Sunday, 8 February 2015

Ni kipigo kibaya zaidi-Ancelotti



*Ni baada ya kufungwa 4-0 na Atletico Madrid


MADRID, Hispania
KOCHA Muu wa Real Madrid Carlo Ancelotti anasema kipigo cha 4-0 kutoka kwa wapinzani wao wa jiji moja (Madrid derby) Atletico Madrid ni kibaya zaidi katika kipindi chake cha kuifundisha timu hiyo.
Kipigo hicho cha Jumamosi ni kikubwa zaidi kwa timu hiyo katika kipindi cha miaka minne.
"Ni rahisi kuchambua mchezo huu kwa sababu Atletico walikuwa timu bora zaidi katika kila muda wa mchezo, " alisema Ancelotti.
"Walicheza zaidi, walikuwa na kiwango bora katika mchezo, walijipanga vizuri, kila mahali walikuwa wazuri. Ni pambano baya zaidi tangu kuwa kocha."
Ancelotti, aliyechaguliwa kuwa kocha wa Real Madrid Juni 2013, alimkaribisha mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or Cristiano Ronaldo katika kikosi chake, ambacho hakikuwa na baadhi ya wachezaji wake kutokana na majeruhi na kufungiwa.
Atletico ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga walitumia nafasi ya kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa na Real Madrid kufikia mechi sita.
"Tunatakiwa kutathmini nini kilichotokea lakini hatuwezi kusahau kwamba bado tuko kileleni mwa La Liga. Nina imani kubwa na wachezaji hawa.
Real Madrid ambao ni mabingwa wa Ulaya wako pointi nne mbele ya wapinzani wao Barcelona, ambao leo Jumapili wachezaji na Athletic Bilbao, na Atletico iliyopo katika nafasi ya tatu.
"Bado tunatakiwa kuendelea kupambana na kuangalia kinachotokea, " alisema kocha wa Atletico Diego Simeone alipoulizwa nafasi ya timu yake katika kutetea ubingwa wa Hispania.

No comments:

Post a Comment