Sunday, 8 March 2015

Kipa wa Ivory Coast, TP Mazembe afanyiwa upasuajiLUMBUMBASHI, DR Kongo
KIPA wa Ivory Coast na TP Mazembe Sylvain Gbohouo (pichani)amekwenda Qatar kwa ajili ya matibabu ya maumivu ya goti lake, imeelezwa.

Gbohouo alikuwa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Ivory Coast inayojulikana kama `Tembo katika fainali za Mataifa ya Afrika zilizofanyika Januari huko Guinea ya Ikweta, ambako timu yao ilitwaa ubingwa.

Kipa huyo alikosa fainali ya mashindano hayo dhidi ya Ghana baada ya kuumia goti lake wakati wa mchezo wa nusu fainali dhidi ya DR Kongo.

Gbohouo bado haijaichezea Mazembe ambao ni mabingwa mara nne wa Afrika, tangu aliporejea kutoka katika fainali hizo za Mataifa ya Afrika.

Rais wa Mazembe Moise Katumbi alisema kuwa Gbohouo aliruhusiwa kwenda kufanyiwa upasuaji kwa gharama za Shirikisho la Soka la Ivory Coast.

"Aliondoka wiki iliyopita na bado hajarudi, " alithibitisha Katumbi.

"Sio tatizo kubwa sana lakini ni kwa ajili ya kutatua tatizo mara moja.

"Atarejea katika mazoezi ya kawaida wiki tatu kuanzia sasa."

Katumbi, ambaye kikosi chake wiki hii kitacheza na timu ya Afrika Kusini ya Mamelodi katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, alisema Mazembe itamtegemea kipa mkongwe Robert Kidiaba wakati Gbohouo akiendelea kupona.

No comments:

Post a Comment