Tuesday 25 April 2017

Benitez kupewa fungu zaidi la usajili baada ya kuipandisha Newcastle United hadi Ligi Kuu

LONDON, England
KOCHA wa Newcastle Rafael Benitez (Pichani),  anatakiwa kupewa fedha ili kuimarisha kikosi chake kabla ya timu hiyo haijaanza msimu mpya katika Ligi Kuu, anasema gwiji wa klabu hiyo, Alan Shearer.

Benitez alitumia zaidi ya kiasi cha pauni Milioni 50 katika kipindi kilichopita cha majira ya joto baada ya timu hiyo kushushwa daraja, lakini Shearer anasema kuwa kuna hatari ya kumkosa kocha huyo Mhispania, endapo hatapewa fedha zaidi.

"Nafikiri kama atapewa fungu zaidi la usajili bila shaka kitakuwa kishawishi kikubwa kwake kubaki katika timu hiyo, “alisema mchezaji huyo mwenye rekodi ya kufunga mabao mengi katika timu hiyo.

Newcastle ilipanda daraja baada ya kushinda mabao 4-1 katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Preston uliofanyika Jumatatu.

Nahodha huyo wazamani wa England aliongeza: "Ni mtu mkubwa katika klabu. Anapapenda mahali hapa na ni mvumilivu na muhimu zaidi ni kwa Newcastle kuendelea kumbakisha.
"Nina uhakika atataka timu iimarishwe na atataka hilo lifanyike.”

"Watu wamebaini kuwa timu inahitaji kuimarishwa zaidi ili kufikia pale wanapotaka kuwa, katika nusu ya juu ya Ligi Kuu.

"Sasa ni mahali ambako Newcastle inataka kuwa, kuwa katika Ligi Kuu na hawataki kuwa katika nafasi tatu za chini, ambazo ni za kupambana dhidi ya kushuka daraja.”

Winga wazamani wa Newcastle, Chris Waddle naye aliunga mkono maneno ya Shearer, ambapo anaamini kuwa, Benitez atataka kuimarisha kikosi chake ili kifanye vizuri.


Benitez aliteuliwa kuifundisha Newcastle Machi 2016 lakini alishindwa kuiokoa timu hiyo kuteremka daraja hadi daraja la kwanza.

Prisons yaitoa jasho Makongo wavu wa Muungano

Wachezaji wa Tanzania Prisons (kushoto) wakichuana na wale wa Makocha Sekondari wakati wa mchezo wa mpira wa wavu wa Muungano leo kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam. Magereza ilishinda kwa seti 3-0.
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Tanzania Prisons leo  ilimeichapa Shule ya Sekondari ya Makongo wanawake kwa seti 3-0 katika mchezo wa mashindano ya Muungano ya mpira wa wavu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wachezaji wa Tanzania Prisons (kulia) wakichuana na wale wa Makocha Sekondari wakati wa mchezo wa mpira wa wavu wa Muungano leo kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Makongo imekutana na kipigo hicho ikiwa ni siku moja tu baada ya kuifunga Jeshi Stars ambaye ni bingwa mtetezi kwa seti 3-1.
Katika mchezo huo, Tanzania Prisons ilishinda 25-20 katika seti ya kwanza,kabla ya kuibuka na 25-23 katika seti ya pili huku katika seti ya mwisho ikitamba kwa pointi 25-17.

Kwa upande wa wanaume, Kinyerezi iliifunga Mjimwema kwa seti 3-0, ambapo washindi walifanya kweli kwa ushindi wa 28-26, 25-22 na 25-20.
Akizungumza kando ya mashindano hayo, Katibu Msaidizi wa Chama cha mchezo wa Wavu Tanzania, (TAVA) Alfred Selengia alisema mashindano hayo yana ushindani tofauti na mwaka jana.

“Mashindano yanaendelea vizuri na ushindani ni mkubwa tofauti na mwaka jana. Bingwa atapata kombe na medali pamoja na mshindi wa pili,” alisema Selengia.

Pia Selengia alisema bingwa ndiye atawakilisha nchi kwenye mashindano ya Afrika yatakayofanyika mwakani kwa timu za wanawake na wanaume.
Timu zinazoshiriki ni bingwa mtetezi Jeshi Stars, Chui, Polisi Zanzibar, Moro Stars, Makongo Sekondari, Tanzania Prisons, Saut Mwanza, Mafunzo ya Zanzibar, Dodoma, Mjimwema, Victory Sports na Kinyerezi.

Timu za wanawake ni pamoja na Tanzania Prisons, Jeshi Stars, Shule ya Sekondari ya Makongo, Saut ya Mwanza, Mjimwema na Dodoma.

Monday 24 April 2017

Wavu wa Muungano waanza kwa kasi Dar

Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya Klabu Bingwa ya mpira wa wavu ya Muungano yalianza juzi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hizo za ufungunguzi, Mafunzo ya Zanzibar iliifunga Kinyerezi kwa seti 3-0 huku Chuo wakiitambia Kigamboni kwa seti 3-2.
Makongo waliipeleka puta Polisi Zanzibar kwa seti 3-1 huku Kinyerezi wakipoteza tena dhidi ya Chui pale walipofungwa 3-1.


Katika mchezo mwingine, Mafunzo waliifunga Victory kwa seti 3-0 na Jeshi Stars waliwafunga Polisi Zanzibar kwa seti 3-0.

Simbu apongezwa kung'ara London Marathon

Balozi wa DStv na Mshiriki pekee kutoka Tanzania aliyeshiriki mashindano ya London Marathon yaliyofanyika jana jijini London Alphonce Simbu  ameibuka mshindi wa tano huku akivunja rikodi yake kwa kutumia muda wa 2:09.10 ambao ndio muda wake bora zaidi tangu aanze kushiriki mashindano ya kimataifa.

 Kabla ya hapo rekodi yake ilikuwa muda wa 2:09.21 aliyoiweka mwaka jana kwenye mashindano ya Lake Biwa Marathon nchini Japan.

Simbu ambaye ni mshindi wa medali ya dhahabu wa Mumbai Marathon ameonesha umahiri mkubwa katika mashindano hayo hasa ikizingatiwa kuwa mashindano hayo yalikuwa yanashirikisha vinara wengi wa riadha ulimwenguni wakiwemo Muethiopia Kenenisa Bekele  Wakenya Daniel Wanjiru, Bedan Karoki na Abel Kirui.

Mara baada ya ushindi huo salamu za pongezi zimekuwa zikimiminika huku Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande akisema kuwa kampuni yake imeridhishwa sana na ufanisi aliouonesha katika mashindano hayo. 

Alisema uwekezaji uliofanywa na kampuni hiyo katika kumdhamini Simbu umezaa matunda kwani kiwango cha mwanariadha huyo kimekuwa kikiimarika siku hadi siku.

 “Tumefurahishwa sana na kiwango alichoonyesha Simbu kwenye London Marathon. Hii ni ishara nzuri sana na tunaamini atafanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya riadha ya Dunia yatakayofanyika jijini London Agosti  mwaka huu.”

Kwa upande wake, meneja wa mwanariadha huyo Francis John alisema kuwa ameridhishwa na kiwango alichoonesha Simbu na kwamba punde tu atakaporejea wataanza maandalizi kwa ajili ya ushiriki wake katika mashindano ya Dunia yatakayofanyika Agosti mwaka huu.

Katika mashindano hayo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mkenya, Danie Wanjiru (2:05:48) akifuatiwa kwa karibu na Kenenisa Bekele (2:05:57) na Bedan Karoki.

Regards,

Shumbana.

Sunday 23 April 2017

Simba yaporwa pointi za mezani za Kagera Sugar

Na Mwandishi Wetu
Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limetangaza kuipoka Simba pointi tatu na mabao matatu ambazo ilipewa mezani kutokana na mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar.

Simba ilipoteza mchezo dhidi ya Kagera kwa kufungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba katika Ligi Kuu ya Bara, lakini baadaye ilikata rufaa ikipinga Kagera kumtumia mchezaji Mohamed Fakhi ikidai alikuwa na kadi tatu za njano, na ikapewa ushindi huo kupitia Kamati ya Saa 72.

Mara baada ya kamati hiyo kuipa Simba pointi Kagera ikaomba kupitiwa upya kwa suala hilo na ndipo TFF ikatangaza kuwa suala hilo sasa litakuwa chini ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ambayo ndiyo imetoa maamuzi hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya uamuzi huo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema leo kuwa, kuna sababu kadhaa zimechangia kuchukuliwa kwa maamuzi hayo ambapo alizitaja kuwa ni pamoja na :

“Malalamiko ya Simba hayakuwasilishwa kwa wakati muafaka tangu mchezo ulipochezwa, malalamiko yao hayakuwa katika njia ya maandishi, rufaa ya Simba haikulipiwa ada, kikao cha Kamati ya Saa 72 kilikosa uhalali kutokana na kuwashirikisha watu ambao hawana uhalali wa kuwa kwenye kikao.


“Kutokana na sababu hizo kamati imeamua kutengua maamuzi yaliyochukuliwa na Kamati ya Saa 72 na kurejesha matokeo kama yalivyokuwa, pia kamati imemuagiza katibu mkuu wa TFF kuwapeleka baadhi ya wajumbe wa bodi ya ligi katika Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kwenda kinyume na kazi zao,” alisema Mwesigwa.

TFF yamfungia Haji Manara mwaka mmoja

Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungia Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Simba, Haji Manara (Pichani),  kujihusisha na masuala ya soka kwa mwaka mmoja na kupigwa faini ya Sh. Milioni 9.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu,  Jerome Msemwa amesema jijini Dar es Salaam leo kuwa, hatua hiyo imefikiwa baada ya Manara kukutwa na makosa matatu dhidi ya TFF waliomlalamikia.

Msemwa ameyataja makosa hayo kuwa ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila na la tatu kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.

Kwa makosa hayo yote, anakumbana na adhabu ya kuwa nje ya masuala ya soka kwa mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. Milioni 9 kabla ya kumaliza adhabu yake.

Kosa la kwanza amehukumiwa kwa mujibu wa kanuni ya 41 kifungu cha tisa, ambalo alitakiwa alipe faini ya Sh. Milioni 1, la pili amehukumiwa kwa kanuni ya 53 kifungu cha kwanza na cha pili na anafungiwa miezi mitatu na faini ya Sh. Milioni 3 na kosa la tatu amehukumiwa kwa kanuni ya kwanza na ya pili inayohusu maadili, ambayo alitakiwa afungiwe miaka saba na faini ya Sh. Milioni 5.

Lakini kutokana na kuwa hilo ni kosa lake la kwanza Kamati imetumia mamlaka yake kwa kumpunguzia adhabu hadi miezi 12 na faini ya Sh. Milioni 5 – na adhabu hizo zimeunganishwa, hivyo atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. Milioni 9.

Hata hivyo, Msemwa alisema Manara hakutokea kwenye kikao cha kutoa utetezi wake dhidi ya tuhuma hizo, ingawa taarifa ya kuitwa alifikishiwa yeye na klabu yake pia.

Katikati ya wiki, Manara aliituhumu TFF kufanya njama za waziwazi ili kuwabeba wapinzani wao, Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Manara pia aliwatuhumu viongozi wakuu wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa ni wahaya na viongozi wa zamani wa Yanga, ambao wanataka kuipendelea Kagera Sugar na timu hiyo yao hiyo ya zamani.

Hasira za Manara zilikuja baada ya TFF kulipeleka Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji suala la Simba kupewa ushindi wa zamani na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72.

Kamati ya Saa 72 iliipa Simba pointi tatu na mabao matatu baada ya kujiridhisha beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi aliichezea timu hiyo dhidi ya Simba Aprili 2 akiwa na kadi tatu za njano, ikiwa ni kinyume cha kanuni.


Lakini siku mbili baadaye, Kagera Sugar wakapinga maamuzi hayo na kuomba suala hilo lisikilizwe upya kwa kuwa mchezaji wao hakuwa na kadi tatu za njano siku wanaifunga Simba 2-0 mjini Bukoba.

Friday 21 April 2017

Ukata waitoa Polisi Moro netiboli Afrika Mashariki

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Polisi Morogoro nayo imetangaza kutoshiriki katika mashindano ya netiboli ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Nairobi, Kenya kuanzia keshokutwa Jumapili hadi Aprili 30.

Polisi ni timu ya timu ya Tanzania Bara kujitoa baada ya washindi wa pili Uhamiaji kutangaza mapema kujitoa kwa sababu kama hizo.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Annie Kibira (Pichani) alisema jana kuwa, Polisi imethibitisha leo kuwa haitashiriki katika mashindano hayo kwa sababu ya ukata.

Alisema kwa Bara timu pekee yenye uhakika wa kushiriki mashindano hayo ni Jeshi Stars na inatarajia kuondoka kesho Jumapili kwenda Nairobi.

Wakati huohuo, timu za Zanzibar zilitarajia kuanza safari jana ya kwenda Nairobi kupitia jijini Dar es Salaam, ambako wataondoka leo pamoja na viongozi wanne wa Chaneta.

Timu ya Jesho la Kujenga Uchumi, JKU, itakuwa na wachezaji 12 wakike na 12 wakiume na viongozi watano kushiriki mashindano hayo.

Timu nyingine ya Zanzibar itakayoshiriki mashindano hayo ni ile ya KVZ.


Mbali na Kibira, kiongozi mwingine wa Chaneta ni kaimu katibu mkuu, Hilda Mwakatobe wakati waamuzi ni Eliakimu Christopher na Jenny Butinini.

Simbu kuonekana live DStv London Marathon

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Multchoice-Tanzania kupitia kisimbuzi cha DStv wataonesha mubashara mbio za Marathon za London, ambazo Mtanzania Alphonce Simbu atashiriki.

Macho na masikio ya watanzania yataelekezwa jijini London, kumshuhudia mwanariadha huyo akifanya vitu vyake katika mbio hizo kubwa.

Mbio hizi zitashirikisha wanariadha nyota duniani, ambao watawania kitita cha zaidi ya sh Milioni 200 zitakazotolewa kwa mshindi wa kwanza.

Wanariadha nyota watakaoshiriki mbio hizo ni wale kutoka Kenya, Ethiopia na Eritrea.
Mashindano hayo yataonekana Mubashara kupitia king’amuzi cha DStv  katika chaneli namba 209 ya SuperSport (SS9) kuanzia saa tano asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande alisema kuwa king’amuzi maarufu cha DStv kitaonesha mbio hizo ubashara `live’ nakuwawezesha watu kuona moja kwa moja.

“Wakati wote DStv imekuwa kinara katika kuwahakikishia watanzania wengi uhundo wa aina yake hususan katika ulingo wa michezo na burudani na kwa mara nyingine tena tunauwezesha umma wa watanzania kushuhudia tukio hilo muhimu, ambapo balozi wetu Simbu anatuwakilisha katika mashindano makubwa ya riadha,” akisema Maharage.

Simbu ambaye pia ni Balozi maalum wa DStv, ni Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano maarufu ya Standard Chartered Mumbai Marathon.

Katika mbio hizo za kesho, Simbu anatarajia kuwapa wakati mgumu wanariadha nyota duniani watakaoshiriki mbio hizo.

Multichoice Tanzania inamdhamini Simbu kwa muda wa mwaka mzima kwa lengo la kufanikisha maandalizi yake ya kushiriki mashindano ya Dunia yatakyofanyika jijini London Agosti.


Udhamini huo wa DStv ulianza tangu mwaka jana, ambapo mwanariadha huyo amekuwa akipatiwa posho ya kujikimu pamoja na kusaidia kambi yake ya mazoezi.

Man United, Celta Vigo nusu fainali Ligi ndogo uefa

ZURICH, Uswisi
TIMU ya Manchester United itakutana na Celta Vigo ya Hispania katika mchezo wa nusu fainali wa Ligi ya Ulaya.

Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya England imeshinda mara tatu taji hilo la Ligi ya Ulaya.

Timu ya Uholanzi ya Ajax, ambao ni washindi wa mwaka 1992, itakutana na timu ya Ufaransa ya Lyon katika mchezo mwingine wa nusu fainali.

Mechi za kwanza za nusu fainali zitachezwa Mei 4 huku zile za marudiano zitapigwa Mei 11, wakati fainali ya mashindano hayo itafanyika Mei 24 Stockholm, Sweden.

Kocha wa Man United Jose Mourinho alishinda taji hilo akiwa na Porto mwaka 2003 na atacheza na klabu ya La Liga ya Celta, ambayo haijawahi kushinda taji kubwa la Ulaya.

Ajax, ambayo iliifunga Schalke 4-3 kwa ushindi wa jumla ili kutinga nusu fainali, ina uzoefu katika mashindano ya Ulaya.

Timu hiyo imeshinda taji la Ubingwa wa Ulaya mara nne huku nyuma na Ligi ya Ulaya mara moja, ikiifunga Torino katika fainali ya mwaka 1992.

Real Madrid kuivaa Atletico Madrid, Juventus wapangwa na Monaco Ligi Mabingwa Ulaya

Real Madrid walipotwaa ubingwa wa Ulaya baada ya kuifunga Atletico Madrid mwaka jana.
ZURICH, Uswisi
MABINGWA watetezi Real Madrid watakabiliana na wapinzani wao wakubwa Atletico Madrid katika nusu fainali za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, wakikumbushia fainali ya mwaka jana.

Kikosi hicho cha Zinedine Zidane kinaweza kuwa klabu ya kwanza kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Ulay katika fainali itakayopigwa Juni 3 kwenye Uwanja wa Cardiff.

Klabu ya Ufaransa ya Monaco itacheza na Juventus ya Italia katika mchezo mwingine wa hatua hiyo ya nne bora.

Mechi za kwanza za nusu fainali zitapigwa Mei 2 na 3, huku zile za marudiano itafanyika wiki inayofuata.

Real, ina lengo la kutwaa tena taji kubwa Ulaya ikiwa watafanikia itakuwa ni mara yao ya 12, baada ya kuifunga mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich kwa jumla ya mabao 6-3 na kutinga nusu fainali.

Wakati huohuo, Atletico Madrid ilimaliza ubabe wa mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Leicester kwa ushindi wa mabao 2-1 baada ya mechi zote mbili.

Juventus iliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Barcelona huku Monaco ikiondosha Borussia Dortmund 6-3.

Thursday 20 April 2017

Simbu atua London na kutamba kufanya kweli

Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande (kulia), Alphonce Simbu (katikati) na kocha wa Simbu, Francis John.
Na Mwandishi Wetu
MSHINDI wa Medali ya Dhahabu katika Mbio za Mumbai, Alphonce Simbu amewasilili katika jiji la London tayari kwa kushiriki London Marathon yanayofanyika jijini keshokutwa Jumapili.

Simbu amewasili nchini Uingereza tayari kwa mashindano hayo ambayo yanayotarajiwa kushirikisha wanariadha mashuhuri duniani.

Simbu, ambaye ni Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano maarufu ya Standard Chartered Mumbai Marathon, anatarajiwa kuwapa wakati mgumu manguli wa riadha ulimwenguni wanaoshiriki mbio hizo za London akiwemo Muethiopia Kenenisa Bekele pamoja na wengine kutoka Ethiopia na Kenya.

Akiongea muda mfupi kabla ya kupanda Ndege kwenda Uingereza, Simbu alisema amejiandaa kupambana kufa na kupona kuhakikisha kuwa ananyakua medali kwenye mashindano hayo.

“Nitapambana kwa nguvu zangu zote. Ninakwenda London nikijua wazi kuwa naiwakilisha nchi yangu kwenye mashindano haya makubwa. Nakwenda kupeperusha bendera ya Tanzania” alisema simbu

Aliongeza kuwa “Nina imani nitashinda kwani nimefanya mazoezi ya kutosha na nina ari na moyo wa kushinda. Naomba sala za watanzania wote ili niweze kuleta medali nyumbani” Alisema Simbu.

Simbu kwa sasa yu[o chini ya udhamini wa kampuni ya Multichoice Tanzania kupitia King’amuzi cha DStv ambao ndio wamedhamini kambi yake.
 
 “Nawashukuru sana DStv kwa udhamini wao mkubwa wa kambi yangu ya mazoezi pamoja na mahitaji yangu mengine kwa kipindi kirefu sasa. Kwa kweli wao ndiyo waliofanikisha maandalizi yangu” alisema Simbu

Mbali na wadhamini pia amewashukuru wadau wote wa riadha hususan Chama Cha Riadha Tanzania pamoja na wizara inayohusika na michezo kwa jitihada zao za kuahakikisha safari yake ya kwenda London inafanikiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande alisema kuwa wana imani kubwa sana na Simbu kutokana na mazoezi aliyofanya.

“Tunafurahi sana kuwa baada ya kuweka nguvu kubwa sasa Simbu anakwenda kushiriki mashindano haya akiwa amejiandaa vizuri. Tunaamini atashinda, na pia huu ni mwanzo wa ndoto yetu kubwa, ya kusikia kwa mara ya kwanza wimbo wetu wa Taifa ukipigwa kwenye mashindano ya Olympic. Kwa mwenendo wake, tunaamin Simbu atatufikisha huko” alisema Maharage.
 
Multichoice Tanzania inamdhamini Simbu kwa muda wa mwaka mzima kwa lengo la kufanikisha maandalizi yake ya kushiriki katika mashindano ya Dunia yatakayofanyika jijini London Agosti mwaka huu. Udhamini huu ulianza tangu mwaka 2016, ambapo Multichoice humpatia Alphonce posho ya kujikimu pamoja na kusaidia kambi yake ya mazoezi.


Alphonce anatarajiwa kurejea  nchini Jumatatu, Aprili 24 saa mbili asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro.

Wednesday 19 April 2017

Waandaaji Ngorongoro Marathon watangaza zawadi nono za washindi wa mbio hizo za 10

Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa mbio za 10 za Ngorongoro Marathon wametangaza zawadi za washindi, imeelezwa.

Mbio hizo zimepangwa kufanyika Aprili 29 kuanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Hihadhi ya Bonde la Ngorongoro mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa mmoja wa waratibu wa mbio hizo za kimataifa Meta Petro, washidi kwa upande wa wanaume na wanawake  wapata zawadi sawa.

Petro alisema kuwa mshindi wa kwanza ataondoka na sh Milioni 1, wakati yule wa pili ataenda nyumbani na sh 500,000, huku watatu atapewa 250,000 na wanne sh 100,000.

Alisema maandalizi yanaendelea na yamefikia vizuri kwani jana alikuwa mjini Arusha akishughulikia medali za washindi na zawadi zingine.

Tayari Kampuni ya Vinywaji  baridi ya Bonite Bottlers na Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro wamekubali kudhamini mbio hizo.

Petro aliwataka watu, taasisi na makampuni kujitokeza kudhamini mbio hizo kwani nafasi bado ziko.

Pia aliwataka wanariadha kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ambazo mwaka huu zinaendeshwa chini ya waandaaji wapya, ambapo kauli mbiu ni Kimbiza Jangili.

Mbio hizo zinalengo la kuwawezesha wananchi kuhusu kupiga vita mauaji ya tembo, faru, twiga, simba na wanyama wengine ili kulinda vivutio vya utalii.

Klopp kumalizia kazi yake ya ukocha Liverpool

LONDON, England
JURGEN Klopp anasema kuwa haitakuwa ajabu ikiwa Liverpool ndiko patakuwa mahali pake pa mwisho kufanya kazi ya ukocha.

Klopp, ambaye klabu zake mbili alizowahikufundisha ni Mainz na Borussia Dortmund, alitua Anfield Oktoba mwaka 2015 ambako alisaini mkataba wa miaka sita katika kipindi kilichopita cha majira ya joto.

Na anasema kuwa anapendelea mkataba wa muda mrefu ambao utamuwezesha kutotaka kazi nyingine wakati muda wake utakapomalizika Merseyside.

Lakini anakiri wakati shinikizo la kushinda mataji likiongezeka, huku Liverpool ikiwa na ukame akirejea nyuma mwaka 2012 walipotwaa taji la Kombe la Ligi na hawajawahi kushinda lile la Ligi Kuu tangu mwaka 1992/93.

Klopp alisema: "Sitaweza kuwa katika kazi katika klabu 10 tofauti mara nitakapomaliza kazi yangu ya ukocha.

Kocha Bayern Munich alina na mwamuzi Kassai

MADRID, Hispania
KOCHA wa Bayern Munich Carlo Ancelotti amesema mwamuzi Viktor Kassai hakuwajibika ipasavyo katika mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na ametaka kuanza kutumika mara moja teknolojia ya video.

Kiungo wa Bayern Arturo Vidal alitolewa baada ya kuoneshwa kadi mbili, wakati nyota wa Real Madrid,  Cristiano Ronaldo akifunga katika muda wa nyongeza akiwa katika eneo la kuotea wakati mabingwa hao wa Ulaya wakisonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 6-3 jana.

Tulikuwa tukijia kila kitu wakati tukienda katika mchezo huu isipokuwa mwamuzi tu, “alisema Ancelotti.

"Huwezi kuamua timu inayokwenda nusu fainali kwa mtindo kama huu. Haiwezi kutokea katika kiwango hiki.”
Ancelotti, ambaye ni kocha wazamani wa Madrid, pia alisema kuwa kocha wa Real Zinedine Zidane alikubaliana na tathmini yake kuhusu mwamuzi huyo wa Hungary kushindwa kumudu mchezo huo kwenye Uwanja wa Bernabeu.

"Mwamuzi hakuwa kabisa katika mchezo na hakufanya kazi yake, “alisema Ancelotti.
"Sifikiri kama Real Madrid ilikuwa na ushawishi wowote kwa waamuzi. Waamuzi usiku huu wamechemsha, nilikuwa shishabikii matumizi ya teknolojia ya video, lakini sasa nakiri kuwa inahitajika.”

Teknolojia ya goli inaamua kama mpira umevuka mstari, ambapo ilianza kutumika katika Ligi kuu msimu wa mwaka 2013-14 na Bundesliga walianza kutumia kuanzia mwaka 2015-16.

Na Uingerea pia wanatarajia kutumia videoa kwa ajili ya kumsaidia mwamuzi kubadili maamuzi yake, ambapo hatua hiyo inatarajia kuanza katika kampeni za mwaka 2017-18.

Mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge alimtuhumu Kassai kwa “kuharibu mchezo.”

Alisema: "Ni jambo linalojia hasira kwa mwamuzi kushindwa kutoa maamuzi ya haki….”
"Mchezo ulikuwa mzuri, lakini kwa bahati mbaya mwamuzi alitoa maamuzi ambayo ni wazi ndio yaliyotugharimu. Mwamuzi ndiye aliyeharibu mchezo.”

Katika mchezo huo, Cristiano Ronaldo alifunga mabao matatu `hat-trick’ wakati mabingwa watetezi Real Madrid wakiipiku kitata Bayern Munich katika muda wa nyongeza na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

`Hat-trick’ ya Ronaldo imemfanya mchesaji huyo kuwa wa kwanza kufikisha mabao 100 katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.


Katika usiku huo, majirani wa Real Atletico nao walitinga nusu fainali ya mashindano hayo baada ya kutoka sare ya 1-1 na Leceister City na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kushinda 1-0 mchezo wa kwanza.

Sunday 16 April 2017

Simbu kuanza safari ya kushiriki London Marathon


Na Mwandishi Wetu

MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu kesho Jumatatu atapanda pipa kwenda Afrika Kusini akiwa njiani kwenda Uingereza, ambako atashiriki London Marathon Jumapili ijayo Aprili 23.

Simbu anapitia Afrika Kusini kwa ajili ya kupatiwa viza ya dharura ya kuingia Uingereza baada ya kuikosa ile ya kawaida jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema jana kuwa, Simbu ataondoka kesho Jumatatu kwenda Afrika kusini kushughulikia viza ya kuingia Uingereza kabla ya kwenda nchini humo ambako Jumapili atashiriki London Marathon.

Simbu alifuzu kwa mbio hizo baada ya kumaliza katika nafasi ya tano katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazil 2016 kabla ya kushinda mbio za Mumbai Marathon.

Kwa mujibu wa Gida, tayari mwanariadha huyo ameingia katika orodha ya wanariadha bora kabisa duniani na ndio maana waandaaji wa London Marathon kuna fedha atapewa mara tu atakapoanza mbio hizo (Appearance Fees).

Gidabuday alisema kuwa Simbu hata kama hatashinda mbio hizo lakini akimaliza tu amejihakikishia fungu nono na kama akimaliza, basi ataondoka na maelfu ya dola za Marekani.

Simbu endapo atashinda mbio hizo za London Marathon ataondoka na kitita cha dola za Marekani 55,000 kama zaidi yash Milioni 150, na kama atafanikiwa kuvunja rekodi ataongezewa dola za Marekani 25,000 (ikiwa ni zaidi ya sh Mil 50),

Mshindi wa kwanza hadi wa 12 wa mbio hizo ataondoka na kitita cha fedha, huku wale watakaokimbia muda bora bbila kujali kama umevunja rekodi ya njia au ya dunia, nao wataongezewa fedha za bonasi.

Savio yaendelea kuchanja mbuga, ABC ikiidadabua Don Bosco 73-50 Ligi ya Kikapu RBA Dar es Salaam


Na Mwandishi Wetu

SAVIO imeendelea kuongoza katika Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam ya RBA inayoendelea kushika kasi.

Baada ya mechi za jana kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, ambapo ABC iliifunga Don Bosco kwa pointi 73-50 huku Oilers wakiitambia Chui kwa pointi 68-50, Savio wako kileleni kwa kujikusanyia jumla ya pointi 22.

Vijana au City Bulls wenyewe wako katika nafasi ya pili kwa pointi 21 huku Ukonga Kids wakifuatia katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 19 huku JKT wakiangukia katika nafasi ya nne.

Wakongwe Pazi wenyewe wako katika nafasi ya tano baada ya kujikusanyia poiti 17, Kurasini nao wana pointi 17 lakini wako katika nafasi ya sita, Mabibo Bullet wenyewe wako katika nafasi ya saba.

Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, Halleluya Kavalambi alisema kuwa ABC, Jogoo, UDSM Outsiders na Olilers wanashika nafasi ya nane hadi 10.

Wakati huohuo, Kavalambi alisema kuwa viporo vya baadhi ya mechi vitapigwa Jumatano, ambapo ABC watacheza na Tanzania Prisons saa 10:00 Jioni, huku Jogoo wataoneshana kazi na Mgulani kuanzia saa 12 jioni na Pazi atakwaruzana na Chui kuanzia sasa 2 usiku.