Tuesday 24 March 2020

Makonda apongeza TAA kwa kujidhatiti kwa corona

·       Ataka wananchi kufuata masharti yaliyotolewa
·       Asema kuanzia kesho mitaa kupuliziwa dawa
 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akipimwa joto alipotembelea Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam (JNIA). 
Na Bahati Mollel,TAA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kujipanga vyema kwa kushirikiana na wahudumu wa afya kwa kuweka maji yenye dawa maalum ya kunawa mikono na kupima joto la mwili kwa watu wote wanaoingia na kutoka maeneo ya viwanja vya ndege, ili kuzuia kuingia zaidi kwa watu walioambukizwa ugonjwa wa homa kali ya Mapafu inayosambazwa na virusi vya corona (COVID19).

RC Makonda ametoa pongezi hizo leo alipofanya ziara kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, ambapo alianzia jengo la Tatu la abiria ambalo linahusisha zaidi ndege zinazotoka nje ya nchi, na baadaye kwenda Jengo la Pili la abiria lenye ndege zenye safari za ndani ya nchi na pia nje ya nchi.

Amesema ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na TAA kwa kuhakikisha hakuna ongezeko la watu walioambukizwa wanaoweza kuingia nchini kupitia Kiwanja hiki.

“Nimejionea mwenyewe kila kona kumewekwa sanitizers, na pale nje lipo tanki kubwa lenye maji yenye dawa lazima kila mtu anawe, na hata huku ndani abiria wanaowasili na wanaoondoka wanapimwa joto la mwili kwa mashine ya mkono na ile ya scanner, hivyo ninaimani kwa udhibiti huu hakuna maambukizi zaidi yanayoweza kutokea,” amesema Mhe. Makonda.

Hatahivyo, amesema pia kuanzia tarehe 25 Machi, 2020 asilimia 98 ya ndege zenye safari za nje hazitaingia nchini baada ya zenyewe kufuta safari zao kutokana na kukosekana kwa abiria, hivyo itasaidia kwa asilimia 80 ya abiria kupungua kuingia kwa kuwa ni nchi nyingi zimeweka makatazo na kufunga mipaka yao.

“Sisi hatujafunga mipaka lakini hadi sasa idadi ya abiria wakigeni imeshuka kwa kiasi kikubwa mfano ndege yenye kubeba abiria 250 sasa inabeba abiria 20, hivyo asilimia 80 ya abiria aidha wenyewe kutokana na elimu waliyopata kutokana na huu ugonjwa wameona hakuna sababu ya kusafiri na wengine baada ya kuona masharti yaliyowekwa ya kwenda nchi moja ama nyingine wakaamua kukaa majumbani mwao, na hii inadhihirisha jinsi gani Mhe. Rais John Pombe Magufuli aliposema kuwa kama unaona safari haina ulazima basi usiende,” amesisitiza Mhe. Makonda.

Pia amesema mashirika ya ndege yamekuwa na ushirikiano na JNIA kwa kutoa taarifa kabla ya kutua endapo wanaabiria mwenye kuhisiwa anaugua ugonjwa huo, na ikifika taratibu za kumpeleka katika kituo kilichoteuliwa zinachukuliwa.

“Tunashukuru sana tena na tena hapa JNIA wamesema hata idadi ya wasindikizaji imepunguzwa ili kuondoa kabisa msongamano katika majengo ya abiria, maana wakiwa wengi itakuwa shida zaidi endapo yupo ambaye anamaambukizi,” amesema.

Pia amesema kwa sasa abiria wote wanaowasili kutoka kwenye nchi zilizokuwa na maambukizi wanapekelekwa kwenye hoteli na hosteli zilizoteuliwa na mkoa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa siku 14 kwa gharama zao wenyewe. Katika hatua nyingine amesema leo abiria 200 wa nchi ya Comoro wamezuiwa kuondoka baada ya nchi yao kufunga mpaka kutokana na kuzuia maambukizi ya corona.

Pia amewataka watu wote wanaoingia na kutoka nchini kwa kutumia usafiri wa ndege, mabasi na meli kufuata utaratibu uliowekwa na Mamlaka za juu ili kuepukana na maambukizi, ambapo pia amesema katika usafiri wa umma (Daladala) watu wasipande likiwa limejaa kupita kiasi na amesisitiza kuwa ugonjwa huu hauna umri kuwa vijana hawafi,  hivyo wanajidanganya na wachukue tahadhari zilizowekwa.

Hali kadhalika amesema wananchi na watu wote kutokuwa na hofu kuanzia kesho Jumatano tarehe 25 Machi, 2020, Ofisi yake kwa kushirikiana na Maafisa Afya watapulizia dawa kwenye mitaa ili kuua wadudu mbalimbali; na ofisi yake itaendelea kutoa elimu ya kujikinga na maradhi ya corona.

Naye Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha amesema wameendelea kutoa elimu kwa watu wote wanaoingia na kutoka kwenye kiwanja hicho kwa kuweka mabango yanayoelekeza namna ya kujikinga, na pia wameweka sabuni maalum za kunawa mikono wanapoingia na kutoka maeneo hayo.
  

No comments:

Post a Comment