Wednesday, 4 February 2015

Tanzania wenyeji netiboli Afrika 2015


Mwenyekiti wa Chaneta Annie Kibira katika moja ya mikutano.

Na Mwandishi Wetu
ZAIDI ya nchi 12 zinatarajia kushiriki katika mashindano ya netiboli ya Afrika yatakayofanyika jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Annie Kibira alisema kuwa wanatarajia kupokea wageni kutoka zaidi ya nchi 12 watakaokuja na timu zao katika mashindano hayo ya Afrika.

Kibira alisema kuwa mashindano hayo yatafanyika jijini Dar es Salaam nje ya Uwanja wa Taifa kuanzia Mei 23 hadi 30 mwaka huu.

Alisema kuwa Kamati ya Utendaji ya Chaneta ilikutana hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kuthibitisha kuandaa mashindano hayo makubwa kabisa barani Afrika.

Hatahivyo, Kibira hakuwa tayari kutaja bajeti nzima ya mashindano hayo, lakini alisema kwa kujiamini kuwa wana uhakika wa kuandaa mashindano hayo kwani washiriki wanajitegemea kila kitu.

Alisema kuwa mbali na washiriki kujigharamia kila kitu, pia watalipa ada ambayo itaisaidia Chaneta kuwagharamia waamuzi na wasimamizi wa mashindano hayo ambayo wanatoka katika Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (INF).

Alisema kuwa wamepokea kwa mikono miwili heshima waliyopewa kuandaa mashindano hayo ya Afrika.

Tanzania katika viwango vya ubora wa mchezo wa netiboli Afrika iko katika nafasi ya 15 huku Malawi ikishika nafasi ya kwanza na kufuatiwa na Afrika Kusini.

Aidha, Kibira alisema kuwa timu ya JKT Ruvu ndio pekee kwa Tanzania Bara iliyothibitisha kushiriki mashindani ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Zanzibar mwezi Machi.

Timu nyingine za Tanzania Bara zitakazoshiriki mashindano hayo ya Afrika Mashariki ni pamoja na JKT Mbweni na Uhamiaji Tanzania.

No comments:

Post a Comment