Monday 27 November 2017

Uhamiaji yaanza kwa kishindo netiboli Muungano

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Uhamiaji imeanza vizuri kutetea taji lake la netiboli la Muungano baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 40-39 dhidi ya Mafunzo katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana mjini Zanzibar.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Judithi Ilunda, mchezo huo ulikuwa wa vuta nikuvute na hadi robo ya kwanza inamalizika, timu hizo zilikuwa sare ya 11-11.

Katika robo ya pili, Uhamiaji walikuwa mbele kwa mabao 21-19 na ile ya tatu washindi waliendelea kuwa mbele kwa mabao 36-28.

Ligi hiyo inachezwa kwa makundi,ambapo Kundi A lina timu za Mafunzo, Uhamiaji, Jeshi Stars, Zima Moto na Duma kuhu Kundi B likiundwa na JKU, JKT Mbweni, Polisi Arusha, KVZ na Afya.

Katibu Mkuu wa Chaneta, Judith Ilunda
Aidha, Ilunda alisema kuwa timu za Polisi Morogoro na Madini ya Arusha zimeshindwa kushiriki na kuifanya Tanzania Bara kuwa na timu nne katika mashindano hayo wakati Zanzibar wana timu sita.

Alisema kuwa pamoja na kutotoa taarifaya kutoshiriki lakinihadi sasa timu hizo zilikuwa hazijawasilisha barua zao za sababu ya kushindwa kuwepo katika ligi hiyo ya Muungano.


Ilunda alisema kuwa wanatarajia mashindano hayo yatakuwa na msisimko wa aina yake na kupatikana kihalali mshindi wake.

Ligi hiyo inaendelea asubuhi hii leo Jumanne kwa Zimamoto kucheza dhidi ya Duma, Polisi Arusha itapepetana na mabingwa wa Tanzania Bara JKT Mbweni huku KVA watapelekana puta na Afya na Jeshi Stars watafunga pazia leo kwa kucheza na mabingwa wa Zanzibar Mafunzo.

Sunday 26 November 2017

Arusha Mabingwa wa Riadha ya Wanawake 2017

Wanariadha wakichuana katika mbio za meta 5,000 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.
 Na Mwandishi Wetu
MKOA wa Arusha umekuwa bingwa wa kwanza wa mashindano ya taifa ya riadha yaliyomalizika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Arusha walitawazwa mabingwa baada ya kumaliza wakiwa na medali mbili za dhahabu. Tatu za fedha na moja ya shaba, huku wenyeji Dar es Salaam walishika nafasi ya pili kwa kupata medali mbili za dhahabu na moja ya shaba.
Timu ya mkoa wa Kaskazini Pemba ilitwaa nafasi ya tatu baada ya kupata medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na tatu za shaba.
Katika mashindano hayo yaliyofungwa jana na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida nafasi ya nne ilikwenda kwa mkoa wa Kaskazini Unguja iliyopata medali moja ya dhahabu na moja ya fedha.
Pwani walishika nafasi ya tano baada ya kupata medali moja ya dhahabu na moja ya fedha, huku Tabora wakimaliza wa sita kwa medali moja ya dhahabu na moja ya fedha.
Dodoma walimaliza wa saba wakiwa na medali moja ya dhahabu na moja ya shaba huku Kilimanjaro ikimaliza na medali moja ya dhahabu na kumaliza katika nafasi ya nane.
Kivutio katika ufungaji jana ilikuwa katika mbio za meta 5,000 wakati mwanariadha wa Mwanza, Silvia Masatu licha ya kukimbia akiwa peku, alitoka nyuma na kumshinda Amina Mohamed wa Arusha kwa kutumia dakika 17:52:00.
Mwanariadha wa Mkoa wa Ruvuma, Rose Seif akiruka chini katika mashindano ya taifa ya wanawake leo kwenye Uwanja wa Taifa.
Amina alimaliza wa pili baada ya kuongoza kwa muda mrefu na kumaliza mbio hizo kwa dakika 18:03:37 wakati Anastazia Dolimongo wa Shinyanga alimaliza watatu kwa dakika 18:06:50.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa udhamini JICA, lengo ni kuchagua timu ya taifa itakayosaka viwango vya kushiriko Olimpiki ya 2020 Tokyo.


Wanariadha wa mchezo wa kuruka chini wakipewa maelekezo kabla ya kushiriki katika mchezo huo leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hotuba ya Mkurugenzi wa Shule za Filbert Bayi, Anna Bayi Siku ya Wazazi na Mahafali ya Chekechea 2017



Ndugu Akofa Ata, Mkurugenzi Mkazi, Unilever Tanzania

Ndugu Meja Mstaafu Filbert Bayi M/kiti, Bodi ya Wakurugenzi,
Viongozi wa Elimu Mkoa wa Pwani,
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi,
Wajumbe wa Bodi ya Shule,
Wanakamati wa shule, Wazazi,
Wafanyakazi, Wanafunzi,
Wageni waalikwa,  Mabibi na Mabwana.

SHUKRANI
Kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa baraka zake kwa kuweza kukutana tena mwaka huu tukiwa wenye afya njema.   Kipekee ninawashukuru wote mliohudhuria kwa kukubali mwaliko wetu ili tuweze kujumuika pamoja kusherekea siku hii ya wazazi na mahafali ya watoto wetu wa Chekechea  mwaka 2017. Kwa dakika chache naomba tusimame tuwakumbuke wazazi waliotutangulia mwaka huu wa 2017. 

Mkurugenzi wa Shule za Filbert Bayi, Anna Bayi.
HISTORIA YA  SHULE YA CHEKECHEA NA MSINGI
Mhe. Mgeni rasmi shule zetu za chekechea na msingi ziko katika makundi mawili kama ifuatavyo:-
i)  Kimara Dar es Salaam
    
Mwaka 1996 tulianzisha shule ya chekechea na msingi iliyopo Kimara na tulipata usajili mwaka   
    2000 kwa namba DS/02/7/007.  Mpaka sasa shule ina jumla ya wanafunzi 405 pia tunao waalimu     25 na wafanyakazi wasio waalimu 15

ii)  Mkuza-Kibaha
     Shule hii ilisajiliwa mwaka 2010 kwa namba PW.01/7/008.  Na ina jumla ya wanafunzi 290
     waalimu 17 na wafanyakazi wasio waalimu 10.

HISTORIA YA SHULE YA SEKONDARI
Mhe. Mgeni Rasmi Shule ya Sekondari Filbert Bayi yenye usajili wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi namba S.1377 na kituo cha Mitihani namba S.1437  ilianzishwa rasmi mwaka 2003 kule Kimara palipo Makao Makuu ya taasisi yetu na Kampasi ya shule ya Msingi.

Hatimaye majengo yalipokamilika Februari, 2004 tulihamia hapa Mkuza, Kibaha na kuzinduliwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu Mhe.   Benjamin William Mkapa hapo tarehe 02/03/2005.

MAHAFALI YA CHEKECHEA
Ndugu  Mgeni Rasmi, Shule yetu ina utaratibu wa kufanya sherehe za mahafali ya wanafunzi wa Chekechea. Utaratibu huu ulianza mwaka 2006 na hii ni mahafali ya 12 kwa upande wa Kimara na 7 kwa Mkuza - Kibaha. 

Leo hii tunao jumla ya wanafunzi wa chekechea 71  kwa pande zote mbili Kimara na Mkuza ambao watapokea vyeti vyao vya kuhitimu Elimu hii ya awali. 

MAENDELEO YA SHULE
Ndugu Mgeni Rasmi shule zetu zina  mafanikio makubwa kitaaluma na michezo tangu zilipoanzishwa  kama ifuatavyo:-

i)  Shule za Chekechea 
Ndugu Mgeni Rasmi shule zetu za chekechea zinajitahidi sana katika taaluma ambapo wanafunzi wanaohitimu huingia darasa la kwanza na hatimaye kufika Sekondari.  Ni mategemeo yetu kuwa wanaohitimu leo hii wataendelea hadi watakapohitimu elimu ya msingi na sekondari.

ii)  Matokeo ya Mitihani - Msingi
Mwaka huu wa 2017, wanafunzi  63 wa darasa la saba walifanya mitihani ya Taifa na wamefaulu kwa asilimia (100%),  matokeo yao yanatuhakikishia watachaguliwa kwenda Sekondari.  Pia tunaamini wengi wao watarudi Shule yetu ya Sekondari,  kwani wanajua ubora na huduma za shule zetu. Tunawapongeza walimu wote wa darasa la saba kwa bidii na juhudi zao kubwa walizofanya kuhakikisha watoto wanafanya vizuri katika mitihani yao.

iii) Matokeo ya Mitihani - Sekondari
Mwaka 2016  wanafunzi  29 walifanya mtihani wa kidato cha nne na matokeo yao yalikuwa ni daraja la 1, 2 na 3 hakuna aliyepata daraja IV wala.

Tuna imani na matarajio makubwa zaidi ya haya kwa wanafunzi wetu waliomaliza kidato cha nne hivi karibuni nao watafanya vizuri kwa juhudi kubwa walizoonyesha Wanafunzi na Walimu  kwa ushirikiano na Wazazi.

SAFARI ZA KITAALUMA, MKOA WA IRINGA
Mhe. Mgeni Rasmi, shule zetu za Msingi na Sekondari zina utaratibu tuliojipangia wa kuwa na safari za kielimu kwa kutembelea  maeneo mbalimbali ya kihistoria ndani na nje ya nchi.  Mwezi Agosti mwaka huu  2017, Wanafunzi, Walimu na wafanyakazi wasio Walimu upande wa Sekondari walitembelea  Mkoa wa Iringa katika maeneo mbalimbali ya kihistoria kama vile Isimila, Mbuga za Wanyama za Ruaha, Kiwanda cha maziwa cha Asas nk.

MAZINGIRA
Ndg. Mgeni Rasmi Shule za Filbert Bayi zina utaratibu mahususi wa kutunza  MAZINGIRA ambapo  kila mwanafunzi hupewa mti na eneo la kutunza ikiwa ni zoezi endelevu hadi atakapoondoka shuleni kwetu ili ikamsaidie huko aendako kujua umuhimu wa kutunza mazingira.

ELIMU YA UJASIRIA MALI
Pamoja na masomo ya darasani, vijana wetu wanajifunza masomo ya ujasiriamali kama ufugaji wa kuku, upambaji wa kumbi kwa ajili ya sherehe mbalimbali, upishi, ususi, kunyoa, kupamba  maharusi na kutengeneza nywele. Taaluma hizi ninaamini zitawasaidia kuwa wajasiria mali wakati wamalizapo shule na vyuo.

SOBER HOUSE
Ndugu Mgeni Rasmi Taasisi ya Filbert Bayi inayo kituo kinachosaidia   watu walioathirika na Madawa ya Kulevya ambapo huwaweka kituoni kwa miezi minne kwa kuwafundisha na  kuwatibu, kuwapa ushauri nasaha , kuwajenga kiimani kwa kuwafundisha neno la Mungu na shughuli mbalimbali za Ujasiriamali.  Nashauri wazazi wenye ndugu au watoto wenye shida hiyo wawasiliane na ofisi ili wapewe maelekezo. Lakini pia wanaoguswa kusaidia mahitaji kwa waathirika hawa mf : Sabuni, mafuta na mavazi tunawakaribisha kufanya hivyo.

KITUO CHA AFYA
Taasisi ilianzisha Zahanati 2014 ambayo inasaidia wanafunzi na wananchi wengi wanaotuzunguka hapa shuleni na mwaka 2016 tulipandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya.  Kituo chetu kinatoa huduma ya  vipimo mbalimbali ikiwemo upimaji Malaria, Ultra Sound, Full blood Picture, Cholestrol, Figo, Ini na vinginevyo.  Pia kituo kinatoa huduma ya mama na mtoto (RCH) ambazo zinatolewa bure lakini akinamama wanapojifungua huwa wanachangia gharama.

HITIMISHO
Ndugu Mgeni Rasmi tunakuomba utukamilishie siku hii kwa kutoa machache uliyonayo ikiwa ni pamoja na  kukamilisha sherehe zetu za Mahafali ya watoto wetu wa Chekechea na siku ya  Wazazi mwaka 2017 kwa kuwakabidhi Vyeti wahitimu na zawadi mbalimbali  kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo. 

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.

THE SPEECH OF THE GUEST OF HONOUR- FILBERT BAYI PRE-SCHOOL GRADUATION AND ANNUAL PARENTS DAY 25TH NOV 2017

Mkurugenzi Mkazi wa Unilever Tanzania, Akofa Ata.

Retired Major of the Armed Forces of Tanzania  Mr. Filbert Bayi

Executive Managing Director
Mrs Anna Bayi

Regional and Local Educational officers,

Members of Schools’ Board of Directors

School Committee members
Parents, invited guest, and students    
  
Mwenyekiti wa Shule za Filbert Bayi, Meja Mstaafu Filbert Bayi.
I would to take this opportunity to thank Mr. and Mrs. Bayi for inviting me to be a Guest of Honour on this very important and crucial day to witness Our Children the Pre-School pupils  graduating and the occasion of this year Annual Parents day Celebration.

I want to state that I have been very impressed by what the Chairman of the Board Mr. Filbert Bayi and The Managing Director Mrs. Anna Bayi  for setting up such huge and great investment , on Education , on Sports,  health facilities for both students and community surrounding the school. 

I have been also very impressed by the way the children did their presentation before us  here today expressing excellent intellectual performance.

I have also  witnessed very encouraging  confidence of the pupils and secondary students during their exhibition of their work, they have shown courage, good command of English language and competence of the subject matter. Your pupils and students have really done a good job to my observation, and of course we should appreciates teachers for that great work they are doing.

I should say that I was excited to hear the speech of the Managing Director on Academic performance of Filbert Bayi Pre-Primary, Primary and Secondary school  students. Parents and government should take note of such performance and encourage  such people like Mr. and Mrs. Bayi who are investing on education for our children.

It is natural that any good result demand a great preparation and command a huge cost. We should therefore appreciate that  the  Management of this school has really  created a good environment for learning for our pupils.

Employing of good and competent teachers must also be another factor which has contributed to such good performance. Such performance for standard seven, for Form two and Form four reflect a good picture of the school to the outsiders.

I would like to encourage the parents to continue supporting Mr. and Mrs. Bayi for a continued good work they are doing here.

Our Children and the society around us should appreciate for the additional  services provided here and make use of them such as Filbert Health Centre services in addition to Education services and many others.

Thank and may our good God strengthen you to continue serving our young generation our tomorrow leaders.

Thanks 

Sunday 19 November 2017

Wakenya Watamba KIA Marathon 2017

Na Mwandishi Wetu, Hai
WAKENYA wametamba katika mbio za kwanza za Kilimanjaro International Airport Marathon 2017 baada ya kushika nafasi za juu katika kilometa 21 na 42 kwa wanaume na wanawake.

Ushindi huo umefanya mamilioni ya fedha za zawadi kwenda nchini Kenya baada ya Duncan Kwemboi kushika nafasi ya kwanza katika mbio za kilometa 42 kwa kutumia saa 2:19:10 na Meshack Kirotich kumaliza wa pili kwa kutumia saa 2:21:25.

Mshindi wa tatu katika mbio hizo za marathon naye alikuwa Mkenya, Abraham Too aliyemaliza kwa kutumia saa 2:22:42.

Katika mbio za kilometa 42, ambazo mshindi wa kwanza hadi watatu aliondoka na Sh milioni 5, milioni 4 na milioni 3.

Kwa upande wa wanawake, katika kilometa 42 mbio hizo nazo zilitawaliwa na Wakenya,huku Failuna Abdi ndiye alikuwa Mtanzania aliyeshika nafasi ya juu baada ya kumaliza watatu katika mbio za kilometa 21.

Failuna alimaliza mbio hizo kwa kutumia saa 1:16:22 na kujinyakulia kiasi cha sh milioni 2, huku Dickson Marwa naye wa Tanzania alimaliza watano katika kilometa 21 kwa wanaume.

Marwa ambaye hivi karibuni alitamba katika mbio za Rock City Marathon na zile za Zanzibar, wakati katika mbio za KIA alipata sh milioni 1.5 baada ya kutumia saa 01:06:51.

Abdi akizungumza baada ya kumaliza mbio hizo alisema kuwa anasikitika sana kwa Wakenya kutawala mbio hizo kwani Watanzania kama wangejiandaa vizuri wangeweza kushinda.

Aliwataka wanariadha wa Tanzania kufanya mazoezi kwa bidii ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mbio zingine ndani na nje ya nchi.

Naye Marwa alisema kuwa ushindi ulikuwa mkali hasa kutoka kwa Wakenya ambao walikuwa wengi katika mbio hizo, lakini amefarijika kuwa Mtanzania aliyemaliza katika nafasi ya tano.


Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema kuwa mbio zimeanza vizuri kwa kushirikisha wanariadha wengi, lakini baadhi ya mambo hayakuandaliwa vizuri na kusababisha baadhi ya wanariadha waliomaliza mbio kutopewa medali zao kama walivyoahidiwa.

Mshindi wa mbio za kilometa 21 kwa wanaume, Mkenya Joel Kipmatai alisema kuwa mbio zilikuwa nzuri lakini hawakupata upinzani mkubwa kutoka kwa Watanzania.

Alisema mbio hizo zimeanza vizuri na zinatakiwa kurekebisha matatizo machache ili kuzidi kuziboresha na kuwa moja yam bio kubwa duniani miaka ijayo.

Mgeni rasmi katika mbio hizo za Kwanza za Kilimanjaro Internatinal Airport alikuwa Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Nackson aliyekabidhi zawadi kwa washindi.

Friday 17 November 2017

TAA kusaka hati miliki za viwanja vya ndege




Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama mbele), akiongea na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Transit uliopo kwenye jengo la kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema itahakikisha inapata hati za viwanja vyake vya ndege ili kupunguza uvamizi kutoka kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela  alitoa kauli hiyo leo kwenye mkutano na wafanyakazi uliofanyika katika ukumbi ya Transit uliopo jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI), ikiwa ni moja ya mikakati ya mamlaka hadi kufikia Juni 2018.
Bw. Mayongela alisema tayari wameanza taratibu za kupata hati miliki kwa viwanja 13, vikiwemo vya JNIA na Mwanza zilizofutwa awali.
Hata hivyo, Wananchi wamekuwa na tabia za kuvamia maeneo ya viwanja vya ndege kwa kufanya makazi na mashamba, jambo ambalo ni hatarishi kiusalama.
Bw. Mayongela alisema mkakati mwingine ni kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya viwanja vya ndege 58 vinavyomilikiwa na serikali na ambavyo havipo chini ya serikali.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kutoka Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu (hayupo pichani) aliyekuwa akiongelea mikakati na masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya taasisi hiyo.
“Pia tutaanda kikosi kazi kitachosaidiana na wenzetu wa TANROADS katika usimamizi na uangalizi wa viwanja vya ndege  vinavyoendelea kujengwa maeneo mbalimbali nchini,” alisema Bw. Mayongela.
Katika hatua nyingine Bw. Mayongela alisema pia mamlaka inampango wa kuendeleza miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya abiria, Mizigo, ufungaji wa taa za kuongezea ndege na ufungaji kamera za usalama (CCTV) kwenye viwanja vya Arusha, Mwanza, JNIA na Dodoma.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa uweledi na uwazi, ili kufikia malengo yaliyowekwa na hatakuwa tayari kumfukuza mtumishi kazi kwa masuala yasiyokuwa na msingi.
“Ninafungua milango kwa wafanyakazi mje ofisini kwangu kwani hii ni ofisi ya rasilimali watu na sio rasilimali mtu, naweka milango wazi mje tujadili masuala ya kazi ya kujenga na sio majungu,” alisisitiza Bw. Thobias.

Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias (aliyesimama mbele), akizungumza na Wafanyakazi katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Transit uliopo kwenye jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).