Wednesday 25 February 2015

Yanga kujilinda, kushambulia Botswana




Kikosi cha Yanga.
Na Seba Nyanga
YANGA imeondoka leo alfajiri kwenda Gaborone, Botswana huku akisema kuwa itacheza kwa umakini mkubwa dhidi ya BDF katika mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho la Afrika.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, yanga ilitakata kwa kuibuka na ushindi wa bao 2-0 na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kusoga mbele.
Pamoja na nafasi hiyo nzuri, lakini kocha msaidizi wa vijana hao wa Jangwani Charles Boniface Mkwasa alisema kuwa watacheza kwa umakini mkubwa wakijilinda huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza.
Mkwasa ambaye aliwahi kuichezea Yanga na timu ya taifa `Taifa Stars alisema kuwa kamwe hawatabweteka na ushindi huo wa bao 2-0 kwani katika soka lolote linaweza kutokea.
Kocha huyo alisema kuwa pamoja na faida waliyonayo hiyo ya mabao mawili, lakini bado wanatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa BDF kwani sio timu mbaya.
Alisema kuwa kuongoza sio kigezo cha kufanya vizuri katika mchezo unaokuja na ndio maana watacheza kwa tahadhari ili kuhakikisha wanapata ushindi mwingine Botswana.
Alisma kuwa pamoja na kujilinda lakini watahakikisha wanashambulia pia ili kupata mabao ambayo yatazidi kuwachanganya na kuwapa kazi ya ziada wapinzani wao hao.
Alisema kucheza kwa tahadhari kutawafanya kuwa makini zaidi na kufanya vizuri katika mchezo huo na kuwawezesha kusonga mbele katika hatua inayofuata.
Yanga iliondoka leo alfajiri na wachezaji 20 pamoja na viongozi saba kwenda Gaborone nchini Botswana tayari kwa mchezo huo utakaofanyika kesho nchini humo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment