Tuesday, 23 May 2017

Manji atangaza kuachia ngazi Yanga

Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji ametangaza kuachia ngazi rasmi kuiongoza klabu hiyo, imefahamika.

Kwa mujibu wa Katiba, Yanga sasa itakuwa chini ya uongozi wa Makamu mwenyekiti wake, Clement Sanga hadi pale uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo utakapofanyika.

Akielezea kujiuzulu kwa, Mani alisema kuwa ameamua kukaa pembeni ili kuwapisha wengine nao waiongoza klabu hiyo.

"Nimeamua nipumzike nipishe wengine waongoze, Yanga ni yetu sote nilipoingezewa muda tu kwa demokrasia, lakini haimanishi kuwa Mimi ndio nitakua Mwenyekiti milele, " alisema Manji ambaye hata hivyo si mara yake ya kwanza kutangaza kuachana na klabu hiyo.

Agosti mwaka jana pia alitangaza kujiuzulu  ikiwa ni siku chache tangu alipotangaza kutaka kuikodi timu hiyo kwa muda wa miaka 10, huku asilimia 75 za timu hiyo zikiingia kwake na kutoa asilimia 25 kwa timu hiyo kila mwaka kitu kilichopingwa na wadau wengi wa Soka ikiwemo Serikali.

Hata hivyo, wanachama wa klabu hiyo walimpigia magoti na kumsihi asitishe azma yake hiyo, ambayo alikubali kuendelea na uongozi hadi juzi Jumamosi alipoijulisha rasmi kamati yake ya utendaji kuwa ni muda muafaka kwa yeye kukaa pembeni.

"Nia yangu yakujiuzulu ni ya muda mrefu, sikutaka kufanya maamuzi katikati ya ligi ningewachanganya wachezaji, nashukuru tumetetea ubingwa wetu naiacha Yanga ikiwa na kikosi bora na hata makocha pia.

" Yapo mengi mazuri ninayojivunia Yanga ikiwemo umoja na mshikamano, ikumbukwe nilingia wakati kuna mgogoro mkubwa, nikafanikiwa kumaliza hivyo ni muda sahihi na muafaka kwa Mimi kukaa pembeni.

Ikumbukwe Yanga ni klabu ya wanachama, Yanga ni kubwa kuliko mtu yoyote, naamini watakaofuatia wataendeleza pale nilipoishia, " alisisitiza.

Kwa upande wa Katibu wa Yanga Charles Mkwasa akizungumzia hilo alisema "Nimeona taarifa ya Mwenyekiti wetu kwenye mitandao, na nilikuwa nawasiliana naye kila siku kwa email na hajawahi kunieleza hili, ila kama kweli ni maamuzi yake basi tutayaheshimu," alisema.


Hatahivyo, kuondoka kwa Manji kunaweza kukawa si pigo sana kwa klabu hiyo ya Jangwani ambayo tayari imesaini mamilioni ya fedha kwa kudhaminiwa na Sports Pesa huku ikielezwa kuwa kuna makampuni kadhaa ambayo yapo mbioni kudhamini timu hiyo ya mtaa wa Twinga na Jangwani.

Monday, 22 May 2017

Wanafunzi wa Filbert Bayi wafanyiwa tafrija nzito kwa kutwaa medali Kanda ya Tano Riadha

Mwenyekiti wa shule za Filbert Bayi, Filbert Bayi akiwa na wanafunzi wa shule hizo baada ya tafrija ya wanafunzi hao baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya umri wa miaka 18 juzi Kibaha mkoani Pwani.
Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Filbert Bayi (FBF) imesema kuwa itaendelea kugharamia elimu ya wanariadha watakaofanya vizuri katika michezo na masomo.

Hayo yalisemwa juzi na mwenyekiti wa shule hizo, Bayi wakati wa hafla ya kuwapongeza wanafunzi wa shule iliyowalioshiriki mashindano ya 12 ya riadha Kanda ya Tano ya Afrika.
Mashindano hayo ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 13 na 14 mwaka huu.

Bayi alisema kuwa wataendelea kugharamia ada na mahitaji mengine yote ya wachezaji wenye vipaji ili waendelea kusoma katika shule hiyo iliyopo Mkuza Kibaha mkoani Pwani.

Katika mashindano hayo shule hiyo ilitoa wanariadha watano waliounda timu ya taifa ilishika nafasi ya pili kwa matokeo ya jumla huku ikimaliza ya kwanza kwa upande wa wasichana.

Wanafunzi wa shule hiyo walikuwemo katika timu ya taifa ya Tanzania iliyoshiriki mashindano hayo ni Rose Thesuni alipata medali tatu za dhahabu katkika mbio za meta 400, kuruka juu na zile za kupokezana vijiti za meta 4x400.

Thesuni alipata medali ya fedha katika mchezo wa kupokezana vijiti wa mbio za meta 4x400 huku Bitrina Alexander akipata medali moja ya dhahabu katika mbio za kupokezana vijiti za meta 4x100, medali ya fedha katika meta 4x400 na shaba katika meta 400.
Dorcus Ilanda mwenyewe alipata medali ya fedha katika mbio zakupokezana vijiti za meta 4x400 na medali ya shaba katika meta 800 wakati Regina Mpigachai akipata medali za fedha katika meta 800 na kupokezana vijiti 4x400.

Mwanariadha mwingine wa shule hiyo ni Esther Martin aliyeshiriki mbio za meta 3000 na kumaliza katika nafasi ya nne kwa kutumia dakika 10:23.18.
Mwanafunzi mmoja hugharimu kiasi cha sh milioni  1.6 kwa temu kwa mwanafunzi mmoja, ambapo kwa mwaka kila mwanafunzi anagharamiwa sh milioni 3.2.

Alisema kuwa pamoja na gharama kubwa lakini wataendelea kuwagharamia wanafunzi wenye vipaji ili kuviendeleza vipaji vyao katika mchezo huo.

Naye katibu msaidizi wa RT, Ombeni Zavalla aliipongeza FBF kwa kuwatunza watoto hao na kuwataka kuendelea kuwagharamia ili kuwajengea msingi wa maisha yao katika michezo na elimu.
Aliwataka wanafunzi hao kutumia muda wao vizuri kwa ajili ya masomo na michezo.

Thesuni aliyepata medali tatu za dhahabu na moja ya fedha alimshukuru Bayi kwa kuwawezesha kugharamiwa elimu na mahitaji mengine na kuahidi kuendelea kufanya vizuri kitaifa na kimataifa.

Wanafunzi hao walitwaa jumla ya medali 11, ambapo mbali na kukata keki katika hafla hiyo, pia walipewa zawadi ya fedha taslimu.Sunday, 21 May 2017

Yanga wapokewa kifalme wakitokea Mwanza

  

Arsenal yashindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya

Mshambuliaji wa Everton, Kevin Mirallas (kulia) akikimbizwa na mchezaji wa Arsenal Alex Iwobi (katikati) wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya England leo kwenye Uwanja wa Emirates Jijini London. Arsenal ilishinda mabao 3-1.
LONDON, England
PAMOJA na kushinda mabao 3-1 dhidi ya Everton katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya England, Arsenal imeshindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kumaliza  katika nafasi ya tano.

Timu hiyo ambayo ilianza siku ikiwa pointi moja nyuma ya Liverpool iliyokuwa katika nafasi ya nne, ilionekana kama ingeweza kumaliza ya nne baada ya kupata bao la kuongoza katika dakika ya nane.
Lakini Liverpool, ilihitaji ushindi tu wa aina yoyote ili imalize katika nafasi ya nne, ambapo ilianza kuifunga Middlesbrough kabla ya mapumziko na kuibuka na ushndi wa mabao 3-0.

Manchester City yenyewe ilimaliza ya tatu baada ya kupata ushindi rahisi wa mabao 5-0 dhidi ya Watford.

Ligi ya Ulaya kwa Arsenal

Hatua ya Arsenal kufuzu kucheza Ligi ya Ulaya kwa mara ya 19 mfululizo ilifikia tamati jana baada ya kumaliza katika nafasi ya tano.

Imani ilikuwepo kwa mashabiki wa nyumbani wakati Hector Bellerin alipoifungia the Gunners bao la mapema huku taarifa zikizagaa kuwa, Liverpool ilikuwa katika wakati mgumu dhidi ya wapinzani wao Hull City ambao tayari walishashuka daraja.
Kiungo wa Liverpool, Georginio Wijnaldum (kushoto) akiwania mpira pamoja na mchezaji wa Middlesbrough, Grant Leadbitter walati wa mchezo wa Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Anfield mjini Liverpool, kaskazini magharibi ya England.
Liverpool sasa itacheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya mwisho msimu wa mwaka 2014-15.

Manchester City ilitwaa nafasi ya tatu na kufuzu moja kwa moja kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kushinda 5-0 dhidi ya Watford.

Mabingwa Chelsea imekuwa timu ya kwanza ya Uingereza kushinda mara 30 katika ligi kubwa katika mechi 38 za msimu mmoja wakati timu hiyo ikimuaga nahodha wao wa muda mrefu, John Terry huku ikipata ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya Sunderland.

The Blues, ambayo imetwaa ushindi wake wa sita wa Ligi Kuu siku tisa zilizopita, ilijikuta nyuma baada ya bao la mapema la Javier Manquillo lakini ilijibu mapema kupitia Willian.

Eden Hazard alifunga bao lake la 17 la msimu na kuifanya timu yake kuongoza kabla nafasi yake haijachukuliwa na Pedro.

Katika mechi zingine za ligi hiyo, Burnley ilifungwa na West Ham mabao 2-1 huku Hull City ikipokea kichapo cha mabao 7-1 kutoka kwa washindi wa pili wa ligi hiyo, Tottenham.


Nyota ya Samatta yaendelea kung'ara Ubelgiji

Na Mwandishi Wetu
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta usiku wa jana amecheza vizuri kwa dakika zote 90 timu yake, KRC Genk ikilazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Lokeren Uwanja wa Daknam mjini Lokeren, Ubelgiji kwenye mchezo wa Kundi B kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Ligu ndogo ya UEFA mwakani.

KRC Genk walitangulia kwa bao la penalti la kiungo mkongwe wa umri wa miaka 33, Mbelgiji Koen Persoons aliyejifunga dakika ya nne, kabla ya mshambuliaji mwenye umri wa miaka 31, Mbelgiji pia Tom De Sutter kuisawazishia Lokeren dakika ya 57.


Pamoja na sare hiyo, Genk inaendelea kuongoza Kundi B katika mchuano wa kuwania tiketi ya Europa League mwakani kwa kufikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi tisa na Samatta jana ameichezea Genk mechi ya 58 tangu ajiunge nayo Januari mwaka jana kutoka TP Mazembe ya DRC akiwa amefunga mabao 19.

Tuesday, 16 May 2017

Yanga yatetea ubingwa wake wa Bara

Mshambuliaji wa Yanga, Amis Tambwe (kulia) akiwania mpira na kiungo mshambuliaji wa Toto African, Yusuph Mlipili wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. 
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga leo wamefanikiwa kutetea ubingwa wao baada ya kuifunga Toto African ya Mwanza kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 68, ambazo zinaweza kufikia wa Simba, lakini endapo tu Yanga watafungwa katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mbao FC mjini Mwanza Jumamosi.

Pamoja na Simba kuwa na uwezekano wa kuifikia Yanga kwa pointi, lakini ni ndoto kwa timu hiyo kuifunga Mwadui kwa zaidi ya mabao 12.

Yanga ina mabao 57 ya kufunga na kufungwa 13, hivyo ina wastani wa mabao 44 wakati Simba imefunga mabao 48 na imefungwa 16, hivyo ina wastani wa mabao 32 iipitwa na Yanga kwa mabao 12.

Pamoja na katika soka lolote linawezekana, lakini timu kufunga mabao 12 katika mchezo mmoja ni jambo lisilowezekana kwani tangu msimu huu uanze, hakuna timu iliyowahi kufunga zaidi ya mabao hayo.

Katika mechi 29, ambazo Simba tayari imeshacheza, haijawahi kushinda zaidi ya mabao matano, hivyo timu hiyo tayari msimu huu imeshindwa kutwaa taji hilo.

Katika mchezo huo wa jana, Amis Tambwe ndiye aliyeiwezesha Yanga kuondoka na pointi zote tatu na kujihakikishia ubingwa mara ya tatu mfululizo baada ya kufunga bao katika dakika ya 82 baada ya kupata pasi kutoka kwa Juma Abdul.

Ligi hiyo inatarajia kukamilika Jumamosi kwa mechi za Simba dhidi ya Mwadui ya Shinyanga, Yanga na Mbao FC ya Mwanza, Azam FC na Kagera Sugar, Majimaji na Mbeya City, Stand United dhidi ya Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar na Toto Africans, Prisons na African Lyon na Ndanda FC na JKT Ruvu.

Vikosi vilikuwa:-
Yanga:Beno Kakolanya, Vicent Bossou, Juma Mahadhi/Kaseke, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa na Amis Tambwe.

Toto Africans: Lucajo Lerient, David Kissu, Mohamed Soud, Hamimu Abdu, Ramadhani Malima, Yusuph Mlipili, Carlos Protas, Juvenary Pastory/Waziri Ramadhani, Hussein Kasanga na Waziri Junior.

Sunday, 14 May 2017

Tanzania yaonesha nuru mpya katika riadha

Wachezaji,  viongozi na waamuzi wakicheza kwaito baada ya kumalizika kwa mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imeshika nafasi ya kwanza katika mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 18 kwa upande wa wanawake huku ikishika nafasi ya pili katika ushindi wa jumla katika mashindano hayo yaliyomalifika jana kenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Michezo nchini, Yusuph Singo akimvisha medali mmoja wa wanariadha wa Zanzibar walioshiriki mbio za kuokeana vijiti na kutwaa nafasi ya tatu.

Pia wanariadha 13 wa Tanzania ia wamefuzu kushiriki mashindano ya dunia ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 yatakayofanyika Kenya Julai mwaka huu baada ya kukimbia muda mzuri katika mbio zao.

MATOKEO YA WASICHANA, WAVULANA NA WASHINDI WA JUMLA
Kwa upande wa wanawake, Tanzania ilitwaa medali tano za dhahabu, nne za fedha na tatu za shaba, ikifuatiwa na Kenya akati Sudan ilimaliza ya tatu, Zanzibar ya nne, Eritrea ya tano, Sudan Kusini na Somalia zilifungana katika nafasi ya sita kwa upande huo wa wanawake.
Magwiji wa riadha nchini, Filbert Bayi (kulia) na Juma Ikangaa wakati wa kutoa zawadi kwa washindi wa  mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika kwenye Uwanja wa Taifa.
Tanzania ambayo kwa miaka mingi haijafanya vizuri katika mashindano ya riadha kama timu, jana katika mashindano hayo ya vijana kwa ushindi wa jumla, ilijukusanyia medali saba za dhahabu na fedha saba, huku tatu zikiwa za shaba.

Timu ya Tanzania ya mchezo wa mbio za kupokezana vijiti kwa wavulana ndio ilimalizia medali za dhahabu baada ya kushika nafasi ya kwanza huku wasichana wao wakimaliza a pili nyuma ya Wakenya na kupata medali ya fedha.
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja akimvisha medali mwanariadha wa Tanzania.

Kama timu ya kupokezana vijiti ya wasichana ya mchezo wa meta 400 x 4 ingepata medali ya dhahabu, basi Tanzania ingekuwa mshindi wa kwanza wa jumla, lakini sasa Kenya ndio ilitwaa ushindi wa jumla wa mashindano ya mwaka huu.

Kenya imeshika nafasi ya kwanza baada ya kutwaa medali nane za dhahabu, nne za fedha ba tatu za shaba wakati Zanzibar ilimaliza ya tatu baada ya kutwaa medali nne za dhahabu, fedha tano na shaba nne.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Sudan ilimaliza ya nne kwa kutwaa medali mbili za dhahabu, tatu za fedha na mbili za shaba, wakati Eritrea ilishika nafasi ya tano kwa kuwa na medali tatu za fedha na sita za shaba huku ikiwa haina medali hata moja ya dhahabu.
Sudan Kusini ilimaliza ya sita baada ya kuambulia medali moja tu ya shaba wakati Somalia ilishika mkia baada ya kushindwa kuambulia medali yoyote ile.

Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya nchi saba, ambazo ni wenyeji Tanzania, Zanzibar, Kenya, Eritrea, Sudan, Sudan Kusini na Somalia wakati nchi ambazo hazikufika ni pamoja na Rwanda, Uganda, Ethiopia na Djibout.
Mashindano hayo ambayo yalifunguliwa juzi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, yalifungwa jana na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, Mohamed Kiganja.

Saturday, 13 May 2017

Mwakyembe afungua mashindano ya riadha Kanda ya Tano ya Afrika kwa vijana wa U-17

Wanariadha wa Tanzania baada ya kutwaa medali ya dhahabu katika mbio za kupokezana vijiti za meta  4 X 100 kwenye Uwanja wa Taifa leo.

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrson Mwakyembe amezitaka kampuni mbalimbali kujitokeza kwa wingi kudhamini mchezo wa riadha.

Mwakyembe aliyasema hayo leo mchana wakati akifungua mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana, ambako jumla ya nchi saba zinashiriki.
Alisema kuwa makampuni zaidi yanatakiwa kujitokeza kudhamini mchezo huo, ambao miaka ya nyuma uliipatia sifa kubwa sana nchi kwa wanariadha wake kama akina Juma Ikangaa, Filbert Bayi, Suleimana Nyambui na wengin kufanya vizuri kimataifa.

Mashindano hayo yamedhaminiwa na NMB, Vodacom, PPF na Serengeti Marathon.


Waziri huyo pia alisema kuwa Riadha Tanzania (RT) kama wangeitaarifu mapema wizara, basi uwanja huo ungejaa wanafunzi kushuhudia wenzao wakitimua mbio pamoja na michezo mingine ya riadha.
Mwakyembe alishuhudia baadhi yam bio, ambapo washiriki walichuana vikali katika mbio tofauti tofauti kama zile za kupokezan vijiti za Meta 400 x 100 kwa wanaume, meta 3,000, 800 na zingine.
Katika mbio za meta 100 wanawake, Winfrida Makenji wa Tanzania aliibuka wa kwanza kwa kutumia sekunde 12.7, huku Naila wa Sudan ya Kusini alishika nafasi ya pili kwa kutumia sekunde 12.65 na Zanzibar ilimaliza ya tatu kupitia Kazija Hassan Simai aliyetumia sekunde 13.05.
Katika mbio za meta 800 wasichana, Tanzania ilishika nafasi ya pili kwa kutumia dakika 2:13:51 kupitia kwa Regina Mpigachai huku mshindi akiwa ni Mkenya aliyetumia dakika 02:12:43 na watatu ni Dorcus Boniface wa Tanzania aliyemaliza kwa dakika  02:13:71.
Tanzania ilitamba katika mbio za fainali ya kupokezana vijiti meta 100 x 400 wasichana pale waliposhika nafasi ya kwanza kwa kutumkia  sekunde 51;41 wakifuatiwa na Zanzibar waliotumia sekunde 53:31.
Mashindano hayo yanamalizika leo kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo bingwa wa jumla atajulikana huku nchi za Tanzania, Zanzibar, Eritrea, Sudan Kusini, Kenya na Somali zikishiriki baada ya Uganda, Ethiopia, Djibout na Rwanda zikishindwa kushiriki kwa sababu tofauti tofauti.  Wanariadha wa Tanzania wa washindi wa mbio za kupokezana vijiti kwa wasichana wakiwa na kocha wao Robert Kalhae mara baada ya kushinda mbio hizo leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.