Thursday 29 March 2018

Timu ya Madola Yaondoka na Matumaini Kibao


Wachezaji na viongozi wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Dara es Salaam leo , kabla ya kuondoka kwenda Gold Coast, Australia.
Na Mwandishi Wetu
KUNDI la wachezaji 15 na viongozi kadhaa la timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola, limeondoka leo kwenda Gold Coast, Australia tayari kwa michezo hiyo itakayoanza Aprili 4 hadi 15.

Tanzania katika michezo hiyo inawakilishwa na timu za riadha, ngumi, mpira wa meza na kuogelea.

Timu hiyo ikiongozwa na meneja wao, Nasra Juma iliondoka kwa ndege ya Emirates huku nahodha wake, Masoud Mtalaso akitamba kuwa wako tayari kwa kuiletea nchi medali.
Makamu wa rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau akizungumza na wachezaji wa Tanzania watakaoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola, kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.
Kwa mara ya mwisho Tanzania ilipata medali kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 2006 Melbourne, Australia, ambako Samson Ramadhani na Fabian Joseph walirudi na medali ya dhahabu na shaba katika mbioza marathon na meta 10,000.

Rais na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid na Filbert Bayi wenyewe waliondoka Jumatano mara baada ya timu hiyo kuagwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe huku kiongozi wa msafara, ambaye ni Mkurugenzi wa Michezo Dk Yussuf Singo aliondoka tangu Jumapili.


“Tumekuwa tukifanya mazoezi ya nguvu kwa muda mrefu na ni matarajio yetu kuwa tutafanya vizuri katika michezo hiyo, “alisema Kidunda.

Naye Mtalaso alisema kuwa timu ya mpira wa meza imejiandaa vizuri hasa ukizingatia kuwa walipiga kambi nchini China kwa takribani miezi mitatu wakijifua kwa ajili ya michezo hiyo kabla ya kurejea nchini na kupiga kambi kwa mwezi mmoja Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.


Australia imekuwa sehemu ya bahati kwa timu ya Tanzania, ambapo ilifanya vizuri mwaka 1982 wakati ilipotwaa medali sita: Moja ya ngumi, tatu za riadha na mbili zilitoka katika mbio za uwanjani.
Gidamis Shahanga alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za meta 10,000, wakati Zakaria Barie, ambaye amesafiri na timu hiyo kama kocha, alishinda medali ya fedha katika mbio kama hizo. Juma Ikangaa alirudi na medali ya fedha katika marathon, huku ile ya shaba ikiletwa na bondia wa uzito wa juu, Willy Isangura na mtupa mkuki Zakayo Marekwa naye alileta medali ya shaba.

Mwanariadha wazamani wa Tanzania, Bayi ikiwa ni miaka 44 sasa anaendelea kushikilia rekodi ya Jumuiya ya Madola aliyoiweka mwaka 1974 ya meta 1500 michezo hiyo ilipofanyikia Christchurch, New Zealand. Bayi pia aliweka rekodi ya dunia, ambayo ilikuja kuvunjwa miaka mitano baadae na Sebastian Coe, ambaye sasa ni Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAAF).
Ikiwa ni miaka 12 sasa tangu kufanyika kwa Michezo ya Melbourne, timu ya Tanzania yenye wachezaji 16 inarejea tena Australia, ikiwa pia na micezo ambayo haikuwepo walipofanya vizuri nchini humo kama mpira wa meza na kuogelea.

Timu ya riadha inaundwa na wanariadha wa marathon, Stephano Huche, Said Makula na Sarah Rama­dhani.

Wakati Failuna Abdul atashindana katika mbio za meta 10,000, huku Ali Khamisi Gulam, atafanya vitu vyake katika mbio za meta 100 na 200, akiwa ni mwanariadha pekee wa mbio fupi katika timu ya riadha.

Anthony Mwanga ambaye anasoma Afrika Kusini, yeye atachuana katika michezo ya uwanjani ya miruko na mitupo katika timu hiyo ambayo iko chini ya Barie na Lwiza John.

Kikosi cha timu ya ngumi kinaundwa na Ezra Paulo (bantam), Kassim Mbutike (welter), Seleman Kidunda (middle) na Haruna Swanga (heavy). Timu hiyo iko chini ya kocha Mkenya, Benja­min Oyombi.

Awali kulikuwa na waogeleaji wawili, Hilal Hilal na Sonia Franco, chini ya kocha Kha­lid Yahya Rushaka. Wacheza mpira wa meza wako wanne, ambao ni Amon Tumaini, Masoud Mtalaso, Neema Mwaisyula na Fathiya Paz, ambao wako chini ya kocha Ramadhani Othman Suleiman.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, anatarajia kujiunga na timu hiyo baadae.

Wikiendi ya Mechi za Ligi Kuu ya England Imewadia


Na Mwandishi Wetu
WIKIENDI hiyoo inanyatia nyatia, wapenda soka kama nawaona vile wakila Sikukuu miguu juu, sasa Wakali wa soka DStv wanataka kunogesha zaidi sikukuu yako, shuhudia mechi kali za Premier League.

·       Mashetani wekundu wanakutana na viponde Swansea City, Je mdogo atampiga mkubwa? ukweli utajulikana baada ya dakika tisini siku ya jumamosi saa 11 jioni,  ndani ya SuperSport 10 kwenye kifurushi cha Bomba kw ash.19,000 tu.

·       Na Vinara wa Ligi ya Uingereza msimu huu Manchester City wanaingia Dimbani kuwavaa Everton, Jumamosi hii saa 1.30 usiku kwenye Supersport 3.  Je Rooney ataweza kuifunga timu yake ya zamani? Hakika hii si mechi ya kukosa.

Na Siku yenyewe sasa ya Pasaka, burudani ya ziada inapatikana hapa kwa wale wenye DStv. Jumapili hii tazama mechi kali kati ya Arsenal na Stoke City kuanzia saa 10 na nusu jioni, baada ya hapo tunahamia kwa wakali wa darajani wanapoingia dimbani kuwavaa Tottenham, je Tottenham wataweza kupambana bila harry Kane, yote tutajua Jumapili hii saa 1 kamili usiku, ndani ya Supesport 3 kupitia DStv Compact.

Ni Full Vyenga Bila Chenga mwanzo mwisho… unasubiri nini sasa? Jiunge na DStv leo ufaidi utamu wa soka la Ligi ya Mabingwa UEFA kwa kupiga namba
0659 070707 na ukitaka kujihudumia piga *150*46# kisha fuata maelekezo.



Wednesday 28 March 2018

Serikali Yaiaga Timu ya Madola, Yachimba Mkwara

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akimkabidhi bendera ya taifa nahodha wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola, Masoud Mtalaso, katika hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Rais wa TOC, Gulam Rashid na kulia ni Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola imeagwa, huku Serikali ikisisitiza kuwa kuanzia sasa haitaruhusu timu au mchezaji asiyeandaliwa vizuri kwenda kushiriki mashindano ya kimaataifa nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam wakati akiikabidhi bendera ya taifa kwa ajili ya Michezo hiyo Gold Coast, Australia kuanzia Aprili  hadi 15.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (wa pili kushoto) akiwa na timu ya Tanzania jijini Dar es Salaam jana,  itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola. 

Dk Mwakyembe alisema kuwa ni upotevu wa fedha bure kupeleka lundo la wachezaji ambao hawajaandaliwa vizuri, hivyo kuanzia sasa Serikali kupitia Idaya ya Michezo na Baraza la Michezo watahakikisha wachezaji wanaokwenda nje kushiriki michezo ya mkimataifa, ni wale tu walioandaliwa vizuri na kufikia vigezo vilivyowekwa.
Nahodha wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola, Masoud Mtalaso akitoa ahadi yaushindi baada ya kukabidhiwa bendera ya taifa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (kushoto)
Alisema imekuwa tabia ya baadhi ya vyama au mashirikisho ya michezo nchini kutowaandaa vizuri wachezaji wake,  lakini unapofika wakati wa mashindano ya kimataifa wanawapeleka wachezaji kushiriki wakati hawajawaandaa.

Awali, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema kuwa walitoa mwongozo kwa vyama kuhusu maandalizi ya michezo hiyo, lakini vimeshindwa kabisa kutoa ushirikiana.
Alisema vyama ndivyo vyenye jukumu la kuandaa wachezaji lakini baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa vyama, wamekuwa wakifikiri kuwa jukumu hilo ni la TOC.

Alisema kuwa awali walitakiwa kupeleka wachezaji 34 lakini imebidi wapeleke 16 tu wa michezo ya riadha, ngumi, mpira wa meza pamoja na kuogelea baada ya kushindwa kufikia vigezo vilivyoweka ikiwemo kufuzu.
Alisema kuwa TOC imetumia zaidi ya Sh milioni 180 kwa ajili ya kugharamia kambi ya mwezi mmoja, nauli ya wachezaji, makocha na viongozi wa timu hiyo.
Timu ya taifa ya ndondi itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola 2018
Mwakyembe alikabidhi bendera hiyo kwa nahodha wa timu hiyo inayoondoka leo kwenda Gold Coast, Masoud Mtalaso, ambaye ni mchezaji wa mpira wa meza na aliahidi kufanya vizuri katika michezo hiyo.
Wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa meza wakiwa na nyuso za furaha.

Timu ya taifa ya riadha pamoja na viongozi wao.

Timu ya kuogelea.
Kocha na Matron, Lwiza John.

Meneja wa timu ya Tanzania, Nasra Mohamed.
Kocha Mkuu wa timu ya riadha, Zacharie Barie.


Uchukuzi Sports Waiva Kwa Mei Mosi 2018

Kocha Kingsley Marwilo (katikati) jana akisimamia mazoezi ya timu ya soka ya Uchukuzi yanayofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Airwing, wakijiandaa na mashindano ya Kombe la Mei Mosi yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Aprili 16, 2018.

Na Bahati Mollel,TAA
TIMU za michezo mbalimbali za Uchukuzi SC zimeiva kutokana na mazoezi zinazofanya kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Airwing, kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mei Mosi yatakayoanza Aprili 17 hadi Mei 1 kwenye viwanja mbalimbali Jijini Arusha,

Kocha Mkuu wa timu ya soka, Zeno Mputa amesema wachezaji wake wameiva na wapo tayari kwa mashindano ya Mei Mosi, kutokana na kuripoti kwa wingi na kufanya mazoezi kwa bidii.
Wachezaji wa timu ya kamba ya Wanawake ya Uchukuzi wakifanya mazoezi kwa kuvutana na timu ya wanaume (haionekani pichani) wakijiandaa na mashindano ya kombe la Mei Mosi yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Aprili 16, 2018.
Mputa amesema amewapima wachezaji wake kwa kuwapa mazoezi magumu kwa siku tatu mfululizo, lakini wote waliweza kufika kwenye mazoezi kwa siku zilizofuata.

“Yale mazoezi magumu ni kama copper test na nilifanya hivyo nikiwa na lengo la kupima utimilifu wa mwili, na wamefuzu wote kutokana na kuendelea na mazoezi, siku zilivyofuata tofauti na awali nilidhani watakuwa wamechoka na kushindwa kufanya mazoezi tena,” amesema Mputa.
Hata hivyo, anasema tayari wameshacheza mechi moja ya kirafiki na timu ya Kipunguni na kutoa sare ya bao 1-1, lakini wanategemea mechi nyingine mbili zitakazochezwa baadaye wiki hii ili kujiweka imara zaidi.

Naye kocha wa timu ya kamba kwa wanawake na wanaume, Abunu Issa amesema wachezaji wake wamekuwa wakiripoti mazoezi kila siku na kufanya mazoezi makali, ikiwemo kuvuta kamba wenyewe kwa wenyewe.
Daktari Hawa Senkoro (kushoto) wa timu ya Uchukuzi akimchua misuli mchezaji wa kamba wa wanaume Augustino Saqware baada ya kubanwa na misuli wakati wa mazoezi yanayoendelea kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Airwing ya kujiandaa na michuano ya Mei Mosi itakayofanyika Arusha kuanzia Aprili 16, 2018.
“Timu zangu hizi zimekuwa zikijituma hivyo naamini pia tutafanya vizuri katika mashindano, kwani nimekuwa nikiwapima kila baada ya mazoezi kwa wanawake kuvutana na wanaume na kiwango chao ni kizuri,” amesema Abunu.

Kwa upande wa riadha, Kocha wake Kingsley Marwilo amejihakikishia wachezaji wake kufanya vyema kutokana na mazoezi wanayofanya, yakiwemo ya kujijengea misuli ikiwa ni kufanya mazoezi na wachezaji wa soka.

Timu ya netiboli, inayofundishwa na Kocha Judith Ilunda nayo imeendelea na mazoezi kwenye viwanja vya Bandari Kurasini, ambapo sasa wanacheza na timu za Zanzibar zinazoshiriki tamasha la Pasaka linalofanyika kwa kupokezana na  Tanzania Bara.


 Kipa Paul Chiwangu (kushoto) akijiandaa kudaka mpira wa krosi uliopigwa na Godwin Ponda wakati wa mazoezi yanayofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Airwing ya kujiandaa na mashindano ya Mei Mosi yatakayofanyika kuanzia Aprili 16 hadi Mei Mosi katika viwanja mbalimbali Jijini Arusha.


Uchukuzi SC ndio mabingwa watetezi kwenye michezo ya kuvuta kamba kwa wanaume na wanawake, wakati kwa netiboli walitwaa ushindi wa pili sawa na karata, bao, draft na baiskeli  wanawake, huku katika soka walishika nafai ya tatu.     
Aziza Tamim (kushoto) akimtazama mpinzani wake Stumai Mbato (kulia) wakati wakifanya mazoezi ya kucheza karata kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Airwing wanapojiandaa na michuano ya Mei Mosi  itakayofanyika Arusha kuanzia Aprili 16, 2018. Kwanza kushoto ni Sharifa Amiri anayecheza bao akiwaangalia.    
 
Mweka Hazina wa timu ya Uchukuzi, Bw. Benjamin Bikulamti akitoka kununua maji ya wachezaji wa michezo mbalimbali waliokuwa wakifanya mazoezi kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Airwing kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Mei Mosi yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Aprili 16, 2018.

Tuesday 27 March 2018

`Moto Ulioua Watu 64 Uliwashwa kwa Makusudi'


MOSCOW, Urusi
MOTO mkubwa ulioua watu 64, wakiwemo watoto 41, katika kumbi za burudani nchini Urusi, ulisababishwa na `uzembe’,  amesema Rais Vladimir Putin.

Putin aliyasema hayo wakati alipotembelea eneo la tukio huko Kemerovo, Siberia.
Wachunguzi walisema kuwa alamu za moto zilizimwa kwa makusudi, huku milango ya kutokea nje ikifungwa wakati moto huo ulipoanza juzi Jumapili.

Shirika la Habari la Interfax liliripoti kuwa watu kama 300 walikuwa wamejazana nje ya makamu makuu ya serikali ya mitaa wakitaka kuondolewa kwa viongozi wa mamlaka hiyo.

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, lakini Kamati ya Uchunguzi imesema kuwa kulikuwa na uvunjifu mkubwa wa taratibu  katika duka hilo kubwa la Winter Cherry mall.

"Nini kilichotokea hapa?",alisema Rais wa Urusi baada ya kuweka shada la maua katika eneo hilo la tukio.
"Watu, watoto walikuja kupumzika, lakini sasa tunazungumzia janga. Tumewapoteza watu wengi kwa sababu gani?...”

Jumapili ilikuwa siku ya mapumziko na watoto wengi walifika hapo na kucheza juu ghorofani bila ya kuwa chini ya uangalizi ya watu wazima, ambao kama wangekuwepo wangeweza kuwasaidia.

Irina alisema katika gho;ofaya pili watu walianza kupiga keleke “Moto moto”. Nilijaribu kurudi nyuma, lakini njia yangu ilizuiwa, watu walikuwa wengi.”

Wazazi wa mtoto aliyekuwa akisheherekea siku yake ya kuzaliwa alifanikiwa kuokolewa na marafiki zake. Darina aliungana tena na wenzake katika ghorofa ya kwanza.
Jumba hilo ambalo lilifunguliwa mwaka 2013, lina kumbi nyingi za sinema, migahawa na vituo kadhaa vya bafu za maji ya mvuko.

Baadhi ya maeneo ya jumba hilo kubwa yanadaiwa kuwa kwenye hatari ya kuporomoka.
Moto huo ulianza katika ghorofa ya juu katika jumba Winter Cherry.

Inadaiwa wengi wa waliofariki walikuwa kwenye kumbi za sinema.

Ronaldo Ashindwa Kuiokoa Ureno na Kichapo


GENEVA, Uswisi
MABINGWA wa Ulaya Ureno wakongozwa na mchezaji bora wa dunia wa mwaka, Cristiano Ronaldo, wamepokea kichapo cha aina yake kutoka kwa Uholanzi baada ya kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki hapa.

Winga wazamani wa Manchester United, Memphis Depay na mshambuliaji wazamani wa Liverpool Ryan Babel waliiwezesha timu ya taifa ya Uholanzi kuwa mbele kwa mabao 2-0.

Beki wa Liverpool Virgil van Dijk, ambaye hivi karibuni alitangazwa kuwa nahodha mpya wa timu ya taifa ya Uholanzi, ndiye aliyefunga bao la tatu huku Ureno ikipata pigo baada ya mchezaji wake Joao Cancelo kutolewa katika kipindi cha pili.

Mchezo huo umemfanya mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo kuhitimisha bahati yake ya kufunga mechi tisa mfululizo baada ya kutoka kappa katika mchezo huo.

Nahodha huyo wa Ureno, nafasi yake ilichukuliwa na mchezaji wa Monaco Joao Moutinho katika dakika ya  68, ambapo ameifungia Real Madrid mabao 17 na mawili kwa Ureno, dhidi ya Misri Ijumaa.

Ureno wako katika Kundi B katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia pamoja na Hispania, Morocco na Iran, lakini Uholanzi, ambayo ilifungwa 1-0 na England katika mchezo wa kwanza ikifundishwa na Ronald Koeman, ilishindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Taifa Stars, Congo Kumenyana Leo Uwanja wa Taifa


Na Mwandishi Wetu
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars leo inatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya DR Congo.

Stars inacheza na Congo ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 4-1 ilichopata toka kwa Algeria wiki iliyopita katika mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco alisema wamejiandaa vema kwa mchezo huo baada ya kupoteza dhidi ya Algeria pamoja na kwamba ana majeruhi wawili.

"Tumejiandaa vizuri kwani ninajua Congo ni timu nzuri na sisi tunahitaji ushindi baada ya kupoteza mchezo uliopita. Kikosi changu kina majeruhi Aishi Manula ambaye anasumbuliwa na kifundo cha mguu na Abdulaziz Makame," alisema Morocco.

Naye nahodha msaidizi wa Stars, Himid Mao alisema wao wamejiandaa kuhakikisha wanawapa raha mashabiki kwani makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita wameyafanyia kazi.

Kwa upande wa Kocha wa DR Congo, Ibenge Florent alisema anaamini mchezo utakuwa mgumu kwani Taifa Stars itakuwa inapambana kuhakikisha inashinda mbele ya mashabiki wake huku akimtaja Simon Msuva na Mbwana Samatta kama wachezaji wanaowahofia.

"Tanzania ni jirani zetu pia ni ndugu zetu ndiyo maana tumekubali kucheza nao. Mchezo utakuwa mgumu kwani Taifa Stars haitakubali kufungwa kirahisi mbele ya mashabiki wake na wachezaji Samatta na Msuva tunajua wakipata nafasi wanaweza kufunga bao," alisema Ibenge.

Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 10:00 jioni na viingilio ni Sh 5,000 VIP A na B, huku maeneo mengine ikiwa ni Sh 1,000.

Simba, Yanga Sasa Kutoana Jasho Aprili 29


Na Mwandishi Wetu
MECHI ya watani wa jadi Simba na Yanga ambayo ilikuwa ichezwe Aprili 7 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sasa itachezwa Aprili 29.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPBL), Boniface Wambura alisema wamefanya mabadiliko ya ratiba kwa mechi kadhaa kwa sababu wanataka Ligi Kuu imalizika Mei 26 kama ilivyopangwa.

"Ratiba imebana sana hivyo mchezo wa kiporo wa Njombe na Simba utachezwa Aprili 3 na tumefanya kazi ya ziada kukubaliana na Njombe kwani wanasema ratiba siyo rafiki kwao lakini nashukuru wametuelewa," alisema Wambura.

Pia Wambura alisema mchezo wa Simba na Yanga utachezwa Aprili 29 badala ya Aprili 7 ili kuipa Yanga nafasi kujiandaa na mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wolayta Dicha ya Ethiopita unaotarajiwa kuchezwa Aprili 4 kwenye uwanja wa Taifa.

Mechi ya Simba na Yanga inatarajiwa kuwa ya vuta nikuvute hasa kwa vile timu hizo zimeonesha upinzani mkubwa kileleni mwa msimamo na hivyo mpaka sasa yeyote kati yake anaweza kuwa bingwa.

Simba inaongoza msimamo kwa uwiano mzuri wa mabao baada ya kulingana pointi 46 na Yanga iliyo nafasi ya pili.

Wambura alisema ratiba hiyo inaweza kufanyiwa tena marekebisho endapo Yanga itafuzu kwenye hatua ya makundi huku akisema sababu nyingine zinazofanya ratiba kupanguliwa ni kutokana na timu kutokuwa na viwanja vyao hivyo wamiliki wa viwanja wanapokuwa na shughuli za kijamii mechi zinasogezwa mbele.
Mechi nyingine zilizofanyiwa marekebisho ni Mbao dhidi ya Lipuli utakaochezwa Aprili 6 na tarehe hiyo tena Mwadui Shinyanga.
 
Mtibwa Sugar itacheza na Simba Aprili 9 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Yanga itacheza na Stand United Aprili 11, Simba itaivaa Mbeya City Aprili 12 na Aprili 16 itaikaribisha tena Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Taifa.

Lipuli itakuwa mwenyeji wa Simba Aprili 20 na Majimaji itacheza na Ruvu Shooting Aprili 28.

Wambura alisema wamepata kibali cha kutumia uwanja wa Taifa kwa michezo inayohusu Simba na Yanga isipokuwa mchezo wa Yanga dhidi ya Azam FC utalazimika kuchezwa kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Monday 26 March 2018

Timu Madola Sasa Kuagwa Keshokutwa Jumatano

Mabondia wa timu ya taifa ya Tanzania inayojiandaa kwa Michezo ya Jumuiya ya Madola wakiwa na kocha wao, Moses Oyombi (katikati mbele) baada ya mazoezi yao kwenye ukumbi wa Filbert Bayi Sports Complex Mkuza, Kibaha juzi.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola, ambayo ilitarajia kuagwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, sasa itaagwa keshokutwa Jumatano, imeelezwa.

Habari za uhakika zilizopatikana leo zimesema kuwa timu hiyo haitaagwa kesho kutokana na sababu zisizozuilika na badala yake itaagwa leo na Waziri wa habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Tayari Mkuu wa msafara wa timu hiyo, Dk Yussuf Singo, ambaye ni Mkurugenzi wa Michezo nchini, aliondoka jana Jumapili kwenda Gold Coast kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuipokea timu ya Tanzania nchini Australia.

Timu ya riadha itakuwa na Stephano Huche, Said Makula na Sarah Ramadhani (marathon), Failuna Abdul (meta 10,000), Ali Hamisi Gulam (meta 100/200) na Anthony Mwanga (miruko na mitupo) wakati makocha ni Zacharie Barie na Lwiza John.
Mabondia wa timu ya taifa wakianza na kumaliza mazoezi yao kwa sala kila siku.
Ndondi ni Kassim Mbutike (kg 69), Ezra Paulo (kg 56), Haruna Swanga (kg 91) na Seleman Kidunda (kg 75) na kocha wao ni Benjamin Moses.

Timu ya kuogelea inaundwa na Hilal Hilal na Sonia wakati kocha wao ni Khalid Yahya Rushaka.
Nahodha wa timu ya taifa ya mpira wa meza ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola, Masoud Mtalaso (kulia) akifanyishwa mazoezi na Mkenya Kennedy Kajali katika kambi ya timu hiyo Kibaha mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.
Timu ya mpira wa meza inaundwa na Amon Tumaini, Mtalaso, Neema Mwaisyula na Fathiya Pazi wakati kocha wao ni Ramadhan Othman Suleiman.

‘Brazil Nzuri Lakini Bado Inamuhitaji Neymar’


MUNICH, Ujerumani
BRAZIL ni moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika fainali za Kombe la Dunia 2018, lakini kuumia kwa nyota Neymar bado kunaidhoofisha timu hiyo, anasema winga wa Ujerumani Leroy Sane.

Sane pia ni kiungo wa vinara wa Ligi Kuu ya England, Manchester City.

"Brazil haimtegemei Neymar kama ilivyokuwa mwaka 2014," alisema winga wa Manchester City Sane.

"Wako katika nafasi nzuri na wana wachezaji nyota wachache wapya, lakini bado inafanya tofauti Neymar awepo au asiwepo.

Ujerumani itaikaribisha Brazil katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaofanyika leo Jumanne kwenye Uwanja wa Olimpiki mjini Berlin, ikiwa ni sehemu ya kuipa mazoezi timu hiyo kwa ajili ya Kombe la Dunia Juni nchini Urusi.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza tangu Ujerumani ilipoifunga Brazil kwa mabao matano ndani ya nusu saa wakati ikishinda 7-1 katika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014.

Katika mchezo huo, mshambuliaji wa Brazil Neymar alikuwa nje kutokana na maumivu. Mchezaji huyo ghali kabisa duniani anauguza jeraha lake baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu.

Anatarajia kuwa fiti kwa wakati kwa ajili ya Kombe la Dunia, ambalo litaanza Juni 14.

Brazil iliifunga Urusi mabao 3-0 Ijumaa katika mchezo mwingine wa kimataifa wa kirafiki, huku mabao matatu yakifungwa na Miranda, Paulinho na Philippe Countinho aliyefunga kwa penalti katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Moscow wa Luzhniki, ambao utaandaa fainali ya Kombe la Dunia Julai 15.

Ujerumani ilijipima nguvu kwa kutoka sare ya 1-1 na Hispania huko Duesseldorf wakati bao la mapema la Rodrigo Moreno kwa wenyeji lililofuta lile la Thomas Mueller la kipindi cha kwanza.

Kocha Mkuu wa Ujerumani, Joachim Loew alisema kuwa kipigo cha mabao 7-1 kitadumu kwa miaka 10, 20 au 30 ijayo kila timu hizo zitakapokutana.

Loew alisema kuwa anatarajia kufanya mabadiliko matano kutoka katika timu iliyotoka sare na Hispania.

Mueller na Mesut Ozil wamepewa mapumziko na Loew, wakati kiungo wa Liverpool Emre Can ameachwa kutokana na maumivu ya mgongo.

Sunday 25 March 2018

Mamlaka Hifadhi ya Ngorongoro Yadhamini Mbio


Na Mwandishi Wetu, Karatu
MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) itadhamini Ngorongoro Marathon 2018 zitakazofanyika Aprili 21 kwa Sh milioni 30.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Karatu, Arusha Mkurugenzi wa mbio hizo, Meta Petro alisema jana kuwa mamlaka hiyo imekubali kudhamini mbio hizo zitakazofanyika Aprili 21 mwaka huu.

Petro alisema kuwa NCAA ndio mdhamini mkuu wa mbio hizo, ambazo mwaka huu ni za 11 kufanyika tangu zilipoanzishwa na zimekuwa zikikua mwaka hadi mwaka.

Alisema kuwa anatarajia mbio za mwaka huu kushirikisha wanariadha wengi kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo wakimbiaji mbalimbali nyota.

Mbali na NCAA, wadhamini wengine ni Kampuni ya Vinywaji ya Bonite, ambao wamekubali kuendelea kudhamini mbio hizo kwa kutoa bidhaa mbalimbali zenye thamani ya Sh milioni 15.

Petro alisema kuwa anawashukuru wadhamini hao na bado milango iko wazi kwa wengine kujitokeza kusaidia kudhamini ili kuzidi kufanikisha mbio hizo, ambazo zitaanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Ngorongoro na kumalizika katika viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.



Wambura Aendelea Kupinga Maamuzi ya TFF


Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliyefungiwa maisha na Kamati ya Maadili, Michael Wambura ameibuka na kulaani uteuzi wa Kamati ya Utendaji kumteua Athumani Nyamlani kukaimu nafasi hiyo.

Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, juzi ilimteua Nyamlani kukaimu nafasi hiyo, huku ikimthibitisha Kidao Wilfred kuwa Katibu Mkuu katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Wambura katika taarifa hiyo kupitia mwanasheria wake, Emmanuel Muga alisema kuwa anapinga uteuzi huo wa Nyamlani kuchukua nafasi yake wakati rufaa yake aliyokata bado haijasikilizwa na kutolewa uamuzi.

Taarifa hiyo ya kurasa moja inaeleza kuwa Kamati ya Utendaji Machi 24, 2018 iliendesha zoezi la uteuzi lisilo halali na kuvunja ibara namba 34 (1) ya Katiba ya TFF, ambayo inaeleza kuwa nguvu ya kumchagua na kumuondoa makamu wa rais ni ya Mkutano Mkuu.

Pia Wambura ameshtushwa na kitendo cha kuwabadilisha baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Rufaa, ambapo uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji sio wa haki na unaopigana na ibara ya 34 (2) ya Katiba ya TFF.
 
Ibara hiyo inasomeka: “Chombo hicho huru cha kisheria cha TFF wajumbe wake hawaruhusiwi kuondolewa kabla ya kipindi chao bila ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu.


Nyamlani anachukua nafasi ya Wambura aliyefungiwa maisha na Kamati ya Maadili kutojihusisha na masuala ya mpira, na Kidao alikuwa akikaimu nafasi hiyo takribani miezi nane sasa.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Utendaji, ambacho kilikutana kwenye hoteli ya Sea Scape zinasema, Nyamlani amepata sifa za kukaimu nafasi hiyo kwa sababu kanuni na taratibu za TFF zinatamka kuwa nafasi za kuchaguliwa mjumbe atakaye kaimu awe mjumbe wa Kamati ya Utendaji aliyedumu kwa kipindi kirefu.

“Kanuni zinamtaka mjumbe wa muda mrefu ambaye yupo kwenye Kamati ya Utendaji, na ukiangalia kwa sasa wajumbe ambao wana muda mrefu ni Nyamlani, Ahmed Mgoyi na Khalid wa Tanga ila sasa Nyamlani ndio amewazidi wote, hivyo kamati ilimkaimisha yeye hadi uchaguzi mdogo utakapotangazwa,” kilisema chanzo hicho.
 
Hata hivyo, kazi ya kumwidhinisha Nyamlani kukaimu nafasi hiyo haikuwa rahisi kwani ililazimika kupigwa kura ili kumpitisha, ambapo zile za ndio zilikuwa nyingi, hivyo akapitishwa mpaka pale mkutano mkuu wa TFF utakavyoamua vinginevyo.

Nyamlani ambaye alikuwa makamu wa Rais kipindi cha uongozi wa Leodgar Tenga,  aliingia kwenye Kamati ya Utendaji kwa kuteuliwa na Rais Wallace Karia yeye na Ahmed Mgoyi.

Kidao alikuwa akikaimu nafasi ya ukatibu mkuu baada ya yule wa awali, Selestine Mwesigwa, yeye na Malinzi kushtakiwa kwa madai ya ubadhilifu na makosa mengine.