeria, Guinea, Madagascar, Burundi

Kundi C: Senegal, Algeria, Kenya, Tanzania

Kundi D: Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini, Namibia

Kundi E: Tunisia, Mali, Mauritania, Angola

Kundi F: Cameroon, Ghana, Benin, Guinea-Bissau

Friday 12 April 2019

DStv Yazindua Kampeni Kuishangilia Serengeti Boys


Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk Yussuf Singo (kulia) akimkabidhi mpira msanii, Amisa Mobeto wakati wa hafla ya kuzindua kampeni ya kuishangilia timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys, iliyoandaliwa na DStv kwenye hoteli ya Double Tree Masaki jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu ya taifa ya vijana ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 itakayoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika ya Afcon 2019 itakayoanza jijini Dar es Salaam Jumapili.

Serengeti Boys itafungua dimba kwenye Uwanja wa Taifa kwa kucheza dhidi ya mabingwa mara mbili wa Afrika na mabingwa mara tano wa dunia Nigeria.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk Singo aliyasema jijini Dar e Salaam jana wakati wa hafla ya DStv ya kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo iliyopo katika Kundi A pamoja na Nigeria, Angola na Uganda.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk Yussuf Singo (wa pili kulia), Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania, Ronald Shelukindo (watatu kulia), mchezaji wazamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Amri Kiemba (kushoto) na Salum Salum wa DStv kulia kabisa.

Hafla hiyo iliwahusisha wachezaji wazamani, wasanii na wadau wengine wa michezo kuhakikisha wanatumia nafasi au tasnia zao kuwahamasisha watu kujitokeza kwa wingi kuujaza uwanja huo wa Taifa.

Singo alisema kuwa DStv ambayo imekuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo ya michezo mbalimbali hapa nchini, imebuni kitu cha maana kuhakikisha watoto wetu hao wanaungwa mkono kwa watazamaji kuingia kwa wingi uwanjani na kuwashangilia.
Shumbana.
Naye Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania , Ronald Shelukindo alisema wakati akimkaribisha Singo kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kujitokeza kuishangilia Serengeti na wale ambao hawatakuwa na nafasi ya kwenda uwanjani, basi wataziona mechi hizo kupitia DStv.

Alisema  kuwa DStv imeanzisha kampeni hiyo ya uhamasishaji inayojulikana kama ‘DStv Inogile’ na imehakikisha kuwa michuano mbalimbali ya kimataifa inarushwa mubashara tena katika kifurushi cha chini kabisa cha DStv Bomba cha Sh. 19,000 tu.
Baadhi ya wachezaji wazamani walioudhuria hafla hiyo Double Tree Masaka, Dar es Salaam.
Kwa upande wa michuano ya Afcon ya U-17, Shelukindo alisema DStv itakuwa ikifanya kampeni kwa njia mbalimbali ikiwemo kwa njia ya mitandao na matangazo mbalimbali kuhamasisha na kuitia nguvu timu ya taifa ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Baadhi ya wachezaji wazamani waliodhuria hafla hiyo ni pamoja na Sekilojo Chambua, Edibily Lunyamila, Magoso, Kiemba, Madata Lubigisa na wengineo, wakati wasanii ni Mobeto, Nancy Sumari, John Makini na wengine.