Wednesday 25 September 2019

Messi Aumia Barca Ikishinda Kiduchu


BARCELONA, Hispania
LIONEL Messi alipata maumivu wakati akianza kwa mara ya kwanza msimu huu katika mchezo, ambao Barcelona ilipata ushindi kiduchu wa mabao 2-1 dhidi ya Villarreal kwenye Uwanja wa Nou Camp.

Messi, ambaye alikuwa akiponya majeraha ya nyama za paja, alibadilishwa mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kujitonesha tena.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina, alianza mchezo wake wa 400 wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga alipiga mpira wa kona uliomkuta Antoine Griezmann aliyepiga kichwa juu ya mwamba, kabla Arthur hajafunga na kufanya matokeo kuwa 2-0.

Bao la kwanza la Barcelona lilifungwa katika dakika ya sita na Griezmann kabla Santi Cazorla hajaifungia Villarreal bao la kufutia machozi katika dakika ya 44.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Barca Ernesto Valverde alielezea maumivu ya Messi kuwa ni “tatizo dogo”, ambalo halitakawia kupona.

"Wakati kitu chochote kinapotokea kwa Messi, kila kitu kinasimama, sio tu uwanjani, lakini pia hata jukwaani mambo yanasimama, “alisema.

"Kama kuchukua tahadhari tuliamua kutofanya kitu hatari, kinadharia hakuna cha ziada, lakini kesho tutaona nini kinaendelea.”

Ingawa wako mbali na hali yao ya kawaida, kimsimamo Barcelona wamepanda hadi katika nafasi ya nne katika msimamo wa La Liga na kupunguza presha baada ya kuanaza msimu vibaya.

Baada ya maumivu, nahodha huyo wa Barca alipata matibabu nje ya uwanja kabla ya kuendelea hadi mapumziko.

Mshambuliaji huyo nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji Mfaransa wa Ousmane Dembele mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Kwingineko, timu iliyopanda daraja ya Granada ilishika usukani wa La Liga – wakiwa pointi sawa na Athletic Bilbao na Real Madrid – baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Real Valladolid.

Real Madrid jana ilitarajia kucheza dhidi ya Osasuna wakati Bilbao waliopo mkiani watachezaji dhidi ya Leganes.

Mamlaka ya Viwanjaj vya Ndege Yamaliza Kwa Kishindo Maonesho ya Utalii 2019 Mkoani Iringa

  Mhandisi Ibrahim Kibasa (kulia) akipata ufafanuzi kutoka kwa Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisongole (wapili kulia) wakati alipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo, na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ali Hapi Wengine ni Robert Kisongo (kushoto) mkazi wa Iringa na Ofisa Masoko na Biashara wa TAA, Mbura Daniel.
  Wazee wa Kimila wa Mkoa wa Iringa kuanzia kulia Anthony Mbuta, Augustino Mkini na Kassian Ngenz wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), baada ya kutembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka hiyo, yaliyofungwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ali Hapi. Maonesho hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa, 
Mhandisi Astelius John (wa pili kushoto) akimpa maelezo mbalimbali yanayohusu viwanja vya ndege Tanzania vilivyopo chini ya serikali, Wingred Nkoma, wakati alipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la mamlaka hiyo, yaliyofungwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ali Hapi kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa.
    Maumivu Mdegela (mwenye koti) pamoja na watoto wake wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa Afisa Masoko na Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakati walipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini yaliyomalizika Septemba 22, 2019 kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa. Maonesho hayo yamefungwa na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Ali Hapi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ali Hapi  (wa kwanza kulia), pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe Richard Kasesela wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisiongole, wakati walipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Maonesho hayo yalifungwa na Hapi.

JAMAFEST, URITHI WETU WAPANDA MLIMA KILIMANJARO


Wawakilishi wa Matamasha ya JAMAFEST na URITHI FESTIVAL  kutoka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro pamoja na wa Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuanza safari ya SIKU SITA kuelekea Kilele cha Uhuru Kama sehemu ya matukio ya Matamasha hayo yaliyozinduliwa na Makamu wa Rais ,Mama Samia Suluhu Hassan. (Na Mpigapicha Wetu).

Na Mwandishi Wetu, Moshi
WAWAKILISHI wanne kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika matamasha JAMAFEST na URITHI FESTIVAL wanaendelea na safari ya siku sita ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuelekea kilele cha Uhuru ikiwa ni sehemu ya matamasha hayo yaliyozinduliwa Jumapili na Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan.
Wanaopanda Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya matamasha hayo makubwa kwa nchi za Afrika Mashariki ni pamoja na Joel Acana kutoka nchini Uganda, Luca Waiganja kutoka nchini Kenya na Anita Brown wa Tanzania wakiwakilisha tamasha la JAMAFEST huku Jocktan Makeke akiwakilisha tamasha la Urithi Festival.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga washiriki hao, Mwakilishi wa Katibu Mkuu waWizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita alisema chanzo cha tamasha la JAMAFEST ni utekelezaji wa maelekezo ya sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kutaka Malikale na Utamaduni kutumika kama vivutio vya Utalii.
 “Sekretarieti ilizielekeza nchi wanachama  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2012 zihakikishe Malikale na utamaduni unatumika kama kivutio cha utalii ili uweze kutumika katika maendeleo ay nchi za afrika Mashariki,”alisema Mwita.
Alisema baada ya maelekezo hayo, sekretarieti ilianzisha tamasha la Sanaa na Utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki likiwa tayari limefanyika katika majiji matatu; Kigali (Rwanda), Nairobi (Kenya), Kampala (Uganda) na sasa linafanyika Dar es Salaam Tanzania.
Kwa Tanzania, tamasha la JAMAFEST lilizinduliwa Jumapili sambamba na tamasha la URITHI FESTIVAL, tamasha ambalo liko kwenye ngazi ya kitaifa likiwa na maudhui kama ya tamasha la JAMAFEST.
Wakati Jamafest inaunganisha wana Afrika Mashariki na kutumika kama kivutio cha Utalii au zao la utalii, Urithi festival linafanya mambo hayo hayo kwa Tanzania, kamba unaunganisha Watanzania na inatumika kama zao la Utalii.
Mapema mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Victor Kitansi aliwakapongeza waratibu wa matamasha hayo kufanya uamuzi wa kutumia sehemu ya matukio kuwa ni kushiriki kupanda Mlima Kilimanjaro.
Tamasha la JAMAFEST ambalo hufanyika kila baada ya miaka miwili kuzunguka nchi wanachama linafanyika kwa muda wa siku nane huku Tamasha la Urithi Festiva likifanyika katika mikoa 12 ya Tanzania Bara kwa kila mkoa kuionesha kivutio ambacho kitatumika kama zao la Utalii.

Usalama Viwanja Vya Ndege Waimarishwa

Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisongole (kushoto) akifafanua mambo mbalimbali yanayohusu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) walipotembelea maonesho ya Karibu Utalii Kusini, yanayofanyika kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeimarisha usalama kwa abiria, mizigo na wageni kwenye viwanja vyake vyote 58 inavyovisimamia.

Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisongole amesema usalama huo ni pamoja na mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo, ambapo ukaguzi unafanywa kwa umakini na maafisa usalama waliothibitishwa (certified screeners) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

“Tunawakaribisha wageni wa ndani na nje ya nchi kutumia viwanja vyetu vya ndege kwani vina usalama wa uhakika, zikiwemo kamera za usalama, X-ray mashine na ukaguzi mwingine zaidi, ambazo zinafanikisha zoezi zima la usalama,” amesema Mwenisongole.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bahati Mollel akimpa maelezo Hamis Hassan alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka hiyo la Karibu Utalii Kusini yanayofanyika kwenye Viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa.


Mwenisongole amesema pia tunatambua juhudi za serikali ya Awamu ya Tano, iliyopo chini ya Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupitia TAA inampango wa kujenga uzio kwenye kiwanja cha ndege cha Iringa, ambapo zabuni imeshatangazwa ili kupatikana kwa mkandarasi wa ujenzi huo.

Pia amewaita wawekezaji kuwekeza kwenye viwanja vya ndege kwa kuwekeza kwenye maduka yenye bidhaa mbalimbali pamoja, hoteli na karakana za ndege.
Grace Sanga mkazi wa Kiwanja cha ndege, Dkt. G. Nyamubi wa Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Iringa alipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka hiyo.
 Naye Mhandisi Astelius John amesema TAA imefanya maboresho makubwa kwenye viwanja vya ndege kikiwemo kiwanja cha ndege cha Iringa, ambapo kumefanyiwa upanuzi wa jengo la abiria na ukarabati wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege.

“Tunaboresha viwanja vya ndege ili viweze kuwa bora na kuhudumia abiria wengi wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa na sasa kwa Kiwanja cha Ndege Iringa hii ni kutokana na maboresho ya jengo la abiria    kubwa ambalo lina uwezo wa kuhudumia  abiria wanaotumia kiwanja cha Iringa kutoka 35 kwa siku hadi kufikia 200,” amesema.


Kwa upande wake Afisa Usalama, Miyaga Juma ametoa ushauri kwa wananchi na wageni kutoka ndani na nje ya nchi watumie Kiwanja cha ndege cha Iringa, kwani kina usalama madhubuti, kazi inayofanywa na Maafisa usalama wenye kufuata miongozo mbalimbali ya kiusalama, aidha TAA imenunua mashine ya kisasa ya Ukaguzi ili kurahisisha ukaguzi na kuwepo kwa mfumo wa kamera (CCTV) ambao unahifadhi kumbukumbu za matukio hali inayoboresha usalama Kiwanjani.

Monday 16 September 2019

Menejimenti ya TAA yapata mafunzo ya usimamizi wa Fursa na vihatarishi

 Menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), leo kwenye ukumbiwa mikutano wa Watu Mashuhuri wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wamepata mafunzo ya usimamizi wa fursa na vihatarishi kwa wadau wa nje na ndani ya taasisi yaliyokwenda sambamba na kuwapa ufahamu juu ya Viwango vya Kimataifa vya ISO 9001:2015; 14001:2015 NA 45001:2018 vinavyotolewa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO), mbele ni Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Ali Helal kutoka Kampuni ya Ascent Emirates ya Dubai. Mafunzo hayo yaliyohusisha Menejimenti ya TAA, na yataendelea tarehe 19 na 20 Septemba, 2019 kwa kuhusisha Mameneja na Mabingwa wa kusimamia mfumo (Champions).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama (wanne kulia), akisisitiza jambo kwenye mafunzo ya usimamizi wa fursa na vihatarishi kwa wadau wa nje na ndani ya taasisi iliyokwenda sambamba na kuvitambua viwango vya Shirika la Viwango la Kimataifa vya ISO 9001:2015; 14001:2015; na 45001:2018 iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa kushirikisha Menejimenti ya taasisi hiyo. Mafunzo hayo yametolewa na Ali Helal wa Kampuni ya Ascent Emirates ya Dubai (aliyesimama). Mafunzo hayo yaliyohusisha Menejimenti ya TAA, na yataendelea tarehe 19 na 20 Septemba, 2019 kwenye ukumbi wa VIP-JNIA kwa kuhusisha Mameneja na Mabingwa wa kusimamia mfumo (Champions).

Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Viwango wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Vedastus Fabian (wa pili kushoto waliokaa), akifafanua jambo kwenye mafunzo ya siku moja ya   usimamizi wa mafunzo ya usimamizi wa fursa na vihatarishi kwa wadau wa nje na ndani ya taasisi pamoja na kuvitambua viwango vya Shirika la Viwango la Kimataifa vya ISO 9001:2015; 14001:2015; na 45001:2018 yaliyotolewa na Mkuu wa Mafunzo wa Kampuni ya Ascent Emirates ya Dubai. Mafunzo hayo yaliyohusisha Menejimenti ya TAA, na yataendelea tarehe 19 na 20 Septemba, 2019 kwenye ukumbi wa VIP- JNIA kwa kuhusisha Mameneja na Mabingwa wa kusimamia mfumo (Champions).


Sunday 15 September 2019

Wafanyakazi TAA Watakiwa Kufanya Kazi Kwa Bidii


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama (kushoto), akimkabidhi zawadi ya ngao, Theobald Benigius wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius  Nyerere (JNIA) katika sherehe ya kuwaaga Wastaafu baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria na taratibu za Utumishi wa Umma.

Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wametakiwa kuchapa kazi kwa bidii ili kurudisha hadhi ya taasisi hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Julius Ndyamukama wakati akiwaaga wastaafu watatu wa mamlaka hiyo.

Hafla hiyo ilikuwa mahsusi kwa ajili ya kuwaaga wastaafu kutoka Idara ya Uandisi na Huduma za Ufundi ya Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), ambao ni Mhandisi Theobald Benigius, Ernest Kivela na Bertha Kipenda, ambao wamestaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha akimkabidhi mmoja wa wastaafu wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa JNIA, Mhandisi Bertha Kipenda zawadi ya vifaa vya mazoezi katika hafla ya kuwaaga iliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.


Alisema kuwa juhudi, maarifa na upendo ndio vigezo vitatu, ambavyo ni chachu ya kuipandisha na kuirejesha kileleni taasisi hiyo, ambayo ilianza kupoteza hadhi mbele ya uso wan chi na jamii, tofauti na huko nyuma, ambako ilikuwa ikifanya vizuri zaidi.

Alisema kwa sasa hadhi ya taasisi hiyo imeshuka mbele ya uso wa nchi na kusababisha baadhi ya kazi ilizokuwa ikizifanya zamani, sasa kufanya na taasisi nyingine.

“Nashauri tupendane na tuchape kazi kwa bidii, kwani sura yetu kama TAA hapo katikati ilidorora kwani tumepoteza kazi nyingi, hivyo tukitaka kurudisha hadhi yetu kama itatakiwa kusukumana, tutafanya hivyo kwa lengo hilo, ingawa najua wapo ambao hawataki hivyo,” alisema.

Hatahivyo, amewashukuru watumishi wenzake kwa kumpokea vizuri tangu kuteuliwa kwake kuongoza taasisi hiyo takribani miezi sita iliyopita, ambapo amewataka kushirikiana zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama, akiongea na watumishi walioudhuria hafla ya kuwaaga watumishi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), waliostaafu hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Pia ameweka angalizo kwa Watumishi wote kuwa muda wote atakaokuwepo hapo kama Mkurugenzi Mkuu, atalazimika kuwasumbua na kuwasukuma, ili sura ya TAA iliyopotea, kurejea katika hali yake yazamani.

 “Tukitaka kurudisha hadhi yetu kama ilivyokuwa zamani hivyo itahusu tusukumane na kusumbuana kidogo nitaomba mnivumilie, lakini lengo likiwa ni kutaka kurudisha TAA ya zamani, ingawa najua wapo wasiotaka,” alisema.

Aliwapongeza wastaafu hao na kuwataka kendelea kufanya kazi huko waliko ili kuendelea kuziimarisha afya zao.

Kwa upande wake
Kaimu Meneja wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mhandisi Diana Munubi (kushoto), akimkabidhi zawadi picha ya ua Ernest Kevela (wa kwanza kulia) katika hafla ya kuwaaga wastaafu wa Idara hiyo iliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha alisema watumishi hao walikuwa na nidhamu kubwa na kufanya kazi kwa bidii, pasipo kuchoka wala kuwa na malalamiko, ambapo amewataka wengine waliobaki kuiga mfano huo uliotukuka.

Lakini, pia amewataka Wastaafu hao kuendelea kufanya mazoezi kwani wamekuwa wakifanya kazi ngumu wawapo katika kituo chao cha kazi cha JNIA.

Watumishi kutoka Idara na vitengo mbalimbali vya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiserebuka kwa kucheza muziki katika hafla ya kuwaaga watumishi wenzao wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi waliostaafu hivi karibuni.


Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi, Mhandisi Alex Kalumbete amesema wastaafu hao walikuwa na uvumilivu mkubwa katika utumishi wa umma kutokana na kazi ngumu walizokuwa wakifanya za kiuhandisi.

Kaimu Meneja Uhandisi na Huduma ya Ufundi JNIA, Diana Munubi amesisitiza upendo uendelee kuwepo baina ya watumishi kama vile wastaafu hao walivyokuwa wakiuenzi wakati wa utumishi wao wote wa umma.

Mmoja wa wastaafu hao, Bw. Theobald Benigius kwa niaba ya wenzake ameishukuru TAA kwa kuwezesha kufanya kazi vizuri hadi utumishi wao kukoma kwa kustaafu, na amewaomba watumishi wenzake kuwa wavumilivu na tabia njema kwani wataweza kustaafu vizuri
.