Saturday 30 April 2016

Manchester United yataka kuchelewesha ubingwa wa Ligi Kuu ya England kwa Leicester City Jumapili



Kikosi cha Manchester United.

MANCHESTER, England
KIKOSI cha Manchester United huenda kisibadilike kutoka kile kilichoshinda mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA wakati timu hiyo Jumapili itakapokutana na `bingwamteule wa Ligi Kuu Leicester.

Wachezaji kama Luke Shaw, Bastian Schweinsteiger na Will Keane wataendelea kubaki nje ya uwanjani katika pambano hilo la aina yake.

Leicester City wenyew watajaribu kutwaa taji hilo la Ligi Kuu bila ya kuwa na mshambuliaji wake hatari Jamie Vardy, anayetumikia nyongeza ya adhabu ya kufungiwa mechi moja zaidi kufuatia kutoa maneno makali wakati akitolewa nje na mwamuzi walipocheza dhidi ya West Ham.

Mchezaji aliyechukua nafasi yake walipocheza dhidi ya Swansea wiki iliyopita, Leonardo Ulloa, ataanza katika mchezo huo dhidi ya Man United baada ya kupona maumivu ya mgongo.

MAONI YA WACHAMBUZI

Guy Mowbray: "Nimetabiri kuwa katika mchezo huo Man United itaifunga Leicester City'.

"Ndio, wanaweza kuongeza mwishoni mwa mchezo.

"Kitu ambacho hatutakuwa na wasiwasi nacho ni kwamba Leicesterwatakuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya England, wakikumbushia Arsenal mwaka 2002 kwa kuthibitisha hilo kwenye uwanja huo, ambayo umewahi kuandaa sherehe nyingi za ubingwa mara nyingi kuliko mahali kwingine.

"Man United watataka kushinda mchezo huo kwenye Uwanja wa Old Trafford, ili waweze kumaliza angalau katika nafasi ya nne za juu.”

"Mei Mosi mi alama ya kuanza vizuri, mwanzo mpya…”

WANACHOSEMA MAKOCHA

Kocha wa Manchester United Louis van Gaal: "Nafikiri tunatakiwa kuwafunga kwa sababu bado tuko katika mbio za kusaka nafasi ya nne. Hatuwezi kukubali wawe mabingwa wikiendi hii kwenye uwanja wetu wa Old Trafford.

"Nafikiri wanaweza kuwa mabingwa baadae wiki ijayo. Hatuharibu sherehe yao, ila tunaiharisha tu kidogo.

Kocha wa Leicester City Claudio Ranieri: "Ni kitu kisichoaminika, ni historia na hilo tunalijua.

"Ni muhimu kumaliza historia kama sinema ya Kimarekani. Wakati wote mwishoni ni mzuri, umalizika vizuri.

"Ni nafasi nzuri lakini kwa sababu hii tunatakiwa kuangalia. Acha niw kimya, tusubiri, tuna muda bado.

"Niliwaambia, kila kitu kipo mikononi mwetu na lazima tuendelee. Watu wengine watafurahia hilo lakini mimi lazima kusonga mbele.

UTABIRI WA LAWRO

Mchezo huu sio lazima Leicester ishindi lakini kwa Manchester United, wanatakiwa kushinda kwa kuwa wanahitaji ushindi ili waendelee kubaki katika nne bora.

Nafikiri mchezo huo utamalizika kwa sare, ambayo itakuwa nzuri kwa Leicester, ingawa utachelewesha ubingwa wao hadi Jumatatu usiku wakati Tottenham watakapocheza na Chelsea.

Wednesday 27 April 2016

Marwa, Failuna washinda Heart marathon 2016


Wanariadha wa mbio za kilometa 21 wakijiandaa kwa mbio hizo za Heart Marathon kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
DICKSON Marwa na Failula Abdul jana walishinda Heart Marathon, mbio zilizoanzia na kumalizikia kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la Mlimani.

Katika mbio hizo za kilometa 21, Marwa wa Dar es Salaam aliibuka wa kwanza kwa upande wa wanaume kwa kutumia saa 1:10.42 wakati Abdul wa Arusha aliwashinda wanawake wenzake kwa kutumia saa 1:20.31, ambapo kila mmoja alipata Sh 500,000. 

Washindi wa pili na tatu kwa wanaume ni Panuel Mkungo na Eric Mombo wote wa Holili, Rombo mkoani Kilimanjaro waliomaliza kwa saa 1:11.88 na 1:13.46. 


Wakimbiaji wa kilometa tano wakijiandaa kabla ya kuanza kwa mbio hizo.
Akizungumza kabla ya kutoa zawadi kwa washindi, mgeni rasmi wa mbio hizo ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Michezo nchini, Alex Nkeyenge amewataka Watanzania kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.


Alisema asilimia kubwa ya Watanzania wamekuwa wakiendelea kusumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza  kutokana na wengi wao kutokuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi.  

"Michezo ni afya pamoja na ajira kama tunataka kuona magonjwa haya yanatoweka kabisa nchini, basi tujenge utamaduni wa kufanya mazoezi pamoja na kubadili mitindo yetu ya maisha, alisema Nkeyenge. 

Aidha, alisema Serikali imeahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa waandaaji wote wa mashindano yoyote endapo watahitaji msaada.  Hakuna Serikali isiyopenda michezo niseme tu Serikali ipo bega kwa bega na nyinyi na wale wote watakaokuwa wakianzisha mashindano yoyote, aliongeza Nkeyenge. 

Pia ametoa mwito kwa washiriki wote wa Heart Marathon pamoja na washindi kuhakikisha wanaendeleza vipaji vyao vya mbio na wale wote walioshindwa wasikate tamaa. 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Heart Marathon, Dk Chakou Khalfan amewashukuru washiriki wote na kuahidi kuhakikisha mbio hizo zinakuwa na muendelezo mwaka hadi mwaka na kuenea nchi nzima, lengo likiwa ni kuwajengea Watanzania utamaduni wa kupenda mazoezi pamoja na kuwajenga wakimbiaji ili waweze kushiriki mashindano hata ya kimataifa.

Alisema mashindano hayo yamegawanya kwa kilometa ambapo mbio ndefu zilikuwa zile za kilometa 21, 10, tano, meta 700 na zile za watoto wadogo za meta 50. 

Aidha, mashindano hayo pia yalitoa fursa kwa washiriki kupima afya zao bure ikiwemo kuangalia magonjwa mbalimbali hasa yale yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na mengineyo. 

Katika mbio za baiskeli za matairi matatu za walemavu, Mohammed Abdallah wa Dar es Salaam aliibuka wa kwanza kwa kutumia dakika 38.12 huku,Simon Mulewa aliibuka wa pili kwa dakika 39.10 na Romanus Nyambulage alimaliza wa tatu kwa kutumia dakika 45.15.

Wachezaji Uchukuzi SC waibiwa gesti Dodoma katika mashindano ya Mei Mosi




Kocha Rose Mkisi akihamasisha timu yake ya kuvuta kamba ya wanaume ya TPDC walipocheza na Ukaguzi katika michuano ya Mei Mosi. TPDC walishinda kwa mivuto 2-0.

Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI wa timu ya Uchukuzi SC inayoshiriki kwenye mashindano ya Mei Mosi mkoani hapa, juzi wameibiwa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 1.5 katika nyumba ya kulala wageni waliyofikia ya MT iliyopo Chadulu mjini hapa. 

Mkuu wa Upelelezi wa wilaya, Charles Chalula, alipoulizwa juu ya tukio hilo jana alikiri taarifa kufika ofisini kwake, na tayari jeshi hilo linawashikilia watu watatu akiwemo mhudumu wa hoteli hiyo.

Pia alisema atawasiliana na mkurugenzi wa hoteli hiyo, aliyemtaja kwa jina moja la Haule ili aweze kurudisha fedha za wachezaji, ambazo walilipa kukaa hapo hadi Mei 2 mwaka huu michezo itakapokamilika. 

"Ni kweli wachezaji wamekuwa na hofu na usalama wao na mali zao, nitamtafuta mmiliki wake akiwezekana arudishe fedha zao leo hii hii (jana) ili waweze kuhamia hoteli nyingine, ila nitahakikisha suala la upelelezi tunalifanya haraka ili hivi vitu vilivyoibwa vipatikane haraka, alisema Chalula. 

Timu ya kamba ya wanaume ya Ukaguzi wakivutana na wenzao wa TPDC, lakini walishindwa kwa mivuto 2-0.
Kwa mujibu wa taarifa ilizonazo gazeti hili, wizi huo ulitokea majira ya saa 10:00 jioni wakati wengi wa wachezaji hao wakiwa Uwanja wa Jamhuri kuishangilia timu ya soka soka iliyokuwa inapambana na CDA ya hapa. Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Mbali ya soka, wachezaji wengine wa Uchukuzi ni wa michezo ya kuvuta kamba, bao, drafti na karata. Mmoja wa wachezaji hao, Ally Suleiman katika chumba chake ameibiwa kompyuta mpakato yenye thamani ya Sh milioni 1.2, fedha taslimu Sh 120,000 na mashine inayohifadhia nyaraka mbalimbali yenye thamani ya Sh 180,000.

Thea Samjela wa Uchukuzi SC (kuilia) akichuana na Regina Mutimangi wa TPDC katika mchezo wa bao.
Suleiman aliyefungua kesi ya wizi iliyopewa jalada namba IR/3844/2016 pia aliibiwa vitu mbalimbali ikiwemo kadi ya Bima ya Afya na leseni ya udereva. Mchezaji mwingine, Tracius Dionis alisema wezi hao waliingia chumbani kwake na kutawanya vitu kwenye begi lake, lakini hawakuiba chochote zaidi ya kuchukua seti ya televisheni, mali ya nyumba hiyo ya kulala wageni.

Aliongeza kuwa, walifungua chumba cha mchezaji mwingine, Aminiel Ombeni ambaye amesafiri kwenda Moshi kuzika baada ya kupata msiba wa mama yake, na bado haijajulikana vilivyoibwa kwani begi lake lilikutwa katika  chumba cha mteja aliyefika juzi mchana.

Naye Katibu Mkuu wa timu ya Uchukuzi, Alex Temba alisema wamesikitishwa na tukio hilo kwani haijawahi kutokea katika mikoa yote waliyowahi kushiriki michezo ya Mei Mosi.


Neema Makassy  wa Uchukuzi SC (kulia) akitafakari katika mchezo wa bao dhidi ya Joyce Kimondi wa Ujenzi.
Temba aliomba jeshi la polisi kuonyesha ushirikiano kama lilivyoahidi siku ya kwanza timu ziliporipoti mkoani hapa kuwa watatoa ulinzi mkubwa, basi watekeleze ahadi yao kutokana na wachezaji wote ni wageni mkoani hapa.

"Suala hili limetusikitisha sana huyu ni mfanyakazi mwenzetu pamoja na kwamba tupo katika suala la michezo lakini aliendelea na kazi za ofisi na jana tu alikuwa akituma taarifa mbalimbali, basi tunawaomba polisi watusaidie hivi vitu vipatikane, na hata waongeze ulinzi kwani ni tukio la aibu kuwaibia wageni, alisema Temba.