Tuesday 31 March 2015

Muhammad Ali amtabiria ushindi Pacquiao



NEW YORK, Marekani
BONDIA nyota wazamani Muhammad Ali anataka Manny Pacquiao kuibuka na ushindi dhidi ya Floyd Mayweather, kwa mujibu wa binti wa bondia huyo gwiji.

Rasheda Ali alibainisha kuwa baba yake anaheshimu sana uwezo wa Pacquiao lakini pia anakubali jinsi anavyojimudu ulingoni.

'Baba yangu ana mkubali sana Pacquiao,' alisema. 'Baba yangu yuko upande wa Manny, na ni shabiki mkubwa wa bondia huyo.

'Anajua Manny ni bondia mkubwa lakini anamkubali zaidi pia kwa kile anachofanya nje ya ulingoni. Ni sawa na mtu wa kujitolea sana.'

Rasheda aliongeza kuwa baba yake anakubali uwezo binafsi wa Mayweather lakini alikiri ni watu wawili tofauti kabisa.

Mabondia hao watapigana Mei 2 katika pambano la aina yake na linalosubiriwa kwa hamu kubwa litakalofanyika Las Vegas.
'Hakuna ubishi atashinda pambano hilo, ' Rasheda alisema 'Itamkumbusha baba yake wakati alipkuwa akipigana. '

Wakati pambano hilo likiwa limebakiza kama mwezi mmoja kabla ya kufanyika, Pacquiao ameendelea kuwapa taarifa mashabiki zake kabla ya pambano lake hilo dhidi ya Mayweather.

Alituma picha za mazoezi yake katika Instagram na zile za mahojiano ili kuwafanya mashabiki kuwa na taarifa za mara kwa mara.

Real Madrid yasajili beki kisiki wa Porto



MADRID, Hispani
KLABU ya Real Madrid imethibitisha kumsajili beki wa kulia wa timu ya Porto ya Ureno Danilo (pichani) kwa ada ya uhamisho ya pauni Milioni 22.8, `aliyejifunga kuichezea timu hiyo hadi mwaka 2021.

Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 23, alikuwa akihusishwa na mabingwa hao wa Ulaya kwa miezi kadhaa huku Danilo wiki moja iliyopita alisikika akisema kuwa, anajivunia kuhusishwa na vijana hao wa kocha Carlo Ancelotti.

Na, Jumatano usiku, klabu hizo mbili zilitangaza kuwa beki huyo ataondoka Dragao katika kipindi cha majira ya joto na kusaini mkataba wa miaka sita huko Santiago Bernabeu.

"Porto walisema kuwa wamefikia makubaliano na Real Madrid kwa uhamisho wa kudumu wa Danilo kwa uhamisho wenye thamani ya euro Milioni 31.5," ilisema klabu hiyo ya Ureno.

Real Madrid ilithibitisha katika taarifa yake kuwa Danilo atajiunga na vigogo vya soka vya Hispania.

Wapinzani wachukua nchi Nigeria baada ya kumuangusha Jonathan


Rais Goodluck Jonathan (kushoto) na Muhammadu Buhari wiki iliyopita walikubaliana kukubali matokeo ya uchaguzi.

ABUJA, Nigeria
MTAWALA wazamani wa kijeshi Muhammadu Buhari amekuwa mgombea wa kwanza wa upinzani kushinda uchaguzi mkuu nchini Nigeria.

Chama cha Jenerali Buhari kilisema kuwa, mpinzani wake ambaye alikuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, alikubali matokeo hayo na kumpongeza mwanajeshi huyo mstaafu.

Wakati akikubali kushindwa, Jonathan alikuwa amepitwa na Buhari karibu kura milioni mbili.

Waangalizi wa uchaguzi huo waliupongeza lakini kulikuwa na tetesi za vurugu, zilizosababisha wasiwasi kuwa zingesababisha maandamano na vurugu.

"Rais Jonathan alimpigia simu Jenerali Muhammadu Buhari, mshindi wa uchaguzi, kumpngeza, alisema Lai Mohammed, ambaye ni msemaji wa Chama cha Jenerali cha All Progressives Congress (APC).

Msemaji alimpongeza Bwana Jonathan, akisema: "Atabaki kuwa shujaa wan chi hii kwa kitendo chake cha kukubali matokeo."

"Yeyote atakayejaribu kuleta vurugu kwa madai ya kushindwa katika uchaguzi atakuwa akifanya hilo kwa faida yake, " aliongeza.

Hiki ni kipindi muhimu kwa historia ya Nigeria. Haijawahi kutokea rais aliye madarakani kushindwa katika uchaguzi.

Monday 30 March 2015

Venus mbioni kukutana na dada yake Miami Open



MIAMI, Marekani
VENUS Williams (pichani)bado yuko katika mwelekeo wa kukutana na dada yake Serena katika fainali ya mashindano ya Miami Open baada ya kumtoa bingwa namba tano wa dunia Caroline Wozniacki katika hatua ya 16 bora.

Mmarekani huyo alimshindi mpinzani wake wa Denmark kwa 6-3 7-6 (7-1) ndani ya dakika 98.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye kwa miezi saba alikuwa nje ya mchezo huo kutokana na maumivu mwaka 2011, sasa ameshinda mechi saba kati ya nane zilizopita dhidi ya wachezaji 10 bora.

Dada yake Serena alimchakaza Svetlana Kuznetsova 6-2 6-3 na kutinga robo fainali.

Mdada huyo mwenye umri wa miaka 33 atakutana na Sabine Lisicki katika robo fainali baada ya Mjerumani kumfunga Sara Errani 6-1 6-2.

Wakati huohuo, Venus, atakutana na Mhispania Carla Suarez Navarro, ambaye anarudi mchezoni baada ya kufungwa katika seti ya kwanza dhidi ya nMpoland anayeshika nafasi ya saba Agnieszka Radwanska 5-7 6-0 6-4.

Novak Djokovic, ambaye ndiye bingwa mtetezi kwa upande wa wanaume, alimsambaratisha Mbelgiji Steve Darcis 6-0 7-5.

Wanariadha wa mbio za nyika wawasili bila mwenzao

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania Suleiman Nyambui (kulia) akiteta na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT Peter Mwita walipokwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere jijini Dar es Salaam Jumatatu.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa ya riadha ta Tanzania iliyoshiriki mbio za dunia za nyika zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Guiyang nchini China, imewasili salama jijini Dar es Salaam.

Tanzania ilishika nafasi ya sita katika mbio hizo kubwa duniani na hayo yakiwa ni matokeo mazuri zaidi kuwahi kupata kwa timu ya Tanzania.

Mwanariadha Ismail Juma ndiye aliyeitoa nchi kimasomaso baada ya kumaliza katika nafasi ya tifa huku wenzake wengine wanne wakishindwa kuwemo katika 20 bora.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanariadha hao walisema mbio zilikuwa ngumu lakini walijitahidi na wanafurahia matokeo hayo.

Juma aliyeondoka na kitita cha dola za Marekani 3,000 baada ya kushika nafasi ya sita, alisema mbio zilikuwa ngumu lakini alijitahidi na kumaliza katika nafasi hiyo.

Naye kocha wa timu hiyo Francis John alisema kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa JK. Nyerere kuwa, vijana wake walijitahidi sana na kusisitiza kuwa siri ya mafanikio ni kambi waliyopiga huko Mbulu.

Alisema kuwa timu hiyo ilipiga kambi kwa wiki mbili tu huko Mbulu na kama wangekaa zaidi bila shaka matokeo yangekuwa mazuri zaidi na aliwataka Riadha Tanzania (RT) kuanza kambi mapema kwa ajili ya kushiriki mashindano mbalimbali.
Wanariadha wengine wa Tanzania walioshiriki mbio hizo mbali na Ismail Juma aliyemaliza wa sita ni pamoja na
Alphonce Felix, Bazil John, Joseph Teophil na Fabian Nelson, ambao walishiriki mbio za kilometa 12.
Hatahivyo, wakati wanariadha waliwasili Jumatatu jioni kwa ndege ya Emirates, Nelson hakuwemo na alitarajia angewasili mapema na ndege ya Qatar lakini ndege hiyo ilitua yeye hakuwemo na hakukuwa na taarifa zozote za kutowasili kwake.


Katibu Mkuu wa RT Suleiman Nyambui (katikati) akizungumza na mwandishi wa habari wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK. Nyerere wakati wakisubiri kurejea kwa timu ya Tanzania iliyoshiriki mbio za dunia za nyika nchini China Jumatatu. Kulia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji na katibu wa Kamati ya Ufundi ya RT Rehema Killo.

Mwanariadha Bazil John akiwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa JK. Nyerere wakati timu ya taifa ya Tanzania ilipowasili ikitokea China ambako ilishiriki mbio za dunia za nyika.

Mwanariadha Alphonce Felix (kushoto) akipokewa na Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (Suleiman Nyambui timu ya nyika ya dunia ya Tanzania ilipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK. Nyerere jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa RT Suleiman Nyambui (katikati) akiwa na wachezaji wa Tanzania walioshiriki mbio za dunia za nyika timu hiyo ilipowasili Jumatatu. Kushoto ni kocha wa timu hiyo Francis John.
Timu ya taifa ya riadha iliyoshiriki mbio za nyika za dunia ikiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa JK. Nyerere jijini Dar es Salaam

Katibu msaidizi wa Riadha Tanzania Ombeni Zavalla (kulia) akisalimiana na kocha wa timu ya taifa iliyoshiriki mbio za nyika za dunia Francis John timu hiyo ilipowasili jijini Dar es Salaam ikitokea China. Kushoto ni Katibu Mkuu wa RT Suleiman Nyambui na wa pili kulia mjumbe wa kamati ya utendaji ya RT Rehema Killo.