Wednesday 4 February 2015

`Hakuna wa kuvaa viatu vya Ferguson'





LONDON, England
KLABU ya Manchester United bado haijapata mbadala wa kocha wazamani wa timu hiyo Sir Alex Ferguson, kwa mujibu wa wakala maarufu wa wachezaji na makocha Jorges Mendes.

Ferguson aliachia ngazi kama kocha wa Man United Mei mwaka 2013 baada ya kuiwezesha timu hiyo kutwaa mataji 38 katika kipindi cha miaka 27 aliyokuwa klabu hapo.

Nafasi ya kocha huyo ilichukuliwa na Mscotland mwenzake David Moyes, aliyedumu kwa takribani miezi 10 tu.

Kwa sasa timu hiyo inafundishwa na Mholanzi Louis van Gaal ambaye tayari ana miezi nane hapo Old Trafford baada ya kuiongoza Uholanzi kucheza nusu fainali ya Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka jana.

Mendes ambaye ni wakala wa wachezaji wengi hapo Old Trafford alisema kuwa, Mkurugenzi Mtendaji ni mtu sahihi kuiongoza Manchester United kushinda vikombe muhimu.

Akimkosoa Van Gaal, Mendes alisema: "Kama bado mngekuwa na Sir Alex Ferguson bila shaka timu ingejihakikishia pointi 12 au 15 zaidi hadi sasa."

Man United kwa sasa iko katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, ikiwa pointi 10 nyuma ya vinara Chelsea na pointi tano nyuma ya Manchester City, na imefuzu kucheza raundi ya tano ya Kombe la FA.

Mendes, ambaye ni wakala wa wachezaji wakubwa duniani, akiwemo Cristiano Ronaldo, Diego Costa na Angel Di Maria, anafikiri kuwa mtu pekee anayeweza kuziba nafasi ya mkongwe Ferguson ni Jose Mourinho.
"Ni ngumu sana kumpata mtu kama Sir Alex Ferguson kwa sababu, ni mtu wa kipekee na kumpata mtu wa namna hiyo ni vigumu sana, " alisema Mendes. "Hapa England yupo mmoja tu na ni Jose Mourinho."

Mendes pia ni wakala wa Mourinho na ninafikiri Mreno mwenzake huyo atabaki Chelsea na kamwe hatakwenda Old Trafford.

"Nina uhakika Jose atabaki," alisema Mendes. "Atakuwa Sir Alex Ferguson wa klabu ya soka ya Chelsea. Anawapenda mashabiki, analipenda jiji na ninafikiri atabaki pale kwa zaidi ya miaka 10."
Mendes anaamini kuwa kipa David De Gea, ambaye ni mteja wake mwingine, kamwe hatakwenda kokote.

Muhispania huyo mwenye umri wa miaka 24, aliyejiunga na Man United kwa ada ya uhamisho ya pauni Milioni 17.8, alikuwa akihusishwa na kuhamia Real Madrid kwa kitita kikubwa.

"Amebakiza mwezi mmoja katika mkataba wake na ninafikiri ataendelea kubaki Manchester," alisema Mendes mwenye umri wa miaka 49, aliyeelezwa kuwa ana utajiri wa zaidi ya pauni Milioni 1 zilizotokana na uhamisho.

"Mchezaji ataamua, lakini kwa sasa ana furaha pale."
Mendes pia alisema kuwa Radamel Falcao, yuko kwa mkopo akitokea Monaco, atakuwa katika klabu kubwa hata kama Man United watamsajili kwa mkataba wa kudumu au hawata fanya hivyo.

No comments:

Post a Comment