Friday 31 August 2018

MAB yampongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAA


 Na Mwandishi Wetu

BODI ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Richard Mayongela (Pichani) kwa kuthibitishwa rasmi katika nafasi hiyo.

Awali Bw. Mayongela alikuwa akikaimu nafasi hiyo kwa takribani miezi 11  iliyopita.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa MAB, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema kwa niaba ya bodi nzima amesema "Nimepokea taarifa rasmi ya kuthibitishwa kwako kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania. Ninakupongeza."

Mhandisi Prof. Lema amesema kutokana na wadhifa huo, anatumaini makubwa Mkurugenzi huyo ataendelea kuiongoza Mamlaka hiyo kwa utendaji makini na kwa weledi wa hali ya juu unaozingatia ufanisi na uadilifu usio na shaka yoyote. 

Pia amemtaka Bw. Mayongela kujenga timu yenye nguvu kwenye Mamlaka 
itakayoongozwa kwa misingi ya dira sahihi na mwelekeo mmoja kwa 
wote, unaoheshimu na kuzitumia fani za kila mtumishi wa Mamlaka
ipasavyo kwa manufaa mapana ya Taifa.

"Mungu akuzidishie hekima katika majukumu yako," amesema Mhandisi Prof. Lema.

Uthibitisho huo uliwasilishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issac Kamwelwe na kusomwa katika mkutano wa Mameneja wa Viwanja vya Ndege Tanzania uliofanyika hivi  karibuni Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias.

Halikadhalika, Bw. Mayongela baada ya uthibitisho huo rasmi aliwashukuru 
Watumishi wote wa Mamlaka na kusema hatua hiyo imechangiwa na juhudi za pamoja na ushirikiano kwa kipindi chote cha takribani miezi 11 alichokuwa akikaimu nafasi hiyo.

"Bila nyie nisingeweza kufanya kitu chochote, na hali kadhalika bila ushirikiano wenu peke   yangu nisingeweza," amesema Bw. Mayongela.

Hatahivyo amewasisitizia Watumishi wenzake kuchapa kazi kwa weledi, bidii, maarifa na uzalendo mkubwa usioweza kutiliwa mashaka ya aina yoyote kwa kuwahudumia Wadau na Watanzania wote kwa ujumla ili kuleta tija kubwa kwa taifa.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA)

Thursday 30 August 2018

MultiChoice Yatangaza Washindi Watakaopata Fursa ya Mafunzo ya Filamu Nairobi, Kenya

Na Mwandishi Wetu
MULTICHOICE  Tanzania, Imetangaza  washindi  wanne waliokidhi vigezo katika shindano la MultiChoice Talent Factory lilizinduliwa rasmi mapema mwezi Mei mwaka huu . Programu hii itawezesha jumla ya vijana 60 kutoka katika nchi mbalimbali barani Afrika kuweza kupata mafunzo ya filamu kwa kipindi cha mwaka mmoja katika vituo vitatu tofauti, kimojawapo kikiwa nchini Kenya (Nairobi) ambapo vijana hawa watakuwapo ifikapo tarehe 01 Oktoba mwaka huu. 

Mchakato mzima  wa kupatakana kwa washindi hawa ulichukua takribani muda wa miezi miwili ambapo kwa hapa nyumbani Tanzania tulipokea maombi kutoka kwa vijana zaidi ya 160, yaliyofuatiwa na mchujo ulifanyika tarehe 20 Julai Mwaka huu hapa Dar es Salaam Tanzania.

“Maendeleo ya nchi yetu kwa muda mrefu yamekuwa yakitambuliwa kwa uwekezaji katika maliasili nyingi tulizonazo kama vile madini, kilimo, mifugo, wanyamapori, na kadhalika huku sekta ya ubunifu ikiwa haijapewa kipaumbele kikubwa na hivyo sekta ya sanaa na ubunifu kuwa na mchango mdogo katika ukuaji wa uchumi wetu.

 Ili kuhakikisha kuwa tunasaidiana na serikali katika mkakati wake wa kuifanya sekta ya ubunifu na sanaa kuwa moja ya mihimili ya uchumi wetu, MultiChoice imeanzisha programu hii na tumeanza na sekta ya filamu. 


Vijana wa kitanzania waliofanikiwa kufudhu katika mchakato huu ni Sarah Kimario  kutokea Dar es Salaam, Wilson  Nkya kutoka Kigoma, Jamal Kishuli kutoka Arusha na Jane Moshi kutoka mkoa wa Kilimanjaro, alisema Ronald Shelukindo, Meneja Uendeshaji MultiChoice Tanzania.


Tumebarikiwa kwa vipaji vingi katika fani mbalimbali na bila shaka tukiwekeza katika vipaji vya vijana wetu bila shaka tutafanikiwa kupanua wigo wa ajira na uchumi wetu na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.

Amesema mafunzo hayo yataanza rasmi mwezi Oktoba mwaka huu itawawezesha vijana hawa wanne kutoka Tanzania kuungana na vijana wengine kutoka nchi mbali mbali za Afrika katika vyuo maalum vya mafunzo ya utengenezaji wa filamu ambavyo vitakuwa nchini Nigeria, Kenya na Zambia.


Kwa upande wao, washindi waliotangazwa kufudhu katika program hii wametoa shukrani zao za dhati hususani kwa kampuni ya MultiChoice sambamba na serikali ya Tanzania kwa ujumla. Akiongea katika hafla nhiyo, 

Wilson Nkya mmoja kati ya vijana waliopata fursa hiyo alisema kuwa “ Kipekee hii ni fursa tuliyokuwa tukiisubiri kwa muda mrefu na tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa Kampuni ya MultiChoice, serikali na jamii yote kwa ujumla.  Tunaahidi kufanya kila liwezekanalo na mtegemee matokeo chanya kutoka kwetu’, alimalizia Wilson.



UEFA Yapanga Makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya, Nyota Cristiano Ronaldo Kukutana na Man United


ZURICH, Uswisi
MANCHESTER United itaungana na Cristiano Ronaldo baada ya kupangwa na mabingwa wa Ligi Kuu ya Italia, Serie A, Juventus katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Ronaldo, ambaye aliichezea Man United kwa mafanikio makubwa katika miaka ya 2003 na 2009, alijiunga na Juve kwa gharama ya pauni milioni 99.2 mwezi uliopita baada ya miaka tisa ya kuitumikia Real Madrid.

Valencia na Young Boys ni timu zingine zilizopangwa katika Kundi H.
Tottenham wenyewe wamepnagwa katika kundi gumu, ambapo itawabidi kukabiliana na wakali Barcelona, wakati washindi wa pili wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu huu, Liverpool watakabiliana na Paris St-Germain (PSG) na Napoli.

Mabingwa PSV Eindhoven na Inter Milan wanakamilisha Kundi B, ambalo pia litakuwa na timu ya England Tottenham  na Red Star Belgrade ni timu nyigine ambayo itacheza na kikosi cha kocha Jurgen Klopp katika Kundi C.

Mabingwa wa Ligi ya England Manchester City wamepangwa katika Kundi F pamoja na Shakhtar Donetsk, Lyon na Hoffenheim.

Mabingwa watetezi Real Madrid, ambao wameshinda taji hilo kwa miaka mitatu mfululizo, wenyewe wako katika Kundi G pamoja na Roma, CSKA Moscow na Viktoria Plzen.

Ratiba Kamili ya Makundi:
Kundi A: Atletico Madrid, Borussia Dortmund, Monaco na Club Brugge.

Kundi B: Barcelona, Tottenham, PSV Eindhoven na Inter Milan.

Kundi C: Paris St-Germain, Napoli, Liverpool na Red Star Belgrade.

Kundi D: Lokomotiv Moscow, Porto, Schalke na Galatasaray.

Kundi E: Bayern Munich, Benfica, Ajax na AEK Athens.

Kundi F: Manchester City, Shakhtar Donetsk, Lyon na Hoffenheim.

Kundi G: Real Madrid, Roma, CSKA Moscow na Viktoria Plzen.

Kundi H: Juventus, Manchester United, Valencia na Young Boys.

Nditiye aiagiza TAA kufanya ukaguzi wa mwisho wa viwanja vya wananchi waliohamishwa Kipawa ili wakabidhiwe

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) , Richard Mayongela leo kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa eneo la kuondokea na kuwasili abiria mashuhuri, VIP. 

Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, ameagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, wakakague viwanja 537 vilivyotengwa maeneo ya Msongola, kwa ajili ya waliokuwa wakazi wa eneo la Kipawa jijini Dar es Salaam Jumanne wiki ijayo ili kujiridhisha kama viwanja hivyo vipo na  vinafaa.

Mhandisi Nditiye ametoa agizo hilo leo Agostri 30, 2018, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwe nye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo alieleza wasiwasi wake kuwa kampuni iliyopewa kandarasi ya kuwatafutia viwanja wananchi hao haijatekeleza wajibu wake ipasavyo licha ya kuwa tayari imelipwa kiasi cha shilingi bilioni 3.7.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Richard Mayongela akimkaribisha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto) ili azungumze na waandishi wa habari baada ya kutembelea TAA.

“Nakuagiza Mkurugenzi wa TAA, kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Wilaya Jumanne ijayo muende mkakague eno hilo la viwanja 537 muone kama vipo kwa sababu kumekuwa na shida sana na hawa wenzetu wa Tanzania Remix Centre  nyinyi wenyewe mnajua, kuna shida ya miundombinu, sasa lazime mjue eneo hilo linafikika, na viwanja hivyo vinajengeka.” Alisema

Ofisa Tarafa wa Ukonga Jijini Dar es Salaam, Nicodemus Shirima akizungumza wakati wa ziara hiyo ya Naibu Waziri Nditiye. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha.
Alisema Wananchi wako tayari kushirikiana na serikali katika kuhakikisha upanuzi wa uwanja unakwenda vizuri.

Kampuni ya Tanzania Remix Centre ilipendekezwa na Manispaa ya  Ilala na kupewa kandarasi ya kutafuta viwanja kwa ajili ya makazi mapya ya wananchi waliokuwa wakiishi eneo la Kipawa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo kulikuwepo na mivutano kati ya Mamlaka na Wananchi ambapo baadhi yao walipeleka shauri hilo mahakamani na hiovyo kufanya zoezi hilo la kuwahamisha wananchi hao kwenye eneo hilo jipya kusuasua.
Rosemary Shimata, mwakilishi kutoka Tanzania Remix Centre.

Hata hivyo akitoa taarifa kwa Mhe. Naibu Waziri Nditiye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw.Richard Mayongela alisema, Novemba mwaka jana, TAA ilikutana na wadau wakiwemo wananchi, Manispaa ya Ilala, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Kampuni iliyoingia ubia na Manispaa ya Ilala katika kutafuta viwanja kwa ajili ya wananchi hao.

“Mradi huu ulihusisha upatikanaji wa viwanja 1,600 kwa mujibu wa mkataba wa awali ambapo fidia yake ilipaswa kufanywa kwa awamu mbili ya watu 800, hata hivyo kwa mujibu wa sheria kipinde kile ilitaka mwananchi apewe eneo lakini alipwe fidia pia.” Alisema na kufafanua kuwa.

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza na waandishi wa habari alipofanya ziara Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA. Mwingine ni Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Richard Mayongela.
“Sasa wananchi wa Kipawa na Kigilagila walilipwa fidia kwa mujibu wa sheria na kwao hakukuwa na tatizo, kwa maana walipewa fedha taslimu na viwanja maeneo ya Pugu Mwakanga.” Alisema Bw. Mayongela

Akieleza zaidi Bw. Mayongela alsiema Baada ya kufanya tathmini, ilibainika kuwa wananchi wa Kipunguni A na Kipunguni Mashariki ambapo kulikuwa na viwanja 1,186 baada ya kufanya tathmini viwanja vilivyohitajika siyo 1,600, bali ni 1,186, kwa ajili ya fidia ya wananchi wa maeneo hayo mawili na katika viwanja hivyo viwanja 537 serikali ilishatoa kiasi cha shilingi bilioni 3.7 ili kutekeleza zoezi hilo.
 
Sisi kwa kushirikiana na mbia wa Mnaispaa ya Ilala yaani Tanzania Remix Centre, tukaandaa vile viwanja na viwanja vile vimeshapatikana na kuanzia hivi sasa, viwanja hivyo vitagawiwa kwa wananchi.

Aidha, katika hatua nyingine, Mhe. Nditiye amesema wakati umefika sasa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kuanzisha kitengo cha Estate ili kihakikisha viwanja vyake vyote nchini vinakuwa na hati miliki.

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto) akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Richard Mayongela baada ya Nditiye kuzungumza na waandishi wa habari.
“Naguagiza uunde kitengo cha Estate kisichozidi watu 10 ili kihakikishe kila kiwanja kinachomilikiwa na TAA kinakuwa na hati miliki na hii itaepusha migogoro na wananchi.” Alisema.

Tuesday 28 August 2018

Viwanja vya Ndege Songwe, Kigoma, Mwanza navyo vyakabiliana na Ebola vikifuata mfano wa JNIA

Ofisa Afya wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, Bw. Peter Maseke (katikati) akikagua hati za kusafiria za mmoja wa abiria aliyekuwa akisafiri kuelekea Dar es Salaam, ambapo pembeni yake ni mashine maalum inayotambua abiria wenye homa kali, ambayo ni moja ya dalili za ugonjwa wa Ebola.


Na Mwandishi Wetu

UONGOZI wa Viwanja vya Ndege vya Songwe na Kigoma, umejiandaa kwa kushirikiana na maafisa afya, kuhakikisha hakuna mgonjwa mwenye dalili za Ebola anaingia nchini, akitokea maeneo ya Tunduma na nchini Burundi.

Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, Bw. Pius Kazeze alimwambia Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi.Bahati Mollel kwa njia ya simu kuwa, tayari Maafisa wa Afya wameshafunga mashine maalum (thermo scanners) inayotambua joto la mwili la abiria ambaye anasafiri kwa kupitia kiwanja hicho, na likizidi 38 anatakiwa kutoa taarifa za afya yake.

Mmoja wa abiria akikaguliwa na mashine ya mkono, iliyoshikwa na Afisa Afya wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, Bw. Peter Maseke, ikiwa ni moja ya njia za kudhibiti wagonjwa wa Ebola wasiingie nchini. Ugonjwa huo umetangazwa hivi karibuni kusambaa nchini Kongo.
Bw. Kazeze amesema Kiwanja cha Songwe ni tofauti kidogo na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo zaidi wanakagua abiria wanaoondoka kwa kuwa wengi wanatoka mpakani maeneo ya Tunduma na kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

“Tayari maafisa Afya wamefunga mashine ya ukaguzi wa afya eneo la nje la kuondokea abiria kwani kwetu huku tunapata abiria wengi wanaotoka nchi jirani wanaopitia mpakani Tunduma, hivyo wengi wao wanatoka nchi zinazopakana na Kongo, ambayo inasadikika ugonjwa wa Ebola umeibuka kwa kasi kubwa,” alisema Bw. Kazeze.

Hatahivyo, amesema mbali na mashine hiyo kubwa iliyowekwa sehemu maalum, pia wanamashine mbili ndogo zinazotumiwa kwa kushikwa mkononi na maafisa Afya, lakini wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa Watumishi wa afya, ambao tayari wameshaomba kuongezewa mmoja ili kufanikisha kazi hiyo kuwa rahisi.

Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma, Bw. Theophan Bileha amesema wapo mbioni kiweka kifaa hicho kwa kuwa wanatarajia abiria kutoka Burundi watakaowasili kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), itakayoanza safari zake kuanzia Agosti 30, 2018.

“Tumeshafanya kikao na wenzetu wa Afya, na wameahidi kuleta mashine mojawapo, tunatarajia abiria wanaotoka Bujumbura, kwani tumeambiwa ATCL itaanza kwenda huko kuanzia tarehe 30, na hawa wapo watakaoshuka hapa na wengine wanakwenda kwenye viwanja vingine kulingana na ratiba ya ndege hii,” alisema Bw. Bileha.
 
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigoma, Dk. Peter Nsanya amesema mashine hiyo itawekwa kiwanjani hapo kwa kipindi, ambacho ndege zinatua na baada ya ratiba za ndege kumalizika, wanahamishia eneo la Bandarini kwa kuwa pia kuna abiria wanaotoka maeneo mbalimbali.

“Sisi tumejipanga kukabiliana na maradhi haya ikiwa na kuhakikisha hatutaruhusu uingie nchini, na ndio maana tunaratiba za ndege, ambapo tutakuwa tunakwenda kutoa huduma, na baadaye kuhamia bandarini,” amesema.

Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Mohamed Maulid amesema wamejiandaa kwa kushirikiana na Maafisa Afya wamekuwa wakitumia mashine ya mkono kwa ukaguzi wa abiria wanaotoka nchi za Uganda, Nairobi na Kongo.

Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka. Hivi karibuni  umetangazwa kutokea nchini Kongo na kusababisha vifo.

Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na misuli, mwili kulegea, kutapika, kuharisha, vipele na kutokwa damu.

Juzi Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kilitangaza kuchukua hatua kali za kuweka zuio kwa abiria wanaongia nchini kupitia Kiwanja hicho, ambapo kumefungwa vifaa ambavyo vinabaini joto la abiria na endapo litazidi nyuzi joto 38, atatakiwa kutoa maelezo zaidi ya maisha yake.

Pia abiria wote wanaowasili kwa ndege zinazotoka nchi jirani na Kongo wanatakiwa kupitia eneo maalum ambalo hutakiwa kunawa mikono yao kwa dawa maalum ili kuua vijidudu mbalimbali.

 IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO CHA MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA)


Sunday 26 August 2018

JNIA Yajidhatiti Kudhibiti Ugonjwa wa Ebola


1.       Mlango wa kuingilia abiria kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wanaotoka nje ya nchi, ambao baadhi ya ndege zimelengwa kutokana na abiria wake aidha kupita au kuanzia safari kwenye nchi ya Kongo iliyotangazwa kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola.

Na Mwandishi Wetu

KITENGO cha Afya katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kimeweka udhibiti madhubuti wa  kujikinga na usambazaji wa magonjwa ambukizi, ikiwemo Ebola.

Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka. Hivi karibuni  umetangazwa kutokea nchini Kongo na kusababisha vifo.
Eneo maalum la ukaguzi wa afya kwa abiria mara baada ya kuingia kwenye sehemu ya wanaowasili kutoka nje ya nchi, ambapo kumefungwa mashine maalum zenye kuonesha joto la mwili na likizidi 38 abiria huyo hufanyiwa mahojiano ya afya yake, kwa kuwa moja ya dalili za ugonjwa wa Ebola ni kuwa na joto kali

Akizungumzia kuhusiana na mikakati hiyo ya kupambana na magonjwa ambukizi ukiwemo wa Ebola,  Ofisa Afya Mfawidhi wa JNIA, Dk. George Ndaki alisema wanatoa mafunzo kwa watumishi na wahusika wote wanaotumia kiwanja hicho katika kujikinga na magonjwa hayo.

“Sisi tumejiandaa vizuri na tumeshafanya jitihada zote tumeshatoa maelekezo, mafunzo na kamati mbalimbali za kiwanja zimejipanga kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza, ikiwemo sisi wenyewe kujikinga na kuwakinga na abiria wote wanaotoka katika nchi hatarishi”, alisema Dkt. Ndaki.

Aidha, akizungumzia kuhusiana na utaratibu ambao Kiwanja kimeweka ili kuhakikisha abiria wenye maambukizi wanapokelewa kwa tahadhari, ambapo wanapowasili na ndege zinazotoka nje ya nchi zinazopakia abiria wanaosafiri kutoka katika nchi zinazoshirikiana na Kongo hutakiwa kusafisha mikono kwa dawa maalum mara waingiapo katika eneo la kuwasili.

1.        Mmoja wa abiria aliyewasili na ndege ya Rwanda Air kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), akinawa mikono kwa dawa maalum inayoua vijidudu vya maradhi mbalimbali yanayoambukiza, ukiwemo Ebola uliotangazwa hivi karibuni umeibuka nchini Kongo.

 Pia abiria hao wanapoingia katika lango la kuwasili la abiria kutoka nje ya nchi, kumekuwa na mashine maalum inaangalia joto la mwili na likizidi nyuzi joto 38 wanamtaka kutoa maelezo zaidi ya afya yake.

“Abiria wote wanapowasili hupita katika eneo maalum ambalo wote hutakiwa kuosha mikono, lakini pia kuna mashine ambazo zimewekwa ili kuweza kuwatambua abiria ambao wanawasili wakiwa na hali ya joto isiyokuwa ya kawaida mfano kuwa na joto la juu sana kuanzia 38oC, ukiachana na hilo kuna fomu maalum ambazo abiria wanapowasili hujaza na pia taarifa kutoka kwa rubani wa ndege kama kuna abiria ana maambukizi kwenye ndege. Baada ya kumtambua mgonjwa basi atapitishwa katika njia ya tofauti na abiria wengine na kupakiwa katika gari la wagonjwa na kupelekwa Temeke Hospital,” alisema Dk. Ndaki.

1.       Ofisa Afya Mfawidhi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dkt. George Ndaki akionesha mashine maalum inayompima abiria (thermo scanners) mara anapopita eneo la ukaguzi wa afya, ambapo linakuwa likisomwa na Afisa Afya kwenye komputa iliyopo (kulia). JNIA wamejidhatiti na makonjwa ya milipuko ukiwemo wa ebola uliotangazwa kuwepo nchini Kongo.

 Naye Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Paul Rwegasha akitoa ufafanuzi juu taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Ebola, ameeleza kuwa tayari JNIA wanazo taarifa za mlipuko wa ugonjwa huo na taratibu zote zimeshachukuliwa kwa kuwakagua abiria wanaotoka nje ya nchi.

“Kwanza kabisa kwa abiria wote ambao wanatokea katika nchi ambazo zinasadikika kuwa na maambukizi wanapowasili wanakuwa sanitized (wanaosha mikono na dawa maalum) ili wasiweze kuleta maambukizi ndani, lakini pia tuna thermo scanners  (mashine ambazo zinaangalia hali ya joto la mtu) anapowasili ambapo tunapogundua mgonjwa anamatatizo tunapeleka isolation (Chumba cha wagonjwa wa kipekee) na baada ya hapo anapelekwa katika vyumba vya waonjwa waliotengwa katika hospitali ya Temeke” alibainisha Bw. Rwegasha.

1.        Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (kulia) akizungumza na waandishi wa habari juu ya udhibiti wa magonjwa ya mlipuko kwenye kiwanja hicho. Hivi karibuni ugonjwa wa Ebola umetangazwa kutokea nchini Kongo.


Katika hatua nyingine Dk. Ndaki alisema mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote ambaye amebainika kuwa na ugonjwa wa Ebola kupitia JNIA.

Dk Ndaki ametaja namna ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola ni pamoja na kuepuka kugusa damu, machozi, jasho, matapishi, kamasi, mkojo au kinyesi cha mtu mwenye dalili za ugonjwa; pia mtu hatakiwi kugusa, kuosha au kuzika maiti ya aliyekufa kwa Ebola; pia usiguse au kula wanyama kama popo, sokwe au swala wa msituni.

Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na misuli, mwili kulegea, kutapika, kuharisha, vipele ma kutokwa damu


“Natoa wito tu kwa wananchi kuhakikisha wanafuata taratibu zote tulizoziweka ili kuhakikisha kwamba hatupati mgonjwa yeyote katika nchi yetu. Kama kila mtu atatekeleza wajibu wake kwa abiria kufuata taratibu, wanaosimamia masuala ya afya wakitimiza wajibu wao, na Kiwanja kikitimiza wajibu wake basi hakika magonjwa ya mlipuko hayataweza kufika katika nchi yetu” alieleza Dkt. Ndaki.


Saturday 25 August 2018

Uchukuzi watakiwa Kulinda Mataji, Kutwaa Zaidi




Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dk Leonard Chamuriho (kushoto) akipokewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari katika viwanja vya TCAA, ambako bonanza hilo lilifanyikia. 

Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Michezo ya Uchukuzi (USC) imetakiwa kubakisha na kuongeza mataji iliyopata katika mashindano yaliyopita ya Mei Mosi na kutwaa ushindi wa jumla baada ya kujikusanyia vikombe 13.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dk Leonard Chamuriho wakati akifungua bonanza la kwanza la Sekta ya Uchukuzi lililofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Ukonga Banana Jijini Dar es Salaam.
Chamuriho kwanza aliipongeza USC kwa kutwaa ushindi huo wa jumla wa mashindano ya Mei Mosi yaliyofanyika mjini Iringa mwaka huu, lakini aliwataka kuulinda ushindi huo na kuongeza vikombe vya michezo mingine, ambayo hawakutwaa nafasi ya kwanza.

“Nawapongeza Uchukuzi Sports Club kwa kutwaa ubingwa, lakini kwa kweli kushinda ni jambo rahisi, lakini kuulinda ushindi huo ni jambo gumu sana, hivyo nawataka muulinde ubingwa huo na muongeze mataji mengine, “alisema Chamuriho.
Alisema kuwa lazima Uchukuzi waendelee kubaki namba moja katika michezo, hivyo alisema watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanaendelea kung’ara katika michezo yote watakayoshiriki.

 Mbali na kuzindua bonanza la kwanza la sekta ya Uchukuzi, pia Chamuriho alizindua rasmi mazoezi ya USC kwa ajili ya mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara na Tawala za Mikoa, Shimiwi, ambayo mwaka huu itafanyika mjini Dodoma mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari (kushoto) akiwafanyisha mazoezi wafanyakazi wa Uchukuzi, akiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dk Leonard Chamuriho  (mwenye track suit) leo.
Pia aliwasisitizia kuwa atajitahidi kutatua changamoto zinazoikabili USC ili kuhakikisha klabu hiyo inatekeleza majukumu yake vizuri ya kuendeleza michezo na kuwawezesha wafanyakazi wa Uchukuzi kuwa na siha bora.

Katibu Mkuu wa USC, Mbura Tenga wakati akimkaribisha mgeni rasmi alisema kuwa lengo la bonanza hilo ni kuwakutanisha wafanyakazi wa wizara bila kujali kada zao, jinsia, rangi au dini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dk Leonard Chamuriho (mbele) wakati wa bonanza la michezo la Uchukuzi leo.
Malengo mengine ni kukuza, kusimamia na kuongoza shughuli za michezo kwa wafanyakazi, kushirikiana na Shimiwi kuendeleza michezo kwa mujibu wa taratibu zinazojulikana.

Pia kuanzisha na kukuza uhusiano mwema kati ya viongozi wa wizara, wafanyakazi na wizara zingine huku kubwa zaidi likiwa kuitangaza Wizara-Sekta ya Uchukuzi kupitia shughuli zake kupitia michezo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari akizungumza wakati wa uzinduzi wa bonanza la michezo la Uchukuzi Sports Club leo. Kulia ni Paul RwegashaMkurugenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA). 
Hivi karibuni USC ilikabidhi makombe 13 ya ushindi wa Mei Mosi kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ambapo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Grayson Mwaigombe alipokea vikombe hivyo kwa niaba ya Chamuriho.

Mbali na mazoezi pia kulikuwa na michezo ya kuvuta kamba, mpira wa miguu, mpira wa wavu na mingineyo, ambayo ilichezwa na wafanyakazi wa Sekta ya Uchukizi, ambao walijitokeza kwa wingi leo.











Tuesday 21 August 2018

Simba Yafungua Pazia Ligi Kuu na Tanzania Prisons kesho


Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Simba ksho wanaingia kwenye mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi hiyo kuwakabili Tanzania Prison katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Simba inashuka dimbani kama Bingwa mtetezi baada ya kutwaa kombe hilo msimu uliopita ikiwa na pointi 69 nyuma ya Azam waliokuwa na 58.

Simba inaingia uwanjani ikiwa na hali ya kujiamini baadaa ya jumamosi iliyopita kutwaa ubingwa wa Ngao ya jamii na hasa uwepo wa kikosi kipana chenye wachezaji wenye uwezo mkubwa.

Ni wazi kuwa Simba itapambana katika kuhakikisha inapata pointi tatu kwani ilifanya jitihada za kutosha katika kujindaa na msimu wa Ligi hiyo baada ya kuweka kambi ya wiki mbili nchini Uturuki.

Kocha wa timu hiyo Patric Aussems alisema kikosi chake kimefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo na kudai kuwa michezo ya kirafiki ilikuwa ni kwa lengo la kuangalia sehemu zenye matatizo.

“Nimetumia michezo ya kirafiki kama maandalizi ya Ligi Kuu nina imani na kikosi kilichopo,ila kuna wachezaji walipata tatizo na kutolewa dhidi ya Mtibwa hivyo nitasikiliza ripoti na wengine watatumika,”alisema Aussems.

Kocha huyo anaimani kuwa kikosi chake kitafanya vizuri kwani pamoja na kukerwa na mbinu ya wachezaji wake kutumia mipira mirefu aliahidi kulifanyia kazi suala hilo.

Michezo mingine ya Ligi hiyo itakuwa ni Ruvu Shooting na Ndanda, Alliance na Mbao Fc,Coast Union na Lipuli ya Iringa, Singida na Biashara Mara na mchezo mwingine ni Kagera Sugar na Mwadui ya Shinyanga.


TFF Yapitisha Waamuzi 82 Kuchezesha Ligi Kuu Bara


Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepitisha majina ya waamuzi 82 kuchezesha Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa mwaka 2018/2019.

Katika orodha hiyo wapo waamuzi wa kati 30,Waamuzi wasaidizi 46 na Waamuzi 6 wa akiba.

Waamuzi hao ndio watakaokuwa na jukumu la kucheza mechi zote za Ligi Kuu katika msimu husika.

Na uteuzi huo umefanyika baada ya mtihani wa vipimo kwa waamuzi hao uliofanyika mjini Dar es Salaam mapema mwezi huu.

Waamuzi waliopitishwa ni Athuman Selukala (Arusha), Erick Onoka (Arusha), Alex Magayi (Dar es Salaam), Elly Sasii (Dar es Salaam), Isihaka Mwalile (Dar es Salaam), Israel Nkongo (Dar es Salaam), Mbaraka Rashid (Dar es Salaam), Nadim Aloyce Leonard (Dar es Salaam) na Liston Hiyari (Dar es Salaam).

Wengine ni Florentina Zabron (Dodoma), Ally Simba (Geita), Amada Simba (Kagera),Jonesia  Rukyaa (Kagera), Hussein Athumani (Katavi), Shomari Lawi (Kigoma), Alfred Vitares (Kilimanjaro), Jacob Adongo (Mara) na Benedict Magai (Mbeya).

Wengine ni Athumani Lazi, (Morogoro), Fikiri Yussuf (Morogoro), Martin Saanya (Morogoro), Abubakar Mturo (Mtwara), Daniel Warioba (Mwanza), Emmanuel Mwandembwa (Mwanza), Ludovick Charles (Mwanza), Ahmad Seif Mbaraka (Pwani), Nassoro Mwinchui (Pwani), Jimmy Fanuel (Shinyanga), Meshack Suda (Singida) na Hance  Mabena wa Tanga.

Waamuzi wasaidizi au washika vibendera waliopitishwa ni Agnes Pantaleo (Arusha), Abdallah Uhako (Arusha), Gasper Keto (Arusha), Frank Komba (Dar es Salaam), Germina Simon (Dar es Salaam), Hamisi Chang'walu (Dar es Salaam), Helen Mduma (Dar es Salaam), Iddi Mikongoti (Dar es Salaam) na Kassim Mpanga (Dar es Salaam).

Wengine ni Lulu Mushi (Dar es Salaam), Omary Kambangwa (Dar es Salaam), Shaffi Mohamed (Dar es Salaam), Soud Lilla

(Dar es Salaam), Charles Simon (Dodoma), Godfrey Msakila (Geita), Janet Balama (Iringa), Rashid Zongo (Iringa), Edgar Lyombo (Kagera) na Grace Wamala (Kagera).

Wamo pia Jamada Ahmada (Kagera), Athumani Rajab (Kigoma), Soud Hussein (Kigoma), Sylvester Mwanga (Kilimanjaro), Leonard Mkumbo (Manyara), Robert Ruemeja (Mara), John Kanyenye (Mbeya), Mashaka Mandembwa (Mbeya), Jesse Erasmo (Morogoro), Nickolas Makaranga (Morogoro), Consolata Lazaro (Mwanza), Frednand Chacha (Mwanza), Josephat Masija (Mwanza), Michael Mkongwa (Njombe), Abdallah Rashid (Pwani) na Kassim Safisha (Pwani).

Wengine ni Khalfani Sika (Pwani), Japhet Kasiliwa (Rukwa), Joseph Pombe (Shinyanga), Julius Kasitu (Shinyanga), Makame Mdogo (Shinyanga), Arnold Bugardo (Singida), Justina Charles (Tabora), Martin Mwaliaje (Tabora), Nestory Livangala (Tabora), Haji Mwarukuta (Tanga) na Mohamed Mkono (Tanga).

Waamuzi wa akiba waliopitishwa ni Steven Daudi Makuka (Iringa), Ahmadi Benard Augustino (Mara), Ally Mkonge (Mtwara), Abdallah Kambuzi (Shinyanga), Shaaban Msangi (Singida) na Omary Mdoe (Tanga).