Saturday, 7 March 2015

Afrika wamtosa Luis Figo Urais FIFA

LUSAKA, Zambia
GWIJI wa soka Afrika Kalusha Bwalya (pichani) anaamini kuwa ni mapema mno kwa Luis Figo kuchuana na Sepp Blatter kwa ajili ya kuwania nafasi ya urais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Bwalya, rais wa Chama cha Soka cha Zambia ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), anasema kuwa nyota huyo Mreno kwanza anatakiwa kujifunza kabla ya kuwania kiti hicho cha juu kabisa.

"Nafikiri Luis Figo alikuwa mchezaji wa aina yake, na wa kiwango cha dunia, " alisema Bwalya.

"Napenda kuona Luis Figo anakwenda kwanza katika Chama cha Soka cha Ureno kujifunza kilichopo katika soka na ndio aje nje.

"Kuna wachezaji wengine, kama akina Davor Suker, ambaye anaoongoza chama Ulaya [Croatia].

"Kwa mawazo yangu Figo ameamua kuwania nafasi kubwa sana, hivyo kwake itakuwa vigumu kwa mchezaji huyo wazamani kuongoza."

Bwalya, ambaye ni mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika wa mwaka 1988, alisema vyama vingi vya nchi tayari vimeshaamua nani wa kumpigia kura katika uchaguzi huo wa Fifa.

Alisema Afrika imeamua kumchagua Blatter kwa ajili ya mkiaka mingine minne ya kukalia kiti hicho cha urais ambacho anakikalia tangu mwaka 1998.

"Sisi kama Africa nikiwemo mimi binafsi-tumesema tutamuunga mkono Blatter kwa ajili ya muhula mwingine tena kwa sababu anaweza kuipeleka mbele soka katika kipindi cha miaka minne mingine ijayo, " alisema Bwalya.

No comments:

Post a Comment