Saturday, 21 March 2015

Mfupa uliomshinda Simba Yanga kautafuna


Mmoja wa wafungaji wa mabao ya Yanga ilipocheza na Mgambo Jumamosi Amis Tambwe.

Na Mwandishi Wetu, Tanga
YANGA ya Dar es Salaam imeendelea kuiwashia indiketa Azam FC katika mbio za Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa wababe wa Simba Mgambo Shooting kwa bao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani.

Yanga ilipata bao lake la kwa kwanza katika dakika ya 78 kupitia kwa Simon Msuva na kuifanya timu hiyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Mrundi Amis Tambwe ambaye alitemwa na Simba kwa `fitiuna’ aliihakikishia Yanga ushindi baada ya kufunga bao katika dakika ya 87 na kuiwezesha timu hiyo kuondoka mjini Tanga na pointi zote tatu.

Kwa ushindi huo, Yanga sasa wamefikisha pointi 37 baada ya kucheza mechi 18 wakifuatiwa na mabingwa watetezi Azam FC ambao wako nyuma kwa pointi nne na hivyo kuzidi kujikita kleleni.

Tambwe alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na mchezaji mmoja wa Yanga.
Hatahivyo, ushindi huo wa Yanga haukuja kirahisi kwani Mgambo Shooting nao walifanya mashambulizi kadhaa lakini bahati haikuwa yao.

Mechi za ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 14 itaendelea Jumapili kwa Simba ya jijini Dar es Salaam kucheza na Ruvu Shooting wakati Coastal Union itawaalika Azam FC huku Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji wa Polisi Morogoro ambayo hivi karibuni ilimtimua kocha wake Rishard Adolf.

No comments:

Post a Comment