Wednesday, 8 February 2017

AVRAM Grant abwaga manyanga kuifundisha timu ya taifa ya ghana `Black Stars'ACCRA, Ghana
AVRAM Grant hatimaye amemaliza kibarua chakuwa kocha wa timu ya taifa ya Ghana, The Black Stars, baada ya kuifundisha timu hiyo kwa zaidi ya miaka miwili.

Mkataba wa kocha huyo Muisrael umebakisha muda mfupi kumalizika ambako katika mashindano ya Mataifa ya Afrika, Ghana ilimaliza katika nafasi ya nne, ambapo alisema hana mpango wa kuongeza mkataba.

Grant alisema alikutana na rais wa Chama cha Soka cha Ghana, Kwesi Nyantakyi na kumwambia nia yake ya kutoongeza mkataba “muda ni muafaka kwangu kuondoka na kwenda kupata changamoto zingine”.

Kocha huyo aliiongoza Ghana kucheza fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2015 na nusu fainali katika mashindano ya mwaka huu.

Wakati akishindwa kuhitimisha ukame wa zaidi ya miaka 30 wa Ghana ikisubiri kutwaa taji la tano, ilifungwa kwa penalti katika fainali na Ivory Coast miaka miwili iliyopita.

Ghana imeendelea kusotea taji hilo baada ya mwaka huu nao kushindwa kulitwaa baada ya kufungwa Cameroon katika nusu fainali.

Wakati akianza kibarua cha kuifundisha timu hiyo Novemba mwaka 2014, Ghana ilikuwa bado ikiweweseksa baada ya kufanya vibaya katika Kombe la Dunia Brazil, ambako walishindwa kupata ushindi hata katika mchezo mmoja.

"Kwa kweli nilikuwa na wakati mzuri sana Ghana nilipoichukua timu hiyo baada ya kufanya vibaya katika Kombela dunia 2014 na kukijenga upya kikosi na kukiwezesha kufikia fainali ya Mataifa ya Afrika ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha miaka 23, na nusu fainali katika mashindano ya mwaka huu, “alisema.

"Na uvumivu na heshima ya mashabiki ni vitu ambavyo sitavisahau maisha mwangu.”

No comments:

Post a Comment