Friday, 30 June 2017

JNIA TB III kuanza kutumika Decemba mwakani

Jengo la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 3 likionekana kwa nje leo.
Na Mwandishi Wetu
UJENZI wa jengo la kuondokea na kuwasili abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 3 utakamilika Septemba mwakani na kuanza kutumika rasmi miezi mitatu baadae, imeelezwa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame  Mbarawa aliyasema hayo leo baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea jengo la kiwanja hicho, ambalo ujenzi wake unaendelea.

Mbarawa alisema kuwa, ujenzi huo unaendelea vizuri na utakamilika Septemba 2018 na kuanza rasmi kutumika Desemba mwaka huo huo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na wafanyakazi kabla ya kutembelea Jengo la Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere Terminal 3 leo.
Alisema jengo hilo litakakuwa likichukua jumla ya abiria milioni 6 kwa mwaka tofauti na jengo lile la Terminal Two, ambalo lina uwezo wa kuchukua abiria milioni 2 tu kwa mwaka, hivyo majengo hayo mawili yakakuwa yakichukua jumla ya abiria milioni 8 kwa mwaka.

Alisema kuwa hatua ya kuchukua abiria wengi litasaidia kuongeza watalii wanaotembelea vizutio vilivyopo nchini.
Waziri Profesa Mkame Mbarawa akisaini kitabu cha wageni leo.
Aliongeza kuwa eneo la maegesho ya kiwanja hicho yatakuwa yakichukua jumla ya ndege 21 kwa wakati mmoja, hivyo kuwezesha watu wengi wakiwemo watalii kuja nchini kupitia katika kiwanja hicho cha ndege.

Pia Mbarawa alimuhakikishia mkandarasi wa uwanja huo kuwa, atalipwa fedha zake zote kwa wakati kama alivyoahidi Rais John Pombe Magufuli alipotembelea kiwanja hicho mapema mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mkandarasi Simba Charles leo. Kulia ni  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mtengeka Hanga.
Mbarawa alitembelea maeneo mbalimbali ya jengo hilo yakiwemo yale ya kukaa abiria wanaondoka na kuwasili, vyumba vya wageni mashuhuri na sehemu tofauti tofauti, ambazo zinajengwa kwa umahiri mkubwa.
Meneja wa Ujenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) wa Kampuni ya BAM International-Africa, Ray Blumrick akimpa maelezo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (watatu kushoto) alipotembelea jengo la kiwanja hicho leo Ijumaa.
Waziri Mbarawa alipata maelezo ya kina ya ujenzi huo kutoka kwa mkandarasi, Simba Charles na Meneja Ujenzi, Ray Blumrick wa Kampuni ya BAM-Unternational-Afrika.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (wa pili kulia) akifurahia jambo na Mkandarasi Simba Charles alipokagua ujenzi wa jengo la Kiwanja kipya cha Ndege cha Kimatafa cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 3 leo.
Tuesday, 27 June 2017

Ngoma azichezesha ngoma Yanga, Simba

Na Mwandishi Wetu
MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma amezikacha klabu za Yanga na Simba na badala yake amemwaga wino timu ya Polokwane City inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, imebainika.

Ngoma anatarajia kutua jijini Dar es Salaam kesho kwa ajili ya kuongeza mkataba wa kuendelea kuichezea Yanga, lakini pia mshambuliaji huyo alishafanya mazungumzo ya awali na viongozi wa Simba na inasemekana ujio wake ulikuwa ni kwa  ajili ya kukamilisha usajili wake kwa kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo msimu ujao.

Kwa mujibu wa Mtandao wa KickOff.com, Ngoma raia wa Zimabwe, amekamilisha zoezi lake la usajili kwenye klabu hiyo, baada ya kuwa huru kufuatia kumaliza mkataba wake wa miaka miwili na mabingwa wa soka Tanzania Yanga.

Taarifa hiyo imesema Ngoma,  alisaini mkataba huo wa miaka mitatu baada ya kufuzu vipimo vya afya na anatarajiwa kujiunga na miamba hao wa ligi ya ABSA,ambao kwasasa wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo.


Akiwa Polokwane City, Ngoma anatarajiwa kukutana na Mzimbabwe mwezake, George Chigova aliyewahi kucheza naye FC Platinum chini ya kocha Norman Mapeza.

Sunday, 25 June 2017

Serikali waipa TOC hekali 20 za ardhi SingidaMkuu wa Mkoa wa Singida, Rehema Nchimbi akiwa na atoto walioshiriki mbio za kilometa 2,5 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Olimpiki Duniani ambayo kitaifa ilifanyika Singida leo kwenye Uwanja wa Peoples.
 Na Mwandishi Wetu, Singida
SERIKALI ya Mkoa wa Singida imetoa ardhi  hekali 20 kwa Kamati ya Ollimiki Tanzania (TOC) kwa ajili ya kujenga kituo cha michezo cha Olimpiki Afrika.

Watoto wakishiriki mbio za kilometa 2.5 wakati wa Siku ya Olimpiki iliyofanyika kitaifa mkoani Singida leo kwenye Uwanja wa Peoples mjini humo.

Nchimbi alitoa ahadi hiyo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Olimpiki iliyofanyika kitaifa mkoani hapa kwenye Uwanja wa Peoples hapa, ambako washiriki walianza mbio na kumalizia kwenye uwanja huo.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania TOC), Filbert Bayi akizungumza na wana habari baada ya kumalizika kwa maazimisho ya Siku ya Olimpiki kwenye Uwanja wa Peoples mjini Singida.

Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alimshukuru Nchimbi na kusema kuwa ofa hiyo ataiwakilisha kwa wenzake akiwemo rais wa kamati hiyo, Gulam Rashid na Kamati ya Utendaji ili kuona wanaipokeaje ofa hiyo.
Katika hafla hiyo mtoto wakike na kiume wenye umri mdogo na mwanamke na mwanaume mwenye umri mkubwa zaidi, kila mmoja alizawadiwa zawadi na Nchimbi iliyotolewa na TOC.
  Mkuu wa Mkoa wa Singida, Rehema Nchinbi akicheza ngome ya Kinyaturu ya Misake. Kulia ni Katibu tawala, Angelina Lutambi. 

Kwa upande wa watoto wenye umri mdogo zaidi waliomaliza wa kwanza katika mbio zao za kilometa 2.5, Careen Msasu mwenye umri wa miaka sita na Stephen Joshua mwenye umri wa miaka 8 ndio walitwaa sh 50,000 kila mmoja kwa kumaliza wa kwanza.

 Bibi wa zaidi ya miaka 90 akipokea zaadi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Rehema Nchimbi baada ya kumaliza na mbio na watoto wadogo.

Kwa upande wa watu wenye umri mkubwa zaidi walioshiriki mbio hizo, Vitus Mutake mwenye miaka 71 na Tatu Chungu mwenye umri wa miaka 59, nao walitwaa sh 50,000 kwa kumaliza wa kwanza huku wakiwa wenye umri mkubwa kuliko washiriki wengine wa mbio za kilometa tano.

Siku ya Olimpiki duniani imekuwa ikifanyika Juni kila mwaka na kuadhimishwa na zaidi ya nchi 200 duniani, ambazo ni wanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).

Siku ya Olimpiki mjini hapa ilianza kuadhimishwa juzi kwa usafi wa mazingira ambao Nchimbi na viongozi wa TOC walisafisha mazingira katika mitaa na maeneo mbalimbali ikiwemo shule ya msingi Mwenge na soko la matunda.


Saturday, 24 June 2017

RC Singida, TOC waendesha zoezi la usafi leo


Mkuu wa  Mkoa wa  Singida, Rehema Nchimbi (watatu kulia), Katibu Mkuu wa  Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi (wapili kulia) na mjumbe wa Kamati ya Utendaji Irine Mwasanga wakati wa kufanya usafi mjini Singida leo sambamba na maadhimisho ya Siku ya Olimpiki inayofanyika kesho.
Na Mwandishi Wetu, Singida
WAKATI maadhimisho ya Siku ya Olimpiki Duniani yanafanyika kitaifa kesho mjini Singida, Mkuu wa Mkoa huo pamoja na viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), leo walifanya usafi katika maeneo mbalimbali.

MKUU wa Mkoa wa Singida, Rehema Nchimbi pamoja na viongozi mbalimbali wa TOC walifanya usafi katika maeneo tofauti tofauti ili kuadhimisha Siku ya Olimpiki ambayo itafanyika kesho Jumapili.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Rehema Mchimbi (katikati) akishiriki katika usafi mjini Singida leo. Kushoto ni Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida (RPC),   
Akizungumzia kuhusu Siku ya Olimpiki, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema kuwa, Nchimbi ndiye atabariki maadhimisho ya Siku ya Olimpiki kwenye Uwanja wa People uliopo mjini Singida.

Bayi alisema kuwa wanafunzi shule mbalimbali za msingi na sekondari pamoja na watu wengine, watashiriki mbio hizo za kilometa 2.5 pamoja na zile za wakubwa, ambazo zitakuwa za kilometa tano.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Olimpiki yatashuhudia washiriki wakikimbia katika mbio hizo, ambayo hayana ushindi lakini mshiriki mwenye  umri mdogo na yule mwenye umri mkubwa zaidi, ndio watakaokabidhiwa zawadi za ushindi.


Maadhimisho ya Siku ya Olimpiki Duniani yamekuwa yakifanyika Juni kila maka , ambapo mwaka jana yalifanyika mjini Mtwara na mgemi rasmi alikuwa mkuu wa mkoa huo, Halima Dendegu na kuwashirikisha wakuu wote wa wilaya za mkoa huo.Serikali, TOC wakutana Dodoma kujadili maandalizi Michezo ya Jumuiya ya Madola 2018

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) na Naibu wake, Anastazia Wambura (kulia),  Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau (kushoto) na  Katibu Mkuu Filbert Bayi waliokutana mjini Dodoma juzi.
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) zimekutana na kujadili kwa kina kuhusu maandalizi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Gold Coast, Australia kuanzia Aprili.

Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola itafanyika Gold Goast kuanzia Aprili 4 hadi 15, mwakani, ambapo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zitakazoshiriki michezo hiyo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe na naibu wake, Anastazia Wambura juzi mjini Dodoma walikutana na Makamu a Rais na  Katibu Mkuu wa TOC, Henry Tandau na Filbert Bayi, ambao walijadili kwa kina maandalizi ya Tanzania kwa ajili ya michezo hiyo.

Bayi alisema kuwa majadiliano yao yalienda vizuri, ambapo waliueleza ujumbe huo wa Serikali kuhusu mpango wa maandalizi wa Diplomasia ya Michezo, ambao ungeziwezesha timu za Tanzania za riadha, kuogelea, ngumi na mpira wa meza kupiga kambi nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi hayo.

Alisema tofauti na mwaka 2014 wakati wa maandalizi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Glasgow, Scotland, Serikali iligharamia nauli na posho za wachezaji walioenda katika kambi katika nchi za  Uturuki, Ethiopia, China na New Zealand kwa kutumia mpango wa Diplomasia ya Michezo.

 Bayi alisema TOC mwaka huu ndio itagharamia nauli na posho kwa wachezaji na makocha watakaoenda kuiga kambi nje ya nchi kwa ajili ya kujiandaa na Michezo ya Jumuiya ya Madola ya Gold Coast mwakani.

Alisema Mwakyembe ambauye aliingia hivi karibuni katika wizara hiyo akichukua nafasi ya Nape Nnauye aliyeondolewa na Rais Magufuli, alikua hana taarifa kuhusu mpango huo wakati TOC ilishasilisha suala hilo maema wakati wa Nape.

Alisema Mwakyembe aliahidi kulifanyia kazi suala hilo na TOC wana mpango wa kukutana na Waziri wa Mambio ya Nchi za Nje, Augustino Maige, ili kuhakikisha timu ya Tanzania inapiga kambo haraka nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi ya michezo hiyo.


Tanzania katika michezo hiyo ya Gold Coast inatarajia kupeleka timu za riadha, ngumi na mpira wa meza, ambazo zinatarajia kupiga kambi Ethiopia, Cuba na China.

Umitashumta yaunda Kamati kubaini vijeba

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
UONGOZI wa Mashindano ya Michezo ya Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) umeunda Kamati Maalumu kwaajili ya kudhibiti wanafunzi wenye umri mkubwa ambao wanashiriki katika mashindano hayo.

Akizungumza jijini hapa, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu, Jeshi Lupembe alisema wameunda kamati hizo ili kuondoa malalamiko yanayoletwa na walimu katika mashindano hayo.

Lupembe alisema kamati alizounda zina watalamu mbalimbali waliobobea katika michezo, ambao hadi sasa uongozi wao umetoa fomu maluumu kwaajili ya malalamiko yahusuyo wanafunzi waliozidi umri wanaoshiriki michezo hiyo.

Akielezea zaidi,Lupembe alisema mikoa inayotuhumiwa kuwa na wachezaji wenye umri mkubwa ni pamoja na Dar es Salaam, Tanga, Kigoma na Mara.

Lupembe alisema kamati yake kazi kubwa inayofanya ni kumhoji mtoto husika, kupeleleza mkoa alikotoka, shule, ofisa elimu, walimu na wazazi kuwahoji ili kujua  umri halali wa mtoto.

Kwa mujibu wa Jeshi, mpaka sasa waliotuhumiwa katika orodha ya watoto waliozidi umri ni 10 na  katika hao kuna watoto watatu wako vizuri, lakini saba waliobaki wameonywa kutoshiriki mashindano hayo.

Aidha, Mkurugenzi Lupembe alisema Serikali itaendelea na jitihada za mazungumzo ya kutafuta udhamini wa mashindano hayo kama ilivyo kwa Michezo ya Shule za Sekondari (Umisseta).


Katika mechi za leo mpira wa miguu kwa wavulana, Mwanza imeshinda 3-0 dhidi ya Manyara, Mpira wa mikono wasichana Mara imeshinda 13-9 dhidi ya Mtwara, Shinyanga 8-5 Dodoma na Mara 6-4 Dar-es-salaam.

SuperSport yapata kibali kurusha UEFA 2020

Na Mwandishi Wetu
Kwa mara nyingine tena Watanzania wamepata uhakika wa kushuhudia michuano mbalimbali mikubwa ya kimataifa baada ya DStv kupitia SuperSport kuingia makubaliano ya kurusha michuano mikubwa ya kimataifa, ikiwemo michuano ya UEFA Euro 2020 pamoja na ile ya kufuzu UEFA Euro 2020  na pia michuano ya Ulaya ya kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Pia kuna lulu nyingine kwa Watazamaji wa DStv hasa washabiki wa kandanda kwani pia mashindano mapya ya Ligi ya UEFA itakayoshindaniwa na timu kutoka nchi zote 55, ambazo ni wanachama wa UEFA.

 Michuano hii pia itakuwa ikioneshwa katika  chaneli ya SuperSport.

Makubaliano haya yanawahakikishia Watazamaji wa DStv kushuhudia michuano yote mikubwa ya soka  kila msimu hadi mwaka 2022.

“UEFA inafurahi kuendelea na kuimarisha uhusiano wake wa muda mrefu na supersport,” amekaririwa Guy-Laurent Epstein, Mkurugenzi Mtendaji wa  UEFA Events SA. 

“Supersport  ni mshirika wa miaka nenda rudi wa UEFA na tunaimani kubwa kuwa SuperSport itaendelea kuwahakikishia Watazamaji matangazo ya kiwango cha juu na pia amsha amsha  ya UEFA 2018-2022 kwa mamilioni ya watazamaji wa mitanange hiyo barani Afrika – Kusini mwa Jangwa la Sahara.

UEFA Euro 2020, ni moja ya michuano itakayokuwa na shamrashamra nyingi ikizingatiwa kuwa itakuwa inatimiza miaka 60 tangu kuanza kwa michuano hiyo. Michuano hiyo itafanyika katika miji 13 ya nchi 13 tofauti barani Ulaya.

Michuano ya kufuzu ya Ulaya (The European Qualifiers) itakuwa ya aina yake wakati ambapo nchi 55 zitakabana koo kuwania nafasi 24 za kushiriki michuano hiyo. Michuano hii ya kufuzu itaanza Machi 2019 hadi Machi 2020. 

“Hii ni mikataba mikubwa na muhimu sana,” alisema Gideon Khobane, Ofisa Mkuu wa SuperSport. 

“Michuano ya Ulaya kwa kawaida huwa na mvuto mkubwa sana kwa  watazamaji wetu hivyo kuyafanya moja ya mashindano muhimu sanan. Tunaamini kuwa michuano hii inaendelea kuwa mikubwa na maarufu Zaidi hivyo bila shaka ushirikiano wa Supersport na UEFA utaongeza chachu katika michuano hiyo.


Kwa maelezo zaidi tembelea  kurasa za mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Instagram na Twitter @DStvTanzania  na  Tovuti - www.dstv.com

Thursday, 22 June 2017

Mamlaka Viwanja vya Ndege yahitimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa maonesho ya shughuli zao


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Salim Msangi (wa pili kushoto) na mwanasheria Ramadhani Maleta wakiwa pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Precision Air jijini Dar es Salaam leo.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inakamilisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya maonesho ya kuonesha shughuli mbalimbali za kila siku wanazozifanya.

TAA ilianza wiki hiyo ya Utumisi wa Umma kwa Makao Makuu kutembelea idara zao mbalimbali ikiwemo ile ya Utawala, eneo la kuwasili na kuondokea abiria mashuhuri au VIP la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Idara ya Usalama, Uhasibu katika eneo hilo.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, salim Msangi (wa kwanza kushoto waliokaa) na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Joseph Nyahende.

Pia Kaimu Mkurugenzi Mkuu alitembelea eneo la Usalama katika JNIA Terminal Two, Idara ya Manunuzi, Usalama na kwingineko, ambako alizungumza na wafanyakazi wa idara hizo, ambao walieleza utendaji wao wa kazi na changamoto wanazokumbana nazo katika majukumu yao ya kila siku.

Siku inayofuata, uongozi wa TAA ulikutana na wafanyakazi wa idara zote katika ukumbi wa Kiwanja cha Ndege cha Terminal One, ambako walidajili matatizo mbalimbali yanayowakabili na uongozi ulitoa suluhisho la matatizo hayo.
Katika kutimiza agizo la Serikali la taasisi zake kuadhimisha wiki hiyo kwa kutembelea idara na kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyakazi katika kutekeleza majukumu yao ya siku hadi siku.

Katika kukamilisha wiki hiyo, TAA jana na kesho ina banda lake nje ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambako mbali na vipeperushi, majarida na mabango yanayoelezea shughuli zao katika idara tofauti tofauti, pia wapo wafanyakazi wanaotoa maelezo kwa abiria na watu wengine wenye matatizo au kutaka kujua zaidi utendaji wa taasisi hiyo.
Katika banda hilo kuna picha kubwa zinazoonesha viwanja mbalimbali vilivyoboreshwa , ambavyo baadhi yao vilikuwa havina rami lakini sasa vimewekewa rami pamoja na mambo mengine yanayofanywa na TAA.


Wiki ya Utumishi wa Umma inamalizika rasmi kesho nchini kote, huku TAA chini ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Salim Msangi ikijitahidi kuwaelimisha wasafiri na wananchi kwa ujumla juu ya taasisi hiyo na idara zake na jinsi zinavyofanya kazi kwa ujumla.Tuesday, 20 June 2017

Afungwa baada ya kumning'iniza mtoto ghorofani

ALGIERS, Algeria
MAHAKAMA nchini hapa imemuhukumu kwenda jela miaka miwili mtu mmoja kwa kosa la kumning’iniza mtoto wake nje ya dirisha katika ghorofa refu ili kupata watu wengi katika ukurasa wake wa Facebook.

Mtu huyo alitupia picha yake akiwa ameng’iniza mtoto nje ya dirisha katika jengo refu, huku picha hiyo ikiwa na maelezo (caption):  "Nataka watu 1,000 watakaolaiki (ingia) katika ukurasa wangu wa Facebook au namuangusha chini mtoto huyu.”

Alihukumiwa kwa kosa na kuhatarisha maisha ya mtoto huyo baada ya kukamatwa Jumapili, Polisi ilisema.

Mtoto huyo alining’inizwa katika katika dirisha la ghorofa ya 15 ya makazi iliyopo katika jiji hili, liliripoti shirika la habari la Al Arabiya.

Mtu huyo, mwenye undugu na mtoto huyo, alikanusha shitaka hilo, akisema kuwa picha hiyo ilitengenezwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii.

"Picha iliyopigwa ilipigwa katika kibaraza iliyokuwa na vizuizi, Hii ilitolewa na kuwekwa nyingine, “alijitetea.

Baba wa mtoto huyo aliitaka mahakama kumsamehe mtu huyo, akidai kuwa alikuwa akicheza tu.
Hatahivyo, jaji alipinga maombi hayo dhidi ya yake, akisema picha ilikuwa haina utata na ilionesha maisha ya mtoto huyo yalikuwa hatarini.


Watu walichangia katika taarifa hiyo walionesha hasira kuhusu tukio hilo la kinyama.

Gaidi auawa akitaka kulipua steshen Ubelgiji

BRUSSELS, Ubelgiji
ASKARI wa Ubelgiji wamempiga risasi na kumuua mtu mmoja anayedai kuwa alikuwa akitaka kulipua stesheni ya treni mjini hapa, imeelezwa.

Mtu huyo aliuawa mara baada ya kuripotiwa kuwa alikuwa akiunganisha vilipuzi na hakuna mtu mwingine aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

Waendesha mashtaka walisema kuwa mtu huyo alikufa. Wanalichukulia tukio hilo kama shambulio la kigaidi.

Machi mwaka 2016, watu 32 waliuawa katika shambulio la kigaidi mjini hapa, tukio mabalo lilidai kutekelezwa na kundi la kigaidi la Islamic State (IS).

Kwa mujibu wa gazeti la Ubelgiji la La Libre Belgique, liliwakariri waendesha mashtaka, mtu aliyeuawa alikuwa amevalia vilipuzi.

Nicolas Van Herrewegen, wakala wa relwe, alisema alikwenda chini katika stesheni, ambako alisikia mtu akipiga kelele.

"Baadae alikuwa akisema 'Allahu Akbar' na alitupa sanduku lake la matairi, “aliliambia Shirika la habari la AFP.

"Nilikuwa nyuma ya ukuta wakati mlipuko mdogo ukitokea. Nilikwenda chini na kuwataarifu wenzangu. Mtuhumiwa aliendelea kuwepo eneo hilo na baadae hatukumuona tena.”

"Haukuwa mlipuko mkubwa lakini kishindo chake kilikuwa kizito, “aliongeza. “Watu walikimbia huku na huko.”

Bwana Van Herrewegen akimuelezea muhusika huyo alisema alikuwa mtu mwenye mwili uliojengeka akiwa na nywele fupi, akiwa amevali shati jeupe na suruali ya jinsi.

"Niliona kama alikuwa na kitu fulani niliona waya, huenda alikuwa amevalia vesti yenye vilipuzi, “alisema.

Mwanasheria Remy Bonnaffe, 23, alikuwa akisubiri treni alifanikiwa kupiga picha ya moto huo mdogo baada ya mlipuko.

Aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa watu waliokuwa karibu na mlipuko huo hawakuumia na hakuna ukuta ulioharibika.

"Nina furaha kuwa hakuna mtu aliyeumia nan i wazi kuwa jaribio hilo halijafanikiwa, limefeli, “alisema.


Arash Aazami ambaye aliwasili muda mfupi katika stesheni hiyo baada ya mlipuko huo, alisema alikuta watu wa usalama, huku watu wengine wakikimbia mitaani kusaka usalama…, “alisema.

Monday, 19 June 2017

Mbio za uongozi TFF zashika kasi kinoma

Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI wazamani wa soka Tanzania, Ally Mayay na Mtemi Ramadhan pamoja na ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shija Rishard (Pichani) wamechukua fimu kutaka uongozi katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi utakaofanyika Agosti 12 mjini Dodoma.

Mayay kiungo na beki wa Yanga kati ya 1999 na 2005 amechukua fomu ya kuwania, wakati Mtemi aliyewika  Ofisa wa juu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shijja Richard naye kujitosa kuwania urais.

Simba SC kati ya mwaka 1981 na 1985 amechukua fomu ya kuwania Umakamu wa Rais. Mayay atapambana na rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi aliyekuwa Katibu wake wakati anacheza Yanga.

Kwa ujumla mbio za kuwania uongozi wa TFF zimezidi kushika kasi baada ya Ofisa wa juu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shija Richard naye kujitosa kuwania urais.

Shija ambaye ni Meneja ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, amechukua fomu hiyo leo Jumatatu katika ofisi za TFF Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, ingawa hakuzungumza lolote kwa maelezo kuwa muda wa kampeni bado.

“Ni kweli nimechukua fomu kuwania urais wa TFF, wengi mtataka kujua mengi kuhusu mimi na kwa nini nimejitosa katika nafasi hii, tuvute subira wakati wa kampeni ukifika nitazungumza, ila kwa leo itoshe kuuthibitishia umma kwamba nimechukua fomu ya urais,” alisema Shijja.

Mgombea huyo ana Shahada ya Uzamili katika masuala ya Sheria za Kodi na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia ana Stashahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Fedha kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam na Stashahada ya Juu ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha (IAA).
Mgombea wa urais, Ally Mayay akizungumza na wandishi wa habari jana baada ya kuchukua fomu. Kulia ni mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais , Mtemi Ramadhan.
Pia Shija amehudhuria mafunzo mbalimbali ya uandishi wa habari na ameandikia magazeti mbalimbali hapa nchini kuanzia mwaka 1997.

 Mgombea huyo aliwahi kuitumikia Taasisi ya Kuzuia na Kupambaana na Rushwa (TAKUKURU) kabla ya kujiunga na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Kwa sasa ni Mhazini Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), akiwa pia amepata kuongoza klabu mbalimbali za mpira wa miguu kwa ngazi tofauti.


Mwaka 2008 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Chama cha Soka wilayani Chato (CDFA), ambapo alisimamia usajili wa chama hicho kuelekea kwenye uchaguzi ambao hata hivyo hakugombea. Pia Shjija amepata kuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Bukoba Veteran iliyopo mkoani Kagera.