Tuesday, 3 March 2015

MCHEZAJI SUNDERLAND MATATANI KWA `KUBAKA'
Adam Johnson.
LONDON, England
MCHEZAJI wa England na klabu ya Sunderland Adam Johnson amekamatwa na polisi kuhusina na madai ya kufanya ngono na msichana mwenye umri wa miaka 15, imeelezwa.
Polisi ya Durham ilisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alikamatwa mapema akifanya ngono na msichana mwenye umri chini ya miaka 16, na aliendelea kuwekwa rumande ya polisi.
Sunderland AFC ilisema kuwa mchezaji huyo amesimamishwa wakati wakisubiri uchunguzi wa polisi.
Inaelezwa kuwa taarifa za kukamatwa kwa mchezaji huyo wa Ligi Kuu ya England ziliibuliwa mapema na gazeti la The Sun.
Winga huyo mzaliwa wa Sunderland alijiunga na klabu ya vijana ya Middlesbrough na alianza kuichezea timu ya wakubwa akiwa na umri wa miaka 17, katika mchezo wa Kombe la UEFA mwaka 2005.
Alitolewa kwa mkopo kwa Leeds United na baadae Watford, alirejea Middlesbrough na baadae mwaka 2010 alihamia Manchester City kwa kitita cha pauni Milioni 7.
Mwaka 2012 alisaini kuichezea Sunderland kwa gharama ya pauni Milioni 10, na Januari mwaka 2014 alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa Ligi Kuu ya England baada ya kufunga hat-trick katika mchezo wa ugenini dhidi ya Fulham.
Pia aliiwakilisha England katika timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 19 na 21, na ile ya wakubwa mara 12. Kwa mara ya mwisho aliichezea England katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Italia agosti mwaka 2012.
Kukamatwa kwake kumekuja muda mfupi kabla hajasafiri na Sunderland kwenda Hull kwa ajili ya mchezo wa Jumanne usiku wa Ligi Kuu ya England.
Hatahivyo, Sunderland ilisema kuwa haina cha kusema zaidi kuhusu kukamatwa kwa mchezaji wake huyo.

No comments:

Post a Comment