Friday, 17 November 2017

TAA kusaka hati miliki za viwanja vya ndege
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama mbele), akiongea na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Transit uliopo kwenye jengo la kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema itahakikisha inapata hati za viwanja vyake vya ndege ili kupunguza uvamizi kutoka kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela  alitoa kauli hiyo leo kwenye mkutano na wafanyakazi uliofanyika katika ukumbi ya Transit uliopo jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI), ikiwa ni moja ya mikakati ya mamlaka hadi kufikia Juni 2018.
Bw. Mayongela alisema tayari wameanza taratibu za kupata hati miliki kwa viwanja 13, vikiwemo vya JNIA na Mwanza zilizofutwa awali.
Hata hivyo, Wananchi wamekuwa na tabia za kuvamia maeneo ya viwanja vya ndege kwa kufanya makazi na mashamba, jambo ambalo ni hatarishi kiusalama.
Bw. Mayongela alisema mkakati mwingine ni kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya viwanja vya ndege 58 vinavyomilikiwa na serikali na ambavyo havipo chini ya serikali.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kutoka Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu (hayupo pichani) aliyekuwa akiongelea mikakati na masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya taasisi hiyo.
“Pia tutaanda kikosi kazi kitachosaidiana na wenzetu wa TANROADS katika usimamizi na uangalizi wa viwanja vya ndege  vinavyoendelea kujengwa maeneo mbalimbali nchini,” alisema Bw. Mayongela.
Katika hatua nyingine Bw. Mayongela alisema pia mamlaka inampango wa kuendeleza miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya abiria, Mizigo, ufungaji wa taa za kuongezea ndege na ufungaji kamera za usalama (CCTV) kwenye viwanja vya Arusha, Mwanza, JNIA na Dodoma.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa uweledi na uwazi, ili kufikia malengo yaliyowekwa na hatakuwa tayari kumfukuza mtumishi kazi kwa masuala yasiyokuwa na msingi.
“Ninafungua milango kwa wafanyakazi mje ofisini kwangu kwani hii ni ofisi ya rasilimali watu na sio rasilimali mtu, naweka milango wazi mje tujadili masuala ya kazi ya kujenga na sio majungu,” alisisitiza Bw. Thobias.

Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias (aliyesimama mbele), akizungumza na Wafanyakazi katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Transit uliopo kwenye jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Tuesday, 14 November 2017

Italia Yashindwa Kufuzu Kombe la Dunia 2018

Wachezaji wa Italia wakifarijiana baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018. Timu hiyo ilitoka suluhu na Sweden katika mchezo uliofanyika San Siro, Italia baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza nchini Sweden, hivyo imetolewa kwa kufungwa 1-0.

ROME, Italia

MABINGWA mara nne wa dunia Italia wameshindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1958 baada ya kushindwa katika mchezo wa mchujo dhidi ya Sweden.

Suluhu dhidi ya Sweden, haikuisaidia Italia kusonga mbele na badala yake wapinzani wao hao ndio wamefuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006 walipofuzu kwa fainali hizo.

Hiyo ina maana kuwa timu ya taifa ya Italia inayojulikana kama Azzurri itakosa mashindano hayo kwa mara ya pili tangu yalipoanzishwa baada ya kushindwa kushiriki wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo mwaka 1930.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Sweden wiki iliyopita, Italia walipokea kichapo cha bao 1-0 kabla ya kutoka suluhu katika mchezo huo wa juzi uliofanyika kwenye Uwanja wa San Siro jijini Milan.

Pamoja na suluhu hiyo, lakini wenyeji ndio walitawala zaidi mchezo huo kwa asilimia 76, licha ya kushindwa kuzifumania nyavu.

PIGO KWA KIPA

Mbali na kutolewa, Italia pia ilipata pigo jingine baada ya kipa wao na baadhi ya wachezaji wengine kuamua kustaafu baada ya timu yao kushindwa kufuzu kwa fainali za mwakani zitakazofanyika Urusi.

Nafasi safi ya Italia kupata bao ilitibuliwa na kipa wa Sweden Robin Olsen alipookoa mpira uliopigwa na mchezaji aliyetokea benchi Stephan El Shaarawy.

Mshambuliaji Ciro Immobile alikosa nafasi kibao na juhudi zake katika kipindi cha kwanza ziliokolewa katika mstari na beki wakati Andreas Granqvist.

Kipa Gianluigi Buffon alisema alikuwa na majonzi makubwa yeye pamoja na wadau wote wa soka wa Italia kwa nchi yao kushindwa kufuzu baada ya kufungwa na Sweden.

Mtu akisoma gazeti la michezo la Italia la "Gazetta dello Sport" huku ukurasa wa mbele ukisomeka "Mwisho" siku moja baada ya Italia kutolewa katika hatua ya kufuzu kwa Kombe la Dunia walipocheza dhidi ya Sweden juzi katika soko la vyakula jijini Rome, Italia.

Buffon, 39, alisema: "Ni aibu kwa mchezo wangu rasmi wa mwisho kwa kuumaliza kwa kushindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia.

"Lawama zinagawanywa kwa kila mmoja. Hakuna mtu wa kutupiwa lawama hapa.”

Mchezaji mwenzake na Buffon wanayecheza pamoja na Juventus Andrea Barzagli na kiungo wa Roma Daniele de Rossi pia alimaliza kipindi chake cha kuichezea Italia, wakati Giorgio Chiellini anatarajia kujiunga nao. Wanne hao wamecheza mechi 461 miongoni mwao.


Kipa Buffon ameichezea timu hiyo mechi 175 katika kipindi cha miaka 20, ambapo alitwaa taji la Dunia 2006 – na anaamini kuwa bado timu hiyo inaweza kufanya vizuri mbeleni.

Maofisa AAKIA Wafurahishwa Ulinzi JNIA

Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu (kulia), akitoa maelezo kwa Maafisa wa Idara mbalimbali kutoka kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA) waliofanya ziara ya mafunzo. Kushoto ni Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama JNIA, Bw. Hamis Mashaka.

Na Mwandishi Wetu

MAOFISA kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), wamefurahishwa na namna ulinzi na usalama wa abiria na mali zao unavyofanywa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), imeelezwa.

Maofisa hao kutoka Idara mbalimbali walitoa kauli hiyo jana katika ziara ya siku moja ya mafunzo JNIA, ambapo walitembelea maeneo mbalimbali na kupata maelezo ya kina kutoka kwa maofisa husika.

                    Maofisa wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), Bw. Shaaban Kombo (kuanzia wa pili kulia), Bi. Zakhia Mohamed, Bw. Salehe Said na Bi. Fatma Yussuf wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu (kulia) akiwaelekeza jambo wakati wa ziara yao ya mafunzo iliyofanyika leo.

Mkuu wa msafara wa maofisa hao, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha AAKIA, Bw. Shaaban Kombo alisema pamoja na kupata mambo mengi ya msingi ya uendeshaji wa viwanja vya ndege, pia wamejifunza namna abiria na mizigo anavyokaguliwa kwa kutumia mitambo ya kisasa kabla ya kupanda ndege.

Bw. Kombo alisema JNIA imekuwa darasa tosha, ambapo pia katika upande wa utoaji wa vitambulisho wamejifunza namna utoaji wa vitambulisho unavyofanyika, ambapo AAKIA hutoa vitambulisho vya kudumu mara utaratibu wa muombaji utakapokamilika, tofauti na JNIA muombaji anaweza kupewa kitambulisho cha muda na kuendelea kufanyakazi huku cha kudumu kikiwa katika matengenezo.

Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Hamis Mashaka (kushoto), akitoa maelezo mbalimbali yanayohusiana na ulinzi na usalama kwa maofisa kutoka idara mbalimbali za Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) cha Zanzibar walipofanya ziara ya mafunzo leo.

“Tumefaidika na mambo mengi ukiangalia sisi kwetu hii ya vitambulisho ni tofauti kabisa, ila kwetu kwa kipindi chote mteja anasubiri kitambulisho cha kudumu anakuwa hawezi kuendelea na kazi zake eneo la kiwanja hadi atakapopata cha kudumu, lakini hapa anakuwa na cha muda kinachomfanya aendelee na shughuli zake huku cha kudumu kikiwa katika matengenezo,” alisema Bw. Kombo.

Naye Mkuu wa kitengpo cha Ulinzi na Usalama cha JNIA, Bw. Lugano Mwansasu alisema ziara ya maofisa wa AAKIA imewafariji na kuanza ukurasa wa mahusiano katika ushirikiano, ambapo nao wamejifunza kulingana na maelezo ya uendeshaji wa AAKIA.

 Meneja Uendeshaji  cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Vedastus Fabian (kulia) akiwapa maelezo mbalimbali Maofisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) walipofanya ziara ya mafunzo leo.

Bw. Lugano alitoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuiga mfano huo wa kupeleka maofisa wake kwenye viwanja mbalimbali vya nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza utendaji kwa lengo la kuboresha huduma za viwanja kwa ujumla. TAA inasimamia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali.

“Kila siku mambo ya uendeshaji yanabadilika, basi tunaiomba mamlaka yetu itusaidie na sisi kwenda kutembelea viwanja vya wenzetu tujifunze huko, zipo changamoto labda sisi hatujui zinatatuliwaje lakini kwa ziara za mafunzo tunaweza kupata mbinu kutoka kwa wenzetu,” alisema Bw. Lugano.

Ofisa Habari katika jengo la Watu Mashuhuri la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (VIP-JNIA), Bw. Kenny Kwenga (kushoto) akitoa maelezo ya namna watu mashuhuri wanavyohudumiwa na maofisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA), walipofanya ziara jana. Kulia ni Msimamizi wa VIP, Bi. Josephine Mwaisukule.

Katika hatua nyingine, Meneja Uendeshaji wa JNIA, Bw. Vedastus Fabian alisema faida ya ziara ya mafunzo ni kujijengea uwezo na mahusiano mazuri baina ya kiwanja kimoja na kingine.

Bw.Fabian alisema ziara hizo zinasaidia katika kutatua matatizo yanayovikumba viwanja vya ndege, ambapo kwa sasa kumekuwa na masuala ya ugaidi, uvushaji wa dawa za kulevia na nyara za serikali.

Saturday, 11 November 2017

Nyota Kibao Kushiriki Tamasha la Karatu 2017

Na Mwandishi Wetu

NYOTA kibao wa riadha wanatarajia kushiriki mbio za kilometa 10 na zile za kilometa tano za wanawake na wanaume zitakazofanyika Desemba 23 mjini Karatu.

Mbio hizo pamoja na michezo mingine kama ya baiskeli, mpira wa wavu, soka, ngoma na kwaya zitakuwa ni hitimisho la Tamasha la Michezo la Karatu 2017.

Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo Meta Petro, mbio za mwaka huu zinatarajia kushirikisha wanariadha kibao nyota kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Alisema baadhi ya wanariadha hao watatoka katika taasisi za kijeshi, huku wengine wakitoka katika klabu za uraiani na sehemu mbalimbali katika mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Filbert Bayi

Tamasha hilo ambalo linaendeshwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) lilianza zaidi ya miaka 10 iliyopita na linafanyika Desemba ya kila mwaka.

Kwa mujibu wa Petro, tamasha hilo hasa mchezo wa mbio limekuwa na lengo la kuibua na kuuendeleza vipaji vya chipukizi ili kuwapata nyota wapya watakaochukua nafasi ya Bayi aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa mbio za meta 1500.

Mbali na meta 1500, Bayi pia aliwahi kutamba na kushikilia rekodi ya dunia ya mbio za maili moja na kutwaa medali ya fedha katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Moscow, Urusi mwaka 1980.

Bayi ni mwenyeji wa Karatu mkoani Arusha na aliamua kuanzisha mbio hizo ili kupata vipaji vipya vitakavyomrithi yeye katika mchezo huo.


Meta Petro

Mbali na mbio za kilometa 10 na zile za tano, pia kutakuwa na mbio za watoto ambazo zitakuwa za kilometa 2.5.