Monday, 30 March 2015

Wanariadha wa mbio za nyika wawasili bila mwenzao

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania Suleiman Nyambui (kulia) akiteta na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT Peter Mwita walipokwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere jijini Dar es Salaam Jumatatu.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa ya riadha ta Tanzania iliyoshiriki mbio za dunia za nyika zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Guiyang nchini China, imewasili salama jijini Dar es Salaam.

Tanzania ilishika nafasi ya sita katika mbio hizo kubwa duniani na hayo yakiwa ni matokeo mazuri zaidi kuwahi kupata kwa timu ya Tanzania.

Mwanariadha Ismail Juma ndiye aliyeitoa nchi kimasomaso baada ya kumaliza katika nafasi ya tifa huku wenzake wengine wanne wakishindwa kuwemo katika 20 bora.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanariadha hao walisema mbio zilikuwa ngumu lakini walijitahidi na wanafurahia matokeo hayo.

Juma aliyeondoka na kitita cha dola za Marekani 3,000 baada ya kushika nafasi ya sita, alisema mbio zilikuwa ngumu lakini alijitahidi na kumaliza katika nafasi hiyo.

Naye kocha wa timu hiyo Francis John alisema kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa JK. Nyerere kuwa, vijana wake walijitahidi sana na kusisitiza kuwa siri ya mafanikio ni kambi waliyopiga huko Mbulu.

Alisema kuwa timu hiyo ilipiga kambi kwa wiki mbili tu huko Mbulu na kama wangekaa zaidi bila shaka matokeo yangekuwa mazuri zaidi na aliwataka Riadha Tanzania (RT) kuanza kambi mapema kwa ajili ya kushiriki mashindano mbalimbali.
Wanariadha wengine wa Tanzania walioshiriki mbio hizo mbali na Ismail Juma aliyemaliza wa sita ni pamoja na
Alphonce Felix, Bazil John, Joseph Teophil na Fabian Nelson, ambao walishiriki mbio za kilometa 12.
Hatahivyo, wakati wanariadha waliwasili Jumatatu jioni kwa ndege ya Emirates, Nelson hakuwemo na alitarajia angewasili mapema na ndege ya Qatar lakini ndege hiyo ilitua yeye hakuwemo na hakukuwa na taarifa zozote za kutowasili kwake.


Katibu Mkuu wa RT Suleiman Nyambui (katikati) akizungumza na mwandishi wa habari wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK. Nyerere wakati wakisubiri kurejea kwa timu ya Tanzania iliyoshiriki mbio za dunia za nyika nchini China Jumatatu. Kulia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji na katibu wa Kamati ya Ufundi ya RT Rehema Killo.

Mwanariadha Bazil John akiwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa JK. Nyerere wakati timu ya taifa ya Tanzania ilipowasili ikitokea China ambako ilishiriki mbio za dunia za nyika.

Mwanariadha Alphonce Felix (kushoto) akipokewa na Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (Suleiman Nyambui timu ya nyika ya dunia ya Tanzania ilipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK. Nyerere jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa RT Suleiman Nyambui (katikati) akiwa na wachezaji wa Tanzania walioshiriki mbio za dunia za nyika timu hiyo ilipowasili Jumatatu. Kushoto ni kocha wa timu hiyo Francis John.
Timu ya taifa ya riadha iliyoshiriki mbio za nyika za dunia ikiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa JK. Nyerere jijini Dar es Salaam

Katibu msaidizi wa Riadha Tanzania Ombeni Zavalla (kulia) akisalimiana na kocha wa timu ya taifa iliyoshiriki mbio za nyika za dunia Francis John timu hiyo ilipowasili jijini Dar es Salaam ikitokea China. Kushoto ni Katibu Mkuu wa RT Suleiman Nyambui na wa pili kulia mjumbe wa kamati ya utendaji ya RT Rehema Killo.

No comments:

Post a Comment