Wednesday 30 August 2017

Waziri aridhishwa na kasi ya ujenzi Terminal 3

Mkurugenzi wa mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Wolfgang Marschick (kushoto) akiwa na  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Prof. Makame Mbarawa (wa pili kushoto) akikagua mradi wa jengo hilo. Kulia ni Meneja wa Mradi, Ray Blumrida.
 Na Mwandishi Wetu
UJENZI wa sehemu ya tatu (Terminal Three) ya Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) unatarajia kukamilika Oktoba mwakani.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof Makame Mbarawa alithibitisha hilo mara baada ya kukamilisha ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa eneo hilo  kiwanja hicho.

Alisema kuwa ujenzi wa Terminal 3 hadi sasa umekamilika kwa asilinia 64, ambapo alisema mkandarasi anaendelea vizuri na Serikali haidaiwi chochote.

Alisema Serikali imefanya malipo yote kwa wakati, ambapo aliongeza kuwa wamefanya hivyo ili kuhakikisha kila kitu kinafanyika kama kilivyopangwa ili sehemu hiyo ianze kutumika rasmi Oktoba mwakani.

Alisisitiza kuwa sehemu hiyo inatarajia kuchukua kwa wakati mmoja ndege 20 za airbus, huku kukiwa na madaraja 20 ya kupandia na kutokea katika ndege.

Alingeza kusema kuwa zaidi ya abiria milioni 8 wanatarajia kupitia sehemu hiyo kwa mwaka, ikiwa ni kama mara nne ukilinganisha na idadi inayohudumiwa sasa katika Terminal Two.

Mbali na kodi na fedha za kigeni nchini, Prof Mbarawa alisema kuwa Tanzania itafaidika kwa kuongezeka kwa ajira na mambo mengine.

Alikiri kuwa Terminal Two ambayo inatumika sasa inakabiliwa na changamoto nyingi, na ndio sababu Serikali imeamua kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi huo.

Alipoulizwa hadi sasa Serikali imetumia kiasi gani cha fedha kwa ujenzi huo, waziri alisema kwa sasa hana kiasi kamili kwa sababu fedha zimekuwa zikitolewa kwa awamu, lakini wananchi wanatakiwa kujua kuwa mradi huo utagharimu sio chini ya bil 560.
“Kufuatia maendeleo mazuri ya ujenzi wa mradi huo Serikali inaangalia uwezekano wa kutoa zabuni kwa ajili ya kampuni za mizigo.

Kwa sasa, waziri alisema kuna kampuni mbili tu za kushughulikia mizigo, ambazo ni Swiss-Port na Nas Dar Airco, ambapo kampuni zaidi zinatakiwa ili kukidhi mahitaji ya abiria.
 “Uwepo wa kampuni nyingi za kushughulikia mizigo kutasaidia kuwepo kwa huduma bora kwani kila moja itataka kushinda na mwenzake iki kupata wateja wengi, “alisema.




Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof Makame Mbarawa akiagana na Mkurugenzi wa Mradi wa Jemgo la Tatu la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), Wolfgang Marschick baada ya waziri kumaliza ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo. 

Tuesday 29 August 2017

Suarez uso kwa uso na Messi Uruguay ikiikaribisha Argentina katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018

MONTEVIDEO, Uruguay
LUIS Suarez keshokutwa Ijumaa atacheza dhidi ya mchezaji mwenzake wa Barcelona Lionel Messi wakati timu hizo za Amerika Kuisni zikisaka nafasi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018.

Uruguay ya Suarez itakuwa mwenyeji wa Argentina anayoichezea Messi katika mchezo huo utakaofanyika Ijumaa.

Huku vinara Brazil wakiwa tayari wameshafuzu kwa fainali hizo za mwakani, macho na masikio sasa yatakuwa kwa timuhizo mbili, ambazo zinasaka nafasi ya kufuzu moja kwa moja katika mbio hizo ndefu za kusaka timu 10 za kufuzu.

Colombia iko katika nafasi ya pili katika msimamo huo ikiwa na pointi 24 wakati Uruguay na Chile tayari zimetwaa nafasi mbili za moja kwa moja za kufuzu zikiwa na pointi 23.

Hiyo ina maana kuwa Argentina iliyopo katika nafasi ya tano itakuwa na kibarua kizito wakati itakaposhika kwenye Uwanja wa Centenario jijini hapa kucheza na wapinzani wake hao wa jadi katika historia ya soka.

Argentina bado inachechemea katika mbio zake hizo za kufuzu, imeshinda mechi sita tu kati ya 14, imeonesha uhai chini ya kocha wake mpya Jorge Sampaoli.

Sampaoli, aliyeongoza ushindi wa Chile katika mashindano ya Copa America 2015, itakuwa imepata nguvu baada ya kuifunga Brazil 1-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Juni.


Ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya timu dhaifu ya Singapore kumemuongezea nguvu Sampaoli.

Chipukizi amtupa nje bingwa US Open

NEW YORK,Marekani
BINGWA mtetezi wa mashindano ya US Open kwa upande wa wanawake, Angelique Kerber (pichani) ametupwa nje ya mashindano hayo baada ya kuchemcha katika mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Mjapan Naomi Osaka.

Mjerumani huyo anayeshikilia nafasi ya sita kwa ubora, alijikuta akigalagazwa na chipukizi mwenye umri wa miaka 19 ambaye anashiklilia namba 45 kwa ubora duniani, ambaye alishinda kwa seti 6-3 6-1 kwenye Uwanja wa Arthur Ashe huko Flushing Meadows.

Ni mwendelezo wa mwaka wa shetani kwa Kerber mwenye umri wa miaka 29, ambaye hajashinda taji lolote tangu alipotwaa ushindi jijini New York miezi 12 iliyopita.

"Bado ni mchezaji yule yule na mtu yule yule, “alisema.

"Najua kuwa nina nguvu na najua nitarejea nikiwa na nguvu zaidi, hilo nina uhakika nalo.

"Najua kuwa sitajisalimisha kama hivi. Kwangu, nitajaribu kusahau mechi hii haraka iwezekanavyo na kuangalia mbele tena
ili kupatya mafanikio.”

Samatta atua kuiongezea nguvu Taifa Stars

Na Mwandishi Wetu
MCHEZAJI wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka nchini Ubelgiji, Mbwana Samatta amewasili katika kokosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana.

Timu hiyo imeanza mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru au Shamba la Bibi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kipute hicho, ambacho kipo katika ratiba ya mechi za kirafiki za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

 Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji pia ndiye nahodha wa Taifa Stars.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema kuwa, wachezaji wote wanaocheza hapa nchini waliingia kambini jana, huku wanaocheza nje wakitarajiwa kuwasili kuanzia leo.

“Jana jioni wachezaji wa timu za Azam FC, Yanga pamoja na Simba SC waliingia kambini na kikubwa cha kwanza Daktari wa timu aliwapima afya zao leo asubuhi na jioni timu ikaanza mazoezi Uwanja wa Uhuru, “amesema.

Lucas amesema kwamba msafara wa wachezaji 18 na viongozi tisa kutoka Botswana unatarajiwa kuwasili Alhamisi kabla ya kufanya mazoezi katika Uwanja utakaotumika kwa mechi Ijumaa.
“Wenzetu tumewasiliana nao na wamesema watakuja na wachezaji 18 na viongozi tisa, 

tunazungumzia msafara wa watu 27 na timu itafika Agosti 31, lakini hatujajua ni muda gani watawasili,”amesema.

Lucas amesema wamekwishafanya mawasiliano na wachezaji wanaocheza nje walioitwa kujiunga na kikosi cha Stars akiwemo Nahodha,  Farid Mussa wa CD Tenerife  ya Hispania, Simon Msuva wa Difaa Hassan El –Jadida ya Morocco na Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini na wote wanatarajiwa kuanza kuwasili kesho.

Kuhusu suala la Uwanja utakaotumika katika mechi hiyo Alfredy amesema, wamethibitisha Uwanja wa Taifa upo katika ukarabati ulioanza siku tano zilizopita na mchezo dhidi ya Botswana sasa ni rasmi utapingwa Uwanja wa Uhuru.

Arsena yatupa ofa ya Man City kumsajili Sanchez

LONDON, England
KLABU ya Arsenal imetupilia mbali ofa ya pauni milioni 50 kutoka kwa wapinzani wao wa Ligi Kuu Manchester City kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji Alexis Sanchez (pichani).

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye alipachika mabao 24 katika Ligi Kuu ya England msimu uliopita, mkataba wake utamalizika katika kipindi kijacho cha majira ya joto na anataka kujiunga na kocha wa City Pep Guardiola.

Arsenal imekuwa ikigoma kumuuza Sanchez, na inataka kumchukua mchezaji wa Man City Raheem Sterling kama sehemu ya mpango huo kabla ya kesho, ambao ni mwisho wa dirisha la usajili.

Lakini Guardiola anajua kuwa anamtaka mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile ili kukiimarisha zaidi kikosi chake kwa upande wa ushambuliaji.

Sterling ambaye mwenye umri wa miaka 22, ambaye ni mshambuliaji wa England alipangwa katika mechi zote tatu za Man City za ufunguzi wa Ligi Kuu ya England msimu huu.

Hatahivyo hajahakikishiwa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza katika timu hiyi yenye maskani yake kwenye Uwanja wa Etihad baada ya kuwasili kwa Bernardo Silva kutoka Monaco.

Sharapova aanza kuonesha makali US Open 2017

NEW YORK, Marekani
MARIA Sharapova (pichani) amerejea kwa kishindo katika mashindano makubwa ya tenisi kwa kumtupa nje bingwa namba mbili kwa ubora duniani, Simona Halep katika mashindano ya US Open.

Mrusi huyo alishinda kwa seti 6-4 4-6 6-3 mbele ya mashabiki karibu 24,000 katika mchezo uliofanyika hapa.

Sharapova, 30, alikuwa akicheza mchezo wake wa kwanza wa mashindano makubwa tangu alipokuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka 15 ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu.

Bingwa huyo wa mwaka 2006 alihitaji kufuzu ili kupangwa katika ratiba kubwa ya mashindano hayo, ambapo sasa anashikilia nafasi ya 146 kwa ubora.

Sharapova alirejea katika mchezo huo Aprili lakini alikuwa akipambana na maumivu ya nyama za paja, akicheza mara moja tu mwezi Mei, na pia alikataliwa kucheza mashindano ya French Open.
Chama cha Tenisi cha Marekani kimechukua hatua tofauti, baada ya kumpatia Mrusi huyo nafasi katika ratiba kubwa mjini New York, na alitumia nafasi hiyo vizuri.

Hii ni mara ya kwanza kwa Sharapova kucheza mashindano makubwa tangu aliposhindwa na Serena Williams mwaka 2016 katika robo fainali ya mashindano ya Australian Open.

MultiChoice Yatangaza Neema kwa wateja wa DStv!

Yafyeka Bei za Vifurushi Vyote! Wapenzi wa Kandanda ‘Meno Nje’ 

Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande akizungumza jijini Dar es Salaam leo kuhusu bei mpya za vifurushi.
Na Mwandishi Wetu
PANGA LA BEI LAFYEKA;  DStv Premium kwa 8.15%, DStv Compact Plus kwa 11.02%, DStv Compact kwa 16.11%, DStv Family kwa 9.09% and DStv Access (Bomba) kwa 4.88%

 Katika kuhakikisha kuwa wateja wake wote na watanzania kwa ujumla wanaendelea kufurahia huduma za DStv, Kampuni ya Multichoice Tanzania imetangaza neema kubwa kwa wateja wake kwa kufyeka bei za vifurushi vyake vyote, huku pia ikiboresha maudhui na vipindi katika vifurushi vyake hususan vile vya bei ya chini!
  
Habari hiyo njema imetangazwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam ambapo amesema bei hizo mpya zitaanza kutumika rasmi Septemba mosi 2017.

“Kumjali na kumsikiliza mteja ni nguzo ya uendeshaji wa biashara yetu. Tumesikia maoni ya wateja wetu na wananchi kwa ujumla kutusihi tuangalie uwezekano wa kupunguza bei, tumechanganua kwa kina na tumeamua kutekeleza matakwa yao, leo hii tumepitisha panga kwenye bei za vifurushi vyetu vyote!” alisema Maharage.
 
Akifafanua kuhusu punguzo hilo, Maharage amesema  kumekuwa na punguzo la hadi asilimia 16, ambalo ni punguzo kubwa sana na litakalowapa ahueni kubwa watumiaji wa DStv. Amezitaja bei mpya kuwa ni;

Bei Mpya za vifurushi vya DStv:

Kifurushi                    Bei ya sasa                     Bei Mpya                % Ya Punguzo
Premium                   TZS 184 000.00            TZS 169 000.00             8.15%
Compact Plus         TZS 122 500.00            TZS 109 000.00                11.02%
Compact                   TZS 82 250.00              TZS 69 000.00               16.11%
Family                        TZS 42 900.00              TZS 39 000.00                9.09%
Access (Bomba)    TZS 19.975.00               TZS 19 000.00                 4.88%

Mara baada ya kutaja bei hizo Maharage aliwaambia waandishi wa habari; “Kwa lugha ya mtaani wanasema ‘Vuma Vimekaza’ – ikimaanisha hali ya kifedha imebana… Multichoice imelisikia hilo na kuamua kuwapa wateja wote wa DSrv ahueni kubwa! Sasa kwa wateja wetu wa DStv, ‘Vyuma vimeachia’”


Maharage amesisitiza kuwa Multichoice itaendelea kuwasikiliza wateja wake na kuhakikisha kuwa inatekeleza kile wanachohitaji wateja wake pale inapowezekana.

“Wateja wetu walituomba tuongeze maudhui ya kitanzania kwenye king’amuzi chetu, tukawasikia, tukaweka chanel maalum kabisa ya Maisha Magic Bongo ambayo ina asilimia 100 ya maudhui ya Kitanzania; wakatuomba tupunguze bei ya vifurushi, tukafanya hivyo mwishoni mwa mwaka jana, na leo tena kwa mara ya pili tumepunguza bei, wakatuomba tuongeze chanel kwenye vifurushi vya bei ndogo, tukafanya hivyo, tukaleta Laliga na Ligi kuu ya uingereza hadi kwenye kifurushi cha chini kabisa cha Bomba”.
 
“Kipekee kabisa Wananchi kupitia serikali wakatuomba tuongeze nguvu kwenye kuinua vipaji vya vijana wetu wa kitanzania, tukasikia, tukaitikia, tukaanza katika riadha ambapo tumemdhamini mwanariadha wetu Alphonce Simbu. Sote tunajua matokeo yake, sasa Tanzania inahofiwa kwenye ulingo wa riadha kimataifa! Haya yote tumefanya kwa sababu tunawasikiliza wateja wetu, tunawasikiliza wadau wetu, tunawasikiliza Watanzania” alisema Maharage.

Wakati habari hii ikiwa ni njema kwa watanzania wote, washabiki na wanazi wa kandanda wameonekana kufurahia Zaidi kwani kwa punguzo hilo kuwa wataweza kushuhudia ligi kuu ya uingereza PL pamaja na ligi nyingine kubwa ulimwenguni na makombe maarufu kama UEFA kwa bei nafuu zaidi.


Kwa maelezo Zaidi kuhusu bei mpya na vipindi mbalimbali katika vifurushi vya DStv tembelea; www.dstv.com.

Sunday 27 August 2017

Mayweather amsimamisha McGregory raundi ya 10

LAS VEGAS, Marekani 
Floyd Mayweather ametimiza pambano la 50 katika ngumi za kulipwa akicheza bila ya kupoteza baada ya kumchapa kwa TKO Conor McGregor katika raundi ya 10 ya pambano hilo.

Mayweather amepata ushindi huo dhidi ya bingwa wa michezo ya UFC (ngumi na mateke).

Mwamuzi alilazimika kuingilia na kusimamisha pambano katika raundi ya 10 baada yya kuona Mayweather anamuangushia kipigo kikali McGregor raia wa Ireland ambaye hakuwa akijibu kitu tena.

Hatahivyo, McGregor amewashangaza wapenda ngumi duniani baada ya kuongoza kuanzia raundi ya kwanza hadi ya tatu.

Kuanzia raundi ya nne, Mayweather alianza kucharuka na taratibu ilipofika raundi ya saba, ilionekana McGregor amepoteza mwelekeo.

Katika raundi ya 8, McGregor alionekana kuchoka hasa miguu, hivyo kutoa nafasi kwa Mayweather kumpiga ngumi nyingi zaidi zilizomfanya achoke zaidi. Huenda angeweza kujitoa katika raundi ya 9 lakini akaamua kuendelea raundi ya 10 ambayo ilimshinda kabisa.

Simba yaanza kwa kishindo Ligi Kuu Bara

Na Mwandishi Wetu
SIMBA ya Jijini Dar es Salaam imeanza kwa nguvu Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga Ruvu Shooting ya Pwani kwa mabao 7-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi (pichani) ameonesha uwezo mkubwa baada ya kufunga mabao manne peke yake katika moja ya mechi saba za ufunguzi wa ligi hiyo.

Mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi, walio chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog anayesaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja yamefungwa na Shiza Kichuya, JumaNdanda na Erasto Nyoni.

Okwi alianza kuandika kalamu ya mabao katika dakika ya 18 akimchambua kipa Bidii Hussein baada ya pasi ya Muzamil Yassin na bao la pili akafunga dakika ya 22 baada ya kuwachambua mabeki ndani ya 18 baada ya pasi ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima.

Okwi akakamilisha mabao matatu au `hat-trick’ ambayo ilimuwezesha kupata mpira wake, alilifunga katika dakika ya 35 baada ya pasi nzuri ya Muzamil tena kabla ya kusaidia kupatikana kwa bao la nne.

Okwi aliwatoka wachezaji wa Ruvu Shoting hadi karibu na boksi na kumpasia beki Erasto Nyoni pembeni kushoto, aliyetia krosi iliyosindikizwa nyavuni na winga machachari, Shiza Kichuya kuipatia Simba bao la nne dakika ya 42.

Mshambuliaji wa zamani wa Zesco United ya Zambia, Ndanda akaifungia Simba bao la tano dakika ya 44 akimalizia krosi ya Nyoni, kabla ya Okwi kufunga bao lake la nne na la sita katika dakika ya 52 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Saidi Ndemla.

Beki Erasto Nyoni aliyesajiliwa na Simba akitokea Azam FC alifunga bao la saba katika dakika ya 81 na kuihakikishia timu hiyo ushindi wa mabao 7-0 na kuongoza ligi hiyo.

Katika mechi nyingine za Ligi Kuu siku hiyo ya ufunguzi; Bao pekee la mshambuliaji Mghana, Yahya Mohammed limeipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Mwadui imeshinda 2-1 dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mtibwa Sugar wameilaza 1-0 Stand United Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Mbao FC wameshinda ugenini 1-0 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Tanzania Prisons nayo imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mji Njombe na Mbeya City imeilaza Maji Maji ya Songea 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.


Ligi hiyo inaendelea tena leo kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watakaposhuka kwenye Uwanja wa Uhuru kucheza dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Lipuli ya Iringa.

Friday 25 August 2017

Pazia Ligi Kuu msimu wa 2017/18 kufunguliwa kesho

Kikosi cha Simba
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au Kombe la FA Simba ya Dar es Salaam ni miongoni mwa timu 14 zitakazoshuka dimbani kesho kuanza mchakamcahaka wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba leo itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting ya mkoani Pwani katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Wekundu hao wa Msimbazi wameanza msimu huu vizuri kwa kutwaa Ngao ya Jamii Jumatano kwa kuwafunga watani zao wa jadi Yanga kwa penalti 5-4.

Timu hiyo ina usongo wa kufanya vizuri msimu huu baada ya kushindwa kutamba kwa karibu misiimu minne na hivyo kushindwa kushiriki michuano ya kimataifa.

Mbali na mchezo huo, pia kutakuwepo mechi zingine za Ndanda FC kukutana na Azam FC katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona huku Mwadui ikiwa mwenyeji wa Singida United.

Singida imepanda daraja na imefanya usajili wa nguvu na hivyo kuwa moja ya timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu.

Kagera Sugar ya Bukoba itawakaribisha wagumu Mbao FC katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba huku Mtibwa Sugar ikiikaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Manungu Turiani, timu iliyopanda daraja ya Njombe Mji itacheza na Tanzania Prisons na Mbeya City itakwaana na Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa kwa mchezo mmoja wakati mabingwa watetezi Yanga watakaikaribisha timu iliyopanda daraja ya Lipuli ya Iringa katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.

Timu za Njombe Mji, Lipuli na Sigida United zinashiriki ligi baada ya kupanda daraja kuchukua nafasi ya zile zilizoshushwa daraja za African Lyon, JKT Ruvu na Toto Africans, ambazo zitashiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Makocha mbali mbali wa klabu ya Ligi Kuu wametambiana, ambapo kocha mkuu wa Mwadui FC Jumanne Ntambi amesema timu yake ipo tayari kwaajili ya mchezo dhidi ya Singida united wikiendi hii katika Uwanja wa Mwadui Complex.


Akielezea kuhusu maandalizi ya mchezo huo,Kocha huyo wa zamani wa timu za Panone,JKT Mlale na Kahama United alisema katika michezo michezo yao ya kirafiki waliocheza mpaka sasa wameweza kugundua makosa yao.

Zanzibar yapongeza TAA kushirikishwa TB III

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Salim Msangi akitoa maelezo kwa wajumbe wa  Kamati ya Ardhi, Mawasiliano na Mazingira wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar walipotembea jengo la Terminal 3 la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) leo. Kushoto ni mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamza Hassan Juma, Naibu Waziri wa Maliasili Mohamed Ahmad Salum na kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Juma Makungu Juma.
Na Neema Harrison, TUDARCO
KAMATI ya Ardhi, Mawasiliano na Mazingira ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, imepongeza kushirikishwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), katika mradi wa ujenzi wa Jengo la Tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Hamza Hassan Juma alitoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea jengo hilo, na kupata maelezo na ufafanuzi mzuri kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw.. Salim Msangi, ambayo yanaonesha kwa kiasi kikubwa wameshirikishwa.

“Hongereni sana kwani huu mradi ni tofauti kabisa tumeona maelezo yako yanaonesha ni kwa kiasi gani mmeshiriki kuanzia mwanzo wa ujenzi hadi sasa unakaribia kumalizika, ni tofauti nakwetu siku ya mwisho ndio tunakabidhiwa mradi na tunakuwa hatujui chochote zaidi ya kukabidhiwa tu,” amesema Bw. Juma.

Naye Bw. Msangi amesema ndani ya mradi huo kumekuwa na wahandisi wa idara mbalimbali ikiwemo ya umeme walioanza tangu mradi unaanza ili baada ya mradi kukamilika inakuwa rahisi na kutambua eneo litakalokuwa na tatizo kwa ajili ya marekebisho.

Amesema katika ziara hiyo wameweza kujifunza kutoka kwa Wawakilishi hao ikiwa ni njia ya kupeana uzoefu na chachu ya maendeleo katika Viwanja Vya Ndege, ambapo katika jengo hilo kuna mifumo ya ukaguzi wa mizigo hatua tano, na endapo mzigo utakuwa na tatizo unazuiwa kwa ukaguzi zaidi katika hatua ya mwisho.

“Hii mifumo ni ya kisasa zaidi kwani hata kama abiria akiona mzigo alioweka na hauruhusiwi kupita kwenye kiwanja chetu, asidhani atakuwa amesalimika katika hatua ya tano atazuiwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema Bw. Msangi.

Pia amesema jengo hilo litakuwa mitambo maalum utakayowatambua kirahisi abiria watakaokuwa wakisafirisha madawa ya kulevyia wakiwa wameyameza, ambapo awali ilikuwa rahisi kuwatambua kutokana na utaalam walionao maafisa usalama.

Naibu Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Bw. Mohamed Ahmada Salum amezungumzia kuwa TBIII itatoa ajira kwa wwatanzania wengi .


Bw. Salum amesema JNIA itarajie mashirika mengi ya ndege kujitokeza kwa wingi kufanya safari zake, na zitaongeza pato la taifa.

Kiwanja cha JNIA Terminal 3 kufungwa mitambo ya kisasa kubaini waliomeza dawa za kulevya

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Salim Msangi akizungumza na Kamati ya  Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliotembekea mradi wa ujenzi wa Terminal 3 jijini Dar es Salaam leo.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege (TAA) imesema itafunga mitambo ya kubaini watu waliomeza dawa za kulevya katika jengo la abiria namba tatu (Terminal III) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Hatua hiyo ni katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya na kuhakikisha hakuna dawa zinazopitishwa kupitia uwanja huo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Salim Msangi (kushoto) akielezea jambo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar 
 Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Salim Msangi wakati akijibu maswali mbalimbali ya wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliotembekea mradi wa ujenzi wa jengo hilo leo.

Msangi alisema, mbali na mtambo huo kufungwa katika kiwanja huo ili kuhakikisha hakuna dawa zinazopitishwa lakini pia taasisi nyingine mbalimbali ikiwemo za madini zitakuwa na nafasi katika uwanja huo ili kuhakikisha hakuna madini yanayotoroshwa kwenda nje ya nchi.

"Ni jengo la aina yake kwa kweli, kwa sababu tunataka Airport ya Dar es Salaam iwe ni kiunganishi cha kwenda sehemu nyingine lakini pia kwa kuwa tunafufua shirika letu la ndege iwe ni sehemu ambapo safari zinaanzia hapa na kwenda kuchukua watu katika nchi mbalimbali na kuwaleta hapa," alisema.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wakitembelea Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 3 leo jijini Dar es Salaam

Msangi alisema, hatua hiyo itasaidia kuongeza fedha za kigeni na mapato kwani ndege zilizonunuliwa na serikali zitaweza kwenda katika nchi mbalimbali na hivyo kuleta watalii nchini.
Aidha, alisema sambamba na mradi huo pia wana mpango wa kujenga hoteli ya kisasa karibu na uwanja huo ili kuwarahisishia abiria na wageni ambao wanapenda kukaa karibu na uwanja wa ndege.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Mohamed Ahmed Salim alisema, kupitia ziara hiyo wamejifunza mambo mengi ambayo wataenda kuangalia namna ya kuyaweka katika mradi wa ujenzi wa jengo la abiria namba mbili (Terminal II) katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
Alisema mradi huo awali ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali lakini kwa sasa wameshafikia muafaka na kwamba ujenzi utaanza muda wowote kuanzia sasa na utachukua miezi 18.

"Kwa mwaka jana uwanja ule umehudumia wageni miliomni moja, tulikuwa tunalenga kujenga jengo litakalohudumia abiria milioni moja nukta mbili lakini kwa kuangalia idadi ya watalii inavyoongeza na dira ya maendeleo tukasema ni bora jengo la kuhudumia abiria milioni moja nukta sita," alisema Salum.
Alisema hatua hiyo ilisababisha kuchelewa kuanza kwa ujenzi kwa kuwa walikuwa kwenye majadiliano ya wafadhili wa mradi huo ambao ni China kupitia Benki ya Exim China.

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamza Hassan Juma alipongeza maendeleo ya ujenzi huo pia kupongeza hatua ya serikali kujenga awamu ya pili kwa kutumia fedha za ndani.


"Hii ni nzuri sana, kwasababu inaonesha kuna mambo tunaweza sisi wenyewe, bila kutegemea misaada. Pia tumejifunza mengi tukirudi Zanzibar tutaishauri serikali," alisema Juma.