Wednesday 11 March 2015

Wanafunzi Zanzibar kuchuana mbio za nyika Machi 28


Wanafunzi wa shule za msingi wakichuana hii karibuni.

Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya mbio za nyika kwa shule za msingi na sekondari za Zanzibar yatafanyika kisiwani humo Machi 28 mwaka huu na kushirikisha zaidi ya wanafunzi 500.

Mratibu wa mbio hizo ambazo hufanyika kila mwaka Mussa Abdurabi amesema leo kwa njia ya simu kutoka Zanzibar kuwa, maandalizi yanaendelea vizuri kwa ajili ya mbio hizo.

Amesema kuwa hadi sasa tayari shule 29 kutoka Unguja na Pemba zimethibitisha kushiriki na ni matarajio yake kuwa shule zaidi zitathibitisha kwani muda bado unaruhusu.

Amesema kuwa kila shule itapeleka wachezaji 12, sita wavulana na wasichana idadi kama hiyo, ambao watashiriki katika
mbio hizo za umbali tofauti.

Akifafanua zaidi Abdulab amesema kuwa hadi sasa shule za sekondari zilizothibitisha kushiriki ni 10 wakati za msingi ziko 19.
 
Ameongeza kusema kuwa mbio za kilometa nane zitawashirikisha wavulana wa sekondari wakati zile za kilometa sita zitashirikisha wasichana wa sekondari na wavulana wa shule za msingi.

Abdurab ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) amesema kuwa, mbio za kilometa nne zitashirikisha wavulana wa sekondari na wasichana wa shule za msingi pekee.

Amezitaka shule zilizothibitisha kushiriki kujiandaa vizuri ili kutoa ushindani wa ukweli katika mashindano hayo na kufikia malengo ya kuibua na kuiendeleza vipaji.

Anasema kuwa Idara ya Michezo na Utamaduni moja ya majukumu yake ni kuandaa vijana, kuibua vipaji na kuziendeleza, hivyo siku hiyo ya mbio pia kutakuwa na mchezo wa soka kwa ajili ya kusaka na kuinua vipaji.

No comments:

Post a Comment