Tuesday, 24 November 2015

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuendelea kushirikiana na jamii iliyojirani na viwanja vyake

Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Ramadhan Maleta akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi Mkuu wa TAA wakati wa mahafali ya shule ya sekondari ya Louis Montfort iliyoko Yombo Buza jijini Dar es Salaam hivi karibuni. 
 Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Ramadhan Maleta (kushoto) akimkabidhi zawadi mwanafunzi bora kielimu wa kidato cha nne wa shule ya Louis Montfort, Emmy Mduma wakati wa mahafali ya nne ya shule hiyo iliyopo Yombo, Buza jijini Dar es Salaam.
Mwanafunzi bora kitaaluma katika shule ya sekondari ya Louis Montfort, Emmy Mduma akipokea cheti kutoka kwa Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Ramadhan Maleta wakati wa mahafali ya shule hiyo iliyopo Yombo, Buza jijini Dar es Salaam.

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam `Terminal 3' unavyoendelea kwa kasi

 Baadhi ya waandisi walivyotembelea Uwanja wa ndege wa Terminal 3 jijini Dar es SalaamWaandishi nao walitembelea uwanja huo kujionea maendeleo ya ujenzi, ambao umekamilika kwa zaidi ya asilimia 60.

Monday, 9 November 2015

Buriani bingwa wa Jumuiya ya Madola Michael YombayombaBondia Michael Yombayomba wakati wa uhai wake.


Na Mwandishi Wetu
BONDIA wazamani wa ndondi wa ridhaa nchini, Michael Yombayomba amefariki dunia jana asubuhi katika hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani baada ya kuugua tumbo, imeelezwa.

Baba Mdogo wa bondia huyo, David Yombayomba alisema leo kuwa mtoto wao huyo alilazwa Tumbi kutokana na tatizo ya tumbo kujaa gesi na kutapika kila anapokula chakula kabla kifo hakijamtuka.

Alisema kuwa  mazishi ya bondia huyo wazamani ambaye ni bingwa wa Jumuiya ya Madola wa uzito wa bantam, yatafanyika kesho Jumanne Kibaha mkoani Pwani.

Yombayomba ni bondia pekee wa Tanzania hadi sasa aliyewahi kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1998, alifariki juzi katika hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani, baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa tumbo.

Kwa miaka mingi, Tanzania ilikuwa ikirejea na medali kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, lakini ikiwa ni katika mchezo wa riadha huku ndondi na michezo mingine wakirejea mikono mitupu hadi pale Yombayomba alivyofanya kweli.

Yombayomba alitwaa medali hiyo akiwa chini ya kocha mkongwe na wa muda mrefu wa ndondi hapa nchini Locken Swai ndiye alikuwa kocha wake bondia huyo alipokuwa akitwaa medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola Kuala Lumpur, Malaysia mwaka 1998.

Faida ya Medali:
Yombayomba alitwaa ubingwa huo wa bantam na mara aliporejea nchini aliyekuwa Mkuu wa Polisi  (IGP), Omary Mahita alimpandisha cheo kutoka askari polisi wa kawaida hadi kuwa na sajini (V3).

Yombayomba baada ya kuwa sajeni wa jeshi hilo, alibadilika na mara kwa mara akiwa katika sare za kazi alikuwa akishika kifimbo mkononi.

Baada ya muda alihamishwa kutoka katika Jeshi la Polisi na kupelekwa katika kikosi cha Kuzuia Ghasia Ukonga, ambako hakudumu sana kabla ya kufukuzwa kazi.

Michael Yombayomba (kushoto) akivishwa glovu na kocha Timothy Kingu kabla ya bondia huyo hajaanza mazoezi katika ukumbi wa Mlimani Park jirani na Mlimani city miaka kadhaa iliyopita.
Hakufaidi Usajini
Yombayomba alidumu na cheo hicho kwa miaka mitatu tu kabla hajafukuzwa kazi.

Hatahivyo, baada ya kufukuzwa kazi kwa bondia huyo kulikuwa na maneno mengi huku baadhi wakidai kuwa hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kuwa mlevi wa kupindukia na wengine wakidai ni utoro katika kambi ya taifa kwa ajili ya maandalizi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika London 2002.

Yombayomba alikuwa hafichi unapozungumza naye kwani alikuwa akitupa lawama kwa kocha wake wakati huo (jina tunalihifadhi), kuwa alishindwa kumtetea wakati yeye ndiye aliyempa ruhusa ya kwenda kuaga familia yake kabla ya kwenda London.

David Yombayomba; Baba Mdogo wa Michael.
Inaelezwa kuwa wakati wa kambi hiyo ya Jumuiya ya Madola, viongozi wa Kamati ya Olimpiki (TOC) wakati huo walitembelea kambi na hawakumkuta Yombayomba, na walipouliza kocha akasema hayupo na wala hajui aliko.

Baada ya kutimuliwa ndipo mabosi wake nao wakajuu wakimtaka bondia huyo kueleza sababu za kutoroka kambini.

“Baada ya vyombo vya habari kuandika habari hizo za utoro, bosi wangu aliamuru nifunguliwe mashtaka na baadae nikatimuliwa kazi, lakini kwa chuki za kocha huyo ambaye hakupenda mimi niwepo katika timu hiyo, ambayo nilitarajia kwenda kutetea ubingwa wangu wa Jumuiya ya Madola, “alisema na kuongeza:
  “Huyo kocha alikuwa na chuki zake binafsi kwani alijua nikiendelea kuwepo katika kambi hiyo atashindwa kufanya maovu yake akaamua kunizushia uongo ili niondolewe katika timu na bahati mbaya nikafukuzwa na kazi, “anasema Yomba Yomba.

Medali  ya Dhahabu:
Katika hostori ya ndondi za ridhaa Tanzania hakuna bondia yeyote aliyewahi kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, isipokuwa Yombayomba peke yake.
 
Katika kipindi chote cha zaidi ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, katika ndondi za ridhaa hakuna bondia kama huyo aliyewahi kutwaa medali ya dhahabu katika michezo mikubwa kama hiyo ya Jumuiya ya Madola.
 
Mabondia wengine wa Tanzania tangu ilipokuwa Tanganyika kabla ya kuungana na Zanzibar kama akina Rashind Matumla, Haji Matumla, Makoye Isangura, Titus Simba (marehemu),  na wengineo, waliwahi kutamba katika michezo kama ile ya Mataifa ya Afrika, Afrika na Afrika Mashariki, lakini sio ile ya Jumuiya ya Madola.
 
Kiujumla, Yombayomba ni bondia aliyepata mafanikio zaidi kwa kipindi chote miongoni mwa mabondia wa Tanzania kutokana na kufikia hatua hiyo.

Sasa ni miaka 17 tangu alipotwaa medali hiyo nchini Malaysia.


Wanavyomzungumzia:
Kocha Swai anasema kuwa Yombayomba alikuwa bondia mwenye kipaji cha hali ya juu na alitumia vizuri mkono wake wa kushoto (northpole) kuwachakaza wapinzani wake.

Kocha huyo anasema kuwa mara nyingi mabondia wanaotumia mkono wa kushoto wako wachache na huchezaji wao ni tofauti kabisa na wale wanaotumia mkono wa kulia.

Anasema kuwa, bondia huyo alikuwa mjanja na aliweza kuwasambaratisha wapinzani wake.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT), Makore Mashaga anasema wamempoteza shujaa wa ndondi ambaye bado mabondia chipukizi walikuwa wakihitaji mawazo na ushauri wake katika kupiga hatua katika mchezo huo.

Anasema BFT wako pamoja na familia ya Yombayomba katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.

Kocha wa timu ya taifa, Jonas Mwakipesile alisema kuwa Yombayomba alikuwa bondia mzuri wakati akicheza na rekodi yake itakumbukwa daima.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya BFT, ambaye ni bondia wazamani Anthony Mwang’onda alisema itachukua muda mrefu kwa mabondia wasasa kufikia rekodi ya Yombayomba.

Yombayomba mbali ana kupata cheo hicho, hata kazi ya upolisi aliipata baada ya kutwaa ubingwa wa taifa katika mashindano ya taifa yaliyofanyika Arusha mwaka 2002.

Bondia huyo alitwaa medali ya dhahabu ya uzito wa bantam baada ya kumchapa Mcameroon, Herman Ngoudjo kwa jumla ya pointi 19-13 na kuitoa Tanzania kimasomaso.

Yombayomba ameacha mke na watoto wawili, Scola na Zacharia.

Mungu ailaze roho ya marehemu Michael Yombayomba mahali pema peponi. Amina.