Thursday, 29 October 2015

Ukumbi wa kisasa wa King Solomon ndio habari ya mjini kwa sasa Dar

Mmoja ya milango ya mbele katika ukumbi wa King Solomon.

Ukumbi wa King Solomon kwa mbele.
 

Milango  kwa mbele.
Sehemu ya juu ya ukumbi wa King Solomon uliopo Namanga jijini Dar es Salaam.

 Diamond kumsindikiza mkali Wizkid wa Nigeria Jumamosi


Muimbaji Nassib Abdul au Diamond akiimba wakati wakati wa mazoezi kwenye ukumbi wa King Solomon uliopo Namanga jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kutumbuiza na Wizkid wa Nigeria Jumamosi.


Na Mwandishi Wetu
MSANII wa muziki wa kizazi kipya Nassib Abdul, Diamond Platinum ataimba jukwaa moja na msanii mahiri kutoka Nigeria, Wizkid katika tamasha litakalofanyika katika viwanja vya Leaders Kinondoni Jumamosi.

Akizungumza na waandishi wa habari mratibu wa onesho hilo, Solomon Nassuma alisema kuwa, msanii huyo atawasili Ijumaa mchana tayari kwa shoo hiyo.

Alisema kuwa tiketi za viti maalum ndio zimeshaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali kama vile katika migahawa yote ya Eaters Points iliyopo Oysterbay na Namanga, Onetash, migahawa yote ya KFC pamoja na hotel ya Rainbow Mbezi. 

Aliongeza kuwa kwa wale watakaokata viti maalum kutakuwa na magari kwa ajili kuwachukua kutoka maeneo mbalimbali ambapo watakuwa wameegesha magari yao.

Alisema kuwa maeneo hayo ni katika eneo la ukumbi wa King Solomon Hall na mgahawa wa Eaters point Oysterbay yatawabeba na kuwapeleka moja kwa moja ukumbini na kisha kuwarudisha tena kwenye magari yao baada ya kumalizika kwa onesho.

"Hii inatokana na ukweli kwamba hawa watu wa VIP tunataka wafurahie fedha zao za kiingilio kwa kuwa wamekata fedha kubwa na inatakiwa kuhakikisha kuwa wanafurahia shoo pia" alisema Nassuma.

Aliongeza: "Kwa tiketi nyingine za kawaida zitaanza kuuzwa siku hiyo hiyo ya shoo na naomba wananchi mbalimbali kujitokeza kushuhudia kwani tayari zoezi la Uchaguzi Mkuu lilishamalizika.

Aliongeza kuwa pia watakuwa wasanii wengine kama vile Christian Bella pamoja na Farid Kubanda, Fid Q na wengine.
Baadhi ya madansa wa Diamond wakifanya mazoezi katika ukumbi wa King Solomon jana kwa ajili ya onesho la Jumamosi.
Meneja wa Diamond, Babu Tale alisema kuwa shoo hiyo imekuja wakati mzuri, ambapo Diamond ameshinda tuzo nyingi na tangu ashinde tuzo hizo hajawahi kufanya shoo hapa nchini, na hiyo itakuwa ya kwanza kwake.

"Hii inakuwa ni shoo ya kwanza ya Diamond tangia ashinde tuzo hizo na kwanza inakuwa ni shoo ya live sasa hayo ni mafanikio makubwa na wananchi wataona shoo hiyo wakati wakiwa ndio kwanza wametoka kwenye uchaguzi mkuu" alisema Tale.

Diamond ambae kwa sasa ni mmoja kati ya wasanii wakubwa barani Afrika ambapo ameshinda tuzo ya msanii bora wa Afrika Mashariki na Afrika katika tuzo za Afrima zilizofanyika Marekani huku akiwa pia ni mshindi wa tuzo ya msanii bora wa Afrika ya MTV EMA.

Friday, 23 October 2015

PONGEZI/SHUKRANI ZA TOC KWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA KUENDELEZA MICHEZO KATIKA MIAKA 10 YA UONGOZI WAKENapenda kuchukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kwa kuandaa hafla ya kutoa tuzo kwa wanamichezo 10 bora waliofanya vizuri kwa kuiletea heshima  nchi yetu katika miaka 10 ya uongozi wa mwanamichezo mwenzetu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na kutoa tuzo kwa Wanamichezo bora waliofanya vizuri miaka 10 iliyopita,  vile vile TASWA ilimtunuku tuzo Mhe Jakaya Mrisho Kikwete kwa mchango wako katika michezo.

Mhe. Rais, wakati anazungumza na wanamichezo waliokusanyika katika ukumbi wa Mlimani hapo tarehe 12/10/2015 alisononeka kwa wanamichezo wa Tanzania kutofanya vizuri wakati wa miaka 10 ya uongozi wake pamoja na kuleta walimu katika baadhi ya vyama vya michezo.

Mafanikio hata katika maisha ya kawaida ni mapambano hali kadhalika hata kupata mafanikio katika michezo ni mapambano. Katika miaka ya 70-80 michezo ilikuwa ridhaa, lakini kuanzia miaka ya 90 hadi sasa michezo imekuwa biashara na ajira kubwa kwa wanamichezo.
Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa akimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuendeleza michezo katika kipindi chake chote cha uongozi wake wa miaka 10.
Kwa mfumo huo wa michezo kuwa biashara na ajira kila moja angefikiria kwamba tungepaswa kuwa na wanamichezo wengi  kwa hiari yao kuchangamkia mazoezi ya hali ya juu ili nao waweze kuwa wawakilishi wazuri wa nchi yetu na kujipatia zawadi nono za fedha, lakini badala yake hali inazidi kuwa mbaya.

Hali hii inawezekana vile vile imesababishwa na hali ya ukata wa vyama vya michezo ambao hawana uwezo wa kutafuta vipaji huko walipo hasa Vijijini, Wilayani na Mikoani.

Katika miaka ya 70-80,  Vyama vyetu vilikuwa vinapata ruzuku kutoka Serikalini kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ruzuku ambayo ilikuwa inawasaidia kuendesha ofisi na kuandaa Mashindano  kama ya Taifa ambayo wanamichezo wengi wanakusanyika na vyama husika kufanya uteuzi wa wachezaji bora wenye vipaji ambao huwaendeleza.
Huo mfumo kwa sasa haupo kutokana na hali inayotamkwa na vyama vya michezo kama ukata na Serikali (BMT) kutokuwa na fedha.

Katika risala yake wakati wa tuzo kwa wanamichezo bora, Mhe. Rais alikiri bila kuwekeza tusitegemee kupata mafanikio, lakini nani awekeze, kwa haraka kwa tulio na uelewa mdogo ni Serikali ndiyo iwekeze kama nchi zingine duniani inavyofanya.

Mhe. Rais amefanya mengi kuinua michezo wakati wa uongozi wake. Naomba nitaje chache:
1.     WALIMU WA MICHEZO KUTOKA NJE.
Aliweza kuwalipa mishahara walimu wa michezo kama mpira wa miguu, netiboli, ngumi na riadha (pamoja na walimu wa riadha kutokuwa wa viwango) kupitia mpango wa ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba. Kila mmoja wetu aliona jitihada zake,  na nakiri kwamba kwa namna moja au nyingine, vyama/mashirikisho ya michezo hawakutekeleza wajibu wao kutokana na hali ya ukata.

Hata wanamichezo wetu hawakutambua na kuona michezo kama ajira.
Mhe. Rais anakiri mafanikio yana gharama, bila nchi kuwekeza hafikirii kama tutakuwa na mwelekeo mwema hasa kwa vijana wetu kufanya vizuri katika medani ya Kimataifa. Nchi nyingi zinazofanya vizuri katika michezo ya kimataifa  kwa asilimia kubwa wamewekeza katika michezo. Pamoja na WHVUM kutengewa bajeti ndogo ya michezo, bado suala la kuwekeza haliwezi kukwepeka kwa hali ya sasa ya michezo duniani.

2.    MICHEZO YA UMITASHUMTA/UMISSETA.
Tutakukumbuka hasa pale Mhe Jakaya aliporejesha michezo ya Umitashumta na Umisseta  mwaka 2007 baada ya kusimama kwa zaidi ya miaka 9.
 
Binafsi naamini kilichotufikisha hapa tulipo leo ni pamoja na kutofundishwa kwa elimu ya viungo (PE) sambamba na kutokuwepo walimu wa masomo hayo kwenye shule zetu na kusimama kwa michezo hiyo  na  Michezo ya Majeshi (BAMATA).

Michezo ya Umitashumta/Umisseta ndiyo ilikuwa kiwanda cha kuandaa wachezaji ambapo wanapofanya vizuri hupata ajira katika taasisi za Serikali (JWTZ, Polisi, Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa) lakini kwa sasa imekuwa tofauti kwani taasisi hizo haziajiri kama ilivyo huko nyuma kutokana na kutofanyika Michezo ya Majeshi (BAMATA) ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa.

Ni zaidi ya miaka 8 tangu aliporejesha michezo ya Umitashumta/Umisseta kwa nia na madhumuni ya kupata vipaji vitakavyoendelezwa na kuwa na nafasi nzuri ya kutuwakilisha Kimataifa.

Imekuwa vigumu kuendeleza  vipaji vinavyoonekana katika michezo hiyo kwani hakuna maandalizi yaliyofanywa kuwaendeleza  baada ya michezo hiyo kumalizika. Hata wale wanaomaliza masomo yao katika ngazi husika hawapati ajira kutokana na taasisi za Serikali nilizotaja kutokuwa na ajira rasmi kama ilivyo zamani. Mpaka sasa ni shule chache za binafsi  na taasisi zimekuwa na  mpango wa kuwasajili katika shule zao wanafunzi wazuri wenye vipaji na baadhi yao kutoa elimu bure (Scholarships) na kuwaendeleza katika baadhi ya michezo:

a.Shule ya Sekondari ya Alliance, Mwanza (Mpira wa Miguu na Riadha).
 
b.Shule za Filbert Bayi, Mkuza, Kibaha Mkoa wa Pwani (Riadha na Netiboli)

c.Shule ya Sekondari ya Lord Baden Powel, Bagamoyo (Mpira wa Miguu kwa Wanaume na  Wanawake,  Mpira wa Kikapu, Mpira wa Wavu na Riadha).

d.Shule ya Sekondari ya Winning Spirit, Arusha (Riadha)

e.Shule ya Sekondari ya Makongo, Dar Es Salaam (Mpira wa Miguu, Netiboli Kikapu na Wavu).

Naomba niishauri Serikali (Wizara ya Elimu na Tamisemi) kuunda Kanda ili kila baada ya michezo ya Umitashumta na Umisseta wanamichezo wenye vipaji wawekwe katika shule zilizo katika Kanda zitakazoundwa wakiendelea na masomo hali kadhalika na kucheza kwa Wizara husika kupeleka wataalamu (coaches) katika Kanda husika. Kama hilo haliwezekani, basi shule binafsi na taasisi zisaidiwe ili ziweze kuimarisha zaidi mipango waliyonayo ya kuendeleza michezo

Bila kuwa na utaratibu na mipango mahsusi, michezo ya Umitashumta na Umisseta,  itakuwa kama tamasha tu.

3.     UWANJA WA TAIFA
Hakuna ubishi kwa ushiriki wake katika ujenzi wa uwanja wa Taifa wakati wa uongozi wa Rais wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa akiwa kama Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mpaka alipochaguliwa kuwa Rais wa awamu ya nne na kumalizia kazi za ujenzi zilizobaki.

Uwanja wetu ni mzuri sana, lakini matumizi yake kwa mchezo wa riadha yamekuwa nadra sana kutokana na gharama kubwa ambayo wakati mwingine  Riadha Tanzania inashindwa kuchangia hasa inapotaka kufanya michezo ya Taifa ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka.

4.     MAFANIKIO YA MICHEZO WAKATI WA UONGOZI WAKO.
Mhe. Jakaya wakati wa uongozi wake wa miaka 10 kulikuwa na mafanikio ambayo hayaridhishi kwa nchi kama Tanzania yenye watu zaidi ya Milion 45, lakini kutokana na hali halisi niliyotaja hapo juu naomba nitaje mafanikio hayo kama ifuatavyo:

Samson Ramadhani
1.Samson Ramadhani NYONYI, (Riadha):Marathon>Dhahabu: Michezo ya Jumuiya ya Madola, Melbourne, Australia 2006.

2.Fabian Joseph NAASI, (Riadha): Mita 10000>Shaba: Michezo ya Jumuiya ya Modola, Melbourne, Australia 2006.
Fabian Joseph.
3.Martin SULLE, (Riadha) Km 21.1>Medali ya Fedha>Michezo ya Afrika, Algiers, Algeria, 2007.

4.Timu ya Netiboli, (Netiboli)>Medali ya Fedha>Michezo ya Afrika, Maputo, Msumbiji, 2011.

5.Timu ya Netiboli (Netiboli)>Kushinda Kombe la Mataifa 6, Singapore, 2012.

6.Timu ya Netiboli (Netiboli>Nafasi ya Pili, Mashindano ya Africa, Dar Es Salaam, 2012.

7.Timu ya Mpira wa Miguu watoto wa Mitaani (Street Children World Cup)>Dhahabu, Mashindano Kombe la Dunia, Rio de Jeneiro, Brazil, 2014.

8.Timu ya Mpira wa Miguu-Vijana chini ya Miaka 15>Medali ya Fedha> Michezo ya Vijana Afrika, Gaborone, Botswana, 2014.

5.     SHUGHULI ZA TOC.
Wakati wa uongozi wake wa miaka 10 kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamati ya Olimpiki Tanzania imeweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa vyama vya michezo, baadhi ya hizo shughuli zilikuwa ni kuendesha mafunzo ya ufundi kwa walimu wa michezo kutoka Vyama/Mashirikisho ya michezo wanachama wa TOC kwa kuleta Wakufunzi kutoka nje ya nchi hali kadhalika na Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo kwa viongozi wa Vyama/Mashirikisho ya Mikoa na Taifa kwa nyakati tofauti.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Filbert Bayi (kushoto) akizungumza kabla ya kuwakabidhi hati wachezaji watatu wa Tanzania waliodhaminiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kupiga kambi Eldoret nchini Kenya. kutoka kulia ni Fabian Joseph, Fabian Nelson na Bazil John.
Kwa ujumla Walimu 523 (448/75) na viongozi 380 (304/76) waliweza kupata elimu ya kufundisha wachezaji kwa madaraja tofauti na uongozi na utawala bora.
(Orodha Nyongeza A na Bimeambatanishwa).

HITIMISHO
Kwa niaba ya Kamati ya Olimpiki Tanzania na kwa niaba yangu napenda nichukue nafasi hii kumshukuru Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kutoa posho za kujikimu, mavazi ya taifa, vifaa vya mazoezi na mashindano timu zetu za Taifa zilizowahi kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola (Melbourne, Australia 2006, New Delhi, India 2010 na Glasgow, Scotland 2014) na Olimpiki (Beijing, China 2008, London, Uingereza 2012).
Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi akisaini moja ya hati za kuwadhamini wanariadha watatu wa Tanzania kupiga kambi Eldoret, Kenya huku Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania, Suleuman Nyambui akishuhudia. Kushoto ni Rais wa TOC, Gulam Rashid.
Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru Mhe. Bernard Camillius Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushirikiano na WHVUM kuwatafutia mazoezi ya nje (China, Ethiopia, Uturuki na New Zealand) kwa kutumia mpango wa Diplomasia ya Michezo (Sports Diplomacy) wanamichezo wetu kabla ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, yaliyofanyika Glasgow, Scotland mwaka jana (2014).

Akiwa kama mwanamichezo nambari moja hata baada ya kustaafu bado wanamichezo wenzako tutahitaji ushauri wake katika maendeleo ya michezo katika
nchi yetu.

Mwisho kabisa natoa wito kwa wanamichezo wote kujitokeza na kutumia haki yao ya Kikatiba hapo Jumapili tarehe 25/10/2015 kupiga kura kuchagua mafiga matatu (Diwani, Mbunge na Rais) kwa kipindi cha miaka 5 (2015-2020) ijayo.

Nawatakia Wanamichezo wote kila la kheri katika mchakato mzima na tulinde  amani tuliyonayo.
 
Filbert Bayi,

KATIBU MKUU.


Tuesday, 20 October 2015

Dereva taxi India ahukumiwa kwa kumbaka abiria wakeDELHI, India

MAHAKAMA ya nchini India leo muda mfupi uliopita imemkuta na hatia dereva taxi wa `mtandaoni kwa kosa la kumbaka abiria wake mwanamke mwaka jana, imeelezwa.

Shiv Kumar Yadav pia alikutwa na kosa na jinai la kutishia na kuteka, alisema mwendesha mashtaka wa Serikali. Alikana mashataka hayo.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 26 alichukuliwa na kupelekwa mahali pasipo julikana ambako alibakwa baada ya kuboku safari yake kwa kutumia mtandao akiwa nyumbani Desemba mwaka jana.

Delhi baadae ilipiga marufuku utaratibu wa kukodi taxi kwa kutumia simu au mitandao mingine ya mawasiliano kutokana na matukio ya kialifu.

Hatahivyo, kampuni hiyo iliomba radhi kwa tukio hilo na kubainisha kuwa iko tayari kuweka utaratibu mpya na bora zaidi.

Mwanamke huyo pia alifungua kesi katika mahakama ya Marekani dhidi ya huduma hiyo, ambayo baadae ilimalizwa nje ya mahakama.

Vitendo vya ubakaji vimekuwa vikifuatiliwa kwa karibu nchini India tangu mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23 kubaka na kunyongwa katika basi jijini Delhi Desemba mwaka 2012, ambapo jumuiya ya kimataifa kutaka sheria kali kuhusu vitendo vya ngono na vurugu.