Saturday 2 February 2019

Denis Suarez Kuichezea Arsenal Ikiikabili Man City


LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Arsenal Unai Emery kumpanga mchezaji mpya aliyesajiliwa juzi Denis Suarez  (pichani) na kuichezea kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu ya England dhidi ya Mabingwa wa ligi hiyo Manchester City katika mchezo utakaofanyika kesho.

The Gunners wanasafiri hadi kwenye Uwanja wa Etihad kwa ajili ya mchezo huo unaotarajia kuwa mkali na wa kusisimua baada ya kukamilika kwa dirisha la usajili, ambapo klabu hiyo ilikamilisha usajili wa Suarez kwa mkopo akitokea Barcelona hadi mwishoni mwa msimu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye ameichezea mara mbili timu ya wakubwa ya Man City katika kipindi chake cha mwanzo cha kuichezea klabu hiyo, ndio mchezaji pekee aliyetua Arsenal, ambaye alishindikana kupata mkataba wa kudumu kutokana na ufinyu wa fungu.

Mkataba huo wa mkopo ni pamoja na kuwemo kipengele cha kuweza kuongeza mkataba wa muda mrefu kwa Suarez katika kipindi cha majira ya joto wakati mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania akihusishwa na kiujiunga tena na Emery, wakati akicheza chini ya Mhispania mwenzake katika klabu ya Sevilla.

"Nitafanya uamuzi kesho (leo) lakini endapo ataanza katika mchezo huo nina imani naye, “alisema Emery alipouilizwa ikiwa Suarez ataenda moja kwa moja katika timu ya Arsenal katika mchezo huo wa Jumapili.

"Namjua mchezaji huyo na alianza kujifua binafsi juzi. Leo alikuwa na wenzake. Ni jambo zuri, anaonekana kuelewa haraka.

"Ni mchezaji mwenye kiwango na nafikiri anaweza kutusaidia sisi kutokana na kiwango chake…, “alisema.

Ushindi kwa Manchester City utashuhudia timu hiyo ikiwakaribia vinara wa ligi hiyo Liverpool kwa pointi mbili, ambao watacheza dhidi ya West Ham siku moja baadae.

Kikosi cha Pep Guardiola alikuwa mpinzani wa kwanza wa Emery katika soka la Uingereza, ambako waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal Agosti.

Emery anatarajia kukutana na kikwazo kingine lakini alisema wachezaji wake wako tayari kuonesha uwezo wao dhidi ya wapinzani wazuri.

"Itakuwa mechi ngumu, tunacheza dhidi ya timu bora, “alisema.

"Sasa, Liverpool, wamefanya kazi kubwa sana wakati wa Ligi Kuu msimu huu. Labda wamepoteza baadhi ya mechi., lakini hiyo ni kama ajali tu.

Qatar Mabingwa Wapya Kombe la Asia

Qatar baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Asia kwa mara ya kwanza, abada ya kuifunga Japan kwa mabao 3-1 juzi. (Picha na Mtandao).

TOKYO, Japan
WENYEJI wa Kombe la Dunia 2022 Qatar wametwaa kwa mara ya kwanza kabisa taji la Asia baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya mabingwa mara nne wa taji hilo Japan.

Mshambuliaji Almoez Ali alivunja rekodi ya mchezaji kupachika mabao mengi katika mashindano hayo ya Kombe la Asia pale alipofunga bao lake la tisa kwa kichwa katika mchezo huo wa fainali.

Abdulaziz Hatem aliiweka timu yake kuwa mbele kwa mabao 2-0 baada ya kufunga kwa shuti la umbali wa kama meta 20 kabla Japan haijafunga bao lao la kufutia machozi kupitia kwa  Takumi Minamino akiwa ndani ya boksi.

Mabao yalikuwa 3-1 baada ya Akram Afif (mtoto wa kiungo wazanmani wa Simba, Hassan Afif) kufunga kwa penalti baada ya mchezaji anayeichezea klabu ya Southampton, Maya Yoshida kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Teknolojia ya VAR ilithibitisha kuwa beki huyo wa Southampton, ambayo inajukana kama Watakatifu aliishika kwa makusudi mpira huo, ingawa picha marudio za TV zilionesha kama aliushika kwa bahati mbaya.

Penalti hiyo ya Afif ilikuwa na maana kuwa mchezaji huyo alifunga bao moja na kusaidia mara 10, ikiwemo mara mbili katika mchezo huo wa fainali, wakati wa mechi saba za Qatar katika mashindano hayo huko Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kikosi cha kocha waQatar, Felix Sanchez kimecheza saa 10 na dakika nane bila ya kuruhusu bao hata moja katika mashindano ya mwaka huu ya Asia kabla ya kufungwa na Minamino.

Kijazi Aagiza Makatibu Wakuu Kuhimiza Michezo

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Bi Maimuna Tarishi (mwenye miwani) akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Mhandisi Dr. Leonard Chamuriho kabla ya kuanza kwa mbio za pole (jogging) za bonanza la Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), iliyoanzia kwenye Uwanja wa Jamhuri hadi Ofisi za Bunge na baadaye kurudi Jamhuri


Mwandishi Wetu, Dodoma
KATIBU Mkuu Kiongozi, ambaye pia ni Mkuu wa Utumishi wa Umma, Balozi Mhandisi John Kijazi amewaagiza Makatibu Wakuu kuhimiza michezo mahala pa kazi kwa vitendo ili kuwa na watumishi wa Umma wenye afya njema.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Maimuna Tarishi kwa niaba ya Balozi Kijazi katika Bonanza la Michezo lililoandaliwa na Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), na kufanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Tarishi ameweka msisitizo kwa kuwa michezo ni kazi na kazi ni michezo, ambapo sasa Makatibu Wakuu waweke mazingira yatakayowezesha watumishi wa umma kupitia taasisi zao waweze kushiriki kwenye michezo mbalimbali, ambayo inajenga umoja na ushirikiano baina ya watumishi.


“Haya ni maagizo ya Katibu mkuu kiongozi amenituma nije niseme kwa kuwa yupo katika kazi nyingine, wito ni kwa Makatibu Wakuu wote na wakuu wa taasisi kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi yatakayowezesha watumishi kufanya mazoezi mara kwa mara na hata katika michezo kama hii ya Shimiwi,” amesema Bi. Tarishi.

Amesema sasa uwekwe utaratibu kwa Watumishi wa Umma kushiriki michezo ambayo haitatumia gharama kama wanavyodhania wengine.

“Kwa waajiri hatuna budi kuweka mazingira wezeshi ya kuwawezesha Watumishi kuwa na utaratibu wa kushiriki kwenye michezo yeyote na hii inafanyika bila gharama yeyote kabisa kwani wakati mwingine tunakimbilia hatuna fedha au hajatenga kifungu katika bajeti wakati hata hapa ukiangalia hakuna gharama kubwa iliyotumika,” amesisitiza Bi. Tarishi.
Amewataka watumishi wa umma kufanya mazoezi ya kila wakati ili kujiweka katika afya kwa wakati wote, ambayo itawasaidia kufanya kazi kwa weledi.

Bi. Tarishi ametoa pia maagizo kwa viongozi wa Shimiwi, kwa kuwa sasa wameanza kufufua michezo hii baada ya kusimama kwa muda mrefu, na sasa waendelee mbele kwani yanawakutanisha Watumishi wa maeneo mbalimbali ya kazi ya serikali na husaidia kubadilishana uzoefu.

“Hii ni rai yangu kwenu kwa kuwa sasa mmeanza tena michezo yenu hii tunapenda tuone inasonga mbele kwani hushirikisha watumishi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali, na yanajenga umoja kama watumishi wa umma, na tuwekee maanani na kutekeleza haya,” amesema Bi. Tarishi.

Hatahivyo, amesema michezo ni nidhamu hivyo kuwe na nidhamu kwenye michezo kwani kutasaidia watumishi kufanya kazi kwa bidii na kuwa na ubinifu wa hali ya juu.

Naye Mwenyekiti wa Shimiwi, Daniel Mwalusamba amesema wachezaji wanahimizwa kufanya mazoezi kwa ajili ya kujenga, kulinda na kuimarisha afya zao.

“Michezo ni kazi hivyo wanapaswa kuzingatia taratibu na miongozo inayokuwa imetolewa kila wakati na serikali, na kama agenda ya kitaifa ilivyo ya kujenga Tanzania ya Viwanda, na ili tufanikiwe tunahitaji kuwa na Watumishi wenye afya bora wanaoweza kufanya majukumu yao kwa wakati na kushiriki michezo mbalimbali, ambapo sasa wanaweza kuandaa mabonanza sehemu za kazi kwa siku ya za mwishoni mwa wiki,” amesema Bw. Mwalusamba.

Hatahivyo, amesema katika kikao cha juzi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hazina na kuwahusisha Wenyeviti na Makatibu wa klabu za michezo mahala pa kazi, ambapo wamekumbushwa kusimamia michezo kwa kuwa ni sehemu ya kazi na wanapaswa kusimamia na kutekeleza majukumu yote yanayotolewa na serikali.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, Bi. Bertha Bankwa (wa kwanza kulia mstari wa nyuma) leo akijumuika kufanya mazoezi na watumishi wa Umma katika bonanza la Shirikisho la Michezo Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), lililofunguliwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Bi. Maimuna Tarishi (Hayupo pichani). (PICHA NA BAHATI MOLLEL WA MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA- TAA).
Katika michezo iliyochezwa jana kwa upande wa kuvuta Kamba wanaume timu ya Waziri Mkuu wametoa jasho na Mambo ya Ndani na kutoka sare ya mvuto 1-1; wakati katika netiboli timu ya Utumishi imechapwa na Tamisemi magoli 24-17; huku Afya wakiwashinda GST magoli 9-6.

Katika mchezo wa soka Utumishi wamewachapa Afya magoli 2-0; huku Ardhi wamewashinda Mwanasheria Mkuu kwa magoli 4-0.

Friday 1 February 2019

Shimiwi wahimiza mabonanza kuimarisha afya

Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo la Wizara, Idara, wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi, Daniel Mwalusamba (katikati) akiendesha kikao cha viongozi wa klabu mbalimbali kilichofanyika leo, kwenye ukumbi wa mikutano wa Hazina, jijini Dodoma. Wengine kushoto ni Makamu Mwenyekiti Ally Katembo na kulia ni Katibu Mkuu Moshi Makuka.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKISHO la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala wa Serikali, na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), imehimiza ushiriki wa mabonanza ya michezo mbalimbali kwa Watumishi wa Umma ili kuboresha afya zao.

Mwenyekiti wa Shimiwi, Daniel Mwalusamba amesema leo jijini Dodoma, katika mkutano wa wenyeviti na makatibu uliofanyika kwenye ukumbi wa Naibu Waziri wa Fedha katika jengo la Hazina.

Mwalusamba amesema kwa sasa serikali inahimiza ujenzi wa viwanda, ili tufikie uchumi wa kati, ambapo Watumishi wa Umma wanatakiwa kuunga mkono hatua hiyo iliyotangazwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli.

“Tuondokane na zana ya Shimiwi kuwa imekufa kwani hili ni Shirikisho la michezo ambalo lipo kihalali na linaendeshwa kwa utaratibu, na mapendekezo yote yapo kisheria,” amesema Mwalusamba.

Hatahivyo, Mwalusamba amesema Shimiwi inakumbwa na changamoto za klabu kwa kushindwa kwenda na katibka kwa kufanya chaguzi zake kwa wakati, ikiwa ni kufuata katiba iliyopo.

“Hairihusiwi kikatiba kwenye mkutano mkuu kuingia na viongozi ambao hawajachaguliwa kihalali na kukaa kwa muda mrefu, kwani ni kinyume na katiba yetu ya Shimiwi na pia Katiba Mama ya Serikali, ambayo imeweka wazi juu ya muda wa ukomo wa uongozi,”

Amesema ni kinyume na katiba na viongozi wa shimiwi wanaweza kwenda kwa Katibu Mkuu wa wizara husika, na sasa Shimiwi itafanya ukaguzi na kugundua klabu iliyo na uongozi uliomaliza muda, hali kadhalika katiba za klabu zinapitishwa na baraza, na sio kikundi kinachojiendesha chenyewe bila kufuata katiba.

Ameagiza klabu sugu zikafanye chaguzi zao ili kuepusha mgogoro, kwani  Shimiwi  imekuwa mfano wa kuigwa kwa kufuata taratibu tofauti na mashirikisho mengine.

Kijazi kubariki Bonanza la Shimiwi Dodoma kesho

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WATUMISHI zaidi ya 1,000 kutoka Wizara na Idara za Serikali leo watashiriki kwenye Bonanza la Michezo litakaloongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma ambaye pia ni Mlezi wa Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), litakalofanyika Jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema bonanza hilo litatanguliwa na mbio fupi fupi (jogging) zitakazoanzia kwenye uwanja wa Jamhuri hadi maeneo ya Bunge na kurudi kiwanja cha Jamhuri, ambapo mbali na Katibu Mkuu Kiongozi, pia watashiriki Watendaji Wakuu wa kutoka taasisi mbalimbali za Umma.

Mwalusamba amesema baada ya mbio hizo wachezaji wote walioshiriki ;watafanya mazoezi ya viungo na baadaye kushiriki kwenye michezo ya netiboli, soka na kuvuta Kamba.
Wajumbe wa klabu mbalimbali za Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa wakimsikiliza Mwenyekiti, Daniel Mwalusamba alipoendesha kikao leo kwenye ukumbi wa mikutano Hazina Dodoma.
“Hili bonanza ni moja ya njia ya kuwaweka watumishi wa umma katika afya njema na kuepuka magonjwa nyemelezi, ambapo mtumishi ataweza kufanya kazi kwa weledi na bidi kwa kuwa wanakuwa na afya nzuri,” amesema Mwalusamba.

Pia amesema bonanza hilo litaendelea kesho (Jumapili) kwa michezo mbalimbali.
Akizungumzia uwepo wa mashindano ya michezo ya SHIMIWI, ambayo imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali, Mwalusamba amesema mashindano hayo yapo na hayajafutwa na yatafanyika kulingana na taratibu.

“Hii michezo haijafutwa lakini kumekuwa na mabadiliko ya kiutaratibu, ambapo sasa serikali yetu ipo katika harakati za ujenzi wa viwanda na sisi ni watu muhimu wa kuimiza hilo, hivyo michezo itaendelea kama ilivyopangwa,” amesema Mwalusamba.
Hatahivyo, amehimiza Watumishi wa Umma kuhakikisha wanatekeleza agizo la Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan la watumishi wafanye mazoezi kila Jumamosi ya Pili ya kila mwezi, ili waweze kujiweka vyema katika afya.

Klabu mbalimbali zimekuwa zikiendesha michezo mbalimbali kwa kushirikisha klabu kwa kushirikiana.