Saturday, 21 February 2015

Aguero matumaini kibao ya ubingwa


LONDON, England
MCHEZAJI Sergio Aguero anasema kuwa, Manchester City kamwe hawatakata tamaa katika mbio za kuwafukuza vinara wa Ligi Kuu ya England Chelsea kwani wanajua kuwa wanaweza kulitwaa taji hilo katika dakika za mwisho kabisa za ligi hiyo.
Man City iliyopo katika nafasi ya pili inaweza kuwa pointi 10 nyuma ya vinara Chelsea wakati leo watakapocheza na Newcastle kwa sababu vijana wa Jose Mourinho watakuwa tayari wamecheza na Burnley kwenye uwanja wa Stamford Bridge mapema leo.
Aguero anakumbukwa kwa kufunga katika dakika zamwisho walipocheza dhidi ya QPR katika siku ya mwisho ya msimu wa ligi wa mwaka 2011-12 na kuiwezesha Man City kutwaa taji la Ligi Kuu ya England.
Na huku zikiwa zimebaki mechi 13 kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo, mshambuliaji huyo Muargentina anasema vijana wa Manuel Pellegrini wataendelea kupambana.
"Naamini hii itakuwa moja ya Ligi Kuu kali kabisa katika miaka ya hivi karibuni na tutafanya kila kitu kuhakikisha tunatetea taji letu, " alisema Aguero.
 
Sergio Aguero
"Kwanini hapana? Hatukuwa vizuri msimu uliopita lakini bado tulishinda na wakati wowote nashawishika kuwa tutakuwa mabingwa.
"Kuna safari ndefu ya kwenda na zimebaki mechi nyingi za kucheza, hivyo lolote linawezekana.
"Arsenal na Manchester United zimerejea katika mstari, Southampton hawako nyuma sana na Liverpool na Spurs nao wameonesha mwelekeo mzuri."

No comments:

Post a Comment