Saturday, 26 September 2015

Man City yachapwa 4-1, Arsenal, Liverpool mambo saaafii


Mshambuliaji wa Manchester City, Raheem Sterling akikimbia na mpira walipocheza na Tottenham Hotspur kwenye Uwanja wa White Hart Lane leo. Man City ilifungwa mabao 4-1.

LONDON, England
HARRY Kane jana alimaliza ukame wa kutofunga kwa saa 13 baada ya leo kufunga bao wakati Tottenham ikitoa kichapo kikali cha mabao 4-1 kwa vinara Manchester City 4-1.

Hicho ni kipigo cha pili mfululizo kwa Man City katika mechi za Ligi Kuu  ya England.

Mshambuliaji huyo wa England alifanya matokeo kuwa 3-1 katika dakika 61 baada ya mkwaju wa adhabu wa Christian Eriksen ulipogonga mwamba na kurudi uwanjani, wakati Spurs ikitoka nyuma kufuatia bao la kwanza lililofungwa na Kevin De Bruyne.

De Bruyne kama alikuwa katika nafasi ya kuotea lakini aliweza kuifungia Man city bao katika dakika ya 25, na mwamuzi alishindwa tena kubaini mpira wa kuotea wakati Eric Dier akiwasawazishia wenyeji.

Lakini hakukuwa na tatizo kwa mpira wa kichwa uliopigwa na Toby Alderweireld na kujaa wavuni na kuifanya Spurs kuwa mbele kabla Erik Lamela hajamzunguka Willy Caballero na kuipatia timu yake bao la nne.

Nayo Arsenal leo ilibuka na ushindi mnono baada ya kuifunga Leicester na kuhitimisha timuhiyo kuanza ligi bila kufungwa katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa King Power.

Alexis Sanchez baada ya ukame wa kutofuga, hatimaye jana alifunga hat-trick na kuiwezesha timu hiyo kutoka kifua mbele na pointi zote tatu.

Arsenal ilitoka nyuma na kuibuka na ushindi huo huku mabao mengine yakifungwa na Theo Walcott na Olivier Giroud  aliyefunga akitokea baada ya kuingia uwanjani akitokea.

Wayne Rooney aliifungia Manchester United wakati ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sunderland kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Daniel Sturridge alifunga mara mbili wakati Liverpool ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Aston Villa katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Anfield na kutoa nafuu kwa kocha wa timu hiyo Brendan Rodgers.

Yanga yawalaza mapema Simba kwa kichapo cha mabao 2-0


Na Waandishi Wetu
MABINGWA wa soka Tanzania Bara Yanga leo iliwanyoosha wapinzani wao Simba baada ya kuibuka kidedea kwa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezaji wazamani wa Simba, Amisi Tambwe aliinyoosha timu yake hiyo ya zamani baada ya kufunga bao dakika moja kabla ya mapumziko  kwa shuti kali la guu la kushoto akiwa ndani ya boksi akipokea pasi kutoka kwa Malimi Busungu.

Busungu aliyeingia uwanjani akitokea benchi, alirekebisha makosa yake alipoipatia Yanga bao la pili katika dakika ya 79 alilofunga kwa kichwa akiunganisha mpira uliotupwa na Mbuyi Twitte.


Simba ambayo ilitawala zaidi kipindi cha kwanza, ilikuwa ya kwanza kulilifikia lango la watani zao Yanga lakini krosi ya Hassan Ramadhani ilidakwa na Ally Mustapha.

Katika dakika ya sita, Simba walilifikia tena lango la Yanga na kusababisha mpira kuwa kona, lakini haikuzaa matunda baada ya kudakwa na Mustapha, ambaye aliumia kabla ya kupatiwa matibabu na kuendelea na mchezo.

Simba ilifanya shambulio la nguvu katika dakika ya tisa, lakini Mwinyi Kazimoto akiwa amebaki yeye na kipa wa Yanga Mustapha, alipiga mpira ukagonga nyavu za nje.

Beki wa Simba Juuko Murahid alioneshwa kadi ya njano kwa kumshika mshambuliaji wa Yanga Donaldo Ngoma.

Hamisi Kiiza nusura aipatie Simba bao la kuongoza katika dakika ya 13 baada ya beki wa Yanga, Nadir Haroub kuchanganyana na kipa wake Mustapha, lakini alishindwa kuuweka kimiani.

Kiiza tena nusura afunge katika dakika ya 27 baada ya kupiga shuti kali ambalo liliokolewa na kipa wa Yanga Mustapha.

Katika kipindi cha kwanza Yanga walishindwa kungara katika safu ya kiungo ambayo ilishindwa kuunganisha mabeki na washambuliaji na hadi kumfanya kocha wao kumtoa Simon Msuva.

Dakika ya 37 Kiiza alishindwa tena kuujaza mpira wavuni kufuatia krosi ya Said Ndemla, baada ya mpira wa kichwa kupaa juu ya lango.

Awadhi Juma alishindwa kufunga licha ya kuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini alipiga mpira nje.

Yanga walipata pigo baada ya mchezaji wake Mbuyi Twitte kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Israel Nkongo baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano.

Huu ni mchezo wan ne Yanga inashinda na hivyo kuzidi kukalia kiti cha uongozi katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kujikusanyia pointi 12 huku Simba ikipokea kichapo cha kwanza na kubaki na pointi zake tisa.

Mbali na ushindi huo, Yanga ambayo imecheza nyumbani mechi zote kabla ya jana, ilishinda 2-0 dhidi ya Coastal Union, 3-0 dhidi ya Prisons na 4-1 dhidi ya JKT Ruvu.

Wenzao Simba kabla ya kibano cha jana walishinda ilishinda mechi mbili Tanga 1-0 dhidi ya African Sports na 2-0 dhidi ya Mgambo JKT, kabla ya kuifunga Kagera Sugar 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga wikiendi ijayo itacheza mchezo wake wa kwanza ugenini wakati itakapoifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Simba wataendelea kucheza Uwanja wa Taifa wakati watakapokaribisha Stand United ya Shinyanga.

Simba: Peter Manyika, Hassan Ramadhani/Paper Abdoulaye, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Mussa Mgosi/Ibrahim Ajibu, Hamisi Kiiza na Awadhi Juma.

Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twitte, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Simon Msuva/Malimi Busungu, Salum Telela/Said Makapu, Amiss Tambwe/Deus Kaseke, Donald Ngoma na Haruna Niyonzima.

Mechi zingine leo: Stand United iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT, Tanzania Prisons ilishinda 1-0 dhidi ya Mgambo JKT, Coasta Union ilitoka suluhu na Mwadui ya Shinyanga na Mtibwa Sugar iliilaza Majimaji kwa bao 1-0.

Thursday, 24 September 2015

Arsenal kupepetana na Sheffield Wednesday raundi ya nne Kombe la Ligi englandLONDON, England
TIMU ya daraja la kwanza ya Sheffield Wednesday itaikaribisha Arsenal katika mchezo wa raundi ya nne wa michuano ya Kombe la Ligi baada ya kuifungisha virago Newcastle United  juzi.

Liverpool, ambayo ilihitaji penalti ili kuiondoa Carlisle, itakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Bournemouth.

Manchester United itakuwa mwenyeji wa Middlesbrough, wakati Crystal Palace itasafiri kuifuata Manchester City.

Mabingwa watetezi Chelsea watakuwa wageni wa Stoke City, wakati Southampton ikipangwa na Aston Villa na Norwich City watacheza na Everton.

Hull City, moja kati ya timu tatu za daraja la kwanza zilizomo katika ratiba hiyo, watakuwa wataikaribisha Leicester, ambapo mechi zitachezwa Oktoba 27 na 28 mwaka huu.

Ratiba raundi ya nne Kombe la Ligi

Manchester City v Crystal Palace

Liverpool v Bournemouth

Manchester United v Middlesbrough

Everton v Norwich City

Southampton v Aston Villa

Sheffield Wednesday v Arsenal

Hull City v Leicester City

Stoke City v Chelsea

Waziri Celina Kombani afariki dunia nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani (pichani), amefariki dunia jana akiwa nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah na baadhi ya wabunge waliozungumza jana, walisema Waziri Kombani alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu. 

Kwa mujibu wa Katibu huyo wa Bunge, Kombani alikuwa akisumbuliwa na magonjwa hayo kwa muda mrefu na kwamba mwili wake utarejeshwa nchini kesho. 

Kashilillah alisema Bunge pamoja na Serikali kwa kushirikiana na familia ya marehemu wanafanya taratibu za mazishi.

Hadi kifo chake, Waziri Kombani alikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki mkoani Morogro kwa tiketi ya CCM na pia alikuwa ndiye mgombea wa chama hicho katika jimbo hilo kwa uchaguzi wa mwaka huu.

Pamoja na kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais (Utumishi), Kombani aliwahi kutumikia wizara mbalimbali ikiwemo ya Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na pia Waziri wa Katiba na Sheria.