Saturday, 7 February 2015

DRC washika nafasi ya tatu Afcon
Kongo DRC wakishangilia na medali zao.
MALABA, Guinea ya Ikweta
KONGO DRC Jumamosi ilimaliza ya tatu baada ya kuwafunga wenyeji kwa penati 4-2 baada ya timu hizo kutoka suluhu katika muda wa kawaida katika mchezo wa Mataifa ya Afrika.
Yalikuwa matokeo ya kujifariji zaidi kwa Kongo ambao kwa mara ya mwisho walimaliza mashindano ya Afcon katika nafasi ya tatu mwaka 1998.

Hatahivyo, ilikuwa ni pigo kwa wenyeji, hasa baada ya vurugu kubwa zilizotokea wakati wa mchezo wa nusu fainali ambako walifungwa mabao 3-0 na Ghana Alhamisi.
Robert Kidiaba alikuwa shujaa baada ya kuokoa penati moja wakati Guinea ya Ikweta walikosa penati yao ya kwanza.
Kongo ya DRC ilifunga penati zake kupitia kwa akina Cedrick Mabwati, Lema Mabidi, Chancel Mbemba na Gabriel Zakuani.
Mchezaji aliyeingia kipindi cha pili Raul Bosio alishuhudia penati yake ikiokolewa na Kidiaba, wakati Juvenal Owono na Ellong Doualla walifanikiwa kufunga penati zao lakini wakati tayari makosa yalishafanyika na kushindwa kuliokoa jahazi hilo.
Kipindi cha kwanza timu zote zilionekana kucheza vizuri lakini Guinea ya Ikweta walitawala zaidi dakika 20 za mwanzo.
Kidiaba alikuwa katika kiwango chake bora wakati alipofanya kazi nzuri katika dakika ya nne pale alipookoa michomo ya Balboa na Esue.
Kongo ilipata nafasi mbili za wazi za kufunga wakati nafasi ya kwanza ilikuwa ile ya mshambuliaji Jeremy Bokila aliyenusurika kufunga katika dakika ya 20 alipopiga shuti lililombbatiza beki Daniel Vazquez na kuwa kona.
Hatahivyo, nafasi nzuri zaidi ya kufunga ilikuja katika dakika ya 39 wakati Yannick Bolasie, alipokuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini alishindwa kuuweka mpira huo wavuni licha ya kumpita Randy Iyanga.
Wenyeji Guinea ya Ikweta walipigwa fainali ya pauni 65,000 na Shirikisho la Soka la Afrika kufuatia vurugu zilizotokea wakati wa mchezo wa nusu fainali.

No comments:

Post a Comment