Saturday 30 December 2017

Simba Yarejea Kileleni Ligi Kuu Tanzania Bara

Na Mwandishi Wetu
SIMBA leo imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga Ndanda FC mabao 2-0  katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Alikuwa ni mshambuliaji John Bocco aliyepeleka kilio kwa Ndanda FC iliyokuwa inacheza mbele ya mashabiki wake baada ya kufunga mabao yote mawili katika kipindi cha pili baada ya dakika 45 kumalizika kwa suluhu.

Bao la kwanza alilifungwa dakika ya 52 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Shiza Kichuya na bao la pili alilifunga katika dakika ya 56 akitumia makosa ya mabeki wa Ndanda na kipa wao, Jeremiah Kisubi kuzembea kuokoa mpira mrefu ulioingizwa kwenye eneo la hatari.


Ndanda walijitahidi kupeleka mashambulizi kwenye eneo la Simba, wakiongozwa na mkongwe Mrisho Ngassa, lakini umaliziaji mbovu ukawakosesha kupata bao la kufuta machozi.

Kwa ushindi huo, Simba inafikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi 12, sawa na Azam FC walio nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa mabao.

Azam FC juzi waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wao wa Chamazi Mbagala jijini Dar es Salaam.

Yanga  wenye pointi 21 ambao leo wanashuka dimbani wataendelea kushika nafasi ya tatu endapo watashinda dhidi ya Mbao FC kama watatoa sare au kupoteza na Singida United wakishinda dhidi ya Njombe Mji FC, basi watashuka hadi nafasi ya nne.

Katika Uwanja wa Samora Iringa jana, Tanzania Prisons waliifunga Lipuli FC bao 1-0 lililofungwa na Salum Kimenya na Mtibwa Sugar iliifunga Majimaji mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Manundu Turiani, Morogoro.

Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa, Jeremiah Kisubi, William Lucian, Abdallah Suleiman/Ayoub Masoud dakika 51, Ibrahim Job, Hamad Waziri, Hemed Khoja/Omar Mponda dakika 61, Jacob Massawe, Majid Khamis, John Tibar/Alex Sethi dakika 72, Jabir Aziz na Mrisho Ngassa.


Kikosi cha Simba ni Aishi Manula, Paul Bukaba, Shiza Kichuya, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, John Bocco, James Kotei/Yussuf Mlipili dakika 72, Juma Luizio/Moses Kitandu dakika 54, Muzamil Yassin na Mohamed Ibrahim ‘Mo’/Said Ndemla dakika 38.

Yanga Yatamba Kuipasua Mbao FC Mwanza

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
KOCHA msaidizi wa timu ya soka ya Yanga, Shadrack Nsajigwa ameahidi ushindi katika mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mkoani hapa.

Akizungumza katika mazoezi ya klabu hiyo katika uwanja huo, Nsajigwa alisema timu yake ipo katika hali nzuri na wachezaji wake wote ni wazima.

"Tumefanya mazoezi leo(jana Jumamosi) na tutapambana kuhakikisha tunashinda,wachezaji wote tuliokuja nao wapo katika hali nzuri.Hatuna hofu tumeanda timu kwajili ya ushindi," alisema Nsajigwa.

Akielezea kuhusu wapinzani wake,Nsajigwa alisema Mbao FC ni timu nzuri na ina wachezaji wanaopambana muda wote.

Nsajigwa alisema anawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kuhakikisha wanaishangilia timu yao.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, Yanga wapo katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 23 baada ya michezo 11.

Yanga imeshinda mechi Sita na kutoka sare mechi tano.Yanga imefungwa mabao matano na kufunga mabao 17.Mbao FC wapo katika nafasi ya nane wakiwa na alama 11.


Mbao FC wameshinda mechi mbili na kutoka sare mechi tano.Timu hiyo imepoteza mechi nne  na imefungwa mabao 13 huku yenyewe imefungwa mabao 11.

Friday 29 December 2017

Wenger anyoosha mikono kwa Sanchez

LONDON, England
KOCHA Arsene Wenger anasema kuwa hawezi kumuhakikishia mshambuliaji Alexis Sanchez (pichani) kubaki Arsenal kwa muda mrefu, baada ya mshambuliaji huyo kufunga mara mbili walipocheza jana dhidi ya Crystal Palace.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Chile anaweza kuondoka kama mchezaji huru katika kipindi cha majira ya joto wakati mkataba wake utakapomalizika na amekuwa akihusishwa na kutaka kuhamia kwa vinara wa Ligi Kuu ya England Manchester City, ambao walishindwa kukamilisha usajili wa mchezaji huyo siku a mwisho ya usajili.

Alipoulizwa kuhusu hatma ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 2, kocha huyo Mfaransa alisema: "Hakuna mtu hajuae nini kitatokea. Kwa kweli ni vigumu sana kutabiri.

"Kwa sasa tunaangalia mambo ya muda mfupi, hiyo ikiwa na maana mchezo ujao na wachezaji waliojituma na ambao wako tayari kupambana. Haina uhakika utakuwe;po mahali Fulani kwa muda gani.

"Wakati wote wanahoji, wakati watu hawana mikataba ya muda mrefu, Njia bora ya kuonesha jinsi watu walivyojituma ni jinsi watakavyoonesha kiwango chao uwanjani.”

Maoni yake hayo yamekuja mwezi mmoja baada ya kuzungumza kuhusu wachezaji wote wawili, Sanchez na kiungo Mjerumani Mesut Ozil, ambao mikataba yao ya sasa inamalizika katika kipindi cha majira ya joto, akitaka wabaki kwenye Uwanja wa Emirates.


Jana Alhamisi, Sanchez alifunga mara mbili katika dakika nne wakati Arsenal ikiibuka na ushindi baada ya ndros Townsend akifuta bao la kuongoza la Shkodran Mustafi.

Familia ya Kizimbabwe Yakaa Airport kwa miezi mitatu

BANGKOK, Thailand
KAWAIDA hakuna mtu ambaye hufurahia kukaa muda mrefu katika kiwanja cha ndege, lakini imekuwa tofauti kwa familia moja ya Wazimbabwe, ambao Kiwanja cha Ndege cha Bangkok kumekuwa nyumbani kwao kwa karibu miezi mitatu sasa.

Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji ya Thailand, watoto wanne wenye umri chini ya miaka 11 na watu wazima wanne waliwasili mjini hapa tangu Mei, lakini waligoma kurejea kwao Zimbabwe wakihofia kufunguliwa mashtaka.

Watu hao walibainika baada ya mtu mmoja ambaye alisema kuwa alikuwa akifanya kazi katika Kiwanja cha Ndege cha Suvarnabhumi alipotupia picha katika mtandao wa Facebook ikimuonesha akitoa zawadi ya Krismads kwa msichana mdogo wa kiafrika.

Kwa sasa picha bhiyo ikiwaimeondolewa, Kanaruj Artt Pornsopit alisema familia hiyo imekuwa ikiishi kiwanjani hapo kwa karibu miezi mitatau sasa “kwa sababu ya hali isiyo ya usalama” nchi humo.

"Natumaini wote mtarejea nyumbani kwenu haraka iwezekanazo,”alisema.
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji Pol Col Cherngron Rimphadee alisema familia hiyo awali iliwasili Thailand kama watalii. Walijaribu kupanda ndege kuondoka Bangkok Oktoba kwenda jiji la Hispania la Barcelona kupitia Kiev huko Ukraine.

Lakini walizuiwa kupanda ndege kwa sababu hawakuwa na viza inayowaruhusu kuingia Hispania.

Hatahivyo, pia walizuiwa kuingia Thailand baada ya awali kukaa muda zaidi kuliko viza yao ya awali ilivyokuwa ikiwaruhusu kwa miezi mitano hivyo ilibidi kulipa faini.


Baadae familia bhiyo ilifanya utaratibu mwingine na ndege ya Kimataifa ya Ukraine (UIA) badala yake walipitia Kiev kwenda Dubai na baadae walipita nchi ya tatu kutaka kuingia Ulaya kama wahamiaji.

Ligi Kuu Bara kuendelea Leo Azam, Stand kuumana

Na Mwandishi Wetu
LIGI Kuu Tanzania Bara (VPL) mzunguko wa 12 msimu wa 2017/2018, inaendelea leo Ijumaa baada ya kusimama kwa wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge Cup iliyofanyika nchini Kenya na mechi za raundi ya pili ya Azam Sports Federation Cup (ASFC).
VPL inaendelea tena leo Ijumaa usiku Desemba 29, 2017 kwa Azam FC kuikaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo utakaopigwa kuanzia saa Saa 1:00 usiku.

Kesho Jumamosi Desemba 30, Lipuli na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa kuanzia saa 8:00 mchana; Mtibwa Sugar na Majimaji ya Songea zikutana katika Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro wakati Ndanda itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mechi hizo mbili zitachezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Jumapili, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni huku Njombe Mji FC na Singida United wakitangulia kwa mchezo utakaoanza 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
VPL itakamilisha mechi za mzunguko wa 12 katika mechi zitakazopigwa mwakani, Januari mosi  ambako Mbeya City wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya  na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting zote zikianza kutimua vumbi kuanzia saa 10:00 jioni.


Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani, kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na 17, 2018.

TAA Waomboleza Kifo cha Mwanasheria Delfine

Bi. Delfine Mulogo wakati wa uhai wake.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), inamlilia kwa masikitiko makubwa Mwanasheria wake Bi. Delfine Mulogo (32) aliyekuwa Kituo cha kazi cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) aliyefariki dunia Desemba 25.

Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Bw. Mtengela Hanga akisoma wasifu wa marehemu katika kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine Mbezi Temboni, alisema, atakumbukwa kwa uchapakazi, uhodari na uadilifu wake kazini.

Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine, Padri Fidelis Mfaranyembo lililopo Mbezi Temboni jijini Dar es Salaam, akinyunyizia maji ya baraka kwenye mwili wa aliyekuwa Mwanasheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Delfine Mulogo kabla ya kusafirishwa kwenda Kijiji cha Uru Kishumundu Mkoani Kilimanjaro kwa maziko.

“Tunasikitika kumpoteza mwanasheria huyu kijana, kwa niaba ya Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, tunatoa pole kwa wafiwa kwa kuondokewa na mpendwa wao, lakini sisi kama mamlaka na taifa kwa ujumla tumempoteza mtu muhimu sana aliyekuwa mchapakazi, tutamkumbuka sana marehemu,” alisema Bw. Hanga.

Marehemu ambaye ameacha mume Bw. Alex Temba na watoto wawili, Faith (9) na Harieth (4) alihamishiwa TAA tarehe 01/04/2016 akitokea Halmashauri ya Manispaa ya mji wa Songea alipokuwa akifanya kazi kama mwanasheria kuanzia mwaka 2012.
Bw. Alex Temba (wa pili kushoto), mume wa marehemu aliyekuwa Mwanasheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Delfine Mulogo akiwa na binti yake Faith Temba (mwenye gauni jeupe) wakitoa heshima za mwisho katika kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine lililopo Mbezi Temboni kabla ya kusafirishwa kwa mazishi katika Kijiji cha Uru Kishumundu mkoani Kilimanjaro. 
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Bw. Stephen Msechu alisema marehemu alikuwa mwanachama tangu alipoapishwa kuwa Wakili mwaka 2012 na kupewa namba ya uanachama 3361 na amekuwa akishirikiana nao katika shughuli mbalimbali kwa uadilifu mkubwa.

Hata hivyo, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine lililopo Mbezi Temboni, Padri Fidelis Mfaranyembo aliwataka waombolezaji waliofika kuuaga mwili wa marehemu  Delfine kujiandaa wakati wote kwa kuwa hawajui siku wala saa watakayotwaliwa.

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Lawrence Thobias akitoa heshima zake kwa mwili wa aliyekuwa Mwanasheria Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Delfine Mulogo aliyefariki Desemba 25. Marehemu atazikwa Kijiji cha Uru Kishumundu mkoani Kilimanjaro.
Padri Mfaranyembo alisema pia waombolezaji wahakikishe wanakuwa watu wa sala wakati wote ili kumuombea marehemu aweze kupokelewa na aingie katika ufalme wa mbinguni, kwani ufalme huo upo kwa kuwa kunamaisha baada ya kifo.

“Kuna mwanafalsafa mmoja wa zamani, Plato alitafakari  sana kuwa mwanadamu akifa anakwenda wapi? na akaona kila mwanadamu anabeba roho ya muumbaji  na hivyo unapokufa roho inarudi kwa yule aliyeiumba, "alisema na kuongeza:

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Bi. Agnes Kijazi akimpa pole Bw. Alex Temba kufuatia kifo cha Mkewe Bi. Delfine Mulogo aliyekuwa Mwanasheria kwenye Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) aliyefariki Desemba 25 na atazikwa Kijiji cha Uru Kishumundu mkoani Kilimanjaro.
" Plato anatufundisha ya kwamba mwisho wa maisha yake hapa duniani Mwanadamu anarudi kwa Mungu wake kulingana na namna alivyokuwa akiishi na wengine hapa duniani,” alisema Padri Mfaranyembo.

Pia amemtaka mume wa marehemu Bw. Temba asifadhaike kwa kuondokewa na mkewe, bali ajikabidhi kwa Mungu kwa kumuomba hakika atamsaidia kwa kumtia nguvu na kumpa uwezo wa kuendelea kuwahudumia watoto wake kwa kadri ya uweza wake Mungu.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakijumuika na waombolezaji wengine katika misa ya kumwombea marehemu Bi. Delfine Mulogo aliyekuwa Mwanasheria kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Marehemu alipata elimu ya msingi katika shule ya Oysterbay (1991), baadaye sekondari ya St. Mathew (1998), na baadaye elimu ya Kidato cha Tano na Sita katika shule ya Wasichana ya Kibosho (2004), na mwaka 2008 alihitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini.     
Mweka Hazina wa Klabu ya Uchukuzi, Bw. Benjamin Bikulamchi (kulia), akimkabidhi rambirambi aliyewahi kuwa Katibu wa Klabu hiyo, Bw. Alex Temba aliyefiwa na mkewe Bi. Delfine Mulogo aliyekuwa Mwanasheria Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Viongozi wa Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Bi. Itika Mwankenja na Bi. Joyce Benjamin wakitoa rambirambi zao kwa Katibu Msaidizi wa shirikisho hilo Bw. Alex Temba (kushoto) aliyefiwa na Mkewe Bi. Delfine Mulogo wakati wa misa ya kumwombea marehemu iliyofanyika jana katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine lililopo Mbezi Temboni.
Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa Jina Lake Lihimidiwe.  Amina.

Monday 25 December 2017

Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania yakutana JNIA katika kikao cha kawaida


 Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) katika kikao cha kawaida cha 33 cha kujadili masuala mbalimbali ya utendaji ya mamlaka kwa kipindi cha robo ya kwanza na pili ya mwaka wa fedha 2017/2018.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kulia) akimweleza jambo Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya mamlaka hiyo, Prof. Mhandisi Ninatubu Lema (katikati),  katika kikao cha 33 cha Kawaida cha kujadili robo ya kwanza na pili ya mwaka wa fedha 2017/2018 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, wakiwa katika kikao cha kawaida cha 33 cha kujadili masuala mbalimbali ya utendaji kwa kipindi cha robo ya kwanza na pili ya mwaka wa fedha 2017/2018 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Mjumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Dr. Frederick Mwakibinga (kushoto) akizungumza jambo kwenye kikao cha 33 cha bodi hiyo cha kujadili robo ya kwanza na pili ya mwaka wa fedha 2017/2018, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). 

Mkombozi arudi SHIMIWI kwa kishindo

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja (kulia) akimpongeza Alex Temba mara baada ya uchaguzi wa Shirikisho la Michezo la Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI), uliofanyika hivi karibuni kwenye hoteli ya Mount Uluguru mkoani Morogoro.
 Na Mwandishi Wetu

MWEKA Hazina, William Mkombozi ‘Mgosi’ amerudi kwa kishindo katika nafasi hiyo baada ya kushinda kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Michezo kwa Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI), uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa hoteli ya Mount Uluguru mkoani Morogoro.

Mkombozi aliyewahi kuongoza katika miaka ya mwanzoni ya 2000 akiwa na aliyewahi kuwa mjumbe na baadaye Katibu Mkuu, Bw. Ramadhani Sululu, lakini baadaye alikaa pembeni sasa amechaguliwa tena kwa kura 23.

Naye Alex Temba aliyeongoza kwa muda mrefu katika Klabu yenye wachezaji mahiri ya Uchukuzi, alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi baada ya kushinda kwa kura 28 na kumbwaga Margreth Mtaki aliyepata kura 15.

Hatahivyo, nafasi ya Mwenyekiti ilirudi tena kwa Daniel Mwalusamba aliyekuwa hana mpinzani kwa kupata kura 42;  huku Ally Katembo akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kura 41; wakati Moshi Makuka ametetea nafasi yake ya Ukatibu kwa kura 38 dhidi ya Andrew Sekimweri aliyeondoka na kura sita.

Katika nafasi ya Mweka Hazina Msaidizi, ameshinda Frank Kibona kwa kura 21; wakati walioshinda kwenye ujumbe wa kamati ya utendaji na kura zao zikiwa kwenye mabano ni Apolo Kayungi (44), Assumpta Mwilanga (42), Aloyce Ngonyani (40), Damiani Manembe (39)  na Seleman Kifyoga (31).

Kwa upande wa nafasi ya viti maalum wanawake walioshinda ni Mwajuma Kisengo (20) na Mariam Kihange (18) na waliwashindwa ni Costance Momadi (16) na Buya Masunga (12).


Michezo ya SHIMIWI inayoshirikisha wafanyakazi wa mashirika ya umma imepoteza mvuto kwa kutofanyika takribani miaka miwili mfululizo kutokana na sababu mbalimbali zilizokuwa zikielezwa na uongozi wa juu.

Hatahivyo, kutofanyika kwa michezo hiyo kumewanyima haki watumishi wa umma kushindwa kujenga afya zao na kudumisha umoja na urafiki ikiwa ni pamoja na kukutana na watumishi wengine mbalimbali wa Idara na Wizara nyingine wakati wa michezo hiyo.

Mbali na kutofanyika kwa michezo hiyo pia kumekuwa hakuna mabonanza ya kushirikisha idara za serikali na wizara kwa muda mrefu, ambapo tayari Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika kwa mazoezi ya viungo angalau mara moja kila mwezi ili kujenga afya kwa watumishi wa umma.


 

Kifimbo cha Malkia chatua Brisbane, Australia

Mbio za Kifimbo cha Malkia wa Uingereza zilianza Machi 13 mwaka huu.

BRISBANE, Australia

BAADA ya kuanza safari yake kutoka Buckingham Palace Machi 13 mwaka huu jijini London, Kifimbo cha Malkia hatimaye kimewasili kwa waandaaji wa Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia leo na sasa kinaelekea katika mji wa Gold Coast.

Kifimbo hicho kiliwasili jijini hapa asubuhi ya leo baada ya kusafiri kwa takribani siku 288 na kutembelea mataifa yote ya Jumuiya ya Madola.

Leo ambayo ni siku ya Krismas inabakisha siku 100 kamili kabla ya kuanza kwa michezo hiyo ya 21 tangu kuanza kufanyika kwake.

Balozi wa Gold Coast 2018 na muogeleaji Mcameroon McEvoy alipokea kifimbo hicho kutoka kwa Hugh Graham, ambaye ni makamu wa rais wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa Kanda ya Oceania, kufuatia kuwasili kutoka New Zealand.


Umati mkubwa wa watu akiwemo Borobi, walikusanyika kumuona McEvoy akibeba Kifimbo katika ukumbi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Brisbane, asubuhi ya pilika pilika nyingi katika mwaka.

Serikari yawakoromea Maofisa Michezo, Utamaduni

Na Mwandishi Wetu, Karatu


SERIKALI imesema kuwa maofisa michezo na wale wa utamaduni hawafanyi kazi zao vizuri na ndio maana kumeshindwa kuvumbuliwa vipaji vipya na kusababisha wachezaji wale wale kushiriki katika mashindano mara kwa mara.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifunga tamasha la 16 la Michezo na Utamaduni la Karatu kwenye viwanja vya Mazingira Bora hapa.

Shonza alisema kuwa maofisa michezo na utamaduni wengi wao wamekuwa wakipokea mishahara bure, kwani wameshindwa kufanya kazi zao za kusaidia kuibua vipaji kama wanavyofanya wenzao wa Karatu kupitia tamasha hilo.

Alisema maofisa hao wanatakiwa kwenda chini hatua ya vijiji ili kuibua vipaji na kuviendeleza tofauti na wengi wao, ambao wanapokea mishahara bure bila ya kufanya kazi yoyote.

Aliongeza kusema kuwa ndio maana vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na shughuli zisizofaha kama uvutaji wa bangi, matumizi ya dawa za kulevya na wizi kutokana na kutoshirikishwa katika michezo, hivyo aliwataka maofisa hao kufanya kazi zao vizuri.

Pia aliwataka viongozi wa wilaya ya Karatu kuhakikisha wilayani kwao kuna kiwanja kikubwa cha michezo ili kuwawezesha vijana kutumia kiwanja hicho kuendeleza vipaji vyao.

Alisema ni aibu kubwa kuona wilaya ya Karatu pamoja na vipaji vya michezo vilivypo hakuna uwanja wa maana wa michezo, hivyo aliwataka kukijenga au kuwapokonya wale waliovamia maeneo ya wazi.


Tuesday 19 December 2017

Kocha, Wakala wa Gatlin katika Kashfa ya doping

NEW YORK, Marekani
BINGWA wa dunia wa mbio fupi Justin Gatlin (pichani) anasema kuwa `ameshtushwa na kushangazwa’ na madai ya dawa za kuongeza nguvu zilizotolewa dhidi ya kocha na wakala wake.

Viongozi wa riadha na Taasisi ya Kupambana na Dawa za Kuongeza Nguvu Michezoni wameanza uchunguzi kile ambacho Rais wa mchezo huo duniani ameyaita  ‘madai mazito’ kuhusu Dennis Mitchell na Robert Wagner.

Gazeti la The Daily Telegraph liliandika Wagner – wakala anayehusiana na Gatlin – alitoa dawa hizo zilizopigwa marufuku kwa waandishi wa habari ambao hawakujulikana.

Mkanda wa video uliotolewa na Telegraph unamuonesha mtu ambaye gazeti hilo limesema ni Wagner alimshauri Gatlin kutumia dawa hizo zilizopigwa marufuku, kama vile wanariadha wengine wa mbio fupi wa Marekani.

Gazeti hilo limesema kuwa kocha wa Gatlin, ambaye ni bingwa wa medali ya dhahabu wa Olimpiki Mitchell, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanariadha wanaweza kukwepa kubainika kutumia dawa hizo kwa sababu vipimo vinashindwa kubaini dawa hizo walizotumia.

WOTE WAKANA TUHUMA
Akiandika katika Instagram jana, Gatlin alisema kuwa “atamtimua mara moja” Mitchell "mara nitakapobaini ukweli kuhusu tuhuma hizi ".

Mwanariadha huyo Mmarekani mwenye umri wa miaka 35 alisema “hatumii na hajawahi kutumia” dawa hizo za kusisimua misuli.

Aliongeza: "Suala hilo tayari ameanza kulishughulikia kisheria ili kuhakikisha hakuna watu wengine wanatoa taarifa za uongo kama hizi kuhusu mimi.”

The Telegraph limesema waandishi wa habari ndio walimpeleka wawakilishi wa kampuni ya filamu, ambaye alijifanya kama kocha amabaye anamfundisha kocha mwanariadha wake kuwa nyota.

Taasisi mbalimbali ikiwemo Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) pamoja na Chama cha Maadili, na Taasisi ya Kuzuia Matumizi ya Dawa za Kuongeza Nguvu ya Marekani (Usada) zilisema zimeanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo.

Rais wa IAAF Lord Coe alisema: "Tuhuma hizi ni kubwa sana na ninajua Kamati Huru ya Maadili ya Riadha itachunguza kwa kina kuhusu tuhuma hizo…”


Gatlin, ambaye alitumikia mara mbili vifungo baada ya kubainika kutuia dawa hizo, alishinda medali ya dhahabu katika mbio za meta 100 katika mashindano ya riadha ya Dunia mwezi Agosti jijini London, akimshinda Usain Bolt katika mchezo wa mwisho wa meta 100 kwa Mjamaica huyo kabla hajastaafu kucheza mbio.

Real Ikifungwa na Barcelona ndio basi tena La Liga


MADRID, Hispania
KLABU ya Real Madrid endapo itafungwa katika mchzo wao wa El Classico dhidi ya Barcelona, basi itakuwa imetupwa nje ya mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania ya La Liga kagika mchezo utakaofanyika wikiendi hii.
Endapo itashinda, na ikifuatiwa na ushindi mwingine  kutaiwezesha timu hiyo kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Barcelona na kuwa  pointi tano kabla ya mapumziko ya kipindi cha baridi na kukipa kikosi cha  Zinedine Zidane nafasi ya kupambana.
Mpambano huo wa El Clasico kwa timu hizo kupambana katika mpmbano wa La Liga ni wa kwanza tangu Aprili.
Tangu walipofugwa na Real Madrid katika mchezo wa Supercopa de Espana katika kipindi cha majira ya joto. Barca wametamba zaidi dhidi ya wapinzani wao.

TAARIFA ZA TIMU
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez anatazamia Gareth Bale atacheza kufuatia kufanya vvizuri katika Kombe la Klabu Duniani.

Na Cristiano Ronaldo anataka Bale kucheza katika nafasi ya Isco kutokana na kutoelewana na Muhispania huyo wa Kimataifa.

Majeruhi Paco Alcacer hatakueemo katika kikosi cha Barcelona licha ya kufanya kazi nzuri msimu huu katika klabu hiyo, baada ya kufunga mabao yote katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Sevilla.

HISTORIA YA MECHI ZAO

Mchezo huo wa Jumapili utakuwa ni wa 236 wa kiushindani kukutana timu hizo zenye upinzani wa hali ya juu katika soka.

Zawadi Zaongezwa Tamasha la Karatu 2017

Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa tamasha la kila mwaka la michezo na Utamaduni la Karatu wameongeza zawadi kwa washindi watatu wa kwanza wa michezo yote itakayoshindaniwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo Meta Petro, bingwa wa mwaka huu wa mbio za kilometa 10 kwa wanaume ataondoka na kitita cha sh 500,000 huku mshindi wa pili akipata sh 300,000 wakati watatu ataondoka na sh 250,000.

Zawadi kama hizo pia zitatolewa kwa washindi wa kwanza hadi watatu wa mbio za wanawake za kilometa tano, huku watoto wadogo, ambao watashiriki mbio za kilometa 2.5, wenyewe mwaka huu mshindi wa kwanza, ataondoka na sh 100,000 badala ya 50,000.

Mbali na riadha, pia zawadi kwa washindi wa mbio za baiskeli ambazo zitawashindanisha wanaume katika umbali wa kilometa 60 na wanawake 30, nao mwaka huu wameongezewa zawadi.

Mbali na mbio na baiskeli, pia tamasha hilo linashirikisha mchezo wa soka, mpira wa wavu, kwaya pamoja na ngoma za utamaduni na sarakasi.

Alisema kuwa tamasha la mwaka huu linatarajia kuvuta washiriki wengi baada ya klabu kibao na wanariadha binafsi na wapanda baiskeli kujisajili kwa wingi kwa ajili ya kushiriki michezo hiyo.

Baadhi ya klabu za riadha ambazo zimethibitisha kushiriki tamasha hilo ni pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),ambayo itakuwa na zaidi ya wanariadha 25, Magereza Arusha yenye anariadha 20, Jambo Athletics Club, Ketra zote za Arusha, Lingwa ya Singida na Lyan ya Mbulu.

Mbali na riadha, Petro alizitaja klabu za baiskeli zilizothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Lake Manyara Cycling Club ya Manyara, Hakika ya Arusha , Klabu ya Baiskeli ya Magugu na Arusha Cycling Club kutoka mkoani humo.

Mbali na riadha na baiskeli, tamasha hilo pia litakuwa na mpira wa wavu pamoja na soka, ambazo fainali zake zitafanyika Desemba 22 ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo, ambalo linatarajia kufungwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe.


Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) kwa kushirikiana na TOC, Chama cha Riadha Karatu na kudhaminiwa na Olympic Solidarity,limekuwa chachu ya kuibua vipaji hasa katika mchezo wa riadha.