Sunday, 6 September 2015

RISALA YA MKURUGENZI MKUU, MAHAFALI YA DARASA LA SABA NA KIDATO CHA NNE sept. 2015
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Ndugu Semu Mwakanjala, Kaimu Meneja Mawasiliano kwa Umma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Meja Mstaafu Ndugu Filbert Bayi,
Viongozi wa Elimu Mkoa wa Pwani,
Wajumbe wa Bodi za Shule,
Wazazi, Wafanyakazi, Wanafunzi,
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Tunamshukuru Mungu kwa upendo na rehema tele kutuwezesha kukutana tena mwaka huu 2015, kwenye mahafali ya watoto wetu wa darasa la saba na kidato cha nne.

Ninawashukuru kipekee wazazi, na wageni wote mliokubali mwaliko wetu na kuhudhuria sherehe ya leo ya:-
-          Mahafali ya 5 ya shule ya msingi Kibaha yenye wahitimu 21
-          Mahafali ya 14 shule ya Msingi Kimara yenye wahitimu 47
-          Mahafali ya 10 shule ya Sekondari yenye wahitimu  83

HISTORIA YA  SHULE YA CHEKECHEA NA MSINGI

Mhe. Mgeni rasmi shule zetu za chekechea na msingi ziko katika makundi mawili kama ifuatavyo:-

i)  Kimara Dar es Salaam
Mwaka 1996 tulianzisha shule ya chekechea na msingi iliyopo Kimara na tulipata usajili mwaka 2000 kwa namba DS/02/7/007.  Mpaka sasa shule ina jumla ya wanafunzi 584 pia tunao waalimu 40 na wafanyakazi wasio waalimu 31.

ii)  Mkuza – Kibaha
Shule hii ilisajiliwa mwaka 2010 kwa namba PW.01/7/008.  Na ina jumla ya wanafunzi 339,  waalimu 17 na wafanyakazi wasio waalimu 10.

HISTORIA YA SHULE YA SEKONDARI
Mhe. Mgeni Rasmi Shule ya Sekondari Filbert Bayi ilianzishwa rasmi mwaka 2003 kule Kimara palipo na shule ya Msingi na hatimaye majengo yalipokamilika Februari, 2004 tulihamia huku Kibaha na tarehe 2 / 3 /2005 kuzinduliwa rasmi na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu Mhe.   Benjamin William Mkapa. Shule imesajiliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia namba ya usajili S.1377 na kituo cha mtihani namba S.1437.

 MAFANIKIO NA MAENDELEO YA SHULE
Mhe. Mgeni Rasmi shule zetu zimepata mafanikio makubwa kitaaluma na michezo tangu zilipoanzishwa  kama ifuatavyo:-

i)  Matokeo ya Mitihani upande wa Msingi
-      Mwaka 2014 shule za msingi Kimara na Kibaha waliomaliza darasa la saba walifaulu kwa asilimia mia moja (100%) na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za serikali, japo wengi wao walirudi Filbert Bayi. 

ii) Matokeo ya Mitihani upande wa Sekondari
Mwaka 2014  wanafunzi 38 walifanya mtihani wa kidato cha nne na matokeo yao ni kama ifuatavyo:-
·        Daraja la 1     -      6  
·        Daraja la 2     -    11 
·        Daraja la 3     -    18 
·        Daraja la 4     -      3  
·        Daraja la 0     -      Hakuna
Tuna matarajio makubwa kwamba mwaka huu hawa wanafunzi wanaohitimu leo watafanya vizuri zaidi na hii ni kutokana na juhudi na mikakati kabambe waliojipangia Waalimu na wanafunzi.
      
ELIMU YA UJASILIAMARI
Pamoja na masomo ya darasani, vijana wetu wameanza kujifunza masomo ya ujasiliamali kama ufugaji wa kuku, upambaji wa kumbi kwa ajili ya sherehe mbalimbali, upishi, ususi, unyoaji, upambaji wa maharusi na utengenezaji nywele.

Taaluma hizi ninaamini zitawasaidia kuwa wajasiliamali wakati wakisubiri matokeo yao wamalizapo shule na vyuo.

Mhe. Mgeni Rasmi ni matumaini yangu kwamba utakuwa umepata kwa kifupi mafanikio na maendeleo ya shule zetu.

HITIMISHO
Mhe.Mgeni Rasmi ili kukamilisha sherehe hii siku ya leo tutakuomba ukabidhi vyeti na zawadi kwa wahitimu wote na zawadi maalumu kwa waliofanya vizuri ikiwa ni pamoja na Kitaaluma, Uongozi bora, Nidhamu na Michezo.


ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
                                                                                                                          

No comments:

Post a Comment