Saturday 21 February 2015

MAN United yapigwa na Swansea 2-1



 *Arsenal yatakata, Chelsea yabanwa

Bafetimbi Gomis (kulia) akishangilia bao na mwenzake.
England, England
MANCHESTER United usiku huu imepokea kipigo cha pili katika Ligi Kuu England tangu Novemba wakati bao la dakika za mwisho la Bafetimbi Gomis likiipatia Swansea ushindi wa 2-1.
Bao la Ander Herrera liliiwezesha Man United kuwa mbele, lakini wenyeji walijibu mapigo haraka wakati Ki Sung-yueng alipoujaza mpira wavuni akiunganisha krosi ya Jonjo Shelvey.
Kikosi cha kocha Louis van Gaal kilitawala zaidi kipindi cha pili lakini kilishindwa kabisa kupata bao.
Gomis ndiye aliyeihakikishia ushindi Swansea baada ya kufunga bao katika dakika ya 75 ya mchezo huo na kuipatia timu hiyo ushindi wa kwanza dhidi ya Man United.
Kipigo hicho ni pigo kwa Manchester United katika mbio zake za kutaka kucheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Kwa kupoteza mchezo mmoja tu kati ya 19 katika mashindano yote, Man United ilifanya mabadiliko mara tatu kutoka katika kikosi kilichocheza mechi ya Kombe la FA na kuibuka na ushindi dhidi ya Preston,huku ikimuita Robin van Persie aliyefiti kucheza katika kikosi hicho.
Nayo Arsenal iliibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Crystal Palace huku vinara wa ligi hiyo yenye timu 20 Chelsea wakivutwa shati katika mbio za ubingwa baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Burnley.
Katika mchezo mwingine; Stoke City iliibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Aston Villa huku Hull City ikiondoka na pointi zote tatu baada ya kuifunga QPR kwa bao 2-1.
Sunderland ilishindwa kuutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimisha suluhu na West Brom na Man City ilikuwa mbele kwa bao 5-0 dhidi ya Newcastle hadi tunakwenda mitamboni.

No comments:

Post a Comment