![]() |
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetangaza kusimamisha kwa mwezi mmoja michezo yote
inayokusanya watu wengi, ikiwa ni tahadhari ya kujikinga na virusi vya
ugonjwa wa corona, ambao tayari umeshaingia nchini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (pichani) alitangaza hayo wakati
akilihutubia taifa kwa njia ya radio na televisheni, kuhusu hatua
zinazochukuliwa na serikali dhidi ya janga hilo la corona.
Kwa tamko hilo, kuanzia mechi za mchangani hadi zile za Ligi Kuu
Tanzaia Bara na ile ya Zanzibar, zitakuwa zimesimamishwa kwa mwezi mmoja, kwani
ligi hizo zinahusisha mkusanyiko wa watu wengi.
“Tunatangaza kusimamishia
rasmi michezo yote inayokusanya idadi kubwa ya watu, makundi ya watu kama Ligi
Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Daraja la pili na Umishumta, Umisseta na mashindano
ya mashirika ya umma na michezo mingine kwa kipindi cha mwezi mmoja,” alisema
Majaliwa.
Alisema baada ya tamko hilo wizara yenye dhamana na michezo ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo watasambaza barua kwa mashirikisho yote
nchini wakitakiwa kufanya hivyo.
Kabla ya kutolewa tamko hilo la jana, tayari Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
kupitia waziri wake, Selemani Jafo ilifuta
Mashindano ya Shule za Msingi na Sekondari kuanzia hatua ya mashule, ambayo
yalitarajia kuanza hivi karibuni.
Nchi kadha zikiwemo zile zenye ligi tano kubwa kama England,
Hispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa zimesimamisha ligi zao hadi mwanzoni
mwa mwezi ujao ili kuamgalia mwenendo wa jango hilo la corona, ambalo tayari limewakumba
baadhi ya wachezaji wa ligi hizo.
Mbali na kusimamishwa kwa ligi kubwa Ulaya, Shirikisho la Soka
la Ulaya (Uefa) limesogeza mbele fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2020 hadi
mwakani kuanzia Juni 11 hadi Julai 11, 2021.
Pia Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Ijumaa lilitangaza kusimamisha
mechi zote za kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2021) na jana
ilitangaza kusimamisha fainali za Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji
wa ndani (Chan 2020), ambazo zingefanyika Cameroon mwezi ujao.
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana
lilitangaza kikao cha dharura ambacho kitafanyika leo jijini Dar es Salaam
kuzungumza hatma ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuhusu janga la corona.
Kikao hicho pia kitajadili kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars
inayoendelea kujiandaa na fainali za Kombe la Chan nchini Cameroon pamoja na
mechi za majaribio za timu hiyo.
Rais wa TFF, Wallace Karia aliagiza Kamati ya Uongozi ya Bodi ya
Ligi Kuu Tanzania Bara kuitisha kikao cha dharula leo kujadili mustakabali wa
michuano hiyo wakati huu wa mlipuko wa virusi vya corona.
Karia alisema kikao hicho kitakachoanza saa 3:00 asubuhi
kitafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Golden Tulip, Dar es Salaam.
“Ajenda kubwa katika kikao hicho ni kuangalia mustakabali wa
ligi kutokana na mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona ambao umeingia
nchini,”alisema Karia.
No comments:
Post a Comment