Tuesday 31 October 2017

BMT yaendesha mafunzo kwa walimu wa michezo

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja.

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) linaendesha mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari ili kuendeleza michezo nchini.

Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja alisema jana kwa njia ya simu kuwa, kwa sasa mafunzo hayo yako katika tarafa ya Ntebele wilani Kyela mkoani Mbeya.

Alisema kozi hiyo inatarajia kumalizika Jumamosi, ambapo walimu 49 kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari wanahudhuria mafunzo hayo.

Kiganja alisema kuwa mafunzo yanayotolewa ni pamoja na yale ya ufundishaji soka, mpira wa wavu, netiboli, riadha, mazoezi ya viungo na utawala katika michezo.

Alisema kuwa mbali nay eye (Kiganja) wakufunzi wengine wa mafunzo hayo ya wiki mbili ni pamoja na Danny Korosso, Richard Mganga na Damian Chonya, ambaye anafundisha netiboli.

Alisema baada ya hapo mafunzo hayo yataendelea ama Songwe, Rukwa au Mtwara kutegemea na utayari wa mahali husika kwa ajili ya mafunzo hayo.

Juganja alisema kuwa wameamua kutoa mafunzo tarafani ili kuwapunguzia washiriki gharama za nauli na malazi.

“Tumeamua kuwafuata na kuendesha ya mafunzo ya michezo huko huko ili kuwapunguzia gharama ya nauli na malazi, “alisema Kiganja.


Alisema tayari mafunzo hayo yalishafanyika jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya walimu 80 walihitimu katika mafunzo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

No comments:

Post a Comment