![]() |
Mary Waya (kulia), akizungumza na mwamuzi Jaquline Sikozi Uhamiaji walipocheza na JKT Mbweni na kushinda 35-22. |
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya netiboli ya Uhamiaji Tanzania imetamba kufanya vizuri
katika mashindano ya Afrika Mashariki yanayoanza Jumamosi kwenye uwanja wa Gymkhana
mjini Zanzibar.
Kocha Mkuu wa timu hiyo Mmalawi Mary Waya alisema kuwa timu yao
imejiandaa vizuri na ni matumaini yake kuwa,watafanya vizuri sana katika mashindano
hayo ya Afrika Mashariki huko Zanzibar.
Waya aliwahi kuwa kocha wa netiboli wa timu ya Filbert Bayi na
aliiwezesha timu hiyo miaka miwili mfululizo kuwa mabingwa wa Tanzania Bara
katika mashindano yaliyofanyika Mbeya. Pia alikuwa kocha wa Taifa Queens kwa miaka kadhaa.
![]() |
Nahodha wa Uhamiaji Tanzania, Zakia Kondo (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari. |
Alisema kuwa wachezaji wake wamepokea vizuri mafunzo aliyoyatoa,
hivyo wanachosubiria ni mashindano tu ili waweze kutoa vichapo kwa kila
watakayekutana naye.
Alisema kuwa kwa timu za Tanzania hakuna anayoigopa kwani zote
anazijua michezo yao na alikuwa akizitoa jasho alipokuwa na timu ya Filbert
Bayi.
Waya pia hivi karibuni alikuwa na timu ya taifa ya Malawi ambayo
aliifikisha katika fainali za Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika
Glasgow, Scotland huku Tanzania ikishindwa kufuzu kwa michezo hiyo.
Mbali na Uhamiaji Tanzania, timu zingine za Tanzania Bara
zitakazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na JKT Mbweni na JKT Ruvu inayoundwa
na wachezaji chipukizi.
Pia Uhamiaji ina wachezaji watatu wa kigeni kutoka nchini Malawi, ambao wamekuja kuiongezea nguvu timu hiyo ili iweze kufanya vizuri zaidi na kuweza kupambana na timu za Kenya na Uganda ambazo zimekuwa zikitamba katika mashindano hayo kila mwaka.
Katika kudhihisha kuwa Uhamiaji imepania kufanya vizuri na makali ya Waya yameanza kufanya kazi pale timu hiyo jana ilipowafunga mabingwa wa Tanzania Bara JKT Mbweni kwa bao 35-22 katika mchezo wa kujipima nguvu uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment