Wednesday, 25 February 2015

Wenger ailaumu Arsenal kwa kichapo  *Arsenal yafungwa 3-1 na Monaco Emerates
Dimitar Berbatov akishangilia bao lake dhidi ya Arsenal.
LONDON, England
KOCHA Arsene Wenger ameiponda timu yake ya Arsenal na kuwalaumu kabisa mabeki wake kufuatia kipigo cha bao 3-1 kutoka kwa Monaco katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa kwenye uwanja wa Emirates.
Kocha huyo mwenye ghadhabu alidai kuwa wachezaji wake hawakujiandaa kiakili kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wakati wakipokea kipigo kwa mabao ya Geoffrey Kondogbia, Dimitar Berbatov na mchezaji aliyetokea benchi Yannick Ferreira-Carrasco.
Wenger alitupa lawama za wazi kwa wachezaji wake kwa kupokea kichapo hicho tena kwenye uwanja wao wa nyumbani huku bao lao la kufutia machozi likiwekwa kimiani na Alex Oxlade-Chamberlain.
Kwa matokeo hayo Arsenal sasa angalau inahitaji ushindi wa angalau bao 3-0 katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Machi 17 ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata.
Wenger alisema: ‘Tulikosa nafasi kibao na kiasi fulani beki haikucheza vizuri. Hatukuwa kabisa katika kiwango tulichotakiwa kuwa.
Bao la pili na tatu ni yakujiua. Tulifanya matokeo kuwa 2-1 na hatukuwa na haki ya kuwaachia wafunge la tatu. Sasa inafanya kazi yetu kuwa ngumu zaidi katika mchezo wa marudiano…”
“Katika kiwango hiki haifanyi kazi,. Kiakili hatukuwa tayari, hatukujiandaa vya kutosha kwa ajili ya mchezo huu. Hilo limetugharimu.
“Katika dakika 20 za kwanza za mchezo kulikuwa na nafasi ya sisi kushinda mchezo ule.”

No comments:

Post a Comment