Wednesday 28 February 2018

Lundenga Abwaga Manyanga Miss Tanzania


Uncle Hashimu Lundenga na Basila Mwalukuzi
Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa muda mrefu wa shindano la Miss Tanzania Kampuni ya Lino Agency wametangaza kuachia ngazi kwa kutojihusisha tena na shughuli hizo za urembo.

Tangu mwaka 1994 Lino imekuwa ikiandaa shindano hilo kwa mafanikio lakini kuanzia mwaka juzi ilishindwa na kukumbwa na kashfa kadhaa ikiwemo kumpa taji mrembo asiye na sifa na kushindwa kutoa zawadi kwa washindi hali iliyofanya kufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Lino, Hashim Lundenga ‘Uncle’ alisema wameamua kuachana na shughuli hizo tangu Februari 13, mwaka huu na kuiachia Kampuni ya Look chini ya Mkurugenzi wake Miss Tanzania mwaka 1998, Basila Mwanukuzi.

“Sababu kubwa ya kuacha shughuli hizi ni pamoja na malengo yetu mapya ya kuachia damu changa waendeleze na kuleta chachu ili kuifanya Miss Tanzania iwe juu… ili tusije kupata balaa zaidi tumeamua kumpa mwingine jukumu hili,” alisema.

Lundenga alisema wamejitathmini na kuona kuwa kwa siku za karibuni walishindwa kuandaa shindano hilo kutokana na changamoto mbalimbali ingawa pia, wanajivunia baadhi ya mafanikio ikiwemo kuwahi kumtoa mrembo wa dunia aliyeingia sita bora na kuitangaza nchi kimataifa.

Kwa upande wake, Mwanukuzi alisema anawashukuru Lino lakini pia, waandaaji wa Miss Dunia kwa kumpa kibali kuwa ndiye muandaaji na kuahidi kurudisha heshima ya shindano hilo.

“Tunatambua kumekuwepo na changamoto nyingi hivi karibuni katika uandaaji chini ya Lino, sisi kama Look tumeziona, tumejiandaa kikamilifu na tunaahidi kuboresha na kukuza yarudi katika hadhi yake kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa,” alisema.

Alisema watazindua rasmi shindano hilo mwishoni mwa mwezi huu na kuanza mchakato, wakitarajia kupeleka mrembo katika mashindano ya dunia baadaye mwaka huu.

Alisema kupitia mashindano ya mwaka huu wanataka kufanya uchunguzi kujua ni kitu gani wanatakiwa wafanye kufikia vigezo vya kimataifa au kama kuna figisu au siasa zinatumika wajue nini cha kufanya kwa lengo la kuboresha.

 Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisema kama serikali hawana budi kuishukuru Lino kwa kusaidia vijana wengi wa kike kupata ajira kupitia fani hiyo ya urembo.

“Ni imani yetu shindano lipo mikononi mwa mtu ambaye alipitia kwenye urembo, ni kweli kuna changamoto lakini anaweza kuzigeuza na kuzifanya fursa ili kurudi katika hadhi yake,” alisema na kuhimiza wazazi kutokuwa na wasiwasi tena juu ya shindano hilo.

Mzee Joram kushiriki tena Kili Half Marathon 2018

Mzee Joram Mollel maarufu kama BABU mwenye umri wa miaka 91 akijisajili kushiriki mbio za KM 21 za Tigo Kili Half Marathon katika zoezi la usajili lililofanyika jana katika viwanja vya keys Hotel, jijini Arusha. Tigo Kili Half marathon inatarajiwa kufanyika Jumapili tarehe 4 Machi mwaka huu katika viwanja vya Chuo cha Ushirika, Moshi. 

Yanga Yavunja Mwiko wa Kutoshinda Mtwara


Na Mwandishi Wetu,Mtwara
MABINWA wa soka Tanzania Bara, Yanga leo imefanikiwa kuvunja mwiko wa kutoibuka na ushindi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona baaba ya kuibuka na ushidi wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ushindi huo unawafanya mabingwa hao watetezi kufikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 19, wakizidiwa pointi tano na vinara wa Ligi Kuu, Simba wenye pointi 45.

Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Florentina Zablon wa Dodoma aliyesaidiwa na Abdallah Rashid na Kassim Safisha wa Pwani, hadi mapumziko tayari Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

ius Charles Buswita ndiye aliyeifungia Yanga bao la kwanza  dakika ya tano akimalizia kazi nzuri ya kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Papy Kabamba Tshishimbi.

Beki wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy akaifungia bao la pili Yanga SC dakika ya 29 baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Ndanda kufuatia pasi ya Buswita aliye katika msimu wake wa kwanza Jangwani tangu asajiliwe kutoka Mbao FC ya Mwanza.

Yanga ingemaliza kipindi cha kwanza inaongoa kwa mabao 3-0 kama si kiungo Mkongo, Tshishimbi aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland kukosa penalti dakika ya 38, ambayo ilipanguliwa na kipa Jeremiah Kisubi kufuatia John Tibar George kuunawa mpira kwenye boksi.

Kipindi cha pili, Ndanda walio chini ya kocha Malale Hamsini walibadilika na kuanza kupeleka mashambulizi langoni mwa Yanga hadi kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi.

Bao hilo lilifungwa na Nassor Kapama dakika ya 46 akimalizia kazi nzuri ya kiungo Mrisho Khalfan Ngassa, mchezaji wa zamani wa Fanja ya Oman, Free State Stars ya Afrika Kusini, Yanga, Simba, Azam, Azam FC za Dar es Salaam, Mbeya City, Kagera Sugar na Toto Africans ya Mwanza.

Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa; Jeremiah Kisubi, William Lucian ‘Gallas’, John Tibar George/Ally Suleiman dk77, Hemedi Khoja, Ahmad Waziri Tajiri/Waziri Majogoro dk40, Jacob Massawe, Majjid Khamis Bakari, Nassor Yahya Kapama, Ahmed Siasa Msumi, Baraka Gamba Majogoro na Mrisho Khalfan Ngassa.

Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Raphael Daudi, Pato Ngonyani, Papy Kabamba Tshishimbi/Geoffrey Mwashiuya dk46, Pius Buswita, Ibrahim Ajib na Emmanuel Martin/Yussuf Mhilu dk86.

Wanadamu Watakiwa Kujiandaa Kabla ya Kifo


  Mchungaji Augustino Simalenga wa Kanisa la TAG Kivule leo maeneo ya Kitunda akiombea mwili wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kabla ya kusafirishwa kwa mazishi yatakayofanyika kesho wilayani  ya Rombo.

Na Mwandishi Wetu
MCHUNGAJI wa Kanisa la TAG Kivule, Augustino Simalenga amewataka wanadamu kujiandaa na kumrudia muumba wao, kwani hawajui siku wala saa watakapokufa.

Alitoa kauli hiyo leo kwenye misa ya kumuaga marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), iliyofanyika nyumbani kwake maeneo ya Kitunda, ambapo amewataka watu kujiandaa mapema kwa kuwa hawajui watakapokwenda baada ya kifo.

   Msemaji wa familia ya marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Silvester Shayo (kulia) akitoa shukrani  kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Wafanyakazi wa TAA na watu wote walioshiriki kwenye msiba huo. Marehemu Swai atazikwa kesho wilaya ya Rombo.

 “Neno la Mungu linatukumbusha kuwa tujiandae mapema, ndugu yetu Jerome ameshamaliza kazi, tunatakiwa kujitafakari sisi hatima yetu itakuwaje, kwani wapo waliolala mauti Biblia inasema hao wanapumzika wakisubiri siku atakaporudi Mwana wa Adam atakuja kuwachukua wote waliohai na wale waliokufa wakimuamini Kristu watafufuliwa kwanza ili kwa pamoja wamlaki Bwana wao mawinguni,” alisema Mchungaji Semalenga.

Alisema kila mtu atafakari maisha ya hapa duniani kwani mlango wa kutokea hapa duniani aidha ni kifo au siku Bwana atakapokuja kuchukua watu wake, hivyo ni vyema kujiandaa kwa kutafakari maisha baada ya hapa kwa sasa kuanza kujitengenezea hazina mbinguni.


Ofisa Utumishi Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Priscus Mkawe akisoma wasifu wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa JNIA, kabla ya kuagwa nyumbani kwake Kitunda na kusafirishwa kwenda Rombo kwa mazishi yatakayofanyika kesho.

“Ukisoma kitabu cha Mhubiri sura ya 3 utaona Mungu ameweka kila kitu na wakati wake, upo wakati wa kula na wakati wa kusema, wakati wa kunyamaza, wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa kila kitu kinawakati hata sisi tuliohai ni wakati wetu kuwa hai bali utafika wakati hatutaweza kuwa hai siku zote, na kila jambo lina mwanzo na mwisho, lakini mwisho wa jambo unatengenezwa wakati wa sasa kama maisha yetu ya sasa hatufikiri mwisho basi tukifika mwisho tutakuwa watu wa kujuta, watu wa kuomboleza na lakini sasa Mungu anatupa nafasi ya kuyakabili mambo yanayokuja na hatima ya maisha yetu,” alisisitiza.

Alisema katika kitabu cha Zabuni, kinasema binadamu amepewa maisha mafupi na machache, na kuishi ni miaka 70 na wachache wanaweza kuishi zaidi ya hiyo, ambapo ni tofauti na wanadamu wa kwanza waliishi miaka 100 ambayo nayo yalikuwa mafupi. Hata hivyo alisema baada ya kifo yapo maisha ya milele, ambayo mwanadamu anatakiwa kuyatafakari sasa kwa kujiwekea hazina itakayomwezesha kuishi vyema mbinguni.


 Kaimu Mkurugenzi wa  Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka akiaga mwili wa aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa JNIA, Bw. Jerome Swai, ambaye atazikwa kesho wilayani Rombo.

Mchungaji Simalenga alisema amefanya utafiti katika huduma anazotoa lakini amegundua hakuna mwanadamu anayetaka kwenda jehanamu, hata asiyefanya ibada kwa Mungu anamatumaini ya kwenda mahala pema peponi.

“Mungu ameweka utaratibu na Mwanadamu akiuufuata ndio atafikia kwenye ule mpango ambao Mungu ameuweka, sasa kama hataki kuufuata anajikuta siku za maisha yake atajikuta mahala asipotaka kwa kilio, kujuta na kuomboleza, kwani alikuwa akipuuzia na kuona mambo ya Kimungu ni ya kiduni na watu maskini na wachini, wakati ni mambo ya msingi kuliko kitu chochote duniani,” alisema Mchungaji Simalenga.    

 Bi. Honoratha Emmilian ambaye ni mke wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), akilia kwa uchungu wakati wa kuuaga mwili wa mumewe nyumbani kwake Kitunda. Marehemu atazikwa kesho wilayani Rombo.

Naye Ofisa Utumishi Mkuu wa JNIA, Bw. Priscus Mkawe alisema marehemu Swai ameacha pengo kubwa kutokana na umahiri wake katika utendaji kazi wake uliotukuka.

“Marehemu Swai alikuwa mmoja wa wafanyakazi wa kipekee aliyefanya kazi kwa bidii na kujituma na kutokana na uchapakazi wake aliwahi kuchaguliwa kuwa mfanyakazi hodari kuanzia mwaka 2001, 2003 na 2017, hivyo JNIA na TAA kwa ujumla tumempoteza mfanyakazi hodari sana,” alisema Priscus.
Ndugu wa marehemu Jerome Swai wakiuaga mwili wa mpendwa wao leo nyumbani kwake Kitunda, ambapo anatarajiwa kuzikwa kesho wilayani Rombo. Swai alikuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
  Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Prosper Tesha (mwenye miwani mbele) akijumuika na waombolezaji kwenye msiba wa aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Jerome Swai aliyefariki Jumatatu ya wiki hii na atazikwa kesho wilayani Rombo.
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Jerome Swai likipandishwa ndani ya basi tayari kwa safari ya kwenda Rombo kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho. Marehemu aliajiriwa mwaka 1984.



Tuesday 27 February 2018

KAMATI YA MAADILI YAWAFUNGIA VIONGOZI MVUVUMWA KWA KUGHUSHI LESENI ZA WACHEZAJI


Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Maadili ya TFF iliyokutana Februari 3, 2018 na Februari 17, 2018, katika ofisi za TFF Karume, pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa pia ilipitia na kutoa hukumu ya tuhuma za kutoa taarifa zisizo sahihi na kughushi leseni za usajili zilizowakabili watuhumiwa mbalimbali walioletwa mbele yake.

Tuhuma hizo zilitokana na mechi namba 26 Kundi A ligi daraja la kwanza iliyofanyika Oktoba 29, 2017 kati ya Mvuvumwa FC na Friends Rangers ambapo katika mchezo huo timu ya Mvuvumwa FC iliwachezesha wachezaji watano (5) ambao ni Elias Costa Elias (jezi namba 5), Lukwesa Joseph Kanakamfumu (jezi namba 7), Dunia Abdallah Dunia (jezi namba 1), Doto Justine Kana (jezi namba 12) na Mwarami Abdala Mwarami (jezi namba 8).

Kamati imemtia hatiani kocha na mratibu wa Mvuvumwa FC, Joseph Kanakamfumu kwa makosa yote mawili, kutoa taarifa zisizo sahihi, (udanganyifu) ili kufanikisha usajili wa wachezaji kinyume na taratibu za ligi daraja la kwanza.

Kosa la kwanza Kanakamfumu akiwa kocha wa Mvuvumwa FC aliwaorodhesha wachezaji (Elias Costa Elias, Lukwesa Joseph Kanakamfumu, Dunia Abdallah Dunia, Doto Justine Kana Mwarami Abdala Mwaram) kushiriki mechi namba 26 huku akijua kwamba hawana leseni halali kutoka TFF, wachezaji wote walitoka katika kituo ‘academy’ anayoiendesha hivyo ni dhahiri alijua alichokuwa anakifanya.

Kosa la pili Kanakamfumu aliamua kuwaongeza wachezaji hao baada ya kukabidhiwa timu kwa vile alifahamu uwezo wao na inaonekana alitumia uzoefu wake katika mpira wa miguu kupata leseni za kughushi.

Kwa makosa hayo, kamati inamfungia Joseph Kanakamfumu kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano.


Conte mbioni kuifundisha timu ya taifa ya Italia



Antonio Conte

LONDON, England


KOCHA wa Chelsea Antonio Conte ndiye chaguo namba moja la kuwa kocha wa timu ya taifa ya Italia, makamu wa rais wa Shirikisho la soka la Italia, Alessandro Costacurta alibainisha jana.

"Bado hatujachagua lakini nafikiri Conte ni mmoja wa makocha ambao wanaweza kufanya vizuri. “Miezi kadhaa iliyopita niliwahi kuzungumza naye.”

Nyota huyo wazamani wa AC Milan Costacurta ndiye aliyepewa jukumu la kumtafuta mbadala wa Gian Piero Ventura, ambaye alitimuliwa baada ya timu ya taifa ya Italia kushindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Conte, 48, aliifundisha Italia kutoka mwaka 2014 hadi kucheza robo fainali ya mashindano ya Ulaya, Euro 2016 kabla hajachukuliwa na Chelsea.

Roberto Mancini

Wengine wanaofikiriwa kuwa na uwezo wa kuifundisha Italia ni pamoja na Roberto Mancini, Claudio Ranieri na Carlo Ancelotti.

"(Conte) tayari anajua jinsi ya kuifundisha timu ya taifa ya Italia wakati wengine bado hawajahi kuifundisha, “alisema Costacurta.

Claudio Ranieri 

Conte aliiongoza Chelsea kutwaa taji la Ligi Kuu ya England katika msimu wake wa kwanza wa kuifundisha, lakini kwa sasa inashikilia nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, pointi 19 nyuma ya vinara Manchester City.

Carlo Ancelotti

Costacurta aliendelea kusema: "Hiyo naina maana kuwa sitakuwa na furaha na Mancini au na Ancelotti – ingawa (Ancelotti) anaonekana mwenyewe amejiondoa katika mbio za kuwania kuifundisha timu hiyo.


Trump Afikiria Uchaguzi 2020, Amtaja Meneja Wake


NEWYORK, Marekani

RAIS wa Marekani Donald Trump amemtaja meneja wa kampeni zake za urais mwaka 2020.

Brad Parscale (pichani kushoto), mtaalam wa mitandao, alifanya kazi katika kampeni za Trump 2016 na alisifiwa sana kwa kutumia mitandao ya kijamii vizuri, jambo linalotajwa kumpa ushindi Trump.

Parscale atatumika katika kampeni za uchaguzi mdogo baadae mwaka huu.

Trump anasema Parscale ni mtu sahihi na amekuwa akifanya kila kitu kwa uhakika wa hali ya juu.

Trump alimshinda Hillary Clinton katika Uchaguzi Mkuu wa Marekani uliofanyika Novemba mwaka 2016 na baadae kuapishwa rasmi Januari 20, 2017.


Liverpool Inaweza Kuichakaza Timu Yoyote-Mane


LONDON, England

SADIO Mane anasema kuwa Liverpool "inaweza kuifunga timu yoyote duniani " wakati vijana wa Jurgen Klopp wakiifukuzia nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu na kukufuzu kwa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Kimsimamo, Liverpool wako katika nafasi ya tatu, pointi mbili nyuma ya Manchester United baada ya kufungwa mara moja katika mechi 19 zilizopita za Ligi Kuu huku ikiwa katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kushinda mabao 5-0 dhidi ya Porto katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora.

Kikosi cha Klopp kimefunga mabao 103 katika mashindano yote msimu huu huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa na Mane, mabao 31, Salah na Roberto Firmino ,ambao wamekuwa wakizisambaratisha safu za ulinzi za timu pinzani.

"Naweza kuhisi kuwa klabu kwa sasa inakwenda katika muelekeo sahihi, “alisema Mane alipozungumza hivi karibuni.

"Kulikuwa na miaka kibao migumu pale Liverpool lakini mambo hayo huwa yanatoke katika kila klabu duniani.

"Kwa sasa tuko katika njia nzuri, hivyo kila kitu kinawezekana. Tunajua kuwa tunaweza kusema kuwa katika siku zetu tunaweza kuifunga timu yoyote duniani.”

Mshambuliaji huyo wa Senegal alisema ari ya timu kwenye uwanja wa Anfield ni nzuri na kuna kujiamini miongoni mwa wachezaji.

"Kila mchezaji mmoja mmoja wakati wote anafurahia kucheza na mwenzake, “alisema. “Wakati wote tunajaribu kumsaidia kila mmoja na tunacheza kitimu.”


Wafanyakazi JNIA, TAA Wamlilia Swai


Marehemu Jerome Swai  wakati wa uhai wake

 Na Mwandishi Wetu

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) wamesikitishwa na kifo cha Bw. Jerome Swai (58) aliyekuwa fundi bomba mahiri kilichotokea  tarehe 26 , 2018 kwenye hospitali ya Amana baada ya kuugua kwa muda mfupi.

  1. Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka (kulia), akimpa pole Bi. Honoratha Emmilian aliyefiwa na mume wake marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Bomba (JNIA), alifariki tarehe 26 Februari, 2018 kwenye hospitali ya Amana Jijini Dar es Salaam.

Wafanyakazi hao kwa nyakati tofauti walisema marehemu Swai alikuwa hakubali kushindwa kwa kuhakikisha anatatua tatizo linalohusiana na mabomba ya maji kwa wakati wote anapokuwa kazini.

Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Bi. Hanna Kibopile alisema marehemu ameacha pengo kubwa kutokana na uchapakazi wake uliotukuka.

Meneja Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Vedastus Fabian, akitoa pole kwa Bi. Honoratha Emmilian ambaye ni mke wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa fundi bomba.  

Naye meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara, Bw. Daimon Mwakyosa alisema marehemu alikuwa akifanyakazi kwa bidii na hakukubali kushindwa.

“Marehemu alikuwa akiijua vyema kazi yake na hakukubali kushindwa nakumbuka wakati nikiwa JNIA na tukiwa tumepangwa shift (zamu) moja hakuna kilichoshindikana kwake kuhusu fani yake aliijua vyema kazi yake,” alisema Bw. Mwakosya.

Waombolezaji kwenye msiba wa marehemu Jerome Swai (kushoto), wakipokea pole kutoka kwa Meneja Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Vedastus Fabian. Marehemu Swai alikuwa Fundi Bomba JNIA na alifariki tarehe 26 Februari 2018.

Bi. Fatma Matimba, Kaimu Meneja Utawala JNIA, alisema marehemu Swai alikuwa mchapakazi, ambapo mwaka jana alichaguliwa kuwa mfanyakazi hodari. Pia aliwahi kupewa cheti cha ufanyakazi hodari mwaka 2001 kinachotolewa TUGHE.

Ndugu wa marehemu Jerome Swai wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka (mwenye tai) alipofika kuwafariji, ambapo marehemu alikuwa Fundi Bomba JNIA. 

Marehemu Swai alizaliwa mwaka 1960 wilaya ya Rombo, na kupata elimu katika shule ya msingi Kilesi mwaka 1976, na baadaye kujiunga na Chuo cha Ufundi cha Makalema akisomea fani ya ufundi bomba daraja la tatu, na baadaye kujiendeleza katika Chuo cha Ufundi cha Chang’ombe mwaka 1988 na VETA mwaka 2007.

  1. Baadhi ya Wafanyakazi wa Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), wakiwa kwenye msiba wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Bomba. Swai alifariki rarehe 26 Februari 2018 katika hospitali ya Amana.

Marehemu aliajiriwa na TAA  mwaka 1984 akiwa kama fundi bomba daraja la tatu na baadaye alijiendeleza na kufanikiwa kusoma hadi kufikia daraja la kwanza. Marehemu ameacha mjane Bi. Honoratha Emmilian ambaye naye ni mfanyakazi wa TAA katika Idara ya Utawala akiwa kama mhudumu.

  1. Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Juluius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka aliyeinama (kushoto) akiteta jambo na baadhi ya wafanyakazi wa JNIA waliofika kwenye msiba wa aliyekuwa fundi Bomba, Bw. Jerome Swai.

Mungu aipumzishe Roho ya Marehemu mahala pema peponi. Amina!

Rais Ramaphosa atangaza baraza lake la Mawaziri


JOHANNESBURG, Afrika Kusini

RAIS mpya wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza baraza lake la mawaziri, huku akifanya mabadiliko kadhaa katika nafasi za uwaziri.

Amemteua tena Nhlanhla Nene kuwa Waziri wa Fedha, akibadili uamuzi wa kumtema uliofanywa awali na mtangulizi wake Rais Jacob Zuma.

Bwana Zuma, ambaye anakabiliwa na mashataka ya rushwa, alilazimishwa kuachia ngazi na chama chake mapema mwezi huu.

 Bwana Ramaphosa alichukua madaraka ya urais, aliahidi kupambana na rushwa.

"Nimeamua kufanya mabadiliko haya. Nina hamu ya mabadiliko, kiuchumi na mambo mengine, “alisema Ramaphosa wakati akitangaza uteuzi wake wa mawaziri mjini Pretoria jana usiku.

David Mabuzza, Naibu Waziri wa Chama cha National Congress (ANC) chama tawala, alitangazwa kuwa Naibu Rais wa Afrika Kusini.

Mke wazamani wa Zuma, Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye Ramaphosa alimshinda katika uchaguzi wa Desemba wa ANC, alichaguliwa kuwa waziri katia ofisi ya rais.

Gumzo kubwa lilikuwa kwa Nhlanhla Nene ambaye ameteuliwa kuwa waziri wa fedha, alitimuliwa Desemba mwaka 2015.

Ramaphosa, mwenye umri wa miaka 65 ambaye ni mfanyabiashara wazamai, katika hotuba yake ya kwanza kulihutubia taifa mapema mwezi huu aliahidi kupambana na kuinua uchumi na kutoa ajira.


Monday 26 February 2018

Norway Bingwa jumla Olimpiki Majira ya Baridi 2018

PYEONGCHANG, Korea Kusini

NCHI ya Norway imetwaa ubingwa wa jumla wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi huku Marit Bjorgen akishinda medali ya dhahabu kwa mbio za nyika za wanawake za kilometa 30.

Brorgen alitwaa medali hiyo ya dhahabu katika siku ya mwisho ya michezo hiyo iliyofanyika jijini hapa.

Norway imemaliza michezo hiyo ikiwa imejikusanyia jumla ya medali 14 za dhahabu sawa na Ujerumani, lakini imepata medali 39 kwa ujumla, ikiwa n inane zaidi ya Ujerumani.

Bjorgen, 37, amekuwa mchezaji mwenye medali nyingi zaidi katika michezo hiyo ya mwaka huu kwa kushinda medali ya shaba ya timu, ikiwa ni medali yao ya tano katika michezo ya Pyeongchang 2018 na ni ya 15 kwa ujumla.

Mdada huyo alishinda medali katika kila m,chezo alioshindana katika Olimpiki ya mwaka huu.

Pia alishinda medali ya dhahabu ka katika shindano la wanawake la mbio za kupokezana vijiti la 4x5, alipata medali ya fedha katika kilometa 15.

Akishindana katika Olimpiki yake ya mwisho baada ya miaka 16 ya kushiriki michezo, Bjorgen alimaliza akiwa na medal inane za dhahabu, nne za fedha na tatu za shaba kutoka katika michezo mitano.



Bingwa Euro 2020 kuondoka na pauni Mil34


ZURICH, Uswisi

TIMU 24 zitakazofuzu kwa mashindano ya Euro 2020 zitagawana kiasi cha Euro milioni 371, kiasi ambacho ni rekodi ya ongezeko kulinganisha na zawadi iliyopita.

Hatua hiyo imefikiwa na Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) wakati wa mkutano wake mkuu uliofanyika juzi Bratislava, Slovakia.

Ongezeko ni zawadi za jumla ni asilimi 23 zaidi ya lile la zawadi za mashindano hayo yalipofanyika Ufaransa, Euro 2016, ambako kwa mara ya kwanza nchi 24 zilishiriki katika mashindano hayo.

Kila nchi itakayoshiriki itapokea kiasi cha Euro milioni 9.25 (sawa na zaidi ya Sh milioni 230) kwa ajili ya ushiriki tu, nyongeza na Euro milioni 1.5 katika kila mchezo atakaoshinda hatua ya makundi na Euro 750 000 endapo atatoka sare.

Kutakuwa bna fedha zingine zaidi katika kila raundi atayocheza hatua ya mtoano, ikiwa na maana kuwa mshindi ataondoka na kitita cha Euro milioni 20.25 mbali na zile za hatua ya makundi.

Mshindi wa Kombe la Mataifa ya Ulaya mwaka 2020 ataondoka na kiwango cha juu cha Euro milioni 34, ukilinganisha na Euro milioni 27 alizopata mshindi wa mwaka 2016.

Fainali za Euro 2020 zitapigwa katika miji 12 tofauti ya Ulaya, huku Uwanja wa Wembley jijini London ndio utakaoandaa fainali hizo zitakazofanyika Julai 12.


Chelsea wamuongezea dau Hazard ili abaki


LONDON, England

KLABU ya Chelsea ina mshawishi Eden Hazard kuklubali kusaini mkataba mpya kwa kumuongezea daua hadi kufikia pauni 300,000 kwa wiki.

Klabu hiyo ya Stamford Bridge inamshawishi mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji kusaini mkataba mpya na kuzivunja nguvu timu pinzani zinazotaka kumsajili mchezaji huyo.

Pamoja na mchezaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski, Hazard na mchezaji mwenzake Thibaut Courtois ni miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na Real Madrid mwaka huu.

Chelsea inataka kuwabakisha wachezaji wake hao wote.

Hazard mwenye umri wa mika 27 mkataba wake wasasa unamalizika mwaka 2020.

Mkataba wake huyo una thamani ya pauni milioni 200 na mkabata wake mpya utamfanya kulipwa pauni 300,000 kwa wiki pamoja na bonasi.

Hazard amekuwa akisema mara kwa mara kuwa ana furaha Chelsea ingawa atakuwa akisubiri kuona kile kitakacholetwa na Real Madrid katika ofa yao.

Kocha wa timu hiyo ya Hispania Zinedine Zidane inamtaka sana Hazard lakini nafasi yake hiyo iko katika tishio msimu huu, lakini itategemea na uamuzi wa nyota huyo.


Saturday 24 February 2018

Riadha Tanzania Waitilia Ngumu BMT Tozo Mpya


Na Mwandishi Wetu, Arusha
RIADHA Tanzania (RT) limesema kuwa halitasita tozo za ada mpya za mbio za marathon licha ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuzisitisha hadi watakapokutana Machi 5 mjini Moshi.
RT katika taarifa yake iliyotoa jana imesema kuwa imefedheheshwa na kusitishwa kwa matumizi ya ada mpya kwa waandaaji wa mbio za marathon, ambapo imesisitiza kuwa uamuzi wake uliotolewa Septemba 16 mwaka jana, unabaki pale pale.
 Taarifa iliyotolewa jana mjini hapa na Katibu Mkuu Wilhelm Gidabuday inasema kuwa BMT haiwezi kuipangia RT ada kama ambavyo haiwezi kulipangia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ada za  viingilio kwani RT ni chombo huru.
Alisema kuwa hiyo njia ya RT kujitafutia vyanzo vya mapato ili kutoitegemea serikali katika upatikanaji wa fedha.
“Tunasisitiza kuwa waandaaji wote kuhakikisha wanalipa ada  kulingana  na makundi  yaliyopangwa  na kujisajili  kabla ya kuendesha matukio yao,”anasema Gidabuday.
Anasema kuwa waandaaji wote wanatakiwa kulipa ada zao kwa wakati na wapewea hadi Februari 28 wawe wamekamilisha malipo hayo kabla hawajachukuliwa hatua kali.
Alieleza kuwa kuhusu uamuzi wa BMT kuitaka RT kukutana pamoja na waandaaji wa mbio ni jambo ambalo halitawezekana kutokana  na  kuwa Kamati ya Utendaji haitaweza kuhudhuria kikao hicho kilichoitishwa Machi 5 mjini Moshi.
 “Sababu ya  kushindwa kuhudhuria ni kutokana  na wito mfupi wa kikao hicho, ambapo wajumbe wengi watakuwa wametawanyika sehemu mbalimbali kutokana na majukumu  ya chama, ikiwemo kushughulikia  kambi ya taifa,”aliongeza.
 Gidabuday alifafanua kuwa BMT mara nyingi iliwahi kuihimiza RT ikae na waandaaji ili kupunguza msururu wa mbio  za marathon ambazo hazina tija kwa taifa.
“Ikumbukwe  kuwa Chama cha Waandaaji wa Mbio sio mdau wa RT kwa maana hakitambuliki  rasmi kwetu,wadau halali wa RT ni waandaaji wa mbio ambao wamejisajili na kulipa ada,”alisema.
 Aliisihi BMT kushughulikia masuala ya kiufundi na uhuru wa kikatiba  wa vyama vya michezo ili kuepusha migongano ambayo itarudisha nyuma maendeleo ya michezo.

BMT Yavunja Mkutano Mkuu, Yaunda Kamati BFT

Katibu Mkuu Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja.

Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limefuta Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) uliopangwa kufanyika leo mjini Dodoma na badala yake imeindwa Kamati ya Muda itakayoongoza mchezo huo.
Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja akizungumza kwa njia ya simu leo kutoka Dodoma alisema kuwa, wameshindwa kuendesha uchaguzi huo sababu Katiba ya BFT haielezi lengo la shirikisho hilo.
Mwenyekiti wa Kamati mpya ya BFT, Mutta Lwakatare.
Kiganja aliwataja wanaunda kamati hiyo ya watu sita kuwa ni pamoja na aliyekuwa rais wa BFT, Mutta Lwakatale (mwenyekiti), wakati wajumbe ni Yono Kivela, Samuel Sumwa, Lucas Muta, Aisha Viniatis na Aboubakar Mohamed.
 Aliyataja majukumu yao wanayotakiwa kuyatekeleza ndani ya miezi mitatu kuwa ni pamoja na kurekebisha Katiba, kuitisha Mkutano Mkuu wa kupitisha Katiba pamoja na kuandaa Uchaguzi Mkuu.
Mjumbe wa Kamati ya BFT, Mohamed Aboubakary.
 
Kiganja alisema kuwa pia kamati  hiyo mbali na majukumu hayo, imepewa kazi ya kuendesha na kusimamia shughuli za kila siku za mchezo huo hapa nchini.
 Akielezea sababu za kumrejesha Rwakatale wakati alikuwemo katika uongozi uliopita ambao ulishindwa kutekeleza majukumu yao, Kiganja alisema Rais wa BFT sio mtendaji,ambapo Katibu Mkuu Makore Mashaga ndiye alikuwa mtendaji na ndio maana hakurudishwa.
Mjumbe wa Kamati ya BFT, Aisha Voniatis
 Alisema kuwa kamati hiyo sasa inatakiwa kukamilisha yote hayo ndani ya miezi mitatu na kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika kipindi hicho ili kuwapata viongozi halali.


Friday 23 February 2018

Mechi Kali za Premier League Wikiendi hii


WIKIEND hii kwenye michuano ya Premier League, Liverpool inarudi uwanjani siku 10 baada ya ushindi mzito wa 5-0 walioupata dhidi ya Porto kwenye Ligi ya Mabingwa UEFA, Jumamosi hii kwenye EPL wanawakaribisha Westham United Anfield wakiwa na matumaini makubwa ya kupata matokeo, Je watafanikiwa?

Angalia mechi hii MUBASHARA kwenye DStv Bomba kwa sh.19,000 tu, mechi itachezwa saa 12 jioni ,Supersport 10.

Mechi nyingine zitakazopigwa wikiendi hii kwenye Premier League ni:

        Leicester City dhidi Stoke City saa 9 alasiri kwenye Supersport 3

        Watford vs Everton saa 2 usiku kwenye Supersport 3

        Burnely vs Southampton saa 12 jioni Supersport 5

        Na AFC Bournemouth itacheza dhidi ya Newcastle United saa 12 jioni a kurushwa LIVE kwenye Supersport 10 iliyopo kwenye kifurushi Bomba kw ash.19,000 tu!

Jumapili ndio balaa lenyewe pale Manchester United ambao kwasasa wanashika nafasi ya 2 kwenye msimamo wa EPL wakiwa na pointi 56 wanawakaribisha Chelsea ambao wapo nafasi ya 4 wakiwa na utofauti wa pointi 3 tu! Je, Man Utd atashinda au Chelsea itafunga pengo?

Usikose mechi hii, Jumapili saa 10 jioni kwenye Supersport 3 ya kifurushi DStv Compact kwa sh.69, 000 tu!

Je hujajiunga na DStv?  wahi sasa Ofa ya THE PUNGUZO, burudika na miezi miwili bure kwa kununua Dekoda pamoja na Dish kwa sh.79, 000 tu!

Kujiunga piga 0659 070707, THE PUNGUZO na DStv!!


Zabuni 163 za ujenzi wa hoteli ya nyota nne na maeneo ya biashara Termina 3 zafunguliwa leo

Ofisa Manunuzi na Ugavi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Margareth Mushi akifungua boksi lililohifadhia zabuni za ujenzi wa hoteli ya nyota nne na maeneo ya biashara katika jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.   

 

Boksi lililokuwa limehifadhi nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa hoteli ya nyota nne na maeneo ya biashara kwenye Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere likiwa tupu baada ya nyaraka hizo kuondolewa tayari kwa ufunguzi leo.

Nyaraka za zabuni za ujenzi wa hoteli ya nyota nne na kuwekeza katika maeneo ya biashara kwenye Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere zikiwasili  Jengo la Kwanza la abiria (TB1) ili ziingizwe kwenye ukumbi na kufunguliwa.


Maboksi ya zabuni mbalimbali za ujenzi wa hoteli ya nyota nne na uwekezaji katika maeneo ya biashara kwenye Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere yakishushwa kwenye gari kabla ya kuingizwa katika ukumbi wa mikutano wa Transit uliopo jengo la Kwanza la abiria (TB1).


Wananchi walionunua zabuni za kuwekeza katika ujenzi wa hoteli ya nyota nne na maeneo ya biashara kwenye jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere leo wakifuatilia kwa makini wakati wa ufunguaji wa zabuni hizo katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la Kwanza la abiria (TB1).

Ofisa kutoka kampuni inayotoa huduma ya mizigo ndani ya viwanja vya ndege ya Nas Airco, Bw. David Ngarapi (anayetazama kamera) akifuatilia zoezi la ufunguaji wa zabuni za ujenzi wa hoteli ya nyota nne na maeneo ya kuwekeza katika maeneo ya biashara kwenye Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere zilizofunguliwa leo kwenye ukumbi wa Jengo la Kwanza la abiria (TB1).

Kaimu Mkuu wa Idara ya Manunuzi na Ugavi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Godfrey Kanyama (kushoto) akisikiliza swali kutoka kwa Mama Open Kitchen (Mama Ntilie wa Kishua), wakati wa ufunguzi wa zabuni za ujenzi wa hoteli ya nyota nne na uwekezaji kwenye maeneo ya biashara kwenye Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.