Friday, 6 March 2015

Failuna ajifua kwa mbio za Sokoine, Ngorongoro
Failuna Abdi (wa pili kushoto) akichuana katika mbio za Karatu Desemba mwaka jana. Failuna alishinda mbio hizo za kilometa tano. Kulia mbele ni Mary Naali.
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MWANARIADHA Failuna Abdi yuko katika mazoezi makali akijiandaa kwa ajili ya kushindana katika mashindano mbalimbali yakiwemo yale ya Sokoine na Ngorongoro Marathoni.

Kocha wa mchezaji huyo akizungumza mjini hapa Thomas Daniel alisema kuwa,mwanariadha huyo yuko katika mazoezi makali kwa ajili ya mbio za kilometa 10 za Sokoine na zile za kilometa 21 za Ngorongoro.

Mbio za Sokoine ni kwa ajili ya kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania aliyefariki kwa ajali Edward Moringe Sokoine,zinatarajia kufanyika Monduli Aprili 14 wakati zile za Ngorongoro Marathoni zitapigwa siku nne baadae Karatu katika mkoa huo huo wa Arusha.

Alisema kuwa mwanariadha wake amekuwa katika mazoezi makali huko Ilboru mkoani Arusha na anatarajia kufanya vizuri katika mbio hizo zote.

Failuna amekuwa akifanya vizuri katika mbio mbalimbali alizoshiriki ndani na nje ya nchi na kuwazidi wanariadha wakongwe na wazoefu.

Hivi karibuni mwanariadha huyo alirejea nchini akitokea nchini Brazil, ambako alishiriki katika mbio mbalimbali na kufanya vizuri.

No comments:

Post a Comment