Tuesday 29 November 2016

Mjomba Mrisho Mpoto aendelea kuchengua Ikulu baada ya kupewa shavu katika dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa rais Lungu wa Zambia


 Rais Dk John Pombe Magufuli akimpongeza muimbaji mahiri wa mashairi, Mrisho Mpoto Ikulu jijini Dar es Salaam hivi karibuni wakati msanii huyo akiimba kibao cha Sizonje.

Na Mwandishi Wetu
MUIMBAJI mashuhuri wa mashairi nchini, Mrisho Mpoto ameendelea kupata shavu katika hafla mbalimbali zinazofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mpoto, juzi alitoa burudani kali Ikulu wakati wa dhifa ya kitaifa ambayo Rais John Magufuli alimuandalia mgeni wake Rais wa Zambia, Edgar Lungu.

Katika hafla hiyo, msanii huyo ambaye sasa anatamba na kibao chake cha Sizonje, aliimba wimbo unaosifu na kuelezea ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia.

Wageni waalikwa walifurahia maneno yaliyomo katika wimbo huo, yakiwemo yale yaliyowaelezea waasisi wa mataifa hayo mawili, Julius Nyerere (Tanzania sasa ni marehemu) na Kenneth Kaunda wa Zambia.

Pia alielezea kuhusu Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), bomba la mafuta la Tazama, na mambo mengine mengi, ambayo yanaunganisha nchi hizi mbili.

Hivi karibuni Magufuli alitamka wazi kuwa yeye ndio Sizonje, ambaye nsiye anayezungumzia katika kibao hicho chenye mafumbo kibao.
Akiwa nchini, Rais Lungu mbali na kutembelea Tazara na Tazama, pia alitembelea baadhi ya vitengo vya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (PTA) kabla ya kuondoka jana kurudi kwao.

Sunday 27 November 2016

Mwenye uchungu na michezo nchini Gidabuday ashinda ukatibu Mkuu riadha Tanzania (RT)


Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania (RT), Meta Petro (kulia) na Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya TOC,, ambaye pia mjumbe wa RT, Filbert Bayi wakipiga kura leo kwenye Uwanja wa Taifa.

Na Mwandishi Wetu

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania umefanyika leo kukishuhudia mwanariadha wa zamani, Wilhelm Gidabuday akirithi mikoba ya Katibu Mkuu wa zamani Suleiman Nyambui aliyeko nchini Brunei.

Nyambui kwa sasa ndiye kocha mkuu wa timu ya taifa ya riadha ya Brunei.

Aidha katika uchaguzi huo Anthony Mtaka aliitetea nafasi yake ya Urais wa shirikisho hilo kwa mara nyingine tena kwa kura 73 kati ya kura 74.

Gidabuday alipata kura 38 akiwapita Michael Washa (24) na Gidamis Shahanga (11) huku kura moja ikiharibika katika nafasi hiyo.

Katika nafasi nyingine, William Kalaghe alichukua nafasi ya Makamu wa Rais Utawala kwa kura 59 dhidi ya 15 zilizokwenda kwa Zainab Mbilo huku Dk. Ahmed Ndee alichukua nafasi ya Makamu wa Rais Ufundi kwa kura 74 dhidi ya kura nne za hapana.

Ombeni Zavalla aliyekuwa akikaimu Katibu Mkuu wa RT katika uchaguzi huo alipita bila kupingwa katika nafasi ya Katibu Mkuu Msaidizi kwa kura zote 74 na Gabriel Liginyani akipata nafasi ya Mweka  Hazina wa shirikisho hilo kwa kura 69 kati ya 74. 

Wengine waliopata nafasi ya Ujumbe wa RT ni Lwiza John, Meta Petro, Robert Kalyahe, Dk. Nassoro Matuzya, Rehema Killo, Zakaria Barie, Mwinga Mwanjala, Tullo Chambo, Christian Matembo na Yohana Misese.

 
Katibu Mkuu wa BMT afunguka 

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja aliweka bayana  RT ndio chama pekee cha michezo nchini kinachoongozwa na Mkuu wa Mkoa, kwetu sisi (BMT) ni utajiri, hii ni dalili nzurihivyo ukiboronga unapoteza nafasi zote mbili, na kuongeza

Migogoro kwenye vyama inakimbiza wawekezaji na wafadhili, sio vema pindi mambo ya ndani yanapokuwa hayaendi sawasawa kukimbilia kwenye vyombo vya habari, alisema Kiganja.

 
Gidabuday asutwa, ajitetea

Mjumbe wa BMT na Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa na Usuluhishi ya baraza hilo Jamal Lwambo alimsuta Gidabuday kwa kauli zake ngumu alizowahi kuzitoa awali.

Katibu Mkuu mpya uliwahi kusema kwa RT wasiporudi na medali ungefanya nini ...sasa kama ulivyokuwa ukiisuta RT ukiwa bado hujaikamata nafasi hiyo watu wamekurudisha kundini wana matumaini makubwa kwako, na kuongeza

Kipindi mlichopata ni kifupi sana..hatutarajii kuona migogoro bali tunarajia kuona timu inatengenezwa vizuri ili kuleta heshima ya Tanzania, alisema Lwambo.

Kwa upande wake Gidabuday alisema, Challenge zangu kwa RT nilipokuwa nje ya shirikisho ndizo zilizonifanya nigombee nafasi hii lakini nawashukuru sana RT kwani hawakunijengea chuki kwa kuwakosoa bali walinitazama kwa upande wa uzuri.

Aliongeza, Kwa umbo mimi ni mwembamba natoa ahadi tena kama ukiniona mwakani wakati kama huu nina kitambi basi uje uniulize kulikoni, alisema Gidabuday.

Tullo Chambo atetea nafasi yake

Afisa Habari wa RT na mjumbe wa shirikisho hilo Tullo Chambo alisema, Kwa kweli kinyanganyiro mwaka huu kilikuwa kigumu ukilinganisha na msimu uliopita wakati tukiingia, lakini naamini uongozi huu kwa mara nyingine utajitahidi kufanya makubwa kuinua riadha.


Saturday 26 November 2016

guardiola akiri michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya sio mchezo



MANCHESTER, England
KOCHA wa Manchester City Pep Guardiola anasema kuwa kufanya kwake vizuri katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya haina maana kuwa ana uhakika wa kufanya vizuri katika mashindano hayo msimu huu.

Katika misimu saba kama kocha wa Barcelona na Bayern Munich, Guardiola mwenye umri wa miaka 45 ameshinda mara tatu taji la Ligi ya Mabingwa na hajawhi kushindwa kufuzu kwa nusu fainali.

Man City msimu huu imefikia hatua ya mtoano ya mashindano hayo huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

"Wakati wote inaonekana kama rahisi lakini kila kitu ni kigumu, alisema Guardiola.

Timu hiyo ya kocha huyo Mhispania itamaliza ya pili katika Kundi C, ikiwa na maana kuwa wataikwepa Bayern Desemba 12  wakati itakapopangwa ratiba ya hatua ya 16 bora.

Juventus na Borussia Dortmund ni wapinzani wanaotarajia kkutana pamoja na Monaco, ambao wamemaliza kileleni katika kundi ambalo Tottenham walitolewa katika mbio hizo.

Man City ilitinga hatua ya nusu fainali msimu uliopita, ambapo huku nyuma haijawahi kuvuka hatua ya 16 bora.

"Tunazungumza kuhusu Manchester City kucheza hatua ya nusu fainali lakini kuna timu nzuri kibao Ulaya, alisema Guardiola.

"Kucheza robo fainali sio jambo la kawaida. Wakati unapofanikiwa kucheza nusu fainali au fainali, ni kitu kisicho cha kawaida.

"Kiwango chetu sasa ni kucheza hatua ya mtoano kama ni kiwango chetu cvha chini, ndio miaka sita iliyopita hilo halikuwahi kutokea kamwe.

Mwanamapinduzi FIDEL Castro wa Cuba afariki dunia akiwa na umri wa miaka 90



HAVANA, Cuba
FIDEL Castro, rais wazamani wa Cuba na kiongozi wa mapinduzi ya kikomusti, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90.

Akitangaza kifo hicho mdogo wake, ambaye ndiye rais wa sasa wa Cuba, Raul Castro alisema mauti yalimkuta usiku.
"Kiongozi wa mapinduzi ya Cuba alimafikiri dunia usiku huu, alisema Rais huyo wa sasa wa cuba.

Fidel Castro aliiongoza Cuba nchi ya chama kimoja kwa zaidi ya miaka 50 kabla Raul hajaichukua mwaka 2008.

Mashabiki wake walisema aliirejesha nchi kwa wananchi. Lakini pia alitumuhumiwa kuukandamiza upinzani.

Kuanzia sasa kutakuwa na siku kadhaa za maombolezo ya kitaifa kutoka na msiba huo.