Saturday 25 May 2019

Simba Kukabidhiwa Kombe Lao Jumanne Morogoro


Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Tanzania Bara msimu wa mwaka 2018/19, Simba leo walishindwa kukabidhiwa Kombe lao la Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuahidi kuwakabidhi.

Mchezo huo ambao ulizikutanisha Simba na Biashara ya Musoma, ulichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na ulianza saa 9:00 Alasiri ili kuikabidhi Simba taji lao. Timu hizo zilifungana bao 1-1.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi nchini, Bonface Wambura alisema kuwa wameshindwa kukabidhi kombe jana baada ya kutokuwepo kwa mgemni rasmi, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.

Wambura alisema kuwa kombe hilo sasa Simba watakabidhiwa Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mchezo wa mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar.

Hatahivyo, watazamaji waliofika Uwanja wa Taifa licha ya mvua kunyesha karibu kipindi chote cha kwanza na baadhi ya sehemu za uwanja kujaa maji, walionesha kusikitishwa na kutotolewa kwa taji hilo, ambalo ni la 20 kwa Simba kulitwaa.

Katika mchezo huo, Bishara United ndio walikuwa wa kwanza kupata bao baada ya Innocent Edwin kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 14, ambalo lilidumu kwa dakika tatu, kwani Simba walisawazisha katika dakika ya 17 mfungaji akiwa ni Clatous Chama.

Nyota wa Simba Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco walishindwa kufunga licha ya kulifikia mara kwa mara lango la Biashara, lakini maji yaliwazuia wachezaji hao kufunga.

Katika mchezo mwingine leo, Kagera Sugar imekubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa JKT Tanzania katika mchezo uliofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa JK Park.

NEMC Yawaondoa Hofu Wadau Viwanja vya Ndege


Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche (aliyenyanyua mikono) akisisitiza jambo wakati akiongea na wadau wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), juu ya katazo la mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kuendelea kutumika nchini ifikapo Juni Mosi mwaka huu. Wapili kulia ni Mkurugezi wa JNIA, Paul Rwegasha na wa kwanza kushoto ni mkuu wa kitengo cha Mazingira cha TAA, Maxmilian Mahangila.

Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), leo limewaondolea hofu wadau wanaoendesha huduma mbalimbali kwenye Viwanja vya ndege, katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), uliofanyika kwenye Ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP), kuhususiana na katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki ambalo litaanza rasmi Juni Mosi, 2019.

Mwanasheria wa NEMC, Manchare Heche amesema kwa upande wa viwanja vya ndege ipo mifuko, ambayo itaendelea kutumika kwa mujibu wa Kanuni namba tisa (9) ya sheria ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2019, lakini baada ya kutumika inatakiwa ihifadhiwe sehemu maalum na kupekekwa mahali itakapoteketezwa.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Joachim Philipo akitoa ushauri kwenye mkutano wa wadau wanaotoa huduma mbalimbali JNIA ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na kuhusisha Wataalam kutoka Baraza ka Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambao walitoa maelezo mbalimbali juu ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki litakaloanza rasmi Juni Mosi, 2019 kwa mujibu wa sheria.
“Kweli katazo linahusu Watanzania wote na wageni na hapa Airport wapo wanaotumia nikiwa na maana ya wafanyakazi na wateja wakiwemo abiria, lakini katika sheria ukiangalia kanuni ya tisa 9 ipo mifuko ya vifungashio ambayo haijazuiwa ni kama ile ya kuhifadhi vyakula, dawa, kilimo na inayohifadhia takataka, mfano korosho au keki wanazopewa abiria kwenye ndege mfuko wake upo katika kipengele cha chakula, hivyo itaendelea kutumika lakini baada ya matumizi tu itahuifadhiwa sehemu iliyoelekezwa tayari kwa kwenda kuteketezwa,” alisisitiza Heche.

Alisema kwa upande wa plastiki zinazofungia mizigo ya abiria wanaosafiri kutoka ndani na nje ya nchi kwa usafiri wa ndege itatakiwa kuondolewa abiria anapofika nchini, na zitakusanywa na kuhifadhiwa maeneo maalum kabla ya kupelekwa eneo lililotengwa kwa ajili ya kuziteketeza.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Joachim Philipo akitoa ushauri kwenye mkutano wa wadau wanaotoa huduma mbalimbali JNIA ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na kuhusisha Wataalam kutoka Baraza ka Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambao walitoa maelezo mbalimbali juu ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki litakaloanza rasmi Juni Mosi, 2019 kwa mujibu wa sheria.
Hatahivyo, kutokana na matumizi makubwa ya mifuko ya plastiki nchini imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo ya kuziba kwenye mifereji ya maji, kuua wanyama, na kuharibu ardhi, Heche amesema kufuatia katazo hilo serikali imefuta leseni za viwanda vinavyotengeneza mifuko ya plastiki na pia haijawapa tena leseni wale wote leseni zao zilizomaliza muda, ili kuhakikisha sheria na kanuni ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki namba 394 ya mwaka 2019.   

Heche ametoa angalizo kwa wale wote wanaohusika na ukamataji wa watumiaji wa mifuko hiyo, kutotumia nguvu ili kuepusha mikwaruzano na kutoelewana.

      Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji, Anna Mushi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), leo akizungumza katika mkutano wa wadau wanaotoa huduma mbalimbali JNIA katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na kuwahusisha Wataalam kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutokana na katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki ifikapo Juni Mosi, 2019.

Hatahivyo, amewataka wadau hao kuhakikisha wanadai vitambulisho kwa wale wote watakaofika kwenye maeneo yao ya kazi kudai wanakagua endapo wanaendelea kuuza au kutumia mifuko ya plastiki.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha amesema tayari kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wameshatoa taarifa inayokwenda kwenye vituo vyote vya Kimataifa, ambapo kuna shirika la ndege linaloleta abiria Tanzania, ikitaarifu juu ya katazo la mifuko ya plastiki.
Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche akiwaonesha wadau wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kiwanja cha Ncdege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) moja ya mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kuendelea kutumika nchini ifikapo Juni Mosi, 2019 katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP).  Kulia ni   Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha.
“Hii taarifa inajulikana kitaalam kama ‘timatic pre-information’ ambayo inatumwa kwenye centre zote duniani, ambapo kuna shirika la ndege ambalo linaleta abiria Tanzania itakuwa rahisi wao kupata taarifa ya katazo hilo na kuwafanya wasibebe mifuko hiyo,” amesema Rwegasha.

Pia amewataka wadau wote wanaofanya shughuli mbalimbali kwenye viwanja vya ndege kutoa ushirikiano mkubwa kuwaeleza abiria juu ya katazo hilo, na kuwaelekeza watumie mifuko mbadala, ambayo itakuwa ikipatikana kwenye maduka yaliyopo kwenye majengo ya Kwanza na Pili ya JNIA.

Kwa mujibu wa NEMC imesema watumiaji wa kawaida endapo watakamatwa na mifuko hiyo watatozwa faini ya Tshs. 30,000, kifungo cha siku saba, au vyote kwa pamoja;  wakati kwa muuzaji anapigwa faini ya Tshs 100,000 haizidi Tshs 500,000, kifungo cha miezi mitatu; na watengenezaji watapigwa faini ya kuanzia Tshs milioni 20 na haitazidi bilioni moja na kifungo cha miaka miwili.

Arsenal watangulia Baku kucheza dhidi ya Chelsea

Mchezaji wa Arsenal, Lucas Torreira akiwa mwe ari kubwa akipanda ndege kwenda Baku.

LONDON, England

KLABU ya Arsenal leo imekwea pipa na kwenda Baku tayari kwa nchezo wao wa fainali ya Ligi ya Ulaya utakaopigwa Jumatano, imeelezwa.

The Gunners walipigwa picha wakipanda pipa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Luton leo Jumamosi.

Mesut Ozil alionekana akiwa mtulivu kabisa wakati wakianza safari yao hiyo ya saa sita hadi saba kutoka London hadi Baku.

Arsenal wanatakiwa kuifunga Chelsea katika mchezo huo wa wiki ijayo ili kutwaa taji hilo na kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

Arsenal imesafiri mapema kwenda Baku, siku tano kabla mchezo huo watakaocheza dhidi ya wapinzani wao wa jiji la London, Chelsea.

Kikosi hicho cha kocha Unai Emery kitakabiliana na Chelsea nchini Azerbaijan kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Baku, ambapo wanahitaji ushindi ili kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

Na leo Jumamosi asubuhi, the Gunners walionekana katika picha wakipanda ndege tayari kwa mchezo huo wa fainali utakaofanyika Jumatano ijayo.
Danny Welbeck akionekana yuko fiti tayari kwa mchezo wa fainali ya Ligi ya Ulaya Jumatano wiki ijayo.
Nahodha wa Arsenal Laurent Koscielny, Mesut Ozil, Lucas Torreira na wachezaji wengine walionekana wakiwa katika ari kubwa wakati wakianza safari hiyo ya saa sita kwenda Baku wakitokea jijini hapa.

Danny Welbeck ameshinda mbio zake za kuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo wa fainali ya Ulaya wakati mshambuliaji huyo wa Uingereza naye pia alipigwa picha akisafiri na wachezaji wenzake wa Arsenal akisafiri na timu hiyo ya Arsenal mwishoni mwa wiki.

Mshmabuliaji huyo hajacheza tangu alipoumia kifundo cha mguu Novemba mwaka jana na sasa anatarajiwa kutajwa katika benchi la Emery dhidi ya Chelsea.
Ozil akicheeeka ndami ya ndege kabla ya kupaa kwenda Baku leo.
Huo utakuwa mchezo wa mwisho wa Welbeck katika timu hiyo yenye maskani yake kaskazini ya London, huku mchezaji hyo mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni mchezaji wazamani wa Manchester United ataondoka mwishoni mwa msimu wakati mtataba wake utakapomalizika.

Arsenal inaingia katika mchezo huo wa Jumatano usiku ikiwa na presha kubwa zaidi ya Chelsea ili kupata taji hilo la Ulaya kwa ajili ya mashabiki wao.


Chelsea iliipita Arsenal katika mbio za kusaka nne bora katika Ligi Kuu ya England ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwa hatua ya nne bora na kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

The Gunners nafasi yake pekee iliyobaki ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ni kutwaa taji la Ligi ya Ulaya katika mchezo ho nan i taji la kwanza tangu ili;otwaa taji hilo la Ulaya mwaka 1994.

Monday 20 May 2019

Guardiola Sasa Ataka Taji Ligi ya Mabingwa Ulaya


LONDON, England
MAFANIKIO ya Manchester City yatakuwa na thamani endapo tu timu hiyo itafanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya licha ya kuweka historia ya kutwaa mataji matatu msimu huu, anasema kocha Pep Guardiola.

Kocha huyo wa Man City, anajua kuwa atakosolewa endapo atashindwa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Ulaya.

Ushindi wa 6-0 dhidi ya Watford Jumamosi katika fainali ya Kombe la FA likifuatiwa na taji la Ligi Kuu ya England pamoja na lile la Ligi msimu huu.

"Nilisema tangu awali kuwa najua tutahukumiwa mwishoni kama tumeshinda Ligi ya Mabingwa, “alisema Guardiola.

"Bila ya kutwaa taji la Ligi ya Ulaya, basi tutakuwa hatujafanya jambo la kutosha.

"Hilo nililijua mapema, kwani nilipowasili Barcelona, tulikuwa na bahati tulishinda taji hilo la Ulaya mara mbili ndani ya kipindi cha miaka minne na watu walitarajia  kitu maalum kutoka kwangu, ambacho kingetuwezesha kushinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hapa City, na hilo litaendelea kuwa sahihi.

"Katika klabu hii, rekodi ya klabu katika mashindano ya nyumbani ni nzuri, lakini Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatujawahi kushinda, hivyo sasa tunajukumu la kushinda taji hilo kwa kuwa tuna wachezaji wazuri sana, “alisema.

Man City imeshinda mara nne taji la Ligi Kuu ya England, mawili ya Kombe la FA na manne ya Ligi, tangu klabu hiyo ilipoanza kumilikiwa na Sheikh Mansour mwaka 2008, lakini pamoja na mafanikio hayo haijawahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Beki Vincent Kompany amekuwa katika timu hiyo kwa wakati wote huo, ikiwemo miaka nane akiwa nahodha wa Man City, lakini alitangaza Jumapili kuwa ataondoka katika klabu hiyo na kwenda kucheza soka Ubelgiji.

Kompany, 33, atajiunga na klabu ya Ubelgiji ya Anderlecht kama kocha mchezaji kwa mkataba wa miaka mitatu.

Mkandarasi Terminal 3 JNIA Kukabidhi Jengo Mapema


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (Mwenye suti ya bluu) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mhandisi Julius Ndyamukama  mara baada ya kuwasili kwa ajili ya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi katika jengo la tatu la abiria (TB III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jioni ya leo.

Na Mwandishi Wetu
JENGO la Tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA),  Terminal 3, litakabidhiwa mapema kwa wamiliki, imeelezwa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema kuwa jengo hilo, ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni 6 kwa mwaka, litakabidhiwa Mei 29, ikiwa ni siku moja kabla tarehe ile ya awali iliyoahidiwa na mkandarasi kulikabidhi.

Awali, mkandarasi aliahidi kukabidhi jeingo hilo, Mei 30 kwa wamiliki, ambao ni Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi na Rais John Pombe Magufuli baadae mwaka huu.

JENGO TAYARI
Tayari ujenzi wa jengo hilo umekamilika kwa asilimia 99.5  na sasa vitu vikubwa vinavyofanyika ni kufunga vifaa mbalimbali, vikiwemo vile vya usalama, milango, vitu na vile vya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRA).

Alisema kuwa tayari ujenzi umeshakamilika na watu wa TRA, TTCL, Fire na wengine wanaweka mifumo yao ya huduma ili kukamilisha ujenzi huo.


 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe katikati akiwa anaelekea katika jengo la tatu la Abiria (TB III) kuona maendeleo ya mradi wa ujenzi, kulia kwake ni Mhandisi Msimamizi wa Ujenzi wa jengo hilo Barton Komba na kushoto kwake ni Msimamizi wa miradi ya Viwanja vyote vya Ndege Tanzania Mhandisi Godson Ngomuo.

“Mtendaji Mkuu kwa sasa anahangaika na watoa huduma na wanaotakiwa ni wale wenye uwezo mkubsa na ambao hawafanyakazi kwa mazoea na ni bora wakapata vijana wa kitanzania wenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma katika jengo hilo bora kabisa na la kisasa, “ alisema Kamwele baada ya kukagua jengo hilo.

MAJARIBIO
Alisema baada ya Mei 29  wataanza kufanya majaribio ya matumizi mbalimbali katika jengo hilo, ambalo halina tofauti kabisa na majengo ya viwanja vya Ulaya nan chi nyingine zilizoendelea.

Aidha, Kamwele alisema baada ya kukamilika kwa Jengo l Terminal 3, ujenzi utahamia katika terminai 2, ambalo lenyewe litatumika kwa ajili ya abiria wa hapa nchini ambao wanatoka na kuwasili kutoka mau kwenda mikoani.

Terminal 3 ina madaraja 12, ambayo yana uwezo wa kuegesha ndege kubwa za idadi hiyo kwa wakati mmoja pia kutakuwa na mageti 16 ya kuingilia na kutokea katika ndege.
Alisema kuwa katika kudhihirisha kuwa ujenzi wa Terminal 3 tayari wafanyakazi wamebaki 1,000 kutoka 2,900 ambao walikuwa wakifanya shuhghuli mbalimbali za ujenzi.

Tayari baadhi ya majengo yaliokuwa ofisi za muda zilizojengwa na mkandarasi katika eneo hilo la Terminal 3 kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za ujenzi, zimeshavunjwa.
Waziri alisema ameridhishwa kabisa na maendeleo ya ujenzi wa jingo hilo na baada ya Mei 29, TAA itakuwa ikiendesha mafunzo mbalimbali kwa ajili ya watoa huduma uwanjani hapo.

  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhandisi Msimamizi wa Ujenzi Barton Komba kutoka Wakala wa barabara (TANROADS) alienyoosha mkono juu kuhusu eneo la maegesho ya magari katika Jengo la tatu  la Abiria (TB III) wakati wa ziara yake Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jioni ya leo.

Alisema Mtendaji Mkuu tenda anayohangaika nayo ni watoa huduma kwani wanataka wale wenye uwezo mkubwa, ambao wataendana na ubora wa jingo hilo, hivyo hawataki wale wanaotoa huduma kwa mazoea.

Waziri alipotembelea jengo hilo alishuhudia watu wa TRA, Uhamiaji na wengine wakifunga vifaa vyao, tayari kutoa huduma wakati wowote kiwanja hicho kitapoanza kutumika.

Juni mosi wataanza kutoa huduma kwa majaribio uwanjani hapo, hasa ,ujaribu mifumo mbalimbali kabla ya kutoa taarifa kwa Rais Magufuli kuuzindua jengo hilo la tatu la abiria.

Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa TB III, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TANROADS Mhandisi Crispin Akoo alisema kutokana maendeleo mazuri ya ujenzi Mkandarasi anatarajia kukabidhi jengo mapema.

 “Hadi kufikia terehe 31 Julai 2018 maendeleo yalikua ni asilimia 78.33, lakini hadi kufikia tarehe 18 Mei 2019 ujenzi wote ulikua umefikia asilimia 99.5, ” alisema.

Kuhusu maandalizi ya uendeshaji Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mhandisi Julius Ndyamukama alimweleza Waziri kwamba majaribio na maandalizi ya uendeshaji yalianza tangu mwezi machi mwaka 2018 na yapo katika hatua za mwisho.

“Majaribio ya kwanza ya kwanza ya mifumo na vifaa vinavyotumia umeme yalianza mwezi Julai 2018 kwa sasa yamefikia asilimia 96 na muda sio mrefu yatakamilika.”

Aidha Mhandisi Ndyamukama aliongeza kwamba majaribio hayo yanatarajiwa kufanyika ndani ya miezi mitatu kuanzia mwezi Mei na ifikapo mwezi Agosti yatakua yamekamilika.

Naye Mhandisi Barton Komba alimwambia mwandishi wetu kuwa, kwa wakati mmoja jingo hilo linaweza kuhudumia hadi abiria 2800 bila tatizo, huku kukiwa na checking counter 42, 37 zikitoa huduma kwa abiria wa madaraja ya kawaida na wale wa business huku tano zikitoa huduma kwa Commecial Important People (CIP).