Sunday 21 October 2018

Timu ya Tanzania Yafanya Maajabu Nagai Marathon

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday (kushoto) akiwa na timu ya Tanzania iliyoshiriki Nagai Marathon, wakati wa kuagwa wiki iliyopita. Timu hiyo imefanya `wonders'. Kulia ni Katinu msaidizi wa RT, Ombeni Zavalla.

Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA wa Tanzania wameng'ara katika mbio za Nagai Marathon Japan baada ya kutwaa nafasi za juu.

Mtanzania Marco Joseph wa Talent Athletics Club ya Arusha aliweza kuibuka mshindi kwa upande wa wanaume kilomita 42 akitumia saa 2:21:13 akifuatiwa na Wilbardo Peter wa klabu ya Polisi kwa kutumia saa 2:32:12.

Tanzania pia iling'ara kwa upande wa wanawake km 42 baada ya Angelina John Yumba wa Talent Athletics Club aliyeshinda akitumia saa 2:43:21 muda ambao ni wa kufuzu kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika Doha Qatar mwakani.

Moto wa watanzania haukuishia hapo tu kwani kwenye nusu marathon km 21 wanaume
Fabiano Nelson Sulle wa klabu ya Polisi alishinda kwa saa 1:02:53.

Kwa upande wa wanawake km 21 moto ulizidi baada ya nafasi zote nne za mbele kubebwa na watanzania ambapo Amina Mohamed Mgoo alishinda akitumia saa 1:16:08 akifuatiwa na Rozalia Fabian Duye 1:18:57 (wote wakitokea klabu ya JKT).

Sylivia Masatu wa Maranatha Athletics Club ya Arusha alishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 1:32:52 huku Neema Paulo wa Talent Athletics Club akishika nafasi ya nne kwa muda wa saa 1:41:36.

Timu hiyo ya Tanzania inatarajiwa kurejea nchini Oktoba 24 mwaka huu.

Friday 19 October 2018

Makocha Judo Wapatiwa Mafunzo Yaufundishaji

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi akizungua mafunzo ya makocha wa judo yanayoendelea Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.

Na Mwandishi Wetu, Pwani
WALIMU 30 wa mchezo wa Judo kutoka mikoa mbalimbali wanashiriki mafunzo ya ukocha 'Level III' yaliyoanza jana kituo cha michezo cha Filbert Bayi, Mkuza Kibaha mkoani Pwani.

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa juzi, yameandaliwa na Chama cha Judo Tanzania (JATA), Chama cha Judo Zanzibar (ZJA), na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), chini ya ufadhili wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), kupitia kitengo chake cha Olimpic Solidarity (OS).
Wakufunzi wa mafunzo ya mchezo wa judo wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuza, Kibaha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo Mkuza Kibaha juzi, yanayofundishwa na mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Judo (IJF), Meridja Omar wa Algeria, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema mafunzo hayo ya makocha ni ya level 111.

Bayi alisema kuwa mafunzo hayo ni kati ya mawili ambayo yako kwenye Kalenda ya shughuli za Kamati ya Olimpiki Tanzania mwaka 2018, ambapo mengine kama hayo yalikuwa ya mchezo wa Mpira wa Meza, ambayo yalifanyika wiki chache zilizopitakwa ufadhili wa OS.
Washiriki wa mafunzo ya ufundishaji mchezo wa judo wakiwa katika picha ya pamoja na mkufunzo wao, meridja Omar (wa sita kutoka kulia mstari wa mbele), Mkuza, Kibaha mkoani Pwani. 
Alisema awali TOC waliomba OS kwa kukifahamisha Chama cha Judo Tanzania kuandaa mafunzo ya walimu wa mchezo wa Judo kwa daraja la I (II), ili kupata walimu wengi wa madaraja hayo watakaoweza kueneza zaidi mchezo huo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

"Vyama vya mchezo wa Judo Bara na Zanzibar kwa kufahamu au kutofahamu, wakawasilisha TOC baadhi ya majina wa walimu waliohudhuria mafunzo ya Daraja la I/II yaliyofanyika mwaka 2011... Naipongeza ofisi yangu ya TOC kwa kugundua hilo na kulishughulikia suala hili la kurekebisha daraja kwa kushirikiana na IJF, “alisema Bayi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Judo Tanzania (Taja), Innocent Mallya (kushoto) na mratibu wa mafunzo hayo kutoka Kamati ya Olimpiki Tanzania, TOC, Ame.
TOC imekuwa ikijitahidi kusaidia vyama na mashirikisho ya michezo mbalimbali nchini hasa kwa mafunzo ya walimu, utawala, wanawake na michezo, lakini bado baadhi hawatambui au kama wanatambua basi hawatumii nafasi hizi vizuri.

Alisema TOC ipo tayari kutoa  elimu kwa walimu wa vyama vya michezo, ambao watakuwa na uhitaji pale wakati wao utakapofika.
"Nia na malengo ya Kamati ya Olimpiki ni vyama vya michezo kuwa na walimu wengi, watakaokuwa na taaluma ya kuwandaa wanamichezo watakaokuwa washiriki wazuri kutuwakilisha katika mashindano ya kimataifa na kutuletea medali," alisema.

Aliongeza kuwa, Tanzania ina vipaji vingi vya mchezo wa Judo, kinachokosekana ni walimu wenye ufahamu unaotakiwa katika ngazi za kimataifa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jata, Innocent Mallya, mbali na kushukuru kwa kupata mafunzo hayo, aliwataka washiriki kuzingatia mafunzo na kwenda kuutumia ujuzi huo katika kuzalisha wachezaji wapya huko watokako.
Mkufunzi wa Kimataifa wa Mafunzo ya Makocha wa mchezo wa judo, Meridja Omar kutoka Algeria. 
Mallya, alisema hivi sasa malengo ni kwa vijana kwani katika klabu nyingi hapa nchini wachezaji wengi walioko hawana muda mrefu kuendelea kucheza, hivyo ni jukumu la makocha hao kwenda kuibua vipaji vipya.

Washiriki mbalimbali wa mafunzo hayo walisema kwa nyakati tofauti, mafunzo hayo yatawasaidia kuibua vipaji vipya katika mchezo huo, hasa katika shule mbalimbali nchini.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo kwa makocha wa judo mjini Kibaha, akijitambulisha.
Mafunzo hayo ambayo yatasaidia sana kuuendeleza mchezo huo kwa kuibua vipaji vipya, yanatarajia kukamilika Oktoba 24 mwaka huu, ambako washiriki watakabidhiwa vyeti baada ya kufanya mitihani yao.
Katibu Mkuu wa Chama cha Judo Tanzania (Taja), Inndo Mkuza Kibaha mkoani Pwani.ocent Mallya akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makocha wa mchezo wa judo.


Tuesday 16 October 2018

Taa Yakabidhi Mafuta ya Ngozi kwa Wanafunzi Wenye Ualibino

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Naomi Semadio (kulia) akiteta na Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu, Masoud Babu wakati TAA ilipokabidhi mafuta kwa wwanafunzi walemavu wa ngozi leo Jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege imetoa msaada wa mafuta kwa wanafunzi walemavu wa ngozi wa shule za msingi za Uhuru Mchanganyiko na ile ya Jeshi la Wokovu jijini Dar es Salaam.

Jumla ya chupa 55 za mafuta hayo ya ngozi aina ya Infinity Care SPF 30 Sun Screen, ambapo kichupa kimoja kina gharama ya Sh 25,000 na kufanya gharama yote kuwa ni Sh 1,375,000.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tazania (TAA), Naomi Semadio akimkabidhi mafuta mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi ya Jeshi la Wokovu jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni mwalimu wa shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu, Masoud Babu na kushoto ni Katibu Mkuu wa Taifa Chama cha Wenye Ualibino Tanzania, Mussa Kabimbi.
Akikabidhi mafuta hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela, mwakilishi huyo Naomi Semadio alimkabidhi kila mwanafunzi kichupa cha mafuta hayo kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

Alisema kuwa hatua hiyo ya TAA ya kutoa msaada huo ni sehemu ya kawaida ya sera ya mamlaka hiyo kusaidia jamii kwa kutatua matatizo yake, ambapo kwa vijana hao, changamoto kubwa kwao ni matatizo ya ngozi.
Alisema wamekuwa wakitoa misaada kwa jamii bila kuwepo kwa ubaguzi wa aina yoyote, ambapo hivi karibuni imefanikisha tamasha la urithi wetu lililofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam pamoja na kusaidia Umoja wa Wabunge Wanawake kwa ajili ya kujenga vyoo.

Mwalimu wa shule ya Msingi Jeshi la Wokovu Masoud Babu aliipongeza TAA kwa msaada huo na kusema kuwa wanafunzi wao albino wamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo hiyo ya tatizo la afya, na hasa ngozi.
Alisema asilimia 70 ya watu wenye alboni wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na saratani ya ngozi, pia alitaka kofia na miwani kwa ajili ya kuwakinga wanafunzo hayo.
Alisema gharama ya kumtibu mtoto albino ni kubwa na amewapogeza TAA na kuutumia vizuru msaada huo na amewataka wasiwasahau, waendelee kuwasaidia.

“Msaada huu utakuwa ni mwanzo kwani wanatarajia TAA itaendelea kuwasaidia kwa masuala mbalimbali, hasa ukizingatia mafuta hayo yana gharama kubwa na wengi wanashindwa kumudu gharama zake, “alisema mwalimu huyo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Jeshi la Wokovu, Rehema Mwahalende alishukuru TAA kwa msaada huo kwani utawasaidia wanafunzi hao kuepukana na matatizo ya ngozi, ambayo yanasababisha saratani.
Alisema TAA imeonesha mfano wa kuigwa kwa kuwajali watoto hao na wanatarajia wataendelea kuwasaidia katika nyanja mbalimbali.
Mkurugenzi Msaidizi wa Jeshi la Wokovu Mgulani Jijini Dar es Salaam, Meja Rehema Mwahalende akizungumza baada ya TAA kukabidhi mafuta ya ngozi kwa wanafunzi wa shule hiyo na ile ya Uhuru Mchanganyiko leo Mgulani Jijini Dar es Salaam.

Monday 15 October 2018

Waeleza Umuhimu wa Kutoa Taarifa za Miradi ya Maendeleo

Na Mwandishi wetu
IMEELEZWA kuwa kuna umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi zinazohusu utekekezaji wa miradi ya maendeleo.
  
Wakizungumza katika mkutano wa kuandaa taarifa kwa wadau wa maji katika kata za Kwembe, Msigani na Kibamba, washiriki wamesema sheria na taratibu zilizo wekwa taarifa ni muhimu ili wananchi wawe na mrejesho wa miradi inayowahusu.

 Mwezeshaji wa mkutano huo ulioandaliwa na  Asasi ya Pakacha na kufadhiliwa na The Foundation For Civil Society, Bumija Moses amesema wananchi wanaweza kuleta msukumo wa kiutendaji kwa viongozi kama wakishirikishwa kupata taarifa   za miradi inayojengwa na utekelezaji
wake.
Mkutano huo ulikutanisha wananchi na viongozi kutoka katika katika kata tatu za Kwembe, Msigani na Kibamba.

Mkutano huo ulifanyika Ijumaa mjini Kibaha.

Diwani wa viti maalumu (Chadema) wa kata ya Msigani,mheshimiwa Vicky Mchome amesema ushirikishwaji wa wananchi katika sehemu nyingi, ikiwemo kata yake haupo akitoa wito kwa wananchi kupewa taarifa.

 Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kwembe, Peter Chawala amesema wananchi wasisubiri kushirikishwa, wana haki ya kuuliza viongozi wao ili kupata taarifa zinazowahusu.
  
Adam Kingu, mkazi wa Maramba Mawili amesema licha ya wananchi, wapo
pia baadhi ya viongozi ambao hawapati taarifa za utelekezaji wa miradi ya Maji.

“Unaweza kwenda kumuuliza mtendaji lakini cha kushangaza hajui bajeti  iliyotengwa au hata mradi unaotekelezwa”, amesema Kingu.

Kata za Kwembe, Msigani na Kibamba zina changamoto za upatikanaji wa maji, hivyo kupelekea Pakacha kuunda kamati maalumu iliyowashirikisha wananchi na kupita katika kata zote ili kujua kuna miradi ipi ya maji iliyotengewa bajeti na hatua iliyofikia katika utekelezaji wake.

Mmoja wa mjumbe wa kamati hiyo, Almas Mohamed amesema wamepata malalamiko mengi ya wananchi kutojua utekelezaji wa miradi ya maji iliyopo katika kata zao.

Miongoni ya miradi hiyo ni ujenzi wa kisima cha maji cha Kibamba kilichotengewa milioni 280 kwa utekelezaji wa kuanzia mwezi April mwaka jana mpaka june mwaka huu na ujenzi wa tanki la maji lililopo Kwembe Kingazi B uliotengewa  milioni 55, ukiwa katika hatua za mwisho.

Katibu wa Pakacha, Haroun Jongo amesema serikali inafanya jitihada kubwa kuleta maendeleo kwa wananchi, ndio maana asasi kama Pakacha zinapata fursa ya kuelimisha wananchi.

“lengo la mkutano huo ni kuandaa taarifa kwa kuwashirikisha wananchi, baada ya kufanya upembuzi yakinifu ya miradi iliyopo.

Ufuatiliajia unafanywa kupitia Pets, amesema Jongo

Vichekesho vya Mwantumu vyaongezwa Udambwi-dambwi

Lucas Mhuvile au Joti (mwenye miwani) wakati wa uzinduzi wa msimu wa pili wa vichekesho vya Mwantumu leo katika ofisi za DStv Jijini Dar es Salaam. Kulia ni msanii mkongwe Bafadhili.

 *Sasa Kuonekana Mara Mbili kwa Wiki

*Msimu wa Pili Waja kwa Kishindo Kikubwa

Na Mwandishi Wetu
MSIMU Msimu mpya wa vichekesho maarufu vya Mwantumu ambavyo huonekana kupitia chaneli ya DStv ya Maisha Magic Bongo,  unaanza rasmi Jumanne Oktoba 16,  huku vikiwa vimeongezewa manjonjo ili kuwahakikishia watazamaji na mashabiki wake burudani isiyo na upinzani.

 Vichekesho hivyo vinavyoongozwa na mchekeshaji maarufu nchini Lucas Mhuvile maarufu kwa jina la kisanii JOTI ambaye kwenye vichekesho hivi amevaa uhusika wa watu watatu tofauti.
Joti katikapicha za uhusika tofauti tofauti katika vichekesho vya Mwantumu.
Joti katika vichekesho hivyo anacheza uhusika wa Mzee Mrisho, Kaboba na Mwantumu Sahare,  ambapo vichekesho hivyo vimekuwa ni moja wa vipindi vinavyotazamwa sana na kupendwa na maelfu ya watu hapa nchini ambapo huoneshwa kupitia chaneli maarufu ya Maisha Magic Bongo – DStv 160. 

Majina maarufu pia katika tasnia ya uigizaji na uchekeshaji yatakuwepo msimu huu akiwemo Mzee Fungafunga (Mzee Mwalubadu), Mama Abduli (Mwantumu Mcharuko), Alex Wasponga(Kayombo) na wengineo wengi
  
Shumbana wakati wa uzinduzi wa vichekesho vya Mwantumu leo.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa msimu wa pili wa vichekesho hivyo, Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania Alpha Mria amesema kuwa tangu kuanza kwa msimu wa kwanza wa vichekesho vya Mwantumu mnamo Oktoba 2017, vichekesho hivyo vimekuwa na msisimko wa aina yake na vimepokelewa vizuri sana na watazamaji na hivyo kuvifanya kuwa na mashabiki wengi sana.

 Amesema msimu huu wa pili, watazamaji wa Maisha Magic Bongo na mashabiki wa Mwantumu watashuhudia mikasa ya aina yake, ambapo baada ya Bahati kupata ujauzito, baba yake mzee Mwalubadu anaamua kumpeleka Kaboba katika vyombo vya sheria kwa kosa la kumpa Bahati ujauzito.
Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania Alpha Mria akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwantumu leo.
Hata hivyo suala hilo linafika kwa Babu yake Kaboba mzee Mrisho, ambaye wakati huohuo hataki Kaboba apate matatizo yoyote. Kinachotokea hapo ni drama ya aina yake itakayowaacha watanzamaji wakivunjika mbavu kwa kucheka!

 “DStv kupitia Chaneli yake pendwa ya Maisha Magic Bongo, siku zote imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunatoa msisitizo kwenye maudhui ya ndani na vichekesho hivi ya Mwantumu ni mfano halisi. Hii ni yetu, imetengenezwa hapa tanzania na wazalishaji, waandaaji na waigizaji wote wa hapa hapa nchini” alisema Alpha.
Joti akizungumza leo.
 Vichekesho vya Mwantumu vilianza msimu wa kwanza mnamo Oktoba 2017 Na kuendelea kwa muda wa mwaka mmoja ambapo vilikuwa vikionyeshwa mara moja kwa wiki. Katika msimu huu mpya vichekesho hivyo vitaonekana mara mbili kwa wiki siku ya  Jumanne na  Jumatano  saa moja na nusu usiku. 
Hii itawapa fursa mashabiki na watazamaji wa Maisha Magic Bongo kupata burudani zaidi kwani kumekuwa na maombi mengi ya kuongeza vipindi hivyo kutokana na umaarufu wake.


Thursday 11 October 2018

SBC Kuwapeleka Lebanon Washindi Rotary Marathon 2018

Meneja Masoko wa SBC, Roselyne Bruno akizungumza na waandishi wa habari wakati wakitangaza ofa ya wanariadha wa Tanzania watakaoshinda mbio za Dar Rotary Maratthon kupata ofa ya kwenda Lebanon.

Na Mwandishi Wetu
WASHINDI wawili wa Dar Rotary Marathon zitakazofanyika mwishoni mwa wiki hii, watapata ofa ya kwenda kushiriki Beiruti Marathon nchini Lebanon mwezi ujao.

Meneja Mafunzo na Uwezeshaji wa Kampuni ya Peps nchini, SBC, Rashid Chenja alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, wanariadha wa Tanzania watakaoshika nafasi ya kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake katika Rotary Marathon 2018 kilometa 42, watapata ofa ya kushiriki Lebanon Marathon 2018.
Meneja Mafunzo na Uwezeshaji wa Kampuni ya Peps nchini, SBC, Rashid Chenja katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za Riadha Tanzania (RT). Kushoto ni kiongozi wa wanariadha, Jilala.
   Beirut Marathon itafanyika Novemba 11 nchini Lebanon, ambapo washindi hao wa Tanzania watawezeshwa kila kitu ili kwenda na kushiriki mbio hizo, ikiwemo viza, tiketi ya kwenda na kurudi, bima na mambo mengine ili washiriki vizuri mbio hizo.

Chenja akifafanua alisema kuwa hata kama mwanariadha wa Tanzania atamaliza katika nafasi ya tano katika washindi wa jumla, atakuwa amekidhi vigezo vya kupata ofa hiyo kwa kuwa atakuwa ni Mtanzania wa kwanza katika matokeo hayo ya Rotary Marathon 2018.
Rashid Chenja akizungumza.
Alisema lengo la SBC ni kuhakikisha wanariadha wa Watanzania wanapata motisha zaidi na kuwawezesha kufanya vizuri ili washindie mbio hizo, ambazo kampuni hiyo imedhamini kwa miaka 10 sasa.

Mbio hizo mbali na kupita katika mitaa mbalimbali ya jijini la Dar es Salaam, zitaanzia katika Uwanja wa The Green au Farasi uliopo Oysterbay, ambako washindi watakabidhiwa zawadi zao.
Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla alishukuru kwa SBC kutoa ofa hiyo kwa wanariadha wa Tanzania kushiriki mbio Lebanon, lakini aliwataka kujitahidi kuvunja rekodi ya njia ili kuongeza msisimko katika mbio hizo.

Alisema kwa miaka takribani 10 mbio hizo zimekuwa zikifanyika, lakini rekodi ya njia hiyo hajawahi kuvunjwa, hivyo aliwataka wanariadha kuhakikisha wanaivunja rekodi hiyo ili kuboresha zaidi mbio hizo.
Jilala akizungumza kuhusu ofa hiyo ya SBC kuwapeleka wanariadha Lebanon.
Mbali na mbio za kilometa 42, pia kutakuwa na zile za kilometa 21, 10 na zile za kilometa 5, ambazo ni za kujifurahisha.

MTWARA KUVUNA VIBE KAMA LOTE MSIMU HUU WA TIGO FIESTA 2018


PRESS RELEASE
Wateja wa Tigo kupata faida mara tatu kupitia promosheni za kusisimua

Mtwara, Oktoba 13, 2018 – Huku msimu wa mavuno ya korosho ukiwa umewadia katika mikoa ya nyanda za juu kusini, wakaazi wa Mtwara na viunga vyake wanajiandaa kuvuna vibe kama lote kutoka kwa mastaa wa muziki wa bongo flava katika msimu unaoendelea wa Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa {Katikati} akiongea na waandishi wa Habari kuhusiana na fursa mbalimbali za kibiashara zinatazopatika katika mkoa huo kutokana na ujio wa tamasha la Tigo Fiesta 2018 - Vibe Kama Lote linalotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii katika viwanja vya Nangwanda Sijaona. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Pwani, Joseph Mutalemwa na Mratibu wa Tamasha la Tigo Fiesta, Pancras Mayalla {maarufu kama  Askofu TZA}.

Waandaaji Clouds Media Group, kupitia Katibu Kiongozi wa Kamati ya Maandalizi, Gardner Habash amewaalika wakaazi wa Mtwara waje kupumzika baada ya shughuli ngumu za kuvuna korosho kwa kusikiliza 100% vibe za nyumbani.

‘Kwa wafanyabiashara,  msimu waTigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote ni fursa ya kujiongezea kipato kwa kutoa huduma za usafiri, malazi, vinywaji na chakula na huduma nyingenezo zinazohitajika na maelefu ya mashabiki watakaojitokeza kushuhudia tamasha hili,’ Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Gelasius Byanakwa alisema.

Kupitia shindano la Tigo Fiesta 2018 – Supa Nyota, wasanii wanaochipuka kutoka Mtwara watapata nafasi ya kuonesha vipaji vyao, na wale watakaofanya vizuri watapewa fursa ya kutumbuiza katika tamasha kuu la Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote linalotarajiwa kurindima siku ya Jumapili tarehe 14 Oktoba katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

 ‘Mbali na muziki, wateja wa Tigo pia wanaweza kuvuna hadi mara mbili ya thamani kwa vifurushi vya intaneti watakavyonunua kupitia *147*00#

Mkurugenzi wa Tigo  Kanda ya Pwani, Joseph Mutalemwa  (Kulia) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa (katikati) pamoja na Mratibu wa Tigo Fiesta 2918 , Pancras Mayalla katika Mkutano na waandishi wa habari kueleza maandalizi ya tamasha la Tigo Fiesta 2018 litakalofanyika Uwanja wa Nang'wanda Jumapili hii pamoja na ofa mbalimbali za Kampuni ya Tigo katika msimu huu ikiwemo mfumo wa  malipo kwa wakulima wa korosho kupitia huduma za Tigo Pesa.

Promosheni ya Data Kama Lote itahakikisha kuwa mashabiki wanaweza kufuatilia habari na matukio yote ya msimu wa Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote; au kufurahia kuperuzi kwenye mtandao wenye kasi zaidi wa 4G+,’ Mkurugenzi wa Tigo, Kanda ya Pwani Joseph Mutalemwa alisema.

Wateja wote wa Tigo pia wanaweza kuvuna hadi TSH 10 millioni, zawadi za kila wiki za TSH milioni moja, ama zawadi za kil asiku za TSH 100,000 kwa kushiriki katika shindano la Tigo Fiesta 2018 – Chemsha Bongo. 

Ushiriki katika shindano hilo unapatikana kwa kutuma neno MUZIKIkwenda 15571 au kwa kutembelea tovuti ya http://tigofiesta.co.tz.

Watakaoshusha vibe kama lote mjini Mtwara ni pamoja na kundi la Rostam (Roma and Stamina), Fid Q, Zaid na Weusii (Joh Makini, Niki wa Pili na G-Nako) ambao walikonga mioyo ya wapenzi wa muziki mjini Iringa. Wengine ni wasanii a bongo flava Mesen Selekta na Foby, wakongwe Chegge, Barnaba na Mr Blue, pamoja na akina dada Ruby na Lulu Diva.

TIketi za Tigo Fiesta 2018 – Mtwara zinapatikana kwa bei punguzo ya TSH 5,000 kupitia Tigo Pesa Masterpass QR kwa kupiga *150*01#, kuchagua namba 5 (lipia bidhaa), na kuchagua namba 2 (lipa kwa Masterpass). Tuma kiasi husika cha TSH 5,000 kwenda namba ya Tigo Fiesta 78888888.

Tamasha la Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote tayari limezuru mikoa ya Morogoro, Sumbawanga na Iringa, na linatarajiwa kutembelea mikoa ya Singida, Songea, Moshi, Tanga, Muleba, Kahama, Mwanza, Musoma, Arusha na Dodoma, huku fainali ikiwa Dar es Salaam.

DStv Mubashara Pambano la Taifa Stars Cape Verde

Na Mwandishi Wetu
KING’AMUZI cha DStv kitaonesha mpambano mkali wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya timu ya Tanzania, Taifa Stars itakayocheza leo dhidi ya Cape Verde.


Mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa Capo Verde au Praia, utaanza kuanzia saa 2:00 Usiku na DStv watakuwa mubashara kuonesha kipute hicho muhimu.

Watanzania wataweza kufuatilia mpambano huo kupitia DStv na kushuhudia nyota wao kama akina Mbwana Samatta anayeichezea timu ya Ubelgiji ya KRC Genk, Farid Mussa, Shaaban Idd Chilunda na Simon Msuva.

Tayari kikosi cha Stars kimeshawasili visiwani humo tangu juzi Jumatano kikiwa na ari kubwa ya kupambana na kupata ushindi katika mchezo huo, ambao ni muhimu ili kuweka matumaini ya kufuzu fainali hizo, ambazo Tanzania ilifuzu kwa mara ya mwisho mwaka 1980 zilipofanyika Lagos, Nigeria.

Msimamo wa kundi lao la unaonesha Uganda ndio vinara wakiwa na pointi nne, Lesotho ya pili wakiwa na pointi mbili sawa na Stars, lakini wanatofautiana kwa mabao ya kufunga, wanaoburuza mkia ni Cape Verde wanye pointi moja.

Stars itaingia kwenye mchezo huo huku ikijua wazi kuwa na deni kubwa kwa Watanzania baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupewa sapoti kubwa na Serikali katika maandalizi ya mchezo huo ikiwemo kuandaliwa ndege maalum ya kwenda na kurudi.

Rekodi zinaonesha kuwa timu hizi zimekutana mara mbili mwaka 2008 katika harakati za kufuzu Kombe la Dunia, ambapo Oktoba 11 Stars wakiwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam waliiibuka na ushindi wa 3-1 kwa mabao ya Athuman Iddy, Jerson Tegete na Mrisho Ngassa, waliporudiana Cape Verde walishinda 1-0.

Kocha wa kikosi cha Stars kinachoongozwa na nahodha Mbwana Samatta, Emmanuel Amunike amesema kuwa kikosi chake kipo kwenye hali nzuri na kimejipanga kuwapa furaha Watanzania.

Amesema benchi la ufundi, wachezaji na kila kitu kiko tayari kwa ajili ya mchezo huo, ambao utawawezesha Watanzania kufurahi kutokana na matokeo mazuri watakayopata.

Timu mbili za kwanza kutoka katika kila kundi ndizo zitafuzu kwa fainali hizo, ambazo zitafanyika mwakani nchini Cameroon.

Tuesday 9 October 2018

Raia wa Syria, Sudan Kusini wakamatwa JNIA wakisafirisha mamilioni ya fedha


1.        Kamishna Msaidizi na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa akinyanyua juu moja ya bunda la Dola za Kimarekani zilizokamatwa leo kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), zikisafirisha isivyo halali na raia wa Sudan Kusini Bi. Nada Zaelnoon Ahamed na Bw. Mohamed Belal, raia wa Syria.

Na Mwandishi Wetu
 ABIRIA wawili Raia wa Sudan Kusini na Syria leo wamekamatwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) wakisafirisha fedha taslim dola 70,000 za Kimarekani sawa na shilingi milioni 156 za Kitanzania na paundi 3410 za Sudan bila kufuata taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la JNIA, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi, Barnabas Mwakalukwa alimtaja Raia wa Sudan Kusini Bi. Nada Zaelnoon Ahamed (38) mwenye hati ya kusafiria namba P01563534 amekamatwa saa 10:00 jioni akiwa eneo la ukaguzi wakati akiingia ndani tayari kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ 485) akielekea Nairobi.

1.        Bi.Nada Zaelnoon Ahamed (38) Raia wa Sudan Kusini (katikati mwenye ushungi) akiwa mbele ya waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), baada ya kukamatwa na dola 60,000 za Kimarekani na Paundi 3410 za Sudan.


Hatahivyo, Afande Mwakalukwa amesema abiria huyo am3kamatwa na dola 60,000 za Kimarekani na paundi za Sudan 3410, ambazo zote kwa pamoja alishindwa kutoa taarifa ya fedha alizokutwa nazo kwa mujibu wa sheria ya utakatishaji fedha ya mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

Pia alimtaja Bw. Mohamed Belal (31), Raia wa Syria mwenye hati ya kusafiria namba 003-16L096876 aliyekuwa akisafiri kwa ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia (ET 864) kuelekea Syria kupitia Addis Ababa amekamatwa na dola za kimarekani 10,000 sawa na Tsh. milioni 20 za Kitanzania, ambazo naye alishindwa kuzitolea taarifa.

“Watuhumiwa wote wawili wamezuiwa na hawawezi kuendelea na safari zao kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria zilizopo,” amesema Afande Mwakalukwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewapongeza maafisa usalama wa JNIA kwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha wasafiri, wadau na maeneo yote ya viwanja vya ndege yanabaki salama na vitendo vya kiuhalifu havina nafasi katika viwanja hivyo.

1.        Jumla ya Dola za Kimarekani 70,000 sawa na Tsh. milioni 156 za Kitanzania zikiwa zimekamatwa leo kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), zikisafirishwa na Raia wawili wa Syria Bw. Mohamed Belal na Bi. Nada Zaelnoo Ahamed raia wa Sudan Kusini kwa kutofuata taratibu.

 Bw. Mayongela amesema pamoja na watumishi hao kufanya kazi katika wakati mgumu kutokana na baadhi ya abiria kuwa watata kila wanapotaka kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Ametoa wito kwa wadau, wasafiri na wafanyakazi wote kushirikiana na maafisa usalama, vyombo vya ulinzi na usalama katika kutoa taarifa stahiki ili vitendo vya kiuhalifu kama hivi visipate nafasi kwenye viwanja vya ndege kwani ndio vinatoa taswira ya nchi.

“Viwanja vya ndege visitumike kama uchochoro wa kupitisha nyara za serikali, dawa za kulevyia, fedha haramu au matukio yeyote yanayoashiria uvunjifu wa Amani au uvunjaji wa sheria za nchi,”

Raia wa Syria, Bw. Mohamed Belal (31) mwenye fulana nyeupe akiwa mbele ya waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), baada ya kukamatwa na dola 10,000 za Kimarekani, ambazo hakuzitolea taarifa kwa Maafisa wa Forodha wa kiwanjani hapo.
Pia aliongeza “Niombe wananchi na vyombo vya usalama kufanya kazi kwa weledi kwa sababu wasipofanyakazi kwa weledi matukio kama haya yangeweza kupata nafasi na kuharibu taswira ya nchi, kwa ujumla mwisho wa siku inaharibika, kwani nia yetu na lengo letu ni zuri ni kuhakikisha hatutumiki kwa namna moja au nyingine kufadhili au kuwezesha shughuli za kiuhalifu zifanyike katika maeneo yetu”.

Amesema na hii ni moja ya ushahidi maafisa usalama wanapata mafunzo na kujengewa uwezo wa kuwa na vifaa vya kisasa kwani vitu mbalimbali vimekuwa vikigundulika kupitia mashine za ukaguzi, na pia kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, hivyo ametoa wito watu wasidhubutu tena kujaribu kwa namna yeyote ile akidhani viwanja vya ndege wamelala, kwani ulinzi na usalama unaendelea kuimarika.

Kwa upande wake Meneja wa Forodha wa Kituo cha JNIA, Bw. Njaule Mdendu amesema abiria wote wanaosafiri au kuwasili endapo wanakiasi kikubwa cha fedha za kigeni kuanzia dola 10,000 za Kimarekani sawa na Milioni 10 za Kitanzania anapaswa kutoa taarifa Idara ya Forodha kwa kuwa ni matakwa ya sheria ya mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012 na kanuni za mwaka 2016, na asipofanya hivyo ni kosa la jinai.

 Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (kushoto) akimsikiliza Kamishna Msaidizi wa Polisi, Barnabas Mwakalukwa (aliyesimama) alipokuwa akitoa maelezo kwa waandishi wa habari leo ya kukamatwa kwa Raia wawili wa Sudan Kusini na Syria waliokuwa wakisafirikisha fedha taslim milioni 156 bila kufuata sharia.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wa pili kulia) akisisitiza jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) uliofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Pili la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakati walipokamatwa Raia wawili wa Syria na Sudan Kusini wakisafirisha mamilioni ya fedha bila kufuata taratibu.      

Bw. Mdendu amesema abiria wanapaswa kuchukua fomu maalum akieleza utambulisho wake na kiasi cha fedha anachoingia nacho au kutoka nacho, na fomu atazipata kwenye ofisi zote za forodha za mipakani kwenye viwanja vya ndege, mipaka ya ardhi na majini endapo atakuwa akitumia usafiri wa barabara au majini.

“Hizi fomu pia zipo kwenye tovuti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na akishajaza anawasilisha ofisi za Forodha na kiasi cha fedha anachosafiri au kuwasili nacho na afisa atazihakiki na akiridhika ataruhusu aendelee na safari yake, na napenda kuwatoa hofu watu kuwa fedha zao hawanyang’anyi baada ya kutoa taarifa na ataondoka nayo, lakini endapo usipotoa taarifa ni kosa na inaadhabu yake kulingana na kiasi cha fedha ulichokutwa nacho, hivyo tuwaombe abiria kutimiza matakwa ya kisheria, kwani watu wamekuwa wakifanya makosa bila kujua sheria,” amesema.

Thursday 4 October 2018

BMT YAIGOMEA RUHUSA TIMU YA TAIFA YA RIADHA ILIYOPASWA KUSHIRIKI MASHINDANO YA NUSU MARATHON YA JUMUIYA YA MADOLA

Taarifa kwa vyombo vya habari

Ndg wanahabari,  

Bilashaka watanzania watapenda kujua sababu ya ukimya wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kuelekea mashindano Jumuiya ya Madola ya mbio za nusu marathon ambapo timu ilitarajiwa kuelekea Cardiff Uingereza  Oktoba 4 kwa ajili ya mashindano yanayo tarajiwa kufanyika Oktoba 7 2018, na timu zote zinazoshiriki kurejea makwao Oktoba 8 2018.

Tunasikitika kutoa taarifa rasmi kwamba RT ilipambana na changamoto za kifedha na hatimaye kufanikiwa kupata fedha kwaajili ya safari. Timu ya taifa ya riadha ilikuwa imejiandaa kwa utaratibu tuliojiwekea pamoja na makocha wetu waliopo Arusha. Pamoja na kuwepo na barua zote za mialiko na uhakikisho wa kugharimiwa gharama zote za kukaa uingereza, lakini Baraza la Michezo Tanzania (BMT) iliona ni busara kuinyima timu ya taifa ya riadha haki ya kushiriki mashindano hayo muhimu sana kwa nchi yetu.

“Sijapata kusikia hata siku moja kwamba timu iliyostahili kuagwa kitaifa na kukabidhiwa bendera na kiongozi wa ngazi ya kitaifa inanyimwa ruhusa kwa sababu zisizo za msingi”

Kwa mujibu wa barua iliyopokelewa na RT kutoka BMT imeainisha katazo ambalo halina mashiko yoyote ya kiufundi hadi kusababisha taifa kukosa nafasi muhimu kama ya kushiriki mashindano ya Nusu marathon ya Jumuiya ya Madola. Ni jambo la kushangaza kuona BMT inaingilia kati uteuzi wa wanariadha wa timu ya taifa wakati wao ni wasimamizi wa sheria na kanuni za michezo yote nchini. Lakini kwa barua hiyo inaonekana kana kwamba BMT inawamiliki wanariadha wetu wakati ni Dhahiri hawajasimamia  shughuli yoyote ile ya maandalizi wala kuchangia gharama yoyote ya kambi ya mazoezi hadi leo hii. Wanariadha waliochaguliwa kuwakilisha taifa ni nane. Kati ya hao wanariadha wawili wamo kwenye orodha ya wanariadha watakaokwenda Japan kwenye Nagai Marathon pamoja na msafara wa BMT. Chakushangaza barua ya BMT imeinyima ruhusa timu nzima ya taifa, ilikukidhi matakwa ya BMT yasio na weledi wala maono ya mbali. Wanariadha waliokuwemo kwenye msafara wa kwenda japan ni Fabiano Sullen na Marco Joseph.

Pamoja na jitihada za kuwaeleza BMT kwamba RT tunatumia busara na ufundi zaidi kuhakikisha kwamba nchi yetu inawakilishwa vyema katika mashindano yote mawili, pamoja na hayo BMT imekataa na kuamua kutumia mamlaka yao kibabe. Matokeo yake timu ya taifa ya riadha haitashiriki kwenye mashindano muhimu ambayo wanariadha wetu wangeweza kupata fursa ya kufuzu kwenda kwenye mashindano ya Olimpiki yam mwaka 2020 nchini Japan. Mashindano ya Cardiff yanatambuliwa na Shirikisho la Vyama vya riadha Duniani (IAAF) na hivyo watakaofanya vizuri wanafuzu moja kwa moja kwenda kwenye mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto. Kutokana na uamuzi wa BMT timu haiendi Cardiff kwasababu BMT wameamua kuonyesha kwamba wana nguvu na mamlaka.

Kimsingi BMT inadai kwamba zuio la safari ya Cardiff kwa timu ya taifa imewekwa eti kwa sababu ya Nagai Marathon. Zaidi ya hapo barua hiyo imeeleza kwamba RT haiheshimu msaada mkubwa tunaopata kutoka Japan! Sababu ambayo haina mashiko kwa mchezo wetu wa riadha na ni wazi ni ya kuchukua maamuzi bila ya kufikiria kwa mapana.

RT ingependa kupambanua umuhimu wa mashindano yote mawili (Nagai Marathon na Nusu Marathon ya Jumuiya ya Madola);

1)    Commonwealth Half Marathon inakimbiwa Oktoba 7 (wiki 2 kabla ya Nagai) ambapo wanariadha wangerudi na kuweza kuwahi hiyo mbio ya Nagai
2)    Commonwealth Half Marathon ni mashindano ya medali wakati mbio za Nagai siyo ya medali bali ni ya kujenga ushirikiano kati ya Tanzania na Japan kuelekea Tokyo Olimpiki 2020
3)    Kiufundi hakuna tatizo lolote kwa mwanariadha kukimbia nusu marathon kabla ya marathon. Nusu marathon ndiyo ingekuwa jaribio zuri kuelekea full marathon ya Nagai
4)   Wanariadha walioteuliwa kwenda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola wamefikia vigezo (sababu wameshawahi kushiriki mbio za 21km), hivyo hawaendi kubahatisha au kujaribu
6)    Wanariadha waliochaguliwa kwenda Nagai, ni wale ambao wanakimbia marathon ya km 42 kwa mara ya kwanza, hivyo wanakwenda kwenye majaribio ya mbio ndefu.
7)    Katika safari ya Nagai kuna viongozi watatu wa BMT wanakwenda na timu ya Riadha, huenda hiyo ndiyo sababu ya kuthamini Nagai kuliko Madola
8)    Kwa maana nyingine ni sawa na kusema wajumbe wa BMT wamegeuka kuwa viongozi wa RT. RT itawakilishwa na Naibu KM na Katibu Kamati Ufundi
9)    Madhumuni ya Nagai ni kuimarisha uhusiano hasa kwa wanariadha wanawake kufuatia mashindano yaliyofana ya JICA Ladies Championships, ni jambo la heri sana lakini siyo sababu ya BMT kunyanyasa Shirikisho lenye jukumu la kuendesha program zake kwa uhuru. Kwanini BMT wasiingilie shughuli za TFF? Kuna uhusiano gani kati ya mashindano ya Nagai na ya Cardiff?
Tanzania ni mwanachama wa nchi za Jumuia ya Madola, tunapatashida kumuelewa kiongozi wa michezo ambaye haelewi kwamba ushiriki wetu ni muhimu sana, katika mfumo mzima wa umoja wa nchi za Jumuiya ya Madola na michezo ndiyo jambo kubwa linalohusisha jamii moja kwa moja (The games are the Commonwealth's most visible activity). Je mtendaji mkuu wa BMT hilo halifahamu?

Utata mwingine huu hapa;

Mwanzoni kabisa Kamati ya Ufundi ilimchagua Ndg William Kallaghe (Makamu Rais RT) kuwa sehemu ya msafara wa Nagai, lakini ikaja hoja ya kuupinga uongozi wa juu wa RT kushiriki Nagai (sababu hatuifahamu sana), hoja yenyewe ilikuwa kwamba “hii ni issue inayowahusu wanawake zaidi, lakini tumeamua kutoa nafasi kwa wanariadha wanaume pia” hivyo ikasemekana waende viongozi wanawake ndiyo wanapaswa kuambatana na timu isipokuwa kocha 1 mwanaume.

Sasa mimi nahoji mambo machache;

1)    Katika msafara huo wa Nagai mkuu wa msafara ni Mohamed Kiganja; je yeye ni mwanamke?
2)    Pia kuna Benson Chacha; je yeye pia ni mwanamke?
3)    Kama swala ni la wanawake; BMT hakuna wanawake?
4)    Sina tatizo na Kanali Mstaafu (Juma Ikangaa) maana yeye ni balozi wa JICA lazima aende
5)    Uwepo wa Ombeni Zavala na Rehema Kilo upande wa RT ni sawa sababu wao ni wanawake
Lakini hayo yote tusingehoji kama tusingewekewa vikwazo vyenye dhamira ya kuingilia utendaji wa shughuli zetu za kusaka medali, jitihada za kujitegemea na jitihada za kimkakati kuelekea Tokyo Olympics 2020.

Hili swala la kutojali mipaka ya kiutendaji inahitaji kuangaliwa na Wizara yenye dhamana ya michezo, maana safari hii ni wazi kabisa kwamba watendaji wa BMT wanatumia madaraka yao vibaya. Tunayasema haya yote kwa kujiamini kabisa kwamba BMT wameinyima nchi haki yake ya kimsingi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za jumuia ya madola ambayo Tanzania ni wanachama. Hayati Baba wa Taifa aliona umuhimu wa kujiunga na Jumuia ya Madola, lakini watendaji wa BMT hawalioni.

Watendaji wa BMT wangekuwa makini wasingefanya uharibufu huu;

Agosti 14 hadi 31/2018 msafara ulioongozwa na BMT ulikwenda nchini Burundi, kwa upande wa riadha walikwenda wanariadha ambao wengi wao hawakushiriki, walikula na kulala kwa gharama za serikali, na hata posho walilipwa kila mmoja zaidi ya 700,000. Je kwanini walitumia gharama za serikali kuwagharimia watu ambao hawakushiriki? Unaondokaje kama hujui status ya Local Organizing Committee ya unakokwenda? Ni shilingi ngapi za walipa kodi zimetumika kwa uzembe huo? 

Wanariadha waliokwenda Burundi ni wafuatao;
  1. Michael Gwandu - Long Jump / Triple Jump (Hajashiriki)
  2. Ally Gulam - Mita 100 / 200 (Hajashiriki)
  3. Rose Seif – Mita 200 / 400 (Hajashiriki)
  4. Neema Gadiye - Mita 800 / 1500 (Hajashiriki)
  5. Natalia Sulle - Ameshiriki 21K
  6. Marco Joseph - Ameshiriki 21K
  7. Angelina Yumba - Ameshiriki 21K
Wanariadha watatu walioshiriki hawakwenda Burundi kukimbia Half Marathon, walikwenda kwa ajili ya 10K. Hapo ndipo utaona BMT wamevamia shughuli za RT kwa asilimia 100. Magufuli kasema asiyefanya kazi na asile; sasa kwanini wanariadha ambao hawakufanya kazi wamelipwa na kula bure? Mbaya zaidi wamepoteza muda wao wa kufanya mazoezi sababu wakiwa Burundi hawakua huru kufanya mazoezi kutokana na miundombinu hafifu na usalama wao pia.

Kwa kunyimwa ruhusa tayari RT tumeshawajulisha waandaaji wa Cardiff Commonwealth Half Marathon kwamba tumeshindwa kuja, tumewaomba radhi na kuwatakia mashindano mema kwa nchi zote zitakazoshiriki wakiwemo majirani zetu Kenya, Uganda na Rwanda.

RT tunatambua juhudi za kizalendo za mtanzania mwanariadha ANTHONY MWANGA, anayeishi Afrika Kusini, ambaye aliiwakilisha taifa katika mashindano ya Jumuia ya Madola huko Gold Cost Australia. Mtanzania huyu, alituandalia mazingira mazuri ya timu ya taifa ya riadha ipitie jijini Johanesburg ili kupata visa ya haraka (kama ilivyokuwa kwa mwanariadha Alphonce Simbu) wakati akielekea London Marathon mwaka jana.

Tunawaomba radhi wanariadha wetu ambao kwa mwezi mzima wamefanya mazoezi makali na kwa gharama wakitegemea kwenda kupeperusha bendera ya nchi yao; BMT imezima ndoto yao kwa sasa, waendelee kujiandaa maana kuna mashindano mengi makubwa yanakuja. Nawapongeza sana wanariadha wetu kwa kuahirisha mialiko yao binafsi kusudi waiwakilishe nchi yao ili Tanzania ipate medali na sifa.

Namshukuru Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania pamoja na Makamu Rais wote wawili, Naibu Katibu Mkuu na Kamati nzima ya Utendaji ya RT kwa hatua nzuri walioifikia kimkakati. Changamoto kama hizi za kuingiliwa kiutendaji hazitatukatisha tamaa.

Pamoja na yote yaliyotokea Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) linawatakia wote waliopo kwenye msafara wa Nagai Japan safari njema na yenye mafanikio, wanariadha wanaokwenda Nagai wamepata mafunzo kutoka kwa makocha wanaojitolea bila kudai fidia yoyote, nawapongeza na kuwaambia RT inatambua uzalendo wenu.

Asanteni sana kwa ushirikiano wenu wa mara kwa mara.
  
Imetolewa leo Oktoba 4 / 2018.