Saturday 28 February 2015

Russia waandamana kupinga mauaji ya mpinzani



*Alikuwa akiandaa maandamano makubwa kumpinga Rais Putin


MOSCOW, Russia
MAELFU ya watu wanatarajia kushiriki katika maandamano makubwa katika mitaa ya jiji hili kuonesha heshima kwa mwanasiasa wa upinzani Boris Nemtsov, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Ijumaa.
Mwanasiasa huo Jumapili alitarajia kuongoza maandamano makubwa, lakini wafuasi wake sasa watatumia maandamano hayo  kwa ajili ya kuomboleza kifo chake.
Rais wa Russia Vladimir Putin amelaani mauaji ya Bwana Nemtsov na kuahidi kuwa, Serikali yake itahakikisha wauaji wanapatikana.
Mauaji ya Bwana Nemtsov yanahusishwa na masuala ya kisiasa hasa kutokana na kumpinga Bwana Putin na ugomvi na Ukraine.
Wafuasi wa upinzani wanatarajia kuandamana Jumapili mchana katikati ya jiji la Moscow kabla ya kuelekea huko Great Moskvoretsky Bridge,ambako Bwana Nemtsov aliuawa.

Mamlaka ya jiji la Moscow awali waliidhinisha kuwa hadi watu 50,000 watashiriki katika maandamano hayo lakini waandaaji walisema kuwa watu zaidi wanawea kushiriki kushiriki kutokana na mauaji hayo.
Sarah Rainsford anasema kuwa mauaji hayo yameushtua upinzani wa Russia.
Katika eneo alilopigiwa risasi mpinzani huyo kumuwekwa lundo la mashada ya maua.
Watu wengi wanasema kuwa mauaji ya Boris Nemtsov yamefanyika kwa sababu za mtazamo wake kisiasa na wamemlamu rais Putin kwa tabia yake ya kupinga upinzani.
Nemtsov alizaliwa Oktoba 9 mwaka 1959 ni mwanasayansi na mwanasiasa na alifanikiwa sana kisiasa chini ya rais Boris Yeltsin katika miaka ya 1990, na tangu mwaka 2000 alikuwa akimkosoa Vladimir Putin.
Wakati akiuawa, Nemtsov alikuwa jijini Moscow akisaidia maandalizi ya mkutano wake mkubwa kwa ajili ya kupinga sera za rais Putin za kuiingiza Russia katika vita huko Ukraine na nchi hiyo kuwa katika matatizo ya fedha.

Azam FC yaendelea kuwa nyanya kimataifa



*Yanga waliosonga mbele warejea Jumapili usiku

*KMKM, Polisi Zanzibar nao waendelea kusindikiza


Na Mwandishi Wetu
AZAM FC imeendelea kushindwa kuonesha makali yake katika mashindano ya kimataifa baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika kufuatia kichapo cha bao 3-0 kutoka kwa El Merreikh ya Sudan na hivyo kutolewa kwa jumla a mabao 3-2.
Wawakilishi hao wa Tanzania walienda Sudan wakiwa na faida ya bao 2-0 waliyoyapata katika mchezo wao wa awali uliofanyika kwenye uwanja wao wa Chamazi huko Mbagala wiki mbili zilizopita, hivyo walikuwa wakihitaji sare ya aina yoyote au hata kufungwa 1-0 ili waweze kusonga mbele.
Katika mchezo huo,  El Merreikh pia walikosa penati baada ya mpigaji kupaisha mpira.
Hii ni mara ya pili kwa Azam kuaga michuano katika raundi ya mapema baada ya mwaka jana pia kutolewa na timu ya Ferroviaro de Beira ya Msumbiji katika Kombe la Shirikisho la Afrika.
Azam imetoka ikiwa ni saa chache baada ya KMKM ya Zanzibar nayo kutolewa licha ya kupata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya dhidi ya El Hilal ya Sudan, na kutolewa mashindanoni kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kufungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Sudani wiki mbili zilizopita.
Polisi Zanzibar ambayo inashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho nayo leo ni sawa kama inakamilisha ratiba tu ya kutoka baada ya kufungwa 5-0 katika mchezo wa kwanza na Mounana ya Gabon. Timu hizo leo zinacheza kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Polisi kama inahitaji kusonga mbele katika hatua inayofuata, inatakiwa angalau iibuke na ushindi wa bao 6-0, kitu ambacho hakiwezekani licha ya usemi wa lolote linawezekana katika soka.
Wakati mabingwa wa Tanzania Bara Azam FC wakitolewa, washindi wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita Yanga wanarejea Jumapili usiku baada ya kusonga mbele katika Kombe la shirikisho licha ya kufungwa 2-1 na BDF ya Zimbabwe.
Yanga sasa watacheza na Platnum ya Zimbabwe kati ya Machi 13-15, baada ya Wazimbabwe hao kuwafungisha virago Sofapaka ya Kenya kwa jumla ya bao 4-2.
Timu hiyo ya Zimbabwe katika mchezo wa awali ilishinda 2-1 kabla ya kuibuka na ushindi mwingine kama huo katika mchezo wa marudiano leo Jumamosi.

Buriani Kapteni John Damiani Komba





Kapteni John Damiani Komba
Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Mbinga Magharibi na Mkurugenzi wa kundi la The Tanzania One Theatre (TOT) Kapteni John Komba amefariki funia leo hii.
Habari zilizotufikia na kuthibitishwa na Katibu Mipango wa TOT Plus Gasper Tumaini zinasema kuwa, Komba amefariki leo Jumamosi jijini katika hospitali ya TMJ Mikocheni, ambako alikimbizwa baada ya kuzidiwa na kisukari akiwa nyumbani kwake Mbezi Beachi eneo la Tangi Bovu jijini Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa mbunge huyo alifariki hospitalini hapo wakati akipatiwa matibabu.
Mbunge huyo alizidiwa akiwa nyumbani kwake Mbezi na kukimbizwa hospitalini hapo akisumbuliwa na ugonjwa wa Kisukari.
Tumaini alithibitisha kuwa Komba alifariki dunia hospitalini na alikuwa hana mengi ya kusema kwani wakati huo akizungumza na mwandishi wa habari hizi walikuwa nyumbani kwa Komba wakiendelea na taratibu zingne.
Ni kweli amefariki na sasa tuko kwake tunaendelea na taratibu zingine na taarifa zaidi zitatolewa kesho (Jumapili), alisema Tumaini kwa kifupi.
Bwana Alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe, Amina.

Friday 27 February 2015

Walimu Kinondoni waandaliwa kwa Umisseta



 *Lengo ni kuzalisha walimu wenye ujuzi watakaotoa wachezaji bora

Mratibu wa michezo mkoa wa Kinondoni Mwl. Samuel Robert akizungumza Makongo leo kabla ya ufungaji rasmi wa mafunzo ya walimu wa michezo wa shule za sekondari Kinondoni. 
Na Mwandishi Wetu
KANDA ya Kinondoni imekamilisha mafunzo maalum kwa ajili ya walimu wa shule za sekondari watakaofundisha mikoa yao kwa ajili ya kuiwezesha kanda hiyo kuendelea kutamba katika mashindano ya Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Kinondoni kwa miaka minne mfuulizo imetamba katika Michezo ya Umisseta kwa kutwaa vikombe vingi na kuwa mshindi wa jumla wa mashindano hayo ya kila mwaka.
Mratibu wa michezo Kanda ya Kinondoni mwalimu Samuel Robert amesema leo kuwa, lengo la mafunzo hayo n
i kuzalisha walimu wenye ujuzi ili kutoa wanafunzi wenye uwezo katika michezo mbalimbali na kuiwezesha kanda yao kuendelea kufanya vizuri kitaifa.


Wakufunzi wa mafunzo ya riadha kwa baadhi ya walimu wa Kanda ya Kinondoni Suleiman Nyambui (kushoto aliyekaa) na Mwinga Mwanjala wakiwa katika picha ya pamoja na walimu hao baada ya kumaliza mafunzo hayo leo Makongo jijini Dar es Salaam.
Alisema mafunzo hayo yaliohusisha michezo mbalimbali pia yatasaidia kuongeza ari kwa walimu hao ili wafundishe kwa utaalam zaidi.
Mafunzo hayo ya siku tano yalishirikisha swalimu 30 kutoka shule mbalimbali za sekondari Kanda ya Kinondoni na yalihusu michezo ya mpira wa miguu, kikapu, wavu, netiboli, mpira wa mikono na riadha.
Alisema kuwa kila mchezo ulikuwa na walimu watano na ulifundishwa na wakufunzi walioletwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia vyama au mashirikisho ya kitaifa ya michezo hiyo.
Mafunzo hayo yalitolewa na wataalam wa kitaifa na kimataifa wa michezo hapa nchini kama akina Suleiman Nyambui na Mwinga Mwanjala wa riadha, Manase Zablon wa kikapu na wengine.
Kanda ya Kinondoni kiumisseta wameigawa katika wilaya mbalimbali za Kawe, Ubungo, Wilaya Maalum ya Makongo na Kinondoni yenyewe.
Naye mkufunzi wa riadha Nyambui aliwataka walimu kuzingatia mafunzo hayo ili kuchagua wanafunzi wenye sifa watakaokuwa na uwezo wa kufanya vizuri katika mchezo wa riadha.


Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT) Suleiman Nyambui (mbele) akisisitiza jambo kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya siku tano ya michezo kwa walimu wa sekondari Mkoa wa Kinondoni. Kulia ni mkufunzi mwenzake Mwinga Mwanjala.

Thursday 26 February 2015

Boko Haram waendelea kuua Nigeria




ABUJA, Nigeria
SHAMBULIZI la bomu limeaua watu 32 Kaskazini ya Nigeria, ikiwa ni muendelezo wa matukio ya kundi la Boko Haram.
Imeelezwa kuwa bomu katika kituo cha basi cha Biu limeua kama watu 17, amesema shuhuda mmoja, wakati lile la pili linaelezwa kuwa liliua watu kadhaa.
Huko Jos, mabomu matatu yalitupwa kutoka ndani ya gari na yaliua watu 15 katika kituo cha basi na emeo la Chuo Kikuu.
Uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi huu, uliahirishwa kutokana vurugu hizo za Boko Haram.
Uchaguzi huo sasa unatarajia kufanyika Machi 28 mwaka huu.
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, aliyetembelea mji huo wa kaskazini-mashariki wa Baga, alisisitiza kuwa, jeshi la serikali limeshinda vita dhidi ya Boko Haram.
Jeshi la serikali wiki iliyopita liliurejesha mji wa Baga uliokuwa ukishikiliwa na Boko Haram. Kundi hilo bado linashikilia sehemu kubwa ya kaskani-mashariki ya Borno na zaidi ya watu milioni tatu wamekimbia nyumba zao.
Mashambulizi huko Kano na Potiskum Jumanne yamechukua maisha ya watu zaidi ya 50. Hakuna kundi lililojitokeza na kusema kuwa limehusika namashambulizi hayo.