Wednesday, 23 August 2017

Viwanja vinne vya ndege kuwekewa rada za kisasa

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akisikiliza wataalam alipotembelea jengo la Tower kabla ya kuingia mkataba wa ufungaji wa Rada nne katika viwanja vya ndege nchini. Mwenye tai nyekundu Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Salim Msangi.Thursday, 17 August 2017

JKT yawapongeza wanariadha wake walioshiriki mashindano ya dunia London na kurudi na medali

Wanariadha wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki mashindano ya dunia ya riadha kutoka kushoto ni Alphonce Simbu, Magdalena shauri, Emmanuel Giniki na Stehano Huche wakati wa hafla ya kuwapongeza iliyofanyika Makao Makuu ya JKT Mlalakua leo.
Na Mwandishi Wetu
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limesema kuwa baada ya mwanariadha Alphonce Simbu kurejea na medali kutoka katika mashindano ya 16 ya riadha ya dunia London, Uingereza, wakati umefika kwa wadau kuangalia na michezo mingine ili kulitangaza taifa zaidi.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kumpongeza mwanariadha Simbu aliyetwaa medali ya shaba katika mashindano hayo ya dunia kwa upande wa marathoni na wenzake.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali, Michael Isamuhyo akipokea saluti kutoka kwa Serviceman, Alphonce Simbu.
Tanzania katika mashindano hayo ilipeleka wanariadha nane, wanne akiwemo Simbu ni waajiriwa wa JKT. Wengine ni Magdalena Shauri, Stephano Huche na Emmanuel Giniki, ambao nao walikuwemo katika hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo Mlalakua jijini Dar es Salaam.
Isamuhyo alisema kuwa wakati umefika kuangalia na michezo mingine kama ngumi, mpira wa wavu, kuogelea, netiboli na mingine ili nayo iweze kufanya vizuri na kusaidia kuitangaza nchi nje ya mipaka yake.
Hatahivyo, mkuu huyo alisisitiza kuwa Desemba jeshi lake litaongeza wanariadha ili kuhakikisha wanakuwa wengi na kuongeza changamoto katika kambi ya timu hiyo.

Alisema kuwa ana matumaini makubwa kuwa wanariadha hao pamoja na wengine wa Tanzania watafanya vizuri katika mashindano makubwa yajayo.
Aliongeza kuwa wadau wote washirikiane na kuondoa migongano isiyo ya lazima na JKT wako tayari kuwatoa wanariadha hao wakati wowote ili mradi watumike vizuri kwa ajili ya maslahi ya kitaiffa na sio binafsi.
Mkuu wa JKT, Meja Generali, Michael Isamuhyo akisalimiana na mwakilishi wa MultichoiceTanzania, Johnson Mshana huku Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja akishuhudia leo Mlalakua jijini Dar es Salaam.
Johnson Mshana akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Multichoice-Tanzania, Maharage Chande alisema kuwa watakaa na Simbu ili kujadili mkataba mpya baada ya ule wa awali mwaka mmoja kumalizika baadae mwezi huu.

DStv iliingia mkataba wa mwaka mmoja, ambapo kila mwezi alikuwa akipewa sh milioni 1 kwa ajili ya kujikimu na mkataba mpya unatarajiwa kuwa mnono zaidi ya huo.

Simbu naye aliishukuru JKT, Multichoice-Tanzania, BMT, Riadha Tanzania (RT) kwa mshirikiano na mshikamano waliouonesha hadi kufanikisha ushindi huo wa Tanzania katika mashindanohayo makubwa, ambao alitaka mshikamano huo kuongezeka.
Naye Katibu wa BMT, Mohamed Kiganja alisema kuwa bila majeshi hakuna mafanikio yoyote katika michezo, kwani majeshi yamekuwa na nidhamu kubwa ya kuwalea wachezaji na kuhakikisha wanafanya vizuri.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alisema kuwa analishukuru jeshi kwa kuwalea wanariadha hao na kutaka kuwachukua na wanariadha wengine ili kuleta changamoto katika timu yao ya riadha.

 

 

Service Girl, Magdalena Shauri akimrekebisha kofia Serviceman Alphonce Simbu wakati wa hafla ya kuwapongeza wanariadha hao na wenzao walioshiriki mashindano ya dunia ya riadha London, Uingereza.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Michael Isamuhyo akisalimiana na mwandishi wa The Citizen, Majuto Omary. Katikati ni Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja.

Wednesday, 16 August 2017

Kaimu Mkurugenzi JNIA akutana na wadau

Wadau mbalimbali wa mashirika ya ndege yanayofanya kazi kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakiandika mambo mbalimbali yaliyokuwa yakisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Johannes Munanka alipokutana nao leo katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TBII
Bw. Iqbal Sajan wa Shirika la Ndege la Auric (aliyesisimama) akichangia hoja kwenye mkutano wa mashirika ya ndege ulioitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka wa kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha huduma.

Monday, 14 August 2017

Simbu na wenzake kupokewa kishujaa kesho JNIA

Na Mwandishi Wetu
MSHINDI wa medali ya shaba wa mashindano ya 16 ya dunia yaliyomalizika jijini London, Uingereza jana, Alphonce Simbu pamoja na wenzake wanatarajia kuwasili kesho mchana na kupokewa kifalme.

Tanzania katika mashindano hayo yaliyoanza Agosti 4 na kumalizika jana, ilipeleka wanariadha wanane lakini Simbu peke yake ndiye aliyetwaa medali katika mbio za marathoni kwa kutumia saa mbili na dakika tisa  katika nafasi ya tatu.

Hiyo ni medali ya kwanza kwa Tanzania kupata baada ya miaka 12 baada ya Christopher Isegwe kumaliza wa pili na kupata medali ya fedha katika mbio za marathoni na kuondoka na medali ya fedha katika mashindano yaliyofanyika Helsinki, Finland mwaka 2005.

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wihlehm Gidabuday amesema leo Jumatatu kuwa Simbu na wenzake wataata mapokezi makubwa watakaowasili kwenye Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) kesho mchana kwa ndege ya Emirates wakitokea London kupitia Dubai.

Mara baada ya kuwasili, timu hiyo itapokewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe na kufanya mkutani na waandishi wa habari katika kiwanja hicho kuelezea yaliyojiri London.

Kwa mujibu wa Gidabuday, nje ya kiwanja hicho kunatarajia kuwepo burudani kadhaa vikiemo vikundi vya JKT vitakavyoburudisha wanariadha hao pamoja na wadau mbalimbali wa michezo na hasa riadha watakaofika kuwaokea akina Simbu.

Inaelezwa kjuwa Simbu anayedhaminiwa na DStv na wachezaji wengine watakuwa ndani ya gari la wazi, ambalo litawazungusha katika kitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam wakipitia Ilala, Kariakoo na kwingineko kabla ya kutua katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay jirani na kanisa la Mtakatifu Petro (St Peter’s), ambako Simbu atapumzika kabla ya keshokutwa kwenda kwao Arusha.

Mbali na Simbu, wanariadha wengine waliokuwemo katika timu hiyo ni pamoja na Stephano Huche, Ezekiel Ngimba, Sarah Ramadhani na Magdalena Shauri (Marathoni), Failuna Abdi (Meta 10,000), Gabriel Geay na Emmanuel Giniki (Meta 5,000).

Geay hakukimbia katika mbio zake kutokana na kuwa majeruhi huku Shauri akishindwa kumaliza baada ya kukimbia kwa zaidi ya kilometa 25 kutokana na kuwa na maumivu aliyokuwa nayo hata kabla ya kuondoka nchini.

Nyota ya Simbu ilianza kung’ara katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rio, Brazil 2016 wakati alipomaliza wa tano kwa kutumia saa 2;11:15 kabla ya kumaliza wa kwanza katika Mumbai Marathoni mwanzoni mwa mwaka huu alipotumia saa 2:09:32,  kabla ya kuboresha zaidi muda wake bora binafsi pale aliomaliza wa tano kwa kutumia saa 2:09:10 katika London Marathoni licha ya kuibuka watano.

Sunday, 13 August 2017

Joshua ndiye mwamba Kilifm Marathoni 2017

 
 
Na Mwandishi Wetu, Moshi
Josephat Joshua ndiye mshindi wa mbio za Kilifm International Marathoni 2017 zilizofanyika jana mjini haa kwa uande wa wanaume baada ya kutumia saa 1:04:18 huku Dickson Marwa akimaliza wa pili.

Marwa wiki iliyopita alimaliza wa kwanza katika mbio za Bagamoyo Marathoni.

Kwa upande wa wanawake, Mkenya Shelmith Muruki alimaliza wa kwanza kwa kutumia saa 1:16:13 huku mshindi wa Bagamoyo Marathon kwa wanawake, Angel John alimaliza wa pili kwa kutumia saa 1:18;34 wakati Zakia Mrisho alimaliza wa tatu kwa kutumia saa 1:19:82.
Akizungumza mara baada ya kumaliza mbio hizo, Muruki alisema kuwa zilikuwa nzuri na aliata ushindani mkali kutoka kwa Angel.

Joshua alishinda mbio hizo baada ya kuonesha jitihada kubwa kwa kumpita mshindano wake aliyekuwa akiongoza kwa muda mrefu, Chacha Musinde ambaye alionekana kama ndiye angeibuka na ushindi , lakini aliishia kuwa watatu akipitwa hata na Marwa aliyekuwa katika nafasi la pili la uongozi.

 Mshindi wa kwanza katika mbio za kilometa 21 kwa wanawake na wanaume kila mmoja aliondoka n ash 700,000 huku wa pili wakibeba 500,000 na watatu 300,000 wakati wanne 200,000 na watano 100,000.


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alikuwa mgeni rasmi na alitoa zawadi na kukabidhi medali kwa washindi 10 wa uande wa kike, ambao alitaka mbio hizo kuendeleza jitihada za kuendeleza viaji kwa watoto wadogo ili kuiwaibua akina Filbert Bayi wapya.

Thursday, 10 August 2017

Liverpool yazidi kuigomea ofa ya Barca

LONDON, England
KLABU ya Liverpool imetupilia mbali ofa ya Barcelona ya pauni milioni 90 kwa ajili ya kutaka kumnunua Mbrazil mchezeshaji Philippe Coutinho.

Hiyo ni ofa ya pili kwa Barca kuiwasilisha katika klabu hiyo kwa ajili ya kutaka kumnyakua mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, ambayo ya awali ilikataliwa haraka.

Ofa hiyo ilikuwa ni ya kiasi cha pauni milioni 76 ikongezewa kiasi cha pauni milioni 13.
Hatahivyo, Liverpool imesisitiza kuwa Coutinho, ambaye alijiunga na timu hiyo kutoka Inter Milan kwa ada ua uhamisho ya pauni milioni 8.5, hauzwi.

Barcelona ilimuuza mchezaji wake wa kutegemewa Neymar kwa Paris St-Germain (PSG) kwa rekodi ya ada ya dunia ya kiasi cha pauni milioni 200 wiki iliyopita.

Coutinho aliyefunga mabao 14 msimu uliopita alikaa nje ya uwanja kwa wiki sita akiuguza maumivu ya kifundo cha mguu, alisaini mkataba wa miaka mitano Januari kuendelea kuichezea Barca.

Dk. Chamuriho, MAB wakagua ujenzi Kiwanja cha Ndege cha Songwe

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard Chamuriho (wa pili kutoka kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), Prof. Ninatubu Lema (wa pili kutoka kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Salim Msangi (wa kwanza kushoto) na wajumbe wengine wa MAB wakisikiliza maelezo yanayohusu jengo la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa Songwe kutoka kwa wahandisi, walipotembelea ujenzi huo leo.
Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Serkta ya Uchukuzi), Dk. Leonard Chamuriho leo kwa kushirikiana na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), wamefanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara ya kutua na kuruka  ndege na jengo la abiria la Kiwanja cha Kimataifa cha Songwe mkoani Mbeya.

Tayari ujenzi wa barabara ya kutua kwa ndege yenye urefu wa km. 3.3 umekamilika, ambapo inaruhusu kutua kwa ndege zenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 90 hadi 300, ambapo ndege za mashirika mbalimbali ikiwemo ya ATCL, Precisions na Fastjet zimekuwa zikifanya safari zake mara kwa mara kwenye kiwanja hicho.
Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Ujenzi ya UNETEC, Roupina Jambazian (aliyenyoosha kidole), akitoa maelezo ya ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege ya Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard Chamuriho na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi.
Kiwanja hicho kipo daraja la sita (category 6), ambapo mbali na ndege za abiria, pia kinaruhusu kutua kwa ndege za mizigo ya mazao ya kilimo yakiwemo maua, matunda, nyama, mchele na maharage kupelekwa maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Hatahivyo, pia kimekuwa njia kuu inayotumiwa na watalii na wageni wanaotembelea mbuga za wanyama za Ruaha na Kitulo, pia katika vivutio vingine kikiwemo Kimondo kipo Mbozi, Daraja la Mungu lipo Rungwe na Ziwa Ngozi lililopo juu ya mlima baada ya shimo la volkano kujaa maji na kugeuka ziwa.

Ujenzi wa jengo hilo la abiria litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka tofauti na jengo la awali linachukua abiria 500,000 pekee, unatarajiwa kumalizika baada ya miezi sita kutoka sasa.
Katibu Mkuu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard Chamuriho (aliyechuchuma) akishika upana wa barabara ya kuruka na kutua ndege ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe baada ya kupata maelezo kutoka kwa Wahandisi Washauri wa Kampuni ya UNETEC. Mhandisi Roupina Jambazian na Geofrey Asumenye (walioinama), baada ya kufanya ziara pamoja na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya ndege (MAB) ya kukagua maendeleo ya ujenzi  wa miundombinu.

Wednesday, 9 August 2017

Naibu Mawaziri wafanya ziara ya mafanikio JNIA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Mtengela Hanga akitoa maelezo mbele ya Naibu Mawaziri watatu walipotembelea Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) . Hafla hiyo ilifanyikia katika Jengo la Kuwasili na Kundokea Abiria Mashuhuri au VIP.
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Mawaziri watatu wamesema kuwa kumalizika kwa Terminal Three ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kitatatua kero zilizopo Terminal Two.

Kaimu Mkurugenzi JNIA, Johannes Munanka
Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lamo Makali wakati akitoa majumuhisho ya ziara yake na wenzake wawili, Hamad Masauni na Edwin Ngonyani wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwenye kiwanja hicho.

Manaibu hao walianza ziara hiyo kwa kutembelea maeneo mbalimbali katika Terminal Two na kukutana na changamoto kibao, zikiwemo kero za msongamano wakati wa hutoaji wa viza kwa abiria wanaowasili.

Kero nyingine ni abiria wanatakiwa kutoka nje ya kiwanja kubadili fedha na kurudi ndani ili kupata huduma katika tawi la benki ya NMB lililopo ndani ya kiwanja hicho ili kulipia viza.

Makani alisema itakapomalizika Termina 3 kero karibu zote zitamalizika kwani jengo la kiwanja hicho linakidhi mahitaji yote muhimu, ambazo ni changamoto katika jengo jingine.

Masauni alisema wizara yake itaongeza askari wa uhamiaji ili kuboresha utendaji kazi kiwanjani hapo, kuongeza idadi ya mashine za viza na kubadilisha mfumo wa utendaji ili kwenda na wakati.

Mhandisi Ngonyani alisema kuwa wanataka kuboresha miundo mbinu, ambapo katika terminal 3 kutakuwa na uboreshaji wa maeneo mengi ili kuwahudumia wasafiri wengi kwa mara moja.

Ngonyani aliishauri Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi kupunguza kutoa viza abiria wanapowasili na badala yake zitolewe katika ofisi za balozi za Tanzania nje ya  nchi kama zifanyavyo nchi zingine ili kupunguza msongamano.
  
Mawaziri hao jana baada ya kumaliza kutembelea JNIA walikwenda katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ziara nyingine.


Terminal Three.
Terminal Two.

Msafara wa Naibu Mawaziri walipotembelea JNIA