Tuesday, 31 January 2017

Yanga yachomoa kucheza na mabingwa wa Afrika Mamelodi Sundowns nfasi yake yachukuliwa na Azam FCNa Mwandishi Wetu
YANGA  imekataa kucheza mchezo wa kujipima nguvu na mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini Ijumaa, imeelezwa.

Habari kutoka Yanga, zimesema kuwa kocha wa timu hiyo Mzambia George Lwandamina ndiye aliyegomea mchezo huo akidai kuwa utaingilia program yake ya mazoezi.

Taarifa zaidi zinadai kuwa, Lwandamina amekataa mchezo dhidi ya Mamelodi uliokuwa ufanyike Ijumaa kwa madai kuwa unaingilia mipango yake.

 “Hatutacheza na Mamelodi kwa sababu kocha ameukataa huo mchezo, amesema unaingilia programu zake, kama unavyojua kwa sasa tupo kwenye hatua ngumu ya Ligi Kuu na wakati huo huo tunaingia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika,”kilisema chanzo chetu.

Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Mwadui FC, Yanga SC itamenyana na timu nyingine ya Shinyanga ya Stand United Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa upande wake, waandaaji wa mechi hiyo pamoja na kusikitishwa na kitendo cha Yanga kugomea mchezo huo, lakini tayari wameiteua Azam FC kuchukua nafasi hiyo.

Sasa Memelodi baada ya kucheza na Simba kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,  watahamia Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Ijumaa kucheza na Azam.

Timu hiyo inakuja nchini kwa mwaliko wa klabu ya African Lyon ya Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa African Lyon, Rahim Kangenzi ‘Zamuda’ alisema Mamelodi wanakuja nchini kushiriki kampeni ya kupiga vita ujangili, iitwayo Linda Tembo Wetu. 

Na Zamunda amesema timu hiyo  ya mjini Pretoria itakuwa nchini kwa wiki yote ya kwanza Februari kushiriki kampeni hiyo pamoja na kucheza mechi hizo.

Kuhusu kujiondoa kwa Yanga, Zamunda alisema kwamba hawana cha kufanya zaidi ya kukubaliana nao, lakini amesikitishwa na hilo.

Mkwasa atangazwa rasmi leo kuwa Katibu Mkuu mpya wa Yanga AfricansNa Mwandishi Wetu
MCHEZAJI na kocha wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Charles Boniface Mkwasa (Pichani) leo ametambulishwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya Baraka Deusdedit anayerejea kwenye Idara yake ya Fedha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika Makao Makuu ya klabu hiyo, Jangwani, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba Mkwasa anaanza majukumu yake rasmi Februari 1, mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga akizungumza leo na waandishi wa habari.
Sanga alisema kuwa sababu kubwa ya kumchagua Mkwasa ni kuhimarisha safu ya uongozi wa klabu hiyo  ambapo aliyekuwa kaimu katibu mkuu, Baraka Deusdedit anarejea katika nafasi yake ya zamani ya Ukurugenzi wa Fedha.“Najua wadau wa soka wanajiuliza kwa nini Mkwasa ameshika nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu kwa sabab ya taaluma yake inayojulikana ni ufundisha mpira wa miguu, siyo kweli, Mkwasa anauzoefu mkubwa katika kazi hiyo tofauti na watu wanavyomuelewa,”

“Na hii si mara ya kwanza, hata Zambia, Kalusha Bwalya amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka nchini humu huku wakijua kuwa ni mchezaji mstaafu au kocha, Yanga tumemuona Mkwasa ni bora katika nafasi hiyo,” alisema Sanga.
 
Mkwasa alishukuru kushika nafasi hiyo na kuahidi kuifikisha Yanga katika malengo yaliyowekwa. “Naomba nieleweke wazi kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Yanga na wala siyo kocha, najua kuna watu watafikiria kuwa narejea kwa mlango wa nyuma, kamwe sitaingilia masuala yoyote ya ufundi zaidi ya kufanya yale yaliyomo katika majukumu yangu,” alisema Mkwasa.

“Ninaomba ushirikiano kutoka kwa wanachama, mashabiki, viongozi wenzangu, sisi sote tupo hapa Yanga kwa ajili ya kuiletea maendeleo na si vinginevyo,” alisema.

Mkwasa anarejea Yanga ndani ya mwezi mmoja tangu aondolewe timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na nafasi yake kupewa Salum Mayanga.

Mkwasa aliifundisha Taifa Stars tangu Julai mwaka 2015 baada ya kurithi nafasi ya Mholanzi, Mart Nooij na katika kipindi chake aliiongoza timu hiyo katika mechi 13 za kimatafa, ikishinda mbili, kufungwa sita na sare tano.

Monday, 30 January 2017

TFF na TOC yazindua programu za maendeleo kwa timu za vijana chini ya miaka 20


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na kamati ya Olympic Tanzania TOC, wamezindua kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Tokyo, nchini Japan mnamo mwaka 2020.

Uzinduzi huo uliofanyika kwenye uwanja wa karume jijini Dar es salaam umehudhuriwa na Mkurugenzi wa Michezo Nchini, Yusuph Omari ambaye alikua mgeni rasmi, Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF Jamal Malinzi, Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Henry Tandau, maafisa wa TFF na wadau wengine wa michezo.

 kampeni hiyo inayoihusisha timu ya taifa ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Kilimanjaro Worriers) ambayo itawania kufuzu kucheza michuano ya Olimpiki mwaka 2020, imepewa jina la ‘The Road to Tokyo 2020’.

Rais wa TFF Jamal Malinzi, amesema dhamira kubwa waliyojiweka katika harakati hizo ni kuhakikisha vijana wanaendelezwa kisoka kwa ajili ya kufikia malengo ya kwenda kushiriki michuano ya Olimpiki mwaka 2020.

Rais wa TFF  Jamal Malinzi

Mkurugenzi wa michezo Yusuph Omari “Nimesikia program mbalimbali za TFF, naona zinakuja wakati mwafaka. Niwapongeze kwa mipango yenu mizuri kwa sababu inaleta matumaini. Jambo kubwa ambalo linanisukuma na kuwapongeza ni kuwa na program ya vijana, hatuwezi kufanikiwa kama hatutakuwa na program ya vijana.

“Serikali inatambua haya yote mnayofanya ili kuboresha, Serikali imetenga shule 55 ambazo zitakuwa ni maalumu kwa ajili ya vijana, lengo ni kupata vipaji bora ambavyo vitakuwa vikiendelezwa, huku wakiwa wanapata elimu.

Mkurugenzi wa michezo Yusuph Omari


Saturday, 28 January 2017

Kocha Micho ataka kuiburuza mahakamani Fufa kwa kutomlipa mishahara yakeKAMPALA, Uganda
KOCHA wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, Milutin 'Micho' Sredojevic (pichani), amelitaka  Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa) kutimiza masharti ya mkataba la sivyo atawachukulia hatua za kisheria.

Mserbia huyo, ambaye aliipeleka Uganda Gabon katika mashindano ya Kombela Mataifa ya Afrika (Afcon 2017), kwa mara ya kwanza baada ya kushindwa kufuzu kwa takribani miaka 39, amesema anadai malimbikizo ya mishahara yake.

Micho alisema kuwa wanaweza kulimaliza suala hilo vizuri, lakini kama wakishindwa basi atakimbilia katika vyombo vya kisheria.

Chini ya Micho the Cranes ilitolewa katika hatua ya makundi ya Afcon 2017 nchini Gabon baada ya kufungwa kiduchu na vigogo wa Afrika Ghana na Misri kabla ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mali.

Kiwango cha timu hiyo ya Uganda kilikuwa kizuri sana na kinaonesha dalili kuwa, timu hiyo imeimarika zaidi, hasa ukilinganisha na timu hiyo iliposhiriki mashindano hayo kwa mara ya mwisho mwaka 1978.

Kocha huyo amekuwa akihusishwa na nchi kibao zikiwemo Ghana – baada ya kocha wa the Back Stars, Avram Grant akijiandaa kuondoka baada ya mashindano hayo ya Mataifa ya Afrika.

"Nina mkataba hadi wakati wa mashindano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2019 lakini wakati wote mabeki ya makocha huwa nusu yameshapangwa vitu tayari kubaki na tayari kuondoka,”alisema Micho.

"Uganda inatakiwa kuamua. Kwa kweli niko wazi kwa kila kitu kwa sababu zimekuja ofa nyingi.

Kalusha Bwalya amtabiria ubingwa mwingine wa Afrika kocha Renard wa MoroccoLUSAKA, Zambia
GWIJI wa soka nchini Zambia, Kalusha Bwalya anasema kuwa Herve Renard ana uwezo wa kutwaa tena taji la Mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya kuyaangalia mwenendo mzima wa mashindano hayo hadi sasa.

Endapo kocha Renard atatwaa taji la Afcon itakuwa ni mara yake ya tatu akilibeba huku akiwa na timu tatu tofauti baada ya mwaka 2015 kulitwaa akiwa na Ivory Coast baadaya kulitwaa mwaka 2012 akiwa na timu ya taifaya Zambia ya Chipolopolo.

Nahodha huyo wazamani wa Zambia na Rais wazamani wa Chama cha Soka cha Zambia pia aliiambia BBC kuwa, anafikiri mashindano yanayoendelea Gabon yana timu zenye uwezo, ambazo zinakaribiana kwa uwezo, wakati akiangalia mechi za robo fainali zitakazoanza leo Jumamosi.

Timu ya Morocco inayofundishwa na Renard itakwaana na mabingwa mara saba wa Afrika Misri katika mchezo utakaofanyika kesho Jumapili.

Timu zingine zitakazocheza robo fainali ni:- Burkina Faso v Tunisia na Senegal v Cameroon,ambazo mechi zao zote zitapigwa leo Jumamosi, wakati DR Congo v Ghana zitachezwa kesho Jumapili.